Prof. Mkenda wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia asoma Bajeti ya Makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2022/23

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,797
11,959
HOTUBA YA WAZIRI WA ELIMU,

SAYANSI NA TEKNOLOJIA

PROF. ADOLF FAUSTINE MKENDA (MB),

AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2022/23A. UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,
kufuatia taarifa iliyowasilishwa ndani ya Bunge lakoTukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii iliyochambua makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia FUNGU 46 na FUNGU 18 la Tume ya Taifa ya UNESCO, naomba kutoa hoja kwamba sasa Bunge lako Tukufu, likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia FUNGU 46 na FUNGU 18 kwa mwaka wa fedha 2021/22. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/23.


Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema, kuniwezesha kuendelea kutimiza majukumu yangu na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2022/23. Aidha, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila kitu, hasa kwa amani na mshikamano wa Taifa letu.


Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na kwa kuendelea kumuamini Mheshimiwa Omary Juma Kipanga (Mb) kuwa Naibu Waziri. Napenda pia kumshukuru Rais kwa uongozi na miongozo anayotupatia ambayo imetusaidia sana katika kusimamia Sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Nawashukuru pia Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango Makamu wa Rais, na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna13​

ambavyo wamekuwa wakimsaidia Rais katika kutusimamia na kutuongoza.


Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru wewe, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb) kwa uongozi wako mahiri wa Bunge letu tukufu. Nawashukuru pia Naibu Spika, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb) na wenyeviti wote wa Bunge kwa uongozi wao. Nakupongeza pia Mheshimiwa Spika kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge letu. Nampongeza pia Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb) kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge letu.


Mheshimiwa Spika, naomba kutoa pole kwako wewe Mheshimiwa Spika na kwa Bunge lako Tukufu kwa kuwapoteza waheshimiwa wabunge wafuatao; Hayati Elias John Kwandikwa aliyekuwa Mbunge wa Ushetu na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa aliyefariki tarehe 2 Agosti, 2021, Hayati William Tate Ole Nasha aliyekuwa Mbunge wa Ngorongoro na Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu - Uwekezaji, aliyefariki tarehe

Septemba, 2021, na Hayati Irene Alex Ndyamkama aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa aliyefariki tarehe 24 Aprili, 2022. Natoa pole kwa ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa kuondokewa na wapendwa wetu, na kwa namna ya pekee natoa pole kwa Mheshimiwa Anna Richard Lupembe (Mb) kwa kufiwa na mtoto wake; naungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki kumuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi, Amina.


Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru kwa namna ya pekee Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo


(Mb), Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Aloyce John Kamamba (Mb), na wajumbe wote wa Kamati kwakuchambua na kuishauri Wizara kuhusu Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2022/23. Kamati hii ni makini sana, na imekuwa ikitoa maoni na ushauri wenye lengo la kuhakikisha tunaendelea kuboresha elimu na kuendeleza sayansi na teknolojia kwa manufaa ya Taifa letu.


Mheshimiwa Spika, Napenda pia kuwapongeza wabunge waliochaguliwa hivi karibuni kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni Mheshimiwa Emmanuel Leklshon Shangai Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro na Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani Mbunge wa Jimbo la Ushetu. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha kwa kuteuliwa na Mhe. Rais kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Mheshimiwa Spika, Napenda kumshukuru sana mtangulizi wangu, Mheshimiwa Profesa Joyce Lazaro Ndalichako (Mb), na Katibu Mkuu aliyestaafu kwa heshima zote, Dkt. Leornard Akwilapo, kwa kazi nzuri walizofanya katika Wizara. Wameiacha Wizara pazuri na wameturahisishia kazi sana. Nampongeza sana Mheshimiwa Profesa Joyce Lazaro Ndalichako (Mb) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana Ajira na wenye Ulemavu.Mheshimiwa Spika, namshukuru sana mke wangu Beatrice, watoto na familia kwa upana wake wote, ikiwa ni pamoja na mama mzazi Sekunda, kwa upendo na ukaribu ambao wamekuwa wakinipa na kunijaza nguvu na ari ya kuchapa kazi.

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi, naomba sasa nitoe taarifa ya utelekezaji wa majukumu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia FUNGU 46 na FUNGU 18 kwa Mwaka wa Fedha 2021/22, na Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.


B.\ UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2021/22

TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA BAJETI

11.\ Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Bunge lako Tukufu liliidhinisha kiasi cha Shilingi 1,519,316,801,000.00 kwa ajili ya FUNGU 46 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo Shilingi 480,474,878,000.00 zilikuwa ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 1,038,841,923,000.00 zilikuwa ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo bajeti ya maendeleo inajumuisha ongezeko la fedha za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19. Aidha, kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO - FUNGU 18 liliidhinisha kiasi cha Shilingi 2,679,073,000.00 kwa ajili ya

matumizi ya kawaida ambayo yanajumuisha1,146,780,000Shilingi.00 za mishahara na Shilingi 1,532,293,000.00 za matumizi mengineyo.

Ukusanyaji wa Maduhuli

Mheshimiwa Spika,
katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/22, Wizara kupitia FUNGU 46 ilitarajia kukusanya maduhuli yenye thamani ya Shilingi 540,943,008,495.63 ambapo kiasi cha Shilingi 8,680,995,000.00 kilipangwa kukusanywa na idara na vitengo na Shilingi 532,262,013,495.63 zilipangwa kukusanywa na taasisi zilizo chini ya Wizara. Vyanzo vya maduhuli haya ni ada, ushauri elekezi, ukaguzi wa shule na utoaji wa huduma mbalimbali.

13.\ Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili, 2022 Wizara imekusanya Shilingi 415,796,161,776.80 sawa na asilimia 77 ya makadirio ambapo Shilingi 7,622,836,164.00 zimekusanywa na idara na vitengo na Shilingi 408,173,325,612.80 zimekusanywa na taasisi zilizo chini ya Wizara.

Matumizi ya Kawaida

Mheshimiwa Spika,
hadi kufikia Aprili, 2022, Wizara imepokea Jumla ya Shilingi 396,962,728,624.62 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, kupitia Fungu 46, ambazo ni sawa na asilimia 83 ya fedha za Matumizi ya Kawaida zilizoidhinishwa. Aidha, kupitia Tume ya UNESCO – Fungu 18 Wizara imepokea jumla ya Shilingi 1,723,003,183.30 sawa na asilimia 76 ya fedha iliyoidhinishwa na Bunge lako Tukufu.


Miradi ya Maendeleo

Mheshimiwa Spika
, kwa upande wa miradi ya maendeleo hadi kufikia Aprili, 2022, Wizara ilikuwa imepokea jumla ya Shilingi994,711,772,676.29kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambazo ni sawa naasilimia 96 ya bajeti iliyotengwa. Kati ya fedha hizo Shilingi 684,470,232,276.01 ni fedha za ndani na Shilingi 310,241,540,400.29 ni fedha za nje. Aidha, kiasi cha fedha za nje kinajumuisha Shilingi 64,297,963,057.82 kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19


TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA

Mheshimiwa Spika,
sehemu hii inaelezea utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya Wizara kwa kuzingatia vipaumbele vyake. Taarifa inatoa ufafanuzi wa maeneo ya msingi ya utekelezaji wa Wizara kwa kutoa takwimu na matokeo ya utekelezaji huo. Maeneo yanayotolewa taarifa yamegawanyika kimajukumu kama ifuatavyo:

Usimamizi wa Elimumsingi na Sekondari

Mheshimiwa Spika,
katika Mwaka wa Fedha 2021/22, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa Elimumsingi inatolewa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Ili kufikia azma hiyo, Serikali imeandaa miongozo mbalimbali ikiwemo Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa Wanafunzi wa Elimumsingi kwa lengo la kuimarisha mahudhurio ya wanafunzi na kuboresha ujifunzaji. Mwongozo tayari upo katika utekelezaji. Aidha, Serikali imeandaa miongozo mingine mitatu ambayo ipo katika hatua ya uchapaji na usambazaji. Miongozo hiyo ni:

Mwongozo wa Viwango na Uendeshaji wa Elimu ya

Awali -National Operational Guidelines and Minimum Standards for Pre-Primary Education pamoja na Kiongozi cha Utekelezaji wa Mwongozo huo;

Mwongozo wa Uanzishaji, Usimamizi na Uendeshaji wa Vituo Shikizi vya Shule; na

Mwongozo wa Utoaji wa Elimu ya Kujitegemea katika Shule za Msingi na Sekondari

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utoaji wa elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi, Serikali imeboresha na kutekeleza miongozo mitatu ambayo ni: Mwongozo wa Utekelezaji wa Programu ya Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala; Mwongozo wa Kutoa Huduma kwa Wanafunzi katika Programu ya Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala; na Mwongozo wa Wawezeshaji katika Programu ya Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala. Utekelezaji wa miongozo hiyo umewezesha kuwarejesha shuleni wasichana 3,333 kwa mwaka 2022 ukilinganisha na lengo la kurejesha wasichana 3,000 walioacha shule kwa sababu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika
, Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi ni sehemu ya Elimumsingi. Katika eneo hili, Serikali imeendelea na uimarishaji wake kwa kutekeleza yafuatayo:

imeongeza wigo wa utoaji wa programu za elimu masafa mikoani na kuendesha jumla ya programu 13 katika kampasi za Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ya; Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza. Programu hizo zimewezesha utoaji wa mafunzo ya ualimu na usimamizi wa elimu ya watu wazima kwa vijana na watu wazima 7,185, kati yao wanawake walikuwa 4,075 na wanaume ni 3,110;

imesogeza huduma ya Elimu kwa Njia Mbadala kwa wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali kwa kuwezesha ujenzi wa vituo tisa na kukarabati majengo matano ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima; na

imeendelea kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya sekondari kupitia Elimu kwa Njia Mbadala kwa kufanya mapitio ya mihtasari na moduli za Elimu Nje


ya Mfumo Rasmi kwa hatua ya kwanza ya Kidato cha 1 na 2 na hatua ya pili ya Kidato cha 3 na 4 kwa masomo saba ambayo ni: English, Kiswahili, Geography, History, Civics, Biology na Mathematics.


Mheshimiwa Spika, katika kuongeza ujuzi na maarifa kwa watumishi wanaotekeleza na kusimamia uendelezaji wa Elimumsingi na Sekondari nchini, Serikali imeendelea kutoa mafunzo kama ifuatavyo:

imetoa mafunzo kuhusu huduma ya malezi, unasihi na ulinzi wa mtoto shuleni kwa walimu 243 (wanawake 151 na wanaume 92) wa shule za msingi na sekondari kati ya walimu 200 waliolengwa kutoka katika maeneo ambayo yalikuwa hayajafikiwa na mafunzo hayo. Mafunzo hayo yameimarisha stadi za utoaji wa huduma hizo na kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto;

imetoa mafunzo ya utekelezaji wa mtaala wenye kuzingatia umahiri kwa walimu 4,241 (msingi 2,300 na sekondari 1,941) ambayo yameimarisha uwezo wa walimu kufundisha kwa kuzingatia umahiri;

imetoa mafunzo ya mbinu bora za ufundishaji na ujifunzaji wa somo la hisabati kwa walimu 846 wa shule za msingi na sekondari (wanawake 213 na wanaume 633) kutoka katika halmashauri 20 zenye ufaulu hafifu nchini; na

imewezesha mafunzo kwa walimu wawezeshaji 736 wa masomo ya sayansi na hisabati kwa lengo la kuwajengea uwezo katika uwezeshaji wa walimu wa sekondari 20,000 wa masomo husika katika ngazi ya Halmashauri.


Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika sekta ya elimu. Uwekezaji huo unalenga katika kuongeza fursa za utoaji wa elimu bora. Mafanikio ya uimarishaji wa mazingira hayo ni kama ifuatavyo:

usajili wa jumla ya shule 741 zilizokidhi vigezo kati ya shule 450 zilizolengwa. Mchanganuo wa shule hizo ni kama ifuatavyo; shule za awali pekee (zisizo za Serikali 33), shule za awali na msingi 511 (za Serikali 363 na zisizo za Serikali 148), sekondari 196 (za Serikali 151 na zisizo za Serikali 45) na Chuo cha Ualimu kimoja kisicho cha Serikali;

utoaji wa vibali vya kuanzisha shule 88 zilizokidhi vigezo kati ya 182 zilizoomba. Kati ya hizo, shule za awali pekee ni saba, za awali na msingi 65 na sekondari 16;

kutoa uthibitisho wa wamiliki wa Shule 237 na mameneja 237 kati ya wamiliki 331 na mameneja 331 walioomba ambapo wamiliki wa shule za awali pekee 16, za awali na msingi 181 na sekondari 40;

kutoa vibali vya kuanzisha huduma ya bweni katika shule 68 (shule za awali na msingi 46 na sekondari 22) zilizokidhi vigezo, kati ya shule 75 zilizoomba ili kupunguza adha kwa wanafunzi kutembea umbali mrefu;

kutoa vibali vya kuongeza mikondo kwa shule 21 (awali na msingi 14 na sekondari 7) pamoja na kutoa vibali vya kuongeza tahasusi katika shule za sekondari 19 zilizokidhi vigezo;

kuwezesha ujenzi wa shule mpya 175 (msingi 9 na sekondari 166) ambapo ujenzi wa shule 33 (msingi 9 na sekondari 24) umekamilika na ujenzi wa shule 142 za sekondari upo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji. Aidha, imewezesha ujenzi wa madarasa 3,283, mabweni 112, ofisi 10, matundu ya vyoo 8,096, usimikaji wa vifaa vya kunawia mikono na ununuzi wa matenki ya kuhifadhia maji safi katika shule za msingi 235; na

kuendelea na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mfano Iyumbu - Jijini Dodoma itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa Elimumsingi nchini, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewezesha ununuzi wa magari
kwa ajili ya maafisa elimu msingi katika halmashauri 184 na magari matatu kwa ajili ya Baraza la Mitihani. Aidha, inaendelea na taratibu za ununuzi wa magari 185 kwa ajili ya maafisa elimu sekondari nchini. Lengo la utekekelezaji wa afua hiyo ni kuendelea kuimarisha mazingira ya ufanyaji kazi kwa maafisa elimu na kusogeza huduma karibu na wananchi kwa usimamizi bora wa elimu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa vitabu katika ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari kwa lengo la kuimarisha uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja na hivyo kuboresha ufundishaji, ujifunzaji na kujenga utamaduni wa wanafunzi kupenda kujisomea vitabu. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:

imeimarisha uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi kwa Darasa la VI – VII kwa kuwezesha uchapaji na usambazaji wa nakala 9,903,453 za vitabu vya kiada vya masomo 14 na Kiongozi cha Mwalimu nakala 599,928 ambapo kwa sasa uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi umefikia 1:1;

imechapa na kusambaza vitabu vya kiada nakala 3,139,500 vya masomo ya Elimu ya Awali na Msingi Darasa la I – V vitakavyosaidia kuboresha ufundishaji na ujifunzaji;

imechapa na kusambaza vitabu vya kiada vya maandishi yaliyokuzwa nakala 20,422 kwa masomo 44 ya Darasa la I – VII kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu.

