Maalbino wahofu kutolewa kafara uchaguzi Mkuu
Rais wa Chama cha Maalbino Duniani, Peter Ash, amesema wanahofia mauaji dhidi yao yanaweza kuongezeka zaidi wakati Watanzania wanapoelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
Rais wa Chama cha Maalbino Duniani, Peter Ash.
Alisema hofu hiyo inatokana na wanasiasa wengi barani Afrika, Tanzania ikiwamo, kutegemea zaidi ushirikina katika kupata ushindi kwenye uchaguzi.
Ash ambaye pia ni muasisi na Rais wa Asasi ya Chini ya Jua (UTSS), inayoshughulikia elimu, afya na uchumi kwa maalbino duniani, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
Mkutano huo na waandishi wa habari uliitishwa na Ash katika ofisi za tawi la asasi hiyo zilizoko Mikocheni B jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuzungumzia maendeleo ya vita dhidi ya mauaji ya maalbino katika nchi ambazo matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi vimekithiri.
Tunahofia mauaji dhidi ya jamii ya maalbino yanaweza kuongezeka tunapoelekea uchaguzi, kwa sababu wanasiasa wengi barani Afrika wanategemea ushirikina kupata usindi kwenye uchaguzi, alisema Ash.
Alisema UTSS yenye makao yake makuu nchini Canada, pamoja na mambo mengine, inatoa msaada
kwa ajili ya kuwawezesha maalbino kwenda kupata elimu popote duniani na kwamba, wametenga zaidi ya dola za Marekani 250,000 kwa ajili ya kutekeleza mpango huo.
Alishauri kukamilisha mchakato wa kupitisha sheria ya haki za binadamu ya kimataifa ili ianze kutumika mara moja kwa vile itasaidia kuwalinda maalbino.
Hata Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Kin-Moon, aliwahi kueleza suala hilo alipotembelea Tanzania, alisema Ash.
Alisema hata Tangazo la Haki za Binadamu la Kimataifa limeeleza bayana kwamba, watu wote wana haki sawa mbele ya sheria na pia, wana haki ya kupewa ulinzi dhidi ya ubaguzi au unyanyasaji wa aina yoyote.
Ash alisema kuwa katika kuhakikisha matukio ya mauaji ya albino hayaongezeki nchini, wao wanaiomba serikali kuhakikisha inaimarisha ulinzi kwa albino.
Habari za kuuawa kwa maalbino, zilianza kujitokeza mwishoni mwa mwaka juzi, watu zaidi ya 30 wa jamii hiyo waliripotiwa kuuawa na wengine kukatwa sehemu za viungo na kuleta hofu kubwa miongoni mwa Watanzania.
Hadi sasa baadhi ya watuhumiwa wa mauaji hayo wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili. Hivi sasa Mahakama Kuu ya Tanzania inaendelea kusikiliza kesi mbili za mauaji ya albino katika miji ya Shinyanga na Kahama, mkoani Shinyanga.
Kabla ya kuibuka kwa mauaji hayo, Watanzania walishuhudia ujinga mwingine unaofanana na huo, wa kuchuna watu ngozi kwa imani za kupata utajiri.
Watu waliokuwa wakiendesha vitendo hivyo, wamekuwa wakifanya hivyo baada ya kushauriwa na baadhi ya waganga wa jadi.
Katika kuuonyesha umma hali ilivyo, Agosti, mwaka jana, maalbino walifanya maandamano jijini Dar es Salaam yaliyopokelewa na Rais Jakaya Kikwete katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Katika maandamano hayo, maalbino walimweleza Rais Kikwete kwamba hali ni mbaya sana, hususan vijijini, ambako baadhi yao wamekuwa wakilazimika kulala ifikapo saa 10:00 jioni kwa hofu ya kukamatwa na wauaji.
CHANZO: NIPASHE