Wauza mitumba Dodoma walalamikia kamatakamata

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,314
33,108
Wauza nguo za mitumba katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Mjini, wamelilalamikia zoezi la kuwakamata wafanyabiashara wanaotembeza bidhaa mitaani, kuwa linafanyika `kibabe’ na limelenga kuwanufaisha baadhi ya maofisa wanaowakamata.
Wakiongea kwa nyakati tofauti katika soko la Sabasaba mjini hapa jana, walisema kuwa wanapokamatwa na kwenda kutoa faini ya sh 50,000 kama dhabu, wamekuwa hawapati mzigo wote uliokamatwa.
“Ukienda kulipa faini kama adhabu hupati nguo zako zote na zinazobakia zinakuwa ni zile mbaya,” alisema Hapi Makha. Dimani Iddi, alisema wameamua kufanya biashara hiyo baada ya kukosa ajira kwa kuwa viwanda vilivyokuwepo vimesimamisha uzalishaji.
Aliitaka serikali kuwasaidia wafanyabiashara badala ya kuwanyanyasa na kuwachukulia mitaji yao .
Elizabeth Mazengo ambaye anauza mitumba ofisini na majumbani, alisema biashara hiyo inamwezesha kulipa kodi ya nyumba, kuwasomesha watoto na kula lakini kutokana na kamatakamata hiyo inamlazimu kugeuka ombaomba.
“Ndani ya mkoa wa Dodoma hali ya hewa si nzuri ya kufanya mazao kupatikana sasa wanakuja kutukamata wanategemea tutaishije sisi kama si kugeuka kuwa ombaomba?” Alihoji Sospiter Msendekwa.
Aliishauri serikali kusafisha mazingira badala ya kuwakamata wauza mitumba kwa sababu wao hakuna wanachochafua mitaani.
Nao wauza mnada wa mitumba katika soko la Sabasaba, James Mlokole, alisema kamatakamata hiyo imewafanya kukosa biashara baada ya wamachinga wengi kushindwa kurejesha mitaji yao.
Alisema hali hiyo imewafanya kuuza nguo zao kwa hasara na kushauri halmashauri kutenga muda wa jioni kama ilivyo kwa jiji la Dar es Salaam.
Alisema kwa kufanya hivyo kutawawezesha wamachinga hao kupata mapato yatakayowawezesha kumudu maisha yao ya kila siku.
Alipoulizwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Suzan Bidya, aliwataka kufuata taratibu na sheria zilizotungwa badala ya kulalamika.
“Waende kwenye maeneo waliyopangiwa kama Sabasaba na Bonanza…hizo sehemu wanazofanyia biashara ni njia za magari, baiskeli, watu na wakitandaza barabarani huo ni uchafu,”alisema.



CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
 
Back
Top Bottom