imeendelea kuimarisha upatikanaji wa vitabu kwa wanafunzi wa Elimu Nje ya Mfumo Rasmi kwa kuwezesha kuchapa na kusambaza katika halmashauri zote za Tanzania Bara nakala 1,510,832 za vitabu vya kiada vya Kundirika la Kwanza na la Pili, Kiongozi cha Mwalimu nakala 137,500 na mihtasari nakala 16,041;

imekamilisha uchapaji wa nakala 6,074,000 za vitabu vya kiada aina 29 vya Sekondari Kidato cha 1 - 4 kwa masomo ya Biology, Physics, Chemistry, Mathematics, Agriculture, Home Economics, Kiswahili, Civics, Information and Computer Studies, Geography, History na English. Kazi ya kusambaza nakala hizo katika halmashauri zote Tanzania Bara inaendelea; na

imeendelea na uandishi wa vitabu 34 vya masomo ya ufundi kwa ajili ya wanafunzi wa Kidato 1 – 4 ambavyo vipo katika hatua za ukamilishaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa elimu ya Msingi na Sekondari nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:

imeandaa maudhui ya kielektroniki ya wanafunzi wa Elimu ya Awali jumla ya Masomo 58 ambapo Lugha ya Kiswahili ni 29 na Kiingereza 29 kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za KKK;

imeandaa mfumo wa kielektroniki (Learning Management System - LMS) wenye moduli, miongozo na vitabu mbalimbali vya kufundishia na kujifunzia kwa njia ya mtandao utakaotumika kutoa Mafunzo Endelevu kwa Walimu Kazini (MEWAKA);

imeboresha Maktaba Mtandao ya Taasisi ya Elimu Tanzania kwa kuiongezea uwezo wa kubeba maudhui katika miundo mbalimbali na kuongeza baadhi ya vitabu ambavyo havikuwepo. Maktaba hiyo inapatikana bure kwa anwani ambayo imerahisisha upatikanaji wa vitabu;

imekamilisha uandishi wa vitabu aina 34 vya masomo mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi wa Kidato cha 1 – 6 na kuviweka katika maktaba mtandao inayopatikana bure. Vilevile, imefanya tathmini na kutoa ithibati ya vitabu vya ziada 53 na maudhui ya kielektroniki 17. Aidha, miswada 90 ipo katika hatua mbalimbali za tathmini; na

imenunua vifaa vya studio ya televisheni na redio kwa ajili ya kuandaa programu mbalimbali za kielimu ambazo zitasaidia kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za maktaba nchini kwa lengo la kuamsha ari ya Watanzania kupenda kujisomea na kuelimika. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:

imefanya ukaguzi na kutoa ushauri wa usimamizi na uendeshaji wa Maktaba 13 zikiwemo Maktaba ya Mkoa wa Singida, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Dodoma, Ruvuma, Mbeya, Kagera, Morogoro na Iringa pamoja na Maktaba ya Wilaya ya Mbulu na Maktaba ya Kijiji cha Mbweera iliyopo Wilaya ya Hai;

imetoa ushauri wa kitaalamu katika vituo 286 kati ya vituo 350 vya huduma ya maktaba vilivyolengwa ambapo ushauri ulihusu uanzishaji, upangaji na uendeshaji wa Maktaba za Shule 171, Vyuo 11, Taasisi 82 na Halmashauri 22;

imewajengea uwezo wakutubi 120 kutoka vituo 42 vinavyotoa huduma za maktaba kuhusu namna bora ya kuhudumia jamii; na

imewezesha ukarabati wa maktaba ya Mkoa wa Tabora, Iringa, Kilimanjaro, Kigoma, Rukwa, Morogoro na Kagera.


Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Elimumsingi inatolewa kwa usawa na kuzingatia malezi bora na usalama wa mtoto shuleni pamoja na upangaji na usawazishaji wa walimu wa sekondari katika maeneo yote nchini, Serikali imetekeleza yafuatayo:

inaendelea na ukamilishaji wa Mwongozo wa Programu ya Shule Salama; Mkakati wa Kitaifa wa Upangaji na Usawazishaji wa Walimu wa Sekondari; Mkakati wa Kuimarisha Matumizi ya TEHAMA; na Mkakati wa Kuongeza Udahili wa Wasichana katika Shule za Sekondari; na

imechapa na kusambaza Miongozo ya Kutoa Ushauri Nasaha na Unasihi nakala 44,400 kwa ajili ya wanafunzi wa Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari kwenda Halmashauri zote Tanzania Bara. Miongozo hiyo itasaidia walimu kutoa huduma ya ushauri na unasihi kwa wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia upimaji na tathmini ya wanafunzi wa Elimumsingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimu nchini kwa kutekeleza kazi zifuatazo:

imeendesha upimaji wa Darasa la Nne (SFNA) 2021 kwa watahiniwa 1,561,599 kati ya watahiniwa 1,678,209 waliosajiliwa;

imeendesha Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) 2021 kwa watahiniwa 1,108,023 kati ya watahiniwa 1,132,084 waliosajiliwa;

imeendesha Upimaji wa Kidato cha Pili (FTNA) 2021 kwa watahiniwa 602,955 kati ya watahiniwa 652,611 waliosajiliwa;

imeendesha Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) 2021 kwa watahiniwa 521,351 kati ya watahiniwa 538,024 waliosajiliwa. Aidha, imeendesha Mtihani wa Maarifa (QT) 2021 kwa watahiniwa 8,324 kati ya watahiniwa 9,874 waliosajiliwa;

imesajili watahiniwa 88,805 wa Mtihani wa Kidato cha Sita (ACSEE) na watahiniwa 7,115 wa Mitihani ya Ualimu (Astashahada na Stashahada). Mitihani hiyo imeanza kufanyika tarehe 9 Mei, 2022;

imeendesha Upimaji wa Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa sampuli ya wanafunzi 32,043 wa Darasa la Pili ambapo asilimia 67.00 walifikia kiwango tarajiwa cha ufaulu;

imechapa na kusambaza nakala 561,581 za Pupil Item Response Analysis (PIRA) 2020 na Candidates Item Response Analysis (CIRA) 2020 za vitabu vya taarifa za uchambuzi wa majibu ya wanafunzi katika upimaji na mitihani ya Kitaifa kwa lengo la kuvisambaza na kusaidia walimu na wanafunzi kuelewa mada zilizoonesha ugumu katika ujifunzaji na ufundishaji; na

imekamilisha mfumo wa usahihishaji kwa njia ya kielektroniki (E - Marking) katika ngazi ya Elimu ya Ualimu kwa lengo la kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji wa mitihani.


Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kukusanya maoni kuhusu mitaala inayotumika katika ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu kutoka kwa wadau wa elimu ambapo hadi sasa jumla ya wadau 103,210 wametoa maoni. Wadau walioshiriki katika kutoa maoni ni pamoja na; Waheshimiwa Wabunge, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Taasisi za kidini, Taasisi binafsi, Wataalamu mbalimbali wa elimu, na Wananchi kwa ujumla. Aidha, maoni

hayo yamekusanywa Tanzania Bara na Zanzibar na yatazingatiwa wakati wa uandaaji wa mitaala mipya itakayowajengea wanafunzi ujuzi na maarifa yanayoendana na mahitaji ya jamii katika nchi, Kikanda na Kimataifa. Vilevile, mitaala hiyo itawezesha kuwaandaa wanafunzi kuendelea na ngazi ya elimu inayofuata.

Usimamizi wa Elimu ya Ualimu

Mheshimiwa Spika
, Serikali imeendelea kuongeza fursa za Elimu ya Ualimu kwa kudahili jumla ya wanafunzi wa Astashahada ya Elimu ya Msingi kuwa 10,975 (wanawake 5,824 na wanaume 5,151), Stashahada ya Ualimu Sekondari miaka miwili 2,663 (wanawake 1,037 na wanaume 1,626) na Stashahada maalum ya ualimu sekondari sayansi miaka mitatu 5,540 (wanawake 1,973 na wanaume 3,567) na hivyo kufanya Vyuo vya Ualimu vya Serikali kuwa na jumla ya wanafunzi 19,178. Aidha, katika Vyuo vya Ualimu visivyo vya Serikali, jumla ya wanafunzi 136 (wanawake 87 na wanaume 49) wamedahiliwa na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wanaosoma elimu ya ualimu kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada kuwa 19,314 (wanawake 9,113 na wanaume 10,201).

Mheshimiwa Spika,
katika kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Vyuo vya Ualimu, Serikali imetekeleza afua zifuatazo:

inajenga upya Vyuo vya Ualimu vitatu ambavyo ni Sumbawanga, Dakawa, na Mhonda kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ambapo ujenzi upo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji. Aidha, Serikali inajenga Chuo kipya cha Ualimu Ngorongoro kitakachokuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 400;


imejenga jumla ya madarasa 44, maktaba tatu, maabara mbili, kumbi za mihadhara nne, nyumba za watumishi 18, mabweni matano, na jengo la utawala moja katika Vyuo vya Ualimu 23;


imekarabati jumla ya madarasa 16, maktaba moja, ukumbi wa mihadhara mmoja, nyumba za watumishi nane, mabweni saba, bwalo moja, majengo ya utawala mawili na vyoo; na


imewezesha ununuzi wa kompyuta 425 ili kuboresha ufundishaji wa somo la TEHAMA. Aidha, Serikali imeimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya sayansi kwa vitendo kwa kununua vifaa na kemikali za Maabara za Sayansi katika Vyuo 35 vya Ualimu vya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa Elimu ya Ualimu kwa kutekeleza yafuatayo:

imetoa mafunzo kuhusu ufundishaji na ujifunzaji wa somo la hisabati, sayansi na TEHAMA kwa wakufunzi 355 (wanawake 83 na wanaume 272);

imetoa mafunzo kazini kwa wakufunzi 1,168 wa Vyuo vya Ualimu kuhusu utekelezaji wa mitaala yenye kuzingatia umahiri kwa lengo la kuimarisha uandaaji wa walimu tarajali wenye uwezo wa kufundisha kwa umahiri;

imetoa mafunzo ya Usimamizi na Uendeshaji wa Vituo vya Walimu (TRCs) kwa viongozi wasimamizi wa elimu 985 wakiwemo Maafisa Elimu Mkoa 26, Maafisa Elimu Taaluma Mkoa 26, Maafisa Elimu Msingi wa Wilaya 144, Maafisa Elimu Taaluma Wilaya 144, Wathibiti Ubora Kanda 11, Wathibiti Ubora wa Wilaya 144, Maafisa Elimu Kata 346, na Makatibu Wasaidizi Tume ya Utumishi wa Walimu

– TSC 144;

imetoa mafunzo kwa walimu kazini kuhusu uanzishaji na uendeshaji wa Vituo vya Walimu kwa walimu wawezeshaji 30,490 wakiwemo walimu wa elimu ya awali na msingi 26,657, walimu wa elimu maalum 1,882 na wawezeshaji wa MEMKWA 1,951. Mafunzo hayo yametolewa katika Vituo vya Walimu (TRCs) na baadhi ya shule za msingi kupitia Mpango wa Mafunzo Endelevu kwa Walimu Kazini (MEWAKA) kwa lengo la kujenga umahiri katika ufundishaji;

imetoa mafunzo kuhusu ufundishaji na ujifunzaji kwa Wakufunzi wa Elimu ya Awali na masomo ya lugha 479 (Wanawake 253 na Wanaume 226); na

imetoa mafunzo kuhusu ujumuishwaji wa elimu ya usawa wa kijinsia kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu 834 (wanawake 336 na wanaume 498) wa masomo ya sayansi, hisabati, TEHAMA, elimu ya awali na masomo ya lugha.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia uendelezaji wa Elimu ya Ualimu kwa lengo la kuimarisha ubora elimu hiyo. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:

imetoa mafunzo ya uongozi, usimamizi na uendeshaji wa elimu kwa wajumbe wa bodi 325 wa vyuo vya ualimu kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji;

imeandaa mwongozo wa kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Kutoa Mafunzo Kazini kwa Walimu; na

imeandaa Mwongozo wa Uendeshaji wa Vituo vya Walimu na Vyuo vya Ualimu utakaobainisha majukumu ya watendaji kulingana na ngazi zao.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Vyuo vya Ualimu vinatoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya sasa, Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji kwa kutekeleza yafuatayo:

imeendelea na ukarabati wa maabara za sayansi na TEHAMA katika Vyuo vya Ualimu vya Butimba, Dakawa, Morogoro, Patandi, Tukuyu, Mpwapwa na Kasulu; na

imeendelea kuviunganisha Vyuo vya Ualimu 15 vya Serikali katika Mkongo wa Taifa kwa lengo la kuimarisha mawasiliano, ufundishaji na ujifunzaji kwa njia ya kielektroniki.

Uthibiti Ubora wa Shule na Vyuo vya Ualimu

Mheshimiwa Spika,
katika kuhakikisha Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu inayotolewa nchini inazingatia sheria, kanuni, miongozo na taratibu, Serikali imetekeleza yafuatayo:

imetoa mafunzo ya kuimarisha Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani kwa Walimu Wakuu 7,612 kati ya Walimu Wakuu 7,679 waliolengwa na Maafisa Elimu Kata 3,860 kati ya Maafisa Elimu Kata 3,901 pamoja na wajumbe wa Kamati za Shule wapatao 487 waliokuwa katika mpango wa mafunzo;

imetathmini jumla ya asasi 6,524 kati ya lengo la asasi 7,263 ambazo ni: shule za Awali na Msingi 5,332; Shule za Sekondari 1,162; na Vyuo vya Ualimu 30 kwa lengo la kuinua ubora wa elimu;

imefanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa ushauri uliotolewa katika asasi 1,516 ukilinganisha na lengo la asasi 1,453. Kati ya asasi hizo, Shule za Awali na Msingi 1,156, Sekondari 358, na Vyuo vya Ualimu viwili (2) vilifuatiliwa ili kutathmini utekelezaji wa mapendekezo na ushauri uliotolewa katika tathmini za awali;

imefanya tathmini maalum ya maombi ya usajili katika asasi 698 zikiwemo shule za awali na msingi 492, sekondari 204 na vyuo vya ualimu viwili kwa lengo la kubaini endapo zinakidhi vigezo vya usajili.

Mheshimiwa Spika, Katika kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimumsingi, sekondari na ualimu, Serikali imedahili walimu 1,819 kati ya walimu 2,515 waliolengwa katika ngazi ya Astashahada, Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu kuhusu Uthibiti Ubora wa Shule kupitia Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM).


Usimamizi na Uendelezaji wa Elimu Maalum

Mheshimiwa Spika,
katika kuhakikisha uendelezaji wa elimumsingi na sekondari nchini unafanyika kwa kuzingatia usawa kwa watoto wote, Serikali imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu jumuishi kwa kutekeleza yafuatayo:

imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2021/22 - 2025/26 pamoja na kuzalisha nakala kwa maandishi ya kawaida, maandishi ya breli na maandishi yaliyokuzwa kwa ajili ya wanafunzi wasioona na wenye uoni hafifu kwa lengo la kuelekeza namna ya kutoa elimu bora kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kuanzia ngazi ya Elimu ya Awali hadi Elimu ya Juu;

imetoa mafunzo kazini kwa walimu 1,985 wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa lengo la kuboresha mbinu za kufundishia na kujifunzia. Vilevile, imetoa mafunzo kwa Wathibiti Ubora wa Shule 206 kwa lengo la kuboresha uthibiti ubora wa darasa jumuishi na ufanyaji tathmini ya miundombinu kwa kuzingatia mahitaji ya watoto wenye mahitaji maalum;

imewezesha wanafunzi 91 wenye mahitaji maalum wanaotoka katika kaya zenye kipato duni kwa kuwalipia ada wanafunzi watano; Kuwanunulia vifaa saidizi wanafunzi 50; Kuwalipia BIMA ya afya kwa wanafunzi 28; na Kuwasaidia fedha za kujikimu wanafunzi nane kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanafunzi hao wanapata fursa ya elimu na wanamaliza masomo yao bila changamoto;

imenunua viti mwendo (wheelchairs) 365 na vishikwambi (tablets) 285 kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo na viziwi walioko katika shule za msingi na sekondari kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji;

imewezesha ununuzi wa vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa shule za msingi 654 na sekondari 67;

imenunua na kusambaza vifaa vya kielimu na saidizi 413 vikiwemo bajaji, kompyuta mpakato, vishikwambi, embosser machine na vifaa vya usikivu. Vifaa hivyo ni kwa ajili ya wanafunzi wasioona, viziwi na wenye ulemavu wa viungo katika ngazi ya Elimu ya Juu; na

imeandaa muhtasari na mwongozo wa kufundishia wanafunzi wenye uziwikutoona na kupatiwa ithibati na mamlaka husika. Nyaraka hizo zitatumika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi hao.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha elimu ya michezo na mafunzo ya skauti katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu nchini, kwa kutekeleza yafuatayo:

imetoa mafunzo kwa walimu walezi wa skauti 100 (wanawake 28 na wanaume 72) kutoka shule za msingi katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Manyara, Kigoma, Geita, Mara, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Katavi na Singida. Mafunzo hayo yalihusu namna bora ya uendeshaji wa skauti katika shule za msingi na namna ya kukabiliana na majanga ikiwemo janga la moto; na

imeendesha mashindano ya michezo na sanaa (UMISAVUTA) katika Vyuo vya Ualimu vya Serikali 35 kwa lengo la kuimarisha stadi za michezo vyuoni na kuimarisha afya za wanafunzi katika vyuo hivyo.

Uimarishaji wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi

Mheshimiwa Spika
, Serikali imeendelea kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini Kwa lengo la kuongeza idadi ya wahitimu katika ngazi hiyo. Katika kufikia azma hiyo, yafuatayo yametekelezwa:

imedahili wanafunzi 266,236 (wanawake 132,766 na wanaume 133,470) kati ya lengo la wanafunzi 159,500 waliotarajiwa kudahiliwa katika vyuo vya ufundi nchini kwa mchanganuo ufuatao: Astashahada ya Awali 133,118 (wanawake 66,383 na wanaume 66,735); Astashahada na Stashahada katika fani za Sayansi na Teknolojia Shirikishi wanafunzi 63,832 (wanawake 34,016 na wanaume 29,816); fani ya afya na sayansi shirikishi wanafunzi 50,368 (wanawake 26,119 na wanaume 24,249) na fani ya biashara, utalii na mipango wanafunzi 18,918 (wanawake 6,248 na wanaume 12,670);

imedahili wanafunzi 90,712 (wanawake 31,033 na wanaume 59,679) kati ya lengo la wanafunzi 142,150 katika vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ambapo wanafunzi 428 (wanawake 162 na wanaume 266) ni wenye mahitaji maalum;

imeidhinisha kuanzishwa kwa idara 20 katika vyuo 15 vya ufundi kwa lengo la kuendesha programu za NTA katika bodi za masomo yafuatayo: afya na sayansi shirikishi nane, biashara, utalii na mipango sita na sayansi na teknolojia shirikishi sita;

imedahili wanafunzi 15,037 katika Vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi;

imewezesha vyuo 12 vya maendeleo ya wananchi kujenga ushirikiano wa kitaaluma na vyuo sita vya nchini Canada kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kukuza ujuzi na maarifa;

imeanza ujenzi wa Chuo cha Ufundi Dodoma – DTC chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,500 kinachojengwa katika eneo la Nala. Kukamilika kwa chuo hicho kutaongeza fursa za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini;

imeendelea na ujenzi na ukarabati wa vyuo 14 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs);

imeendelea na ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera ambapo ujenzi huo upo katika hatua za ukamilishaji;

imeendelea na ujenzi wa mabweni mawili, maktaba mbili, nyumba za watumishi kumi, bwalo moja, maabara moja, jengo la utawala moja, kumbi za mihadhara tatu, zahanati moja, hosteli mbili, karakana tatu, kantini moja, chumba cha usanifu kimoja pamoja na kukarabati mtambo mmoja wa kufua umeme kwa kutumia nguvu za maji katika taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi;

inaendelea na ujenzi wa mabweni mawili katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume - Zanzibar yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,536 (wanawake 768 na wanaume 768) ambapo ujenzi umefikia asilimia 30; na

imewezesha ununuzi wa samani na vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Kongwa, Kasulu, Nyasa na Ruangwa.

Mheshimiwa Spika, katika kuwajengea umahiri wahitimu wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Serikali inaendelea na ujenzi wa vituo vya umahiri katika Chuo cha Ufundi Arusha, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji katika Nyanja za Nishati, Usindikaji wa Ngozi, Uchukuzi na TEHAMA.


Mheshimiwa Spika, Katika kuimarisha ubora wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini, Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya utoaji wa elimu na mafunzo kwa kutekeleza yafuatayo:

imetoa namba ya uhakiki wa tuzo (Award Verification Number - AVN) kupitia Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa wahitimu wa vyuo vya ufundi 23,332 kati ya lengo la tuzo 20,000 ili kuepuka udanganyifu wa wahitimu wanaoendelea na Elimu ya Juu na kuvirahisishia vyuo kufanya uhakiki wa Stashahada;

imefanya ulinganifu wa tuzo 143 ili kuthibiti viwango vya elimu ya ufundi nchini;

imeandaa rasimu ya Mfumo wa Tuzo wa Taifa (National Qualifications Framework – NQF ) na Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi
Stadi (The Technical and Vocational Education and Training Development Plan 2021/22 – 2025/26);

imetunga na kuendesha Mitihani ya Taifa ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (CBA na NABE) ambapo jumla ya watahiniwa 34,531 walifanya mitihani hiyo;

imevijengea uwezo vyuo 33 vya ufundi kwa ajili ya kupata usajili kamili ambapo kati ya hivyo, vyuo 17 vilihakikiwa kwa lengo la kuvisajili katika bodi za masomo kama ifuatavyo: afya na sayansi shirikishi vyuo 11, biashara, utalii na mipango vyuo vitano na bodi ya sayansi na teknolojia shirikishi chuo kimoja; na

imefanya ufuatiliaji wa uendeshaji wa vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi kwa lengo la kuhakiki ubora wa mafunzo yanayotolewa ili kubaini endapo vinakidhi viwango vinavyohitajika.


Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kufanya mapitio ya mitaala na miongozo ya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa lengo la kuhakikisha mafunzo yanayotolewa katika ngazi hiyo yanaendana na mipango ya nchi na mahitaji ya soko la ajira. Katika kufikia azma hiyo, Serikali kupitia Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, imetekeleza yafuatayo:

imehakiki mitaala 51 kati ya 150 iliyoandaliwa na vyuo vya elimu ya ufundi kwa lengo la kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanakidhi mahitaji ya soko la ajira;

imeandaa na kuhuisha mitaala 27 ya fani mbalimbali katika sekta tano ambazo ni: umeme (5), magari (8), mitambo (5), kilimo (5) na ukarimu (4). Aidha, mitaala 19 katika fani ya Biashara, Usafirishaji, Ujenzi na Mitambo ya Magari Moshi imeanza kuandaliwa;

imehuisha mihtasari nane kwa ajili ya masomo bebezi na mtambuka ambayo ni Stadi za Maisha, Ujasiriamali, TEHAMA, Sayansi ya Ufundi, Michoro ya Kiufundi, Lugha ya Kiingereza, Lugha ya Kifaransa na Biashara ya Utalii;

imeandaa mwongozo wa mitaala ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na mwongozo wa kuwezesha wanafunzi kusajiliwa kusoma na kubadilishana watumishi katika vyuo vya ATC, NIT na DIT; na

imefanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mitaala na mihtasari iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili katika Vyuo 21 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs).

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini inatolewa kwa vitendo kwa lengo la kukuza na kuendeleza ujuzi na umahiri. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:

imerasimisha ushirikiano na mashirika na taasisi 17 kutoka katika sekta rasmi ili kuwezesha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na walimu. Mashirika hayo ni; Shirika la Umeme Tanzania, Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), TPM (1998) Ltd Morogoro, TOYOTA, Bakhresa Co. Ltd, Kilombero Sugar Co, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mamlaka ya Elimu Tanzania, Tume ya Sayansi na Teknolojia, Benki ya Azania, SIDO, SFD, NSSF, NEEC, JUVE na COMPASSION;

imewezesha wafanyakazi 15 na wanafunzi 2,222 kwenda viwandani kwa ajili ya kupata mafunzo na kuongeza ujuzi na stadi zinazohitajika;

imewezesha na kugharamia mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi 7,605 wa fani mbalimbali; na imetoa mafunzo ya namna ya upimaji na ufundishaji wa mitaala inayozingatia umahiri kwa Wakufunzi 653 kati ya 1,000 waliolengwa ambapo Wakufunzi hao walitoka katika Vyuo 37 vya Elimu ya Ufundi.


Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha utendaji kwa kujengea uwezo rasilimaliwatu katika taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini, kwa lengo la kuwezesha usimamizi wa utoaji wa elimu, kwa kutekeleza yafuatayo:

imewezesha watumishi 31 kuhudhuria masomo katika ngazi za Stashahada, Shahada ya Kwanza na Umahiri. Vilevile imetoa mafunzo kwa watumishi 1,177 (wanawake 591, wanaume 586) kulingana na maeneo ya ubobezi kwa lengo la kuimarisha utendaji;

imetoa mafunzo ya uongozi na maadili kwa viongozi 17 wa sekta ya umma na binafsi na wanafunzi wahitimu wapya 2,118 kupitia Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere;

imetoa mafunzo kuhusu uandishi wa maandiko ya tafiti kwa Wahadhiri 30 wenye Shahada ya Uzamivu;

imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi 2,400 kutoka Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi;

imetoa mafunzo kuhusu programu ya Elimu Haina Mwisho katika vyuo 13 vya Maendeleo ya Wananchi kwa lengo la kuanzisha programu hiyo katika vyuo husika; na imewezesha mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa watumishi 25 kutoka katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na watumishi 93 kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Mheshimiwa Spika, katika kuzijengea taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini uwezo wa kuandaa na kufanya tafiti zenye tija, Serikali imetekeleza yafuatayo:

imewezesha kufanyika kwa tafiti 20 ukilinganisha na tafiti 14 zilizolengwa kufanyika kwa lengo la kutoa maarifa na kutatua changamoto mbalimbali za kijamii;

imewezesha kukamilishwa kwa taarifa za tafiti za Soko la Ajira katika sekta za umeme, vipodozi, madini na uchapishaji kwa ajili ya mapitio ya mitaala itakayoboresha elimu na mafunzo ya ufundi stadi; na


imeandaa mapendekezo ya tafiti na ukusanyaji wa taarifa za soko la ajira katika sekta za Biashara, Usafirishaji, Ujenzi na Mitambo na Magari Moshi.

Usimamizi na uendelezaji wa Elimu ya Juu

Mheshimiwa Spika,
katika kuhakikisha Elimu ya Juu inayotolewa nchini inaendana na mipango ya nchi, soko la ajira la Kikanda na Kimataifa, Serikali imetekeleza yafuatayo:

imefanya tathmini ya Mitaala 72 iliyowasilishwa na Vyuo vikuu nchini na kutoa ithibati kwa mitaala 31. Aidha, mitaala 41 iko katika hatua mbalimbali za kupatiwa ithibati;

imeandaa programu saba za masomo kati ya 15 ambazo ni: Stashahada katika Menejimenti ya Serikali za Mitaa; Shahada ya Kwanza ya Utawala wa Umma katika Maendeleo na Uongozi wa Vijana; Shahada ya Kwanza katika Ufuatiliaji na Tathmini; Shahada ya Umahiri katika Maadili na Uongozi; Shahada ya Umahiri katika Ukaguzi; Shahada ya Umahiri katika Fedha za Maendeleo; na Shahada ya Uzamivu katika Utawala wa Umma kwa ajili ya kuimarisha umahiri, ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi;

imehuisha programu mbili za mafunzo ili ziendane na uhitaji wa soko la ajira na kuandaa programu mpya mbili kwa lengo la kuongeza wigo wa mafunzo na fursa ya elimu kwa watanzania;

imeanzisha programu mbili za shahada ya umahiri (Umahiri wa Sayansi katika Kemia ya Viwanda na Umahiri wa Sanaa katika Tathmini ya Maendeleo) kupitia Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam. Programu hizo zitaongeza wataalam watakaochochea maendeleo ya sayansi na teknolojia; na imeanzisha programu mpya moja ya Masters of Science in Urban Governance and Environmental Studies – URGES kati ya tano zilizotarajiwa kuanzishwa katika Chuo Kikuu Ardhi. Uanzishwaji umezingatia uhitaji wa soko la ajira na ukuaji wa uchumi wa Tanzania, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Dunia kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia uzingatiaji wa sheria, kanuni, miongozo na taratibu katika usimamizi na uendelezaji wa Elimu ya Juu nchini kwa kutekeleza yafuatayo:


imekagua na kutambua taasisi saba za nje zilizowasilisha maombi ya kuanza kupeleka wanafunzi vyuo vya nje ya nchi (Overseas Students Recruitment Agencies - OSRA) kwa lengo la kuzisajili. Vilevile, imefanya ufuatiliaji katika Taasisi 14 zinazopeleka wanafunzi kusoma nje ya nchi kwa lengo la kuhakiki utekelezaji wa miongozo iliyowekwa;

imefanya ukaguzi katika Vyuo Vikuu 30 kwa lengo la kuhakiki ubora wa vyuo hivyo katika utoaji wa Elimu ya Juu; na

imetathmini na kutambua tuzo 2,111 kati ya 2,531 zilizowasilishwa ambazo zilitolewa na Vyuo vya Elimu ya Juu nje ya Nchi. Aidha, maombi 420 yalirudishwa kwa waombaji ili kufanyia kazi mapungufu yaliyobainika.


Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Vyuo Vikuu nchini kwa kutekeleza yafuatayo:

imeratibu maombi ya wanafunzi 112,228 kati ya maombi 120,000 yaliyolengwa kwa wanafunzi kujiunga na Shahada ya Kwanza katika Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu 74 nchini. Kati ya maombi hayo, jumla ya waombaji 100,620 wamedahiliwa katika Vyuo Vikuu mbalimbali. Vilevile, imeratibu udahili wa waombaji 24,839 wa ngazi ya Astashahada na Stashahada katika Vyuo Vikuu ambapo jumla ya waombaji 23,110 walidahiliwa katika kozi mbalimbali;

imeratibu ufadhili wa masomo unaotolewa na nchi rafiki kwa wanafunzi wa kitanzania 111 (Shahada ya kwanza 9, Uzamili 74, na Uzamivu 28) kama ifuatavyo: Uingereza (12), Hungaria (23), China (72), na Mauritius (4);

imewezesha mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wahadhiri na watumishi 4,664 (muda mfupi 3,782 na muda mrefu 882) kutoka katika taasisi za Elimu ya Juu;

imeanza ukarabati wa kituo shikizi cha kufundishia na kujifunzia katika kituo cha Bagamoyo (Satellite Teaching Facilities) kupitia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili – MUHAS kwa lengo la kuongeza fursa za elimu ya afya na sayansi shirikishi;

imeendelea na upanuzi wa Hosteli ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa ghorofa mbili (2) zaidi zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,280 ambapo hatua ya usanifu imekamilika. Kwa sasa hostel hiyo ina uwezo wa

kuchukua wanafunzi 3,840 na kukamilika kwa upanuzi huo kutawezesha kuchukua jumla ya wanafunzi 5,120;

imejenga vituo vitano vya Mikoa vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika Mkoa wa Geita, Kigoma, Simiyu, Lindi na Manyara. Aidha, inaendelea na ukarabati wa Kampasi ya Zanzibar ambapo utekelezaji umefikia asilimia 90;

imeendelea na ujenzi wa jengo la utawala ambalo litaongeza ofisi 50 kwa ajili ya wafanyakazi na ofisi za utafiti katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam. Aidha, imeanza ujenzi wa maabara nne na vyumba vya madarasa kwa shule ya sekondari ya mazoezi yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 920 ambapo ujenzi umefikia asilimia 12;

imeanza ujenzi wa Jengo la Shule Kuu ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Kampasi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo ujenzi umefikia asilimia 15. Aidha, imeendelea na ukamilishaji wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Kituo cha Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa lengo la kutoa huduma mbalimbali kwa wanafunzi ambapo ujenzi umefikia asilimia 97;

imejenga nyumba 30 za wafanyakazi katika Chuo Kikuu cha Dodoma kati ya nyumba 33 zilizopangwa kujengwa ambapo kati ya hizo nyumba 13 zimekamilika na nyumba 17 zipo katika hatua za ukamilishaji. Aidha, imekarabati mabweni sita, madarasa manne (4), ukumbi wa Chimwaga na majengo 34 ya taaluma na utawala;

imeendelea na upanuzi wa maabara ya Baiolojia katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 75; na

imeweka samani katika hosteli nne (4) zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,024 zilizopo Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe kwa lengo la kuongeza nafasi za malazi.

Mheshimiwa Spika, Serikali katika kuongeza fursa na kuimarisha mafunzo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, imejenga jengo la maabara mtambuka lenye maabara nane na madarasa nane lenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 3,200 kwa wakati mmoja ambapo ujenzi huo umefikia asilimia 98. Vilevile, imeendelea na ujenzi na ukarabati wa madarasa, mabweni ya wanafunzi na viwanja vya michezo katika Kampasi ya Mizengo Pinda - Katavi. Aidha, imenunua vifaa vya kisasa vya maabara, mahema pamoja na kufungua shule ya udereva wa mitambo ya kilimo kwa lengo la kuimarisha mafunzo kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika,
katika kuhakikisha kuwa umma unapata taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi za Elimu ya Juu nchini, Serikali imeendelea kutekeleza yafuatayo:

imefanya maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ambapo jumla ya taasisi 74 za ndani ya nchi zilishiriki na wadau 55,000 walihudhuria. Maonesho hayo yalitoa fursa kwa wananchi kufahamu kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi za Vyuo Vikuu;

imeendelea kutoa elimu ya ushirika kupitia redio mbalimbali ambapo vipindi 23 vilirushwa kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na vipindi 11 kupitia redio za kijamii zilizopo mkoani Kilimanjaro. Elimu iliyotolewa ilihusu ushirika na viwanda, mikakati ya kufufua ushirika, kubaini sababu za kudorora kwa vyama vya ushirika na uendeshaji wa vyama vya ushirika wa kahawa na maziwa; na

imeratibu kongamano la kitaalam la kukuza taaluma ya usimamizi wa ardhi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ‘Pursuing Knowledge Frontiers on Land Management and Climate Change Adaptation’ kupitia mradi wa Sida unaofadhiliwa na Serikali ya Sweden. Matokeo ya tafiti kuhusu ufumbuzi wa masuala mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na mazingira, ardhi, makazi ya watu, maafa, maendeleo ya miji na vijiji, ujenzi na miundombinu yaliwasilishwa na kujadiliwa na wadau.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na mataifa mengine katika uendelezaji wa Elimu ya Juu nchini, kwa lengo la kuhakikisha wataalamu wetu wanapata uzoefu na ujuzi wenye kuendana na mahitaji ya Kikanda na Kimataifa. Azma hii imefanyika kwa kutekeleza yafuatayo:

imehuisha Hati za Makubaliano baina ya Tanzania na nchi rafiki ambazo ni: Msumbiji, Algeria, Morocco, Zimbabwe, Poland, Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Jumuiya ya Madola kwa lengo la kuongeza fursa za Elimu ya Juu;

imewezesha kusainiwa kwa hati mbili za makubaliano baina ya Tanzania na Misri, na Tanzania na Kenya zinazolenga kuimarisha na kuendeleza elimu, sayansi na teknolojia;

imeratibu mikutano ya wadau ya kubadilishana uzoefu na kuandaa miongozo linganifu minne katika programu za Shahada ya Kwanza ya Udaktari na Shahada ya Kwanza ya Uuguzi. Aidha, inaendelea na ukamilishaji wa miongozo linganifu miwili katika programu za Shahada za Huduma, Ukarimu na Utalii na TEHAMA; na

imeshiriki vikao vya ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa vya IUCEA, SADC, EAC na UNESCO kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kukuza ubora na maendeleo ya Elimu ya Juu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuongeza fursa za Elimu ya Juu kwa kuboresha huduma za upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini. Lengo la uboreshaji wa huduma ya mikopo ni kuwezesha wanafunzi wenye sifa na uhitaji kuendelea na Elimu ya Juu bila vikwazo. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:

imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 569 kati ya Shilingi bilioni 570 zilizopangwa kutolewa kwa wanafunzi 148,581. Fedha hizo zimetolewa kwa wanafunzi 177,777 kati yao wanafunzi 69,333 ni wa mwaka wa kwanza na wanafunzi 108,444 wanaoendelea na masomo. Kipaumbele cha utoaji wa mikopo kimezingatia waombaji wenye uhitaji mkubwa hasa wale wenye ulemavu, yatima na wanaotoka katika kaya maskini zikiwemo zilizopo chini ya mpango wa TASAF;

imekusanya Shilingi 156,806,093,384.02 sawa na asilimia 78 ya lengo la Shilingi 201,319,005,000.00 zilizokadiriwa kukusanywa kutokana na mikopo iliyoiva. Makusanyo hayo yamechangiwa na mikakati iliyowekwa ya kuelimisha jamii, kuwabaini wanufaika wapya 17,977, utoaji wa ankara za mikopo mipya zipatazo 8,848; ukaguzi wa uzingatiaji wa sheria kwa waajiri wapatao 1,521; na uelimishaji jamii katika urejeshaji wa mikopo;

imefanya maboresho katika mifumo ifuatayo: Mfumo wa Usimamizi wa Mikopo - Integrated Loan Management Systems (iLMS), Mfumo wa Ulipaji wa Mikopo - Digital Disbursement System (DIDiS), Mfumo wa Urejeshaji Mikopo - Individuals and Employers Repayment Portals, na Mfumo wa Usimamizi Fedha - VoteBook Financial Management System (VFMS). Maboresho ya mifumo hiyo yamepunguza muda wa kuomba mikopo na kurahisisha uhakiki, uchambuzi wa maombi ya mikopo na utoaji wa taarifa;

imekamilisha uunganishaji wa Mfumo wa Mikopo (ILMS) na Mfumo wa Mishahara wa Serikali (HCMIS). Uunganishaji huu umewezesha ulinganifu wa deni la mnufaika katika kanzidata ya Bodi ya Mikopo na kanzidata ya mishahara;

imekamilisha tathmini ya awali ya namna bora ya usimamizi wa ugharimiaji wa wanafunzi wenye ufaulu wa juu na wale wanaopata ufadhili wa nje ya nchi;

imekamilisha mapitio ya tathmini ya awali kuhusu vigezo na mahitaji ya kuongeza wigo wa mikopo kwa ngazi ya Stashahada hususan za taaluma za ujuzi wa kuajirika na kujiajiri zinazoweza kuchochea tija katika uzalishaji na mserereko wa kuelekea katika uchumi wa kati;

imeboresha mwongozo wa kutoa mikopo kupitia maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wadau. Aidha, maandalizi ya mapitio na utafiti wa kina kwa lengo la kuboresha na kuhuisha viashiria na vigezo vya utambuzi wa uhitaji na urejeshaji wa mikopo yamekamilika;

imefanya mapitio ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi kwa miaka minne iliyopita na kufanya upembuzi wa hali ilivyo sasa kwa lengo la kukamilisha Mpango Mkakati wa Tano wa Bodi ya Mikopo kwa mwaka 2022/23 – 2026/27; na

imeanzisha ofisi mpya Dar es Salaam kwa lengo kuhudumia kanda ya Mashariki. Hivyo kuongeza jumla ya ofisi za kiutendaji kuwa saba ambazo ni; ofisi ya Zanzibar, ofisi ya Dodoma na ofisi za Kanda ya Mbeya, Arusha, Mtwara, Mwanza na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utoaji wa elimu na mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini, Serikali imeendelea kutekeleza yafuatayo:

imewezesha upanuzi wa maabara ya viumbehai katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa ambapo ujenzi umefikia asilimia 80. Kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa vitendo;

imeanza ujenzi wa maabara kuu ya kemia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambayo itatumika kwa ajili ya utafiti na kutoa huduma za kupima sampuli za viwandani na hivyo kuongeza wigo wa wanafunzi kujifunza kwa vitendo;

imeanza hatua za awali za ujenzi wa miundombinu ya Kituo cha Utafiti wa Viumbe Maji Baridi yaani Multi-Disciplinary Freshwater Research Centre - Chato, Mkoani Geita kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;

imeboresha na kuendeleza Shamba la Mafunzo kwa kupanda miche 500 ya michikichi, malisho ya ng’ombe, kuweka uzio, kufunga mfumo wa umwagiliaji wa matone, ukarabati wa mabwawa matano ya samaki na mabwawa 12 madogo kwa ajili ya vifaranga vya Samaki katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo;

imejenga maabara katika ndaki ya sayansi asilia na hisabati ya Chuo Kikuu Dodoma; na

imekamilisha ujenzi wa kituo cha Umahiri cha Afrika Mashariki cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Kampasi ya Mloganzila kilichozinduliwa rasmi Desemba, 2021 na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Kituo hicho kitaongeza mafunzo na huduma za kibingwa katika matibabu ya moyo na mishipa ya damu.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia taasisi za Elimu ya Juu imeendelea kutoa huduma za ushauri wa kitaalam katika kazi za ujenzi na ukarabati wa majengo mbalimbali kama ifuatavyo:

imetoa ushauri wa kitaalam kuhusu ujenzi wa nyumba za Bunge eneo la Kilimani - Dodoma; majengo ya Mchapishaji Mkuu wa Serikali, Kituo cha Taifa cha Kukabiliana na Maafa – Dodoma; majengo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati;

imetoa ushauri wa kitaalam kuhusu ukarabati wa majengo ya Balozi za Tanzania katika nchi za DRC, Rwanda, Oman, Saudi Arabia, Msumbiji, Malawi, Burundi na Marekani, pamoja na Chuo cha Ualimu Ndala – Tabora na Chuo

cha Ualimu Mpwapwa – Dodoma; na

imetoa ushauri wa kitaalamu kuhusu uimara wa udongo, kokoto na lami zinazotumika katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali na kupima ubora wa maji, usanifu wa miradi ya maji na ujenzi.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha miradi ya ujenzi na ukarabati inafanyika kwa ufanisi kwa kutumia wataalam wa ndani, Serikali kupitia taasisi za Elimu ya Juu imeendelea kutoa huduma za ushauri wa kitaalam kuhusu usanifu na usimamizi kama ifuatavyo:

usanifu na usimamizi wa kampasi ya Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Julius K. Nyerere – Butiama;

usanifu na usimamizi wa vituo vya michezo katika miji ya Dodoma, Geita na Dar es Salaam, Kituo cha mafunzo ya michezo ‘Centre of Excellence and Academy’ katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya pamoja na kituo cha taarifa za afya ‘Health Promotion Centre’ – Singida;

usanifu na usimamizi wa mradi wa ujenzi katika vyuo vinne vya VETA ambavyo ni Kasulu, Ruangwa, Kongwa na Nyasa, Vyuo 20 vya Maendeleo ya Wananchi (FDC), Vyuo vya Ualimu 14 na stendi kuu ya mabasi ya Kahumo -Wilayani Chato - Geita;

usanifu na usimamizi wa miradi ya ujenzi katika vyuo vitano (5) vya VETA pamoja na jengo la madarasa la Chuo cha Ufundi Arusha; na

usanifu na usimamizi wa ujenzi wa nyumba za watu binafsi pamoja na upimaji wa udongo kwa makampuni ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha na kuhamasisha matumizi ya TEHAMA katika taasisi za Elimu ya Juu nchini kwa kutekeleza yafuatayo:

imenunua Backup Software katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam na kitunzia taarifa (data storage) katika mkongo wa Taifa na kuongeza uwezo wa mtandao kutoka 50 Mbps hadi 60 Mbps. Aidha, imetoa mafunzo kwa wanafunzi 1,391 wa mwaka wa kwanza kuhusu ulinzi wa kimtandao;

imeboresha kiungo cha chelezo cha mtandao “internet backup link” hadi kufikia 100 Mbps katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili;

imeweka mfumo wa wireless katika Maktaba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa mtandao kwa watumiaji. Aidha, imeendelea na uboreshaji wa miundombinu ya elimu kwa njia ya kielektroniki kwa kuongeza viunganisho vya “fibre optic” kutoka maeneo ya Kampasi ya Muhimbili; na

imeendelea kuboresha Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Vyuo Vikuu (University Management Information System - UMIS) unaotumika katika ukusanyaji na utoaji wa takwimu na taarifa mbalimbali katika taasisi za Elimu ya Juu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuzingatia masuala mtambuka ikiwa ni pamoja na HIV/UKIMWI, Rushwa

na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza katika utoaji wa elimu kwa ngazi zote za elimu nchini kwa kutekeleza yafuatayo:

imetoa mafunzo kwa Walimu 3,800 wa shule za Msingi na Sekondari kuhusu stadi za maisha zinazozingatia afya ya uzazi, jinsia, na VVU na UKIMWI kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kufundisha wanafunzi stadi za maisha;

imetoa mafunzo kwa Wanachuo 1,819 wanaosoma usimamizi na uongozi wa elimu kuhusu stadi za maisha zinazozingatia afya ya uzazi, jinsia, VVU na UKIMWI, masuala ya rushwa na namna ya kupambana na rushwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kufundisha wanafunzi stadi za maisha;

imetoa mafunzo kwa washiriki 4,174 (wafanyakazi 405 na wanafunzi 3,769) katika taasisi za Elimu ya Juu kuhusu Rushwa, Unyanyasaji wa Kijinsia, VVU na UKIMWI pamoja na huduma ya ushauri nasaha;

imeandaa moduli nne za kufundishia elimu ya stadi za maisha zinazozingatia afya ya uzazi, elimu ya jinsia, VVU na UKIMWI ambapo moduli hizo zitatumika kuendesha mafunzo kwa walimu kazini; na

imetoa elimu ya VVU na UKIMWI, rushwa na majanga mbalimbali kwa Watumishi 123. Pia, wateja waliohudhuria mafunzo walipata huduma ya ushauri nasaha na uelewa wa masuala ya rushwa na namna ya kupambana na rushwa.

Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya Uviko 19

Mheshimiwa Spika,
Serikali katika kupambana na athari za ugonjwa wa UVIKO 19 kupitia sekta ya elimu iliidhinisha afua tatu muhimu za kukabiliana na athari hizo kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO – 19. Katika utekelezaji wa mpango huo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitekeleza maeneo matatu ambayo ni; Kuboresha utoaji wa elimu maalum, Kuongeza fursa na ubora wa Elimu ya Ualimu, na Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi. Kazi zilizofanyika ni kama ifuatavyo:

Afua za Elimu Maalum

imeandika na kuchapa nakala 57,756 za vitabu vya Kiada, Kidato cha 1 - 4 vya maandishi yaliyokuzwa kwa masomo ya Biology, Physics, Chemistry, Mathematics, Agriculture, Home Economics, Kiswahili, Civics, Information and Computer Studies, Geography, History na English. Aidha, imeandika, kuchapa na kusambaza vitabu vya nuktanundu nakala 9,178 kwa masomo hayo ya sekondari kwa ajili ya wanafunzi 353 wasioona. Vitabu hivyo vimeimarisha ujifunzaji na ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum;

imewezesha ununuzi wa vifaa vya wanafunzi wa Elimu ya Juu wenye mahitaji maalumu katika Vyuo Vikuu 11 vya Umma kwa lengo la kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji;

Afua za Elimu ya Ualimu

imewezesha ujenzi wa madarasa 41, kumbi za mihadhara tatu na mabweni 15 katika Vyuo vya Ualimu 23 vilivyonufaika na mpango huo. Ujenzi wa miundombinu hiyo utasaidia katika kupunguza msongamano wa wanafunzi na hivyo kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia;

Afua za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi

inaendelea kuwezesha ujenzi wa vyuo vipya vya ufundi stadi vya Mikoa vinne na ununuzi wa samani katika Vyuo vya Wilaya 25 vya VETA. Aidha, inaendelea na ununuzi na usambazaji wa vifaa na mashine za kufundishia katika vyuo 34 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs). Utekelezaji wa afua hizo unalenga katika kuongeza fursa na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Ununuzi na usambazaji wa vifaa na mashine za kufundishia katika Vyuo 34 vya Maendeleo ya Wananchi utekelezaji umefikia asilimia 30;

inaendelea na ujenzi wa jengo la maabara, madarasa na ofisi katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kwa lengo la kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji kwa vitendo pamoja na kuimarisha mazingira ya watumishi kufanyia kazi; na

inaendelea na ujenzi wa mabweni mawili katika chuo cha Ualimu wa Ufundi Morogoro kwa lengo la kuongeza fursa katika uandaaji wa walimu wa ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Usimamizi na uendelezaji wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu

Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa watumishi kusimamia, kuratibu na kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini kwa kutekeleza yafuatayo:

imetoa mafunzo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka katika Halmashauri 184 za Tanzania Bara kwa lengo la kuboresha uratibu wa masuala ya teknolojia na ubunifu hususan katika kuibua, kutambua na kuwaendeleza wavumbuzi na wabunifu wachanga nchini;

imewajengea uwezo watumishi 182 kati ya 300 waliolengwa katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam ili kuongeza viwango vya ubora katika ufundishaji na utawala kama sehemu ya maandalizi ya kupata ithibati ya viwango vya ubora vya kimataifa (International Organization for Standardization - ISO Certification);

imewezesha jumla ya watumishi 170 wa taasisi zinazohusika na uendelezaji wa sayansi, teknolojia na ubunifu nchini kuhudhuria masomo ya muda mfupi na muda mrefu katika kozi mbalimbali ambapo kati yao watumishi 31 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi na watumishi 139 mafunzo ya muda mrefu (Shahada ya Uzamivu 83, Shahada ya Uzamili 40, Shahada ya Kwanza 12 na Astashahada wanne); na

imetoa mafunzo kwa wabunifu 82 waliopatikana kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) katika utafutaji wa masoko, taratibu za usajili wa hatimiliki, ujasiriamali pamoja na kuandaa

michanganuo ya biashara ili ubunifu uwe fursa ya ajira na kipato kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa kazi za bunifu na matokeo ya tafiti yanatambuliwa Kitaifa na Kimataifa na kuendelezwa kwa lengo la kuongeza kasi ya matumizi yake katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi, Serikali imetekeleza yafuatayo:

imewezesha bunifu 26 kuingia sokoni kati ya bunifu 200 zinazoendelezwa na Serikali ambazo zilipatikana katika Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu mwaka 2019 hadi 2021. Bunifu hizo zitaleta tija ya uzalishaji na huduma katika sekta ya Kilimo, Maji, Nishati, Madini, Afya, TEHAMA na Elimu;

imewaunganisha wabunifu sita na Makampuni ya Kibiashara kupitia Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia ili waweze kupata mbinu na uzoefu wa namna ya kuanzisha na kuendesha biashara na makampuni; na

imetambua teknolojia mpya 90 zilizozalishwa nchini na hivyo kufanya jumla ya teknolojia zilizotambuliwa hadi sasa kufikia 479 kwa lengo la kuwa na kanzidata ya kitaifa itakayorahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu kuhusu teknolojia na bunifu nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika taasisi zinazosimamia maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:

imeanzisha vitalu nyumba (screen houses) vinne katika Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia vyenye ukubwa wa mita za mraba 4,900 kwa ajili ya tafiti za kilimo, kutoa mafunzo kwa vitendo, kufanya majaribio ya teknolojia zilizobuniwa na watafiti pamoja na kuzalisha mazao mbalimbali;

imeendelea na ujenzi wa madarasa matano yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 50 kila moja na mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 160 katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam Kampasi ya Myunga ambapo ujenzi umefikia hatua ya umaliziaji. Aidha, imeweka samani katika jengo la kufundishia la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam Kampasi Kuu; na

imeendelea na ujenzi wa miundombinu katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kama ifuatavyo: maktaba yenye uwezo wa kuchukua watumiaji 2,500 kwa wakati mmoja; mabweni ya wanafunzi yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 800; na maabara za kufundishia zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 600. Ujenzi wa majengo hayo upo katika hatua mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa sayansi, teknolojia na ubunifu nchini, kwa kutekeleza yafuatayo:

imesimamia utekelezaji wa mradi wa vituo vinne vya umahiri “African Centres of Excellence (ACE - II)” katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia. Lengo la kuanzishwa kwa vituo hivyo ni kujenga uwezo katika utoaji wa Elimu ya Juu na utafiti katika maeneo ya Afya na Biolojia ya Molekuli; Kilimo; Maji na Nishati Jadidifu;

imewezesha kuanzishwa kwa kumbi za ubunifu 10 katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vya: Chisalu - Dodoma, Kisangwa - Mara, Sengerema - Mwanza, Kasulu - Kigoma, Katumba - Mbeya, Kilwa Masoko - Lindi, Mto wa Mbu - Arusha, Newala - Mtwara, Kiwanda – Tanga, na Njombe. Lengo la kuanzishwa kwa kumbi hizo ni kuimarisha mfumo wa uendelezaji wa wabunifu;

imeratibu ushiriki wa nchi katika Mkutano Mkuu wa 65 wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) uliofanyika Vienna, Austria mwaka 2021 ambapo Mtafiti Mtanzania (Ndugu Salum Faki Hamad) kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI) alipata tuzo ya uzalishaji wa mbegu bora ya mpunga inayostahimili chumvi na magonjwa;

imeimarisha uhusiano kati ya wadau wa kimataifa, kikanda na kitaifa katika masuala ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ambapo wadau wa kimataifa wameongezeka kutoka washirika 39 hadi 44, kanda ya Afrika Mashariki wameongezeka kutoka 42 hadi 46 na ndani ya nchi kutoka 23 hadi 29. Ushirikiano huo umekuza ujuzi na maarifa katika tafiti mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto za jamii na kiuchumi;

imeshirikiana na mradi wa South African Innovation Support (SAIS) ili kuendeleza kazi za ubunifu nchini ambapo ushirikiano huo umeziwezesha kampuni changa mbili za Fundi App na Exam Net kushiriki katika mashindano yanayojulikana kama Slush 2021 yaliyofanyika Helsinki ‑ Finland. Kupitia mashindano hayo, mshiriki mmoja (Ndugu Godfrey Gervas Kilimwomeshi) kutoka Tanzania aliibuka mshindi wa jumla na kupata zawadi ya vocha yenye thamani ya EURO 3,000; na

imefanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi 10 ya utafiti inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki - IAEA kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania katika Sekta ya Maji, Afya, Kilimo na Mifugo na kubaini kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unafanyika kulingana na makubaliano.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu uendelezaji wa sayansi, teknolojia na ubunifu nchini kwa kutekeleza yafuatayo:

imezalisha na kusambaza taarifa za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu zinazohusiana na uhawilishaji na uendelezaji wa Teknolojia kupitia mabango, vijarida viwili, vipeperushi vinne, factsheet moja na bulletin moja. Taarifa hizo zipo katika Lugha ya Kiingereza na Kiswahili; na

imezalisha na kusambaza infographics na taarifa za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya habari kwa mchanganuo ufuatao: Infographics 489; taarifa nne za utafiti, moja ya ubunifu na makala fupi 47.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia imeendelea kuimarisha na kuhimiza matumizi ya TEHAMA katika taasisi zinazosimamia uendelezaji wa sayansi, teknolojia na ubunifu nchini kwa kutekeleza yafuatayo:

imeboresha na kuimarisha miundombinu na mfumo wa TEHAMA wa Menejimenti ya Utafiti na Ubunifu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kuchakata maombi ya vibali vya utafiti, ufadhili wa miradi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za watafiti na wabunifu; na

imeandaa vipaumbele vya utafiti nchini kwa lengo la kutoa mwelekeo wa shughuli za utafiti kulingana na Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki imeendelea kuongeza miundombinu na kuhakiki vifaa vya mionzi kwa lengo la kudhibiti athari zitokanazo na mionzi ya nyuklia isiyo salama katika jamii na mazingira kwa ujumla kwa kutekeleza yafuatayo:

imeendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa maabara changamano itakayoboresha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika kudhibiti matumizi salama ya mionzi na kuendeleza teknolojia ya nyuklia ambapo ujenzi umefikia asilimia 95;

imeendelea na ujenzi wa maabara na ofisi katika Kanda ya Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza. Kukamilika kwa ujenzi huo kutasogeza huduma za matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kwa wananchi na wafanyabiashara ambapo ujenzi upo katika hatua mbalimbali;

imefanya matengenezo na kuhakiki vifaa na mitambo 40 inayotumia teknolojia ya nyuklia ili kuimarisha ubora wa vifaa, usalama wa wafanyakazi na jamii inayowazunguka; na

imefanya matengenezo na kuhakiki vifaa 40 vya nyuklia kwa matumizi ya ujenzi na viwandani (nuclear gauges and industrial), na mashine za kupima magonjwa (medical x-rays equipment).

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki imeendelea kuimarisha usimamizi, udhibiti na matumizi ya mionzi ya nyuklia nchini kwa kutekeleza yafuatayo:

imesajili vituo vipya 44 vinavyotumia vyanzo vya mionzi nchini kwa lengo la kuimarisha matumizi salama ya mionzi;

imepokea na kutathmini maombi 514 ya umiliki, utumiaji na usafirishaji wa vyanzo vya mionzi kati ya lengo la kupokea vibali 600;

imesajili wataalam 109 wa kutoa huduma za mionzi kwa wagonjwa ili kudhibiti matumizi salama ya mionzi; na

imetoa leseni 375 za kumiliki na kutumia vyanzo vya mionzi ikilinganishwa na leseni 333 zilizotolewa katika mwaka wa fedha 2020/21. Leseni hizo zimetolewa kwa mchanganuo ufuatao:

kumiliki na kutumia vyanzo vya mionzi (329);

uingizaji wa vyanzo vya mionzi nchini (36);

kusafirisha vyanzo vya mionzi nje ya nchi (1);

usafirishaji wa vyanzo vya mionzi ndani ya nchi (7);

uchunguzi wa madini ya urani (1); na

upembuzi na ujenzi wa mgodi wa madini ya Urani (1).

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki imeendelea kuimarisha usalama wa jamii ikiwemo kulinda afya za wafanyakazi wanaotumia teknolojia ya nyuklia kwa kutekeleza yafuatayo:

imekusanya mabaki ya vyanzo vya mionzi kutoka katika vituo vinne ambavyo ni: TANROADS – Kagera (1); Geita Gold Mine (1); na Estim Construction Company Dar es Salaam (2) na kuyahifadhi mabaki hayo katika kituo maalum cha kuhifadhi mabaki ya vyanzo vya mionzi. Jumla ya mabaki ya vyanzo vya mionzi 149 yameendelea kuhifadhiwa katika Jengo la Kuhifadhi Mabaki ya Vyanzo vya Mionzi (CRWMF);

imekagua vituo 14 vinavyomiliki na kutumia vyanzo vya mionzi kwa ajili ya kudhibiti hali ya usalama kwa wagonjwa, wafanyakazi na jamii;

imepima viwango vya mionzi kwa wafanyakazi 2,065 wanaofanya kazi katika vyanzo vya mionzi kati ya wafanyakazi 1,920 waliolengwa ambapo ilibainika kuwa viwango vya mionzi vilivyopo vinakubalika kisheria. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 107 ya wafanyakazi waliosajiliwa katika sekta ya mionzi nchini;

imepima sampuli 31,371 za vyakula, mbolea, na bidhaa za tumbaku ambapo kati ya hizo vyakula kutoka nje ya nchi 9,732, vyakula vinavyosafirishwa nje ya nchi 17,864, mbolea 924, na tumbaku na bidhaa nyingine 2,851; na

imepokea na kuchanganua sampuli 510 za mazingira ili kutambua viasili vya mionzi na kuwalinda wananchi na mazingira kwa ujumla.

Kuimarisha na Kuendeleza Tafiti na Matumizi ya Matokeo yake katika Ajenda ya Maendeleo

Mheshimiwa Spika
, utafiti ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo, kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi pamoja na kuibua maarifa mapya. Serikali kupitia taasisi za elimu, mafunzo, sayansi na teknolojia imeendelea kuimarisha na kuendeleza tafiti na matumizi ya matokeo yake katika kuleta maendeleo na kuboresha ustawi wa jamii. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imewezesha kufanyika kwa tafiti mbalimbali kama ifuatavyo:

imefanya jumla ya tafiti 143 ukilinganisha na lengo la tafiti 129 zilizolengwa kufanyika katika taasisi za Elimu ya Juu kwa kushirikiana na wadau ndani na nje ya nchi. Tafiti hizo zipo katika maeneo ya elimu, mazingira, kilimo, afya, madawa, jinsia, afya za wanyama, samaki, utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na mimea ya asili, kilimo endelevu cha mazao mbalimbali, mabadiliko ya tabianchi, misitu na rasilimalimaji. Aidha, imeandaa mapendekezo 39 ya maeneo ya kufanyia tafiti (research area) katika maeneo ya vipaumbele vya Taifa;

imeendelea kugharimia tafiti na mafunzo katika Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia kupitia miradi 24 ya utafiti kwa lengo la kuzalisha wataalam na teknolojia za kisasa katika maeneo ya Kilimo, TEHAMA, Chakula na Lishe; na

imeendelea kugharimia miradi 32 ya utafiti, ubunifu na miundombinu ya utafiti (tafiti 13, bunifu 16 na miundombinu 3) inayoratibiwa kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Matokeo ya miradi hiyo yatasaidia kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa tafiti na maandiko ya kitaaluma yanatunzwa kwa rejea na matumizi kwa utatuzi wa changamoto mbalimbali za kijamii, Serikali imeendelea kutekeleza yafuatayo:

imeandaa jumla ya machapisho 2,498 ukilinganisha na lengo la machapisho 1,402 katika taasisi za Elimu ya Juu ambayo yapo katika majarida ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa;

imetambua matokeo ya tafiti na vifaa vya kufanyia tafiti katika Taasisi za umma 154 ambazo ni: Utafiti na Maendeleo, Wakala za Serikali na Taasisi za Elimu ya Juu. Vilevile, imeandaa taarifa inayoainisha matokeo ya tafiti hususan zenye manufaa ya moja kwa moja kwa jamii pamoja na uwezo wa vifaa na wataalam katika taasisi hizo; na

imeandaa mapendekezo ya tafiti na ukusanyaji wa taarifa za soko la ajira katika sekta za biashara, usafirishaji, ujenzi na mitambo na magari moshi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia taasisi za Elimu ya Juu imeendelea kutoa huduma za ushauri wa kitaalam na ugani katika nyanja za kilimo, ufugaji, ushirika, utawala, uongozi na ardhi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa kazi za maendeleo ya jamii kama ifuatavyo:

imetoa huduma za ushauri na ugani kwa mashirika, wakulima, wafugaji pamoja na kutoa mafunzo ya utengenezaji wa mitego ya kunasa panya kwa wakulima wa mpunga na ufugaji bora wa samaki;

imetoa huduma za kijamii na ushauri kuhusu usimamizi na uendeshaji wa vyama vya ushirika kwa washiriki 6,878 (wanawake 6,239 na wanaume 4,239) kutoka vyama vya ushirika na vikundi vya wadau mbalimbali;

imetoa ushauri wa kitaalamu katika maeneo ya utawala, uongozi, fedha na biashara, sheria na ujasiriamali;

imetoa huduma za urasimishaji ardhi kwa wakazi wa kata tisa za Wilaya ya Mbarali - Mbeya ambapo jumla ya viwanja 29,400 vimepimwa na hati 3,020 zimetolewa kwa wananchi; na

imeendesha mafunzo ya usimamizi wa ardhi kwa viongozi wa mitaa na wataalam 207 kutoka katika Halmashauri ya Kilwa, Mtama na Ileje za Mkoa wa Lindi na Songwe.

D. TUME YA TAIFA YA UNESCO (FUNGU 18)

Mheshimiwa Spika,
katika mwaka wa fedha 2021/22, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO imetekeleza yafuatayo:

imeshiriki katika Mkutano Mkuu wa 41 wa UNESCO uliofanyika nchini Ufaransa mwezi Novemba, 2021. Katika mkutano huo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilichaguliwa kuwa Mjumbe wa Bodi Tendaji ya UNESCO;

imefanikisha Lugha ya Kiswahili kuwa Lugha ya kwanza Afrika kutambuliwa na Baraza la Umoja wa Mataifa na kupewa siku maalum ya tarehe 7 Julai kuadhimishwa kila mwaka;

imetoa mafunzo kuhusu elimu ya sayansi na hisabati inayozingatia jinsia kwa watumishi 41 wa sekta ya elimu kutoka Pemba na Unguja;

imeratibu upatikanaji na ushiriki wa vijana 80 katika shindano la kimataifa masuala ya Urithi wa Dunia lililohusisha nchi ambazo ni Wanachama wa UNESCO katika Kanda ya Afrika ikiwa ni muendelezo wa kusheherekea Siku ya Urithi wa Dunia – Afrika;

imewezesha utekelezaji wa mradi wa Strengthening the Contemporary Dance Scene in East Africa kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali liitwalo MUDA Africa kupitia Mkataba wa UNESCO wa mwaka 2005 unaohusu Protection and Promotion of the Diversity of Cultural Expressions;

imefanikiwa kusimamia na kuratibu utekelezeji wa miradi sita iliyofadhiliwa na Shirika la Elimu Duniani la UNESCO kama ifuatavyo:

Mradi wa Kukabiliana na Matendo Potofu ya Unyago “Confronting Gender Disparity on Girls’ Initiation Malpractice” ambapo Wadau 40 kutoka Wilaya ya Masasi katika Mkoa wa Mtwara walishiriki;

Mradi wa Mafunzo kuhusu Utoaji Elimu ya Sayansi na Hisabati kwa kuzingatia jinsia “Training on Gender Responsive STEM Education” yalifanyika mkoani Morogoro ambapo washiriki 43 kutoka Zanzibar na washiriki 40 kutoka Tanzania Bara walipata fursa ya kushiriki;

Mradi wa Kuimarisha Radio za Kijamii “Empowering Community Radios: Enhancing Content Diversity and Community’s Participation” ambapo washiriki 35 kutoka mikoa tisa (9) ya Tanzania Bara ambayo ni Geita, Simiyu, Mwanza, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Iringa na Mtwara, na washiriki 22 kutoka Unguja na Pemba walipewa mafunzo kuhusu kuimarisha maudhui na ushirikishaji wa jamii kupata habari;

Mradi wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia “Fighting Against Physical and Sexual Violence in the Local Communities” uliohusisha washiriki 70 kutoka Mkoa wa Tabora walipata fursa ya kujadili, kujifunza njia mbalimbali ambazo wanaweza kutumia katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kushiriki katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia;

Mradi wa Uhifadhi wa Magofu ya Kale ya Kihistoria ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara; na

Mradi wa Uhifadhi na Utunzaji wa Michoro ya Miambani ya Kondoa.

MWELEKEO WA UTEKELEZAJI WA MIPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23

Mheshimiwa Spika
, Kazi kubwa itakayofanyika katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23 itakuwa ni kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 kwa minajili ya kufanya maamuzi kuhusu mambo kadhaa ambayo Sera imeainisha lakini hayajatekelezwa. Kwa mfano, Sera inaainisha kwamba elimu ya lazima, yaani compulsory education, itakuwa ni ya miaka kumi, lakini bado tunatoa elimu ya lazima ya miaka saba. Tunatarajia kuwa kabla ya mwisho wa mwaka huu uchambuzi utakuwa umefanyika na kukamilika kuhusu Sera hii ili maamuzi yaweze kufanyika kuhusu utekelezaji. Pamoja na uchambuzi huo, juhudi zitaendelea za kukusanya maoni ya wadau wote ili maamuzi yatakapofanyika yazingatie maoni ya wadau wote na uchambuzi wa kitaaamu. Mapitio ya Sera yatatoa dira ya mabadiliko yatakayohitajika katika Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978. Tunatarajia pia kuwa ifikapo Desemba 2022 Wizara itakuwa imekamilisha rasimu ya mabadiliko ya mitaala itakayozingatia maoni ya wadau na mwelekeo wa Sera ya Elimu utakaokuwa umependekezwa. Zoezi hilo litazingatia sana uboreshaji wa elimu na utaongeza sana elimu ya ufundi na ujuzi itakayomsaidia mhitimu kuweza kujiajiri na kuajirika.

Mheshimiwa Spika,
mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo na mabadiliko ya mitaala ambayo Serikali inakusudia kukamilisha yataleta mageuzi makubwa ya elimu kupata kutokea hapa nchini. Tunatoa wito kwa wadau kuendelea kutoa maoni yao kwa sababu azma ya Serikali ni kufanya mageuzi makubwa yanayozingatia matakwa ya wananchi, kuongeza ubora wa elimu, kuwezesha wahitimu kujiamini, kuajirika na kujiajiri na pia kuwawezesha wahitimu kumudu utandawazi na kukidhi mahitaji ya uchumi wa nchi yetu. Kwa ujumla mambo yafuatayo yataangaliwa na kuzingatiwa:

Mapitio ya Sera;

Mapitio ya Sheria;

Mabadiliko ya Mitaala;

Idadi (mahitaji) ya Walimu, Wakufunzi na Wahadhiri;

Ubora Stahiki wa Walimu, Wakufunzi na Wahadhiri;

Mahitaji ya Miundombinu; na

Mahitaji ya Vitendeakazi.

Maswala haya saba ni budi yazingatiwe ili kuhakikisha kwamba mageuzi ya elimu tunayoyatarajia yatakuwa kweli yanakidhi mahitaji yetu.


Mheshimiwa Spika, pamoja na mapitio ya sera na mabadiliko makubwa ya mitaala Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2022/23, utajielekeza katika kutekeleza maeneo ya kimkakati yafuatayo:

kupanua na kuimarisha elimu ya ufundi nchini;

kuhimiza uandishi, uchapishaji na uchapaji wa vitabu hapa nchini. Moja ya hatua zitakazo chukuliwa ni Serikali kulipia gharama za uchapishaji na uchapaji wa riwaya bora kila mwaka itakayoandikwa na Mtanzania ili kusaidia na kuimarisha juhudi za uandishi hapa nchini;


kutekeleza juhudi za kukuza sayansi hapa nchini kwa kufanya mambo yafuatayo. Kwanza, kutoa ufadhili wa asilimia mia wa kulipia gharama za masomo za chuo kikuu kwa wanafunzi watakaoongoza katika mitihani ya masomo ya sayansi ya kidato cha sita. Pili, katika kutekeleza Ilani ya CCM, kutoa scholarship kwa Watanzania watakaofanya vizuri sana kwenye masomo yao ya vyuo vikuu kwenye nyanja za sayansi, teknolojia na tiba ili kusoma kwenye vyuo vilivyo bora zaidi duniani kama vile MIT. Tatu, kuhimiza utafiti wa kisayansi na tiba kwenye vyuo vyetu vikuu kwa kutoa tuzo ya shilingi milioni hamsini kwa mhadhiri yeyote atakaeweza kuchapisha matokeo ya utafiti wake kwenye majarida yenye hadhi ya juu kabisa ya sayansi na ya elimu ya tiba. Nne, kuhamasisha sekta binafsi na wadau mbalimbali kufadhili Watanzania kwenda kusoma kwenye vyuo bora kabisa duniani. Tayari mikakati imeanza kuandaliwa kwa kushirikiana na Bwana Rupin Rajan na wadau wengine ili kufanikisha azma hii. Kama nitakavyoeleza, tayari benki ya NMB imekubali kutenga Shilingi bilioni mia mbili (200) kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi.

kuongeza wigo wa shule za ufundi za elimumsingi na sekondari kwa lengo la kuwajengea vijana wetu stadi na maarifa yanayohitajika katika soko la ajira; na

kuimarisha ujifunzaji kwa vitendo katika taasisi za Elimu ya Juu kwa kuanza kujenga kampasi za vyuo zenye kujielekeza katika mafunzo kwa vitendo katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa maeneo hayo ya kimkakati utaenda sambamba na utekelezaji wa vipaumbele vifuatavyo:

Kuhuisha Sera, Sheria na Miongozo ya Utoaji wa Elimu Nchini


Mheshimiwa Spika, mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 yataruhusu mapitio ya Sheria ya Elimu Sura 353 na mitaala ya Elimu katika ngazi zote za elimu na mafunzo kwa lengo la kuhakikisha kuwa inakidhi mahitaji ya sasa na wakati ujao Kitaifa na Kimataifa. Sambamba na mapitio ya sera na sheria, Serikali itaandaa miongozo mbalimbali ikiwa ni pamoja na:

mwongozo wa usimamizi na utawala bora katika elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa;

mwongozo wa kuwatambua na kuwaendeleza wanafunzi wenye vipawa na vipaji katika shule za msingi na sekondari;

mwongozo wa usimamizi na ufuatiliaji wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi kwa lengo la kuboresha mafunzo na usimamizi wa elimu katika ngazi husika; na

mwongozo wa kuanzisha, kukarabati na kuendesha maktaba kwa lengo la kuweka utaratibu unaofaa wa kuanzisha, kukarabati na kuendesha maktaba nchini.

Kuendelea Kuhakikisha Watoto wote wenye Umri wa Kwenda Shule Wanapata Fursa

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wenye sifa za kujiunga katika ngazi mbalimbali za elimu nchini wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata fursa sawa na kuhitimu. Azma hiyo, itafikiwa kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwa ni pamoja na:


itafanya ufuatiliaji kwa lengo la kubaini watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapata fursa sawa ya elimu;

itaendelea kutatua changamoto za utoaji wa elimu nchini pamoja na kuhakikisha wanafunzi wote wanapata fursa sawa ya elimu;

itaendelea kuimarisha mazingira ya ushiriki wa wadau katika utoaji wa elimu nchini; na

itaendelea kuimarisha ushiriki wa mtoto wa kike katika elimu kwa kutatua changamoto zinazomkabili ikiwa ni pamoja na ulinzi wa mtoto aendapo na atokapo shuleni.

Kuendelea Kuongeza Fursa na Ubora wa Elimu ya Awali, Elimumsingi na Sekondari, na Elimu ya Ualimu

Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu katika ngazi ya elimu ya awali, elimumsingi, sekondari na elimu ya ualimu na kutoa mafunzo kwa kutekeleza kazi zifuatazo:

itaendelea kutekeleza sera ya elimu bila ada katika ngazi ya elimu ya awali na elimumsingi kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wote wanapata fursa ya elimu;

itasajili taasisi za elimu 500 (shule za awali na msingi 350, shule za sekondari 148 na vyuo vya ualimu 02) ili kuongeza fursa ya upatikanaji wa Elimu;

itakamilisha mfumo wa usajili wa shule kwa njia ya kielektroniki (online school registration system) kwa lengo la kurahisisha utaratibu wa usajili wa shule;

itatoa mafunzo ya Mwongozo wa Huduma ya Maji, Elimu ya Afya na Usafi wa Mazingira Shuleni (School WASH Guidelines) kwa Waratibu wa Mikoa 17 na Halmashauri 86 pamoja na Wathibiti Ubora wa Shule 61 kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Simiyu, Kagera, Kigoma, Shinyanga na Tabora ili kuimarisha usimamizi ufuatiliaji katika ujenzi wa vyoo na miundombinu ya maji shuleni;

itatoa mafunzo kwa walimu 3,600 wa shule za sekondari kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Shule Salama pamoja na mafunzo ya uelewa kuhusu usawa na ukatili wa kijinsia;

itawezesha ujenzi wa madarasa yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 500 katika Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM); na

itaendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa Ofisi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania Jijini Dodoma ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari, Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania itatekeleza yafuatayo:


itawezesha ujenzi wa madarasa 90 katika shule 20 za msingi na 10 za sekondari ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia;

itawezesha ujenzi wa matundu ya vyoo 1,200 katika shule 30 za msingi na 20 sekondari zenye upungufu ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia;

itawezesha ujenzi wa maabara za sayansi 15 kwa shule za sekondari 15 zenye upungufu ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia na hivyo kuongeza ufaulu katika masomo ya sayansi;

itawezesha ukarabati wa shule kongwe za sekondari tano ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia;

itawezesha ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa shule 30 za msingi na sekondari;

itawezesha ujenzi wa nyumba 80 za walimu katika shule 15 za sekondari na tano za msingi zilizopo katika maeneo yenye mazingira magumu kwa lengo la kuimarisha makazi ya walimu na kuongeza ufanisi; na

itaendelea kutekeleza miradi ya kukuza ujuzi nchini kupitia Mfuko wa Kukuza Ujuzi - Skills Development Fund katika vyuo mbalimbali kwa kutoa mafunzo ili kuongeza wigo wa ajira nchini.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utoaji wa elimu nje ya mfumo rasmi kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Serikali itatekeleza yafuatayo:


itaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kisomo na Elimu kwa Umma (NALMERS) unaolenga kupunguza kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika kwa kuwajengea uwezo maafisa na wataalamu wa kisomo;

itawezesha wasichana takribani 3,000 walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kupata elimu ya sekondari kwa njia mbadala;

itaendelea kuongeza fursa za mafunzo na ujuzi kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu kupitia Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana walio Nje ya Mfumo Rasmi wa Elimu (IPOSA); na

itaongeza udahili wa wanafunzi wa Astashahada, Stashahada na Shahada kutoka 4,430 hadi 5,200.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha na kuendeleza elimu ya ualimu nchini, Serikali itawezesha Vyuo vya Ualimu kujiunga na umoja wa Maktaba za tafiti na Vyuo Vikuu Tanzania -

Consortium of Tanzania University and Research Libraries (COTUL) kwa ajili ya kupata maarifa yaliyo katika mfumo wa kielektroniki (E-resources). Aidha, itaendelea na uunganishaji wa Vyuo vya Ualimu katika Mkongo wa Taifa - National Fiber Optical.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ubora wa elimu ya awali, elimumsingi, sekondari na kuendeleza elimu ya ualimu, Serikali itatekeleza yafuatayo:


itaendelea kukuza ujuzi wa uandishi (writing skills) kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini kwa kuratibu mashindano ya uandishi wa insha katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika; na

itawezesha uchapaji na usambazaji wa nakala 2,000 za Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu 2021/22 - 2025/26 pamoja na kutoa mafunzo kwa Maafisa Elimu 26 wa Mikoa na 184 wa Halmashauri kuhusu uandaaji wa mipango ya elimu kwa kuzingatia mpango huo na kufanya ufuatiliaji na tathmini.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha upimaji na tathmini ya elimumsingi, sekondari na vyuo vya ualimu, Serikali itatekeleza yafuatayo:

itaendesha upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne kwa watahiniwa 1,716,776 wanaotarajiwa kufanya upimaji huo mwezi Novemba, 2022;

itaendesha Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi kwa watahiniwa 1,376,169 wanaotarajiwa kufanya mtihani huo mwezi Oktoba, 2022;

itaendesha Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili kwa watahiniwa 694,336 wanaotarajiwa kufanya upimaji huo mwezi Novemba, 2022; itaendesha Mtihani wa Kidato cha Nne kwa watahiniwa 596,272 na Mtihani wa Maarifa kwa watahiniwa 8,505 wanaotarajiwa kufanya mitihani hiyo mwezi Novemba, 2022;

itaendesha Mtihani wa Kidato cha Sita kwa watahiniwa 93,594 wanaotarajiwa kufanya mtihani huo mwezi Mei, 2023;

itaendesha Mtihani wa Astashahada na Stashahada ya Ualimu kwa watahiniwa 7,135 wanaotarajiwa kufanya mtihani huo mwezi Mei, 2023;

itaendesha upimaji wa umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa sampuli ya wanafunzi 32,363 wa darasa la pili mwezi Januari, 2023;

itawezesha uchapaji wa vitabu vya uchambuzi wa matokeo ya upimaji wa darasa la pili 2021 (PIRA - STNA), vitabu vya uchambuzi wa matokeo ya upimaji wa darasa la nne, 2021 (PIRA - SFNA) na vitabu vya uchambuzi wa matokeo ya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi 2021 (PIRA - PSLE); na

itaendelea kuimarisha mfumo wa usahihishaji wa mitihani kwa njia ya kielektroniki (e–marking) kwa lengo la kuendelea kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa mitihani.


Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara itaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ngazi ya Elimumsingi nchini kwa kutoa mafunzo kazini kuhusu matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu 1,500 kutoka katika shule za sekondari 750. Vilevile, itatoa mafunzo kazini kwa walimu 10,000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo hayo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa vitabu katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari, na kuhamasisha tabia ya wanafunzi kupenda kujisomea vitabu. Katika kufikia azma hiyo, Serikali itatekeleza yafuatayo:

itatoa tuzo kwa waandishi bora wa vitabu vya riwaya zitakazotumika katika kufundishia na kujifunzia;

itawezesha Taasisi ya Elimu Tanzania kuchapa na kusambaza nakala 2,000,000 za vitabu vya masomo manne ya Mathematics, Physics, Chemistry na Biology;

itaendelea na uandishi wa vitabu vya kiada ngazi ya sekondari na elimu ya ualimu (Astashahada na Stashahada) kwa lengo la kupunguza changamoto ya upatikanaji wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia; na

itachapa na kusambaza vitabu vya kimacho na nuktanundu kwa ajili ya shule za msingi na sekondari kwa lengo la kusaidia ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi wenye uoni hafifu na wasioona.

Mheshimiwa Spika, katika kutoa nafasi kwa umma wa watanzania kutumia maktaba za umma kwa ajili ya kupata taarifa sahihi na maarifaili kujikwamua katika ujinga, umaskini na maradhi; Serikali kupitia Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania itaanzisha kanzi data ya kitaifa itakayosaidia kupata taarifa mbalimbali za machapisho na taarifa nyingine za Kiserikali kama vile hotuba za viongozi na hansadi za Bunge. Aidha, itaongeza idadi ya udahili kwa wanafunzi kutoka 618 hadi kufikia 800 katika Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka (SLADS).

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa hamasa ya usomaji wa vitabu na elimu kwa umma kwa: kuendesha programu za usomaji kwa jamii -outreach programme; kufanya makongamano ya usomaji wa vitabu na maonesho ya vitabu; na kuendesha programu maalum za usomaji kwa watoto kwa lengo la kuongeza ari ya usomaji.

Mheshimiwa Spika,
Serikali kupitia Bodi ya Huduma za Maktaba itaendelea kuongeza wigo wa utoaji wa elimu kwa jamii kwa kuimarisha upatikanaji wa machapisho ya kielektroniki (e-books), vitabu vya nuktanundu na vifaa muhimu vya kujifunzia. Vilevile, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya maktaba kwa; kujenga na kukarabati maktaba ya Mkoa wa Tanga, Mara, Mwanza, Singida, maktaba ya Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi Nyaraka Bagamoyo pamoja na kuongeza nakala za vitabu hadi kufikia 2,300,000 kwa lengo la kuboresha huduma za maktaba nchini. Vilevile, Serikali itaendelea kutangaza huduma za maktaba kupitia njia za mawasiliano kama vile runinga, redio, tovuti, mitandao ya kijamii, magazeti na vipeperushi ili kuwajengea uelewa wadau mbalimbali kuhusu majukumu na kazi za Bodi.

Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa elimu ya ualimu nchini kwa kutekeleza yafuatayo:

itaendeleza mafunzo ya elimu ya ufundi katika vyuo vya ualimu kutoka vyuo viwili vilivyopo sasa hadi kufikia vyuo saba kwa kuviwezesha kuwa na; vifaa, mashine,

karakana na walimu wa masomo ya ufundi. Vilevile, itawezesha mafunzo kwa wakufunzi 100 wa masomo ya ufundi katika vyuo hivyo;

itaendelea kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Vyuo vya Ualimu 35 vya Serikali kwa kununua vitabu vya kiada na rejea vya kielektroniki (E-Text books and references) pamoja na samani;

itakarabati maabara za sayansi na TEHAMA pamoja na maktaba katika Vyuo vya Ualimu saba kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa vitendo katika Vyuo vya Ualimu; na

itawezesha utoaji wa mafunzo kuhusu utunzaji na menejimenti ya maabara za sayansi kwa wataalamu 50 wa maabara.

Mheshimiwa Spika, Serikali itatoa mafunzo ya ufundishaji wa masomo ya michezo na biashara kwa wakufunzi
Masomo hayo ni; Physical Education, Fine arts, Music, Theatre Arts, Home Economics and Nutrition, Commerce na Book-keeping. Lengo la mafunzo hayo ni kuendelea kuimarisha uwezo wa wakufunzi kufundisha masomo ya michezo na biashara. Vilevile, Serikali itaendelea kuratibu mashindano ya michezo na sanaa (UMISAVUTA) kwa lengo la kuimarisha afya na kuibua vipaji katika Vyuo vya Ualimu.


Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa somo la hisabati katika elimu ya msingi, sekondari na Vyuo vya Ualimu, Serikali itaendelea kukiimarisha Kituo cha Hisabati – Mathematics Centre kilichopo Chuo cha Ualimu

Morogoro kwa ajili ya kuanzisha programu za mafunzo endelevu kwa walimu.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha elimu inatolewa kwa kuzingatia usawa wa jinsia wenye kuzingatia malezi bora na usalama wa mtoto shuleni na vyuoni, Serikali itaendelea kutekeleza Mkakati wa Jinsia - Gender Strategy pamoja na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mkakati huo. Aidha, Serikali itatoa mafunzo kwa walimu 200 kuhusu unasihi na ulinzi wa mtoto ili kuboresha huduma hiyo katika shule za msingi na sekondari.

Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa miongozo na mikakati mbalimbali ya kusaidia wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali kwa kusimamia utekelezaji wa: Mwongozo wa Utekelezaji wa Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala -Alternative Education Pathway Implementation guideline; Mwongozo wa Wanafunzi wa Elimu Nje ya Mfumo Rasmi; na Mwongozo wa Wawezeshaji.

Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kutekeleza afua mbalimbali zenye lengo la la kupunguza mdondoko wa wanafunzi kupitia utekelezaji wa programu ya shule salama. Aidha, Serikali itatoa mafunzo kuhusu utekelezaji wa mpango huo kwa walimu 3,600 wa sekondari pamoja na kutoa mafunzo ya uelewa kuhusu usawa na ukatili wa kijinsia.

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa elimu maalum, Serikali itatekeleza yafuatayo:

itafanya ufuatiliaji na tathmini katika shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimu vinavyopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa lengo la kubaini changamoto zilizopo na kutoa ushauri wa kitaalamu;

itatoa mafunzo kwa wathibiti ubora wa shule 150 kuhusu ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum; na

itaendelea kuandika, kuchapa na kusambaza vitabu vya sekondari katika mfumo wa breli na maandishi yaliyokuzwa kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu na wasioona ili kuwawezesha kusoma kwa urahisi.

Kuimarisha Mifumo ya Usimamizi wa Utoaji wa Elimu Kuanzia Elimumsingi, Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, na Elimu ya Juu

Mheshimiwa Spika,
Katika kuimarisha uthibiti ubora wa elimu katika ngazi ya elimumsingi, sekondari na Vyuo vya Ualimu, Serikali itaendelea kusogeza huduma ya uthibiti ubora wa shule na Vyuo vya Ualimu katika ngazi ya Halmashauri kwa kujenga ofisi tano za Uthibiti Ubora wa Shule katika Halmashauri ya Pangani, Ubungo, Bunda, Njombe na Tarime. Vilevile, itawezesha ununuzi wa magari 20 ili kuwezesha kazi za uthibiti ubora wa shule.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha miongozo, sheria, kanuni na taratibu za elimu zinazingatiwa katika utoaji wa elimu, Serikali itatekeleza kazi zifuatazo:

itafanya tathmini ya jumla - whole school visits katika asasi 19,800 zikiwemo shule za msingi 17,164, sekondari 2,578 na vyuo vya ualimu 58; na

itafanya ufuatiliaji – followup visit katika asasi 6,994 zikiwemo shule za msingi 5,676, sekondari 1,289 na vyuo vya ualimu 29. Aidha, itafanya ufuatiliaji maalum katika asasi 745.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa elimu kwa kuwajengea uwezo Wakuu wa Shule za sekondari 5,264 kwa lengo la kuimarisha uthibiti ubora wa ndani ya shule ili kuinua ubora wa elimu inayotolewa katika shule husika. Aidha, Serikali imelenga kuandaa mfumo wa kielektroniki wa uthibiti ubora wa shule ili kurahisisha ukusanyaji wa taarifa na kurahisisha kufanya maamuzi.

Mheshimiwa Spika,
katika kuimarisha usimamizi na utoaji wa elimu bora katika ngazi za elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu, Serikali kupitia Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), itadahili walimu 2,343 watakaosoma Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu (DEMA) na Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Elimu (DSQA).

Mheshimiwa Spika
, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa elimumsingi nchini kwa kuziwezesha taasisi za uendelezaji wa elimu katika ngazi hiyo. Taasisi hizo ni pamoja na: Taasisi ya Elimu Tanzania (TET); Baraza la Mitihani

Tanzania (NECTA), Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) pamoja na Idara za Wizara. Uimarishaji huo utafanyika kupitia; ununuzi wa magari 17 kwa ajili ya usimamizi wa afua za elimumsingi.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usimamizi wa maendeleo ya shule na matumizi ya fedha, Serikali itatoa mafunzo ya muda mfupi kwa walimu 28,074 (21,274 usimamizi wa fedha na 6,800 uongozi na usimamizi wa elimu).

Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kuimarisha utendaji kazi wa wasimamizi wa elimu nchini kwa kutoa mafunzo kwa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya, na Wathibiti Ubora wa Shule wa Kanda na Wilaya wapatao 3,829 (tathmini ya kiutendaji 1,836, umahiri wa ufundishaji na ujifunzaji 1,626, na mpango wa ufuatiliaji na tathmini 367). Aidha, Serikali itatoa mafunzo ya uthibiti ubora wa elimu kwa Wathibiti Ubora wa Vyuo vya Elimu ya ufundi wapatao 319.

Mheshimiwa Spika,
katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa taaluma ya uongozi na usimamizi wa elimu, Serikali kupitia Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) itatekeleza yafuatayo:

itakamilisha ujenzi na uwekaji wa samani katika jengo la ghorofa lenye kumbi nne za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 564 pamoja na ofisi 10 katika Kampasi ya Mbeya;

itakarabati ofisi nne , kumbi za mihadhara tatu na nyumba tatu za watumishi katika Kampasi ya Bagamoyo; na
itaanza ujenzi wa Kampasi ya ADEM - Mwanza.


Mheshimiwa Spika, katika kusimamia na kuendeleza Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini, Serikali itaendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 kwa lengo la kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakidhi viwango vinavyohitajika. Vilevile, itaandaa mfumo wa utunzaji na uchakataji wa taarifa za mafunzo ya ufundi stadi (VETdataMIS) nchini.

Mheshimiwa Spika,
katika kusogeza huduma ya mafunzo ya ufundi stadi kwa wananchi, Serikali itajenga Ofisi ya VETA Makao Makuu Jijini Dodoma. Aidha, Serikali itakamilisha ujenzi wa ofisi tano za Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) za kanda katika mkoa wa Arusha, Mbeya, Mwanza, Tabora na Mtwara pamoja na kuanza ujenzi wa ofisi – Dodoma.


Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha uthibiti ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa kutekeleza yafuatayo:

itawezesha uandaaji wa miongozo ya mitaala na uhakiki wa ubora wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi;

itawezesha NACTVET kufanya mapitio ya miongozo ya uandaaji wa mitaala na kutoa ithibati ya mitaala katika vituo vya umahiri (Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam - DIT, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji – NIT, Chuo cha Ufundi Arusha - ATC) vinavyotekeleza afua za kimkakati ambazo ni maendeleo ya TEHAMA na sekta ya ngozi, usafiri wa anga na nishati jadidifu;

itakamilisha Kiunzi cha Ulinganifu wa Sifa na Tuzo za Kitaaluma na Kitaalamu Tanzania ambacho kitaoanisha sifa na ngazi zote za elimu na mafunzo;

itasimika mtandao wa mawasiliano wa ndani (LAN) na nje (WAN) katika vyuo 30 vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi;

itafanya ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi katika vyuo 400 kati ya vyuo 1,298 kwa lengo la kuhakiki ubora wa elimu inayotolewa katika vyuo vya ufundi; na

itanunua magari 20 kwa ajili ya matumizi ya Ofisi za Makao Makuu, Kanda na Vyuo.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uthibiti ubora wa elimu katika ngazi ya Elimu ya Juu, Serikali itatekeleza yafuatayo:


itafanya mapitio ya Sheria ya Vyuo Vikuu Sura 346 kwa lengo la kuihuisha ili iendane na mahitaji ya sasa;

itavijengea uwezo Vyuo Vikuu katika masuala ya ithibati na uthibiti ubora wa ndani ili kuimarisha ubora wa Elimu ya Juu;

itashiriki katika makongamano na mikutano inayohusu uimarishaji wa uthibiti ubora kikanda na kimataifa kwa lengo la kuongeza ujuzi na weledi katika uthibiti ubora wa Elimu ya Juu nchini;

itaboresha mifumo ya TEHAMA ya ukusanyaji na utoaji taarifa za Elimu ya Juu kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati na matumizi yake katika kupanga mipango na kufanya maamuzi; na

itaendelea kusimamia utendaji wa Vituo vya Umahiri vya Afrika katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini -African Centre of Excellence- ACE II ambavyo vipo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Elimu ya Juu inayotolewa nchini inazingatia sheria, kanuni, miongozo na taratibu, Serikali itaendelea kutekeleza yafuatayo:


itafanya ufuatiliaji na tathmini katika Vyuo Vikuu 30 kwa lengo la kuhakiki ubora;

itafanya tathmini ya tuzo 3,000 zilizotolewa katika Vyuo Vikuu vya nje ya nchi na kuzitambua zitakazokidhi vigezo;

itafanya tathmini ya programu 300 za masomo mbalimbali katika Vyuo Vikuu nchini na kuzipa ithibati programu zitakazokidhi vigezo; na

itakagua Asasi/Kampuni tano zinazojishughulisha na uratibu wa wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi kwa lengo la kuzitambua na kuzisajili zile zitakazokidhi vigezo.

Kuendelea Kuongeza Fursa na Ubora wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza fursa za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji na utoaji wa elimu na mafunzo hayo. Katika kufikia azma hiyo, Serikali itatekeleza yafuatayo:


itasajili vyuo 20 vya elimu ya ufundi na vyuo 80 vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi na hivyo kuwa na jumla ya vyuo 538 vya elimu ya ufundi na vyuo 830 vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi mtawalia;

itahakiki udahili wa wanafunzi takribani 250,000 (vyuo vya Serikali 200,000 na vyuo visivyo vya Serikali 50,000) kupitia Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi;

itaongeza ushiriki wa wanafunzi wa kike katika mafunzo ya elimu ya ufundi stadi kutoka asilimia 41 hadi kufikia asilimia 45;

itaendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu ya ufundi stadi na elimu ya wananchi kwa washiriki 15,000 katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 kwa lengo la kuwapatia ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kujiajiri au kuajiriwa;

itaendelea kusimamia ujenzi wa Chuo cha Ufundi cha Dodoma (DTC) kinachojengwa katika eneo la Nala kwa lengo la kuongeza fursa ya utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi;

itakamilisha ujenzi na uwekaji samani katika Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi vya Wilaya 25 na vyuo vinne vya Mikoa. Aidha, itaweka zana za msingi za mafunzo katika vyuo vikongwe 15 vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi;

itafanya maonesho ya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuendeleza bunifu baina ya wadau mbalimbali wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi;

itajenga mabweni nane katika Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi vya Wilaya tano ambazo ni Namtumbo 2, Kasulu Vijijini 1, Ileje 2, Simanjiro 1 na Itilima 2;

itajenga mabwalo manne ya chakula katika Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi vya Wilaya ya Namtumbo, Itilima, Ileje na Urambo;

itakamilisha ujenzi wa ukumbi wa mihadhara na darasa katika Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Utalii na Ukarimu cha Njiro;

itajenga vyuo viwili vya huduma katika Mkoa wa Songwe na Dar es Salaam (Kampasi ya Kigamboni);

itaendelea kukamilisha ujenzi wa vyuo vya Ufundi Stadi vya Wilaya ya Wanging’ombe na Wilaya ya Newala;

itakarabati vyuo viwili vya Ufundi Stadi na Huduma vya Mkoa wa Dar es Salaam na Dodoma;

itaanza ujenzi wa ofisi ya VETA Makao Makuu jijini Dodoma; na

itatunuku wanagenzi 2,800 kutoka sekta isiyo rasmi na kutoa mafunzo kwa wajasiliamali 3,000 kwa utaratibu wa Integrated Training for Enterpreneurship Promotion
(INTEP).


Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya watumishi katika utoaji wa Elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini, Serikali itajenga nyumba nane za watumishi katika Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi vya Wilaya ya Namtumbo 1, Itilima 2, Kasulu Vijijini 3, na Ileje 2. Vilevile, Serikali itakarabati nyumba 25 za watumishi katika Chuo cha; Moshi – Kilimanjaro (10), Singida (2), Kigoma (3), Tabata – Dar es Salaam (10).

Mheshimiwa Spika, Katika kuhakikisha wahitimu wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi wanapata stadi za kuwawesha kujiajiri na kuajiriwa, Serikali itaendelea kuimarisha ujuzi na umahiri kwa wahitimu kwa kutekeleza yafuatayo:


itajenga karakana sita za uchomeleaji na uungaji wa vyuma katika Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma vya Mkoa wa Manyara na Pwani, pamoja na karakana za umeme, bomba, magari na uashi katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma cha Kihonda;

itaviwezesha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 kwa kuvinunulia vifaa vya kiufundi vya kufundishia na kujifunzia. Aidha, itaviwezesha Vyuo 47 vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa kuvinunulia vitabu na kompyuta 1,175 kwa lengo la kuhakikisha ujuzi wa wahitimu unaendana na mipango ya nchi na soko la ajira;

itaendelea kutoa mafunzo kwa wakufunzi 100 katika Taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa ufundishaji wa mitaala inayoendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira; na

itawajengea uwezo walimu 1,000 kutoka katika Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi 50 kuhusu utoaji wa Elimu ya Ufundi na Tathmini ya Mitaala ya Umahiri (CBET). Mafunzo hayo yatasaidia kuwa na walimu mahiri wa kuzalisha nguvu kazi iliyo tayari kutumika katika uzalishaji viwandani.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa yanakidhi mahitaji ya soko la ajira, Serikali itatekeleza yafuatayo:

itafanya ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa lengo la kuhakikisha ubora unazingatiwa katika utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi; na

itahakiki mitaala 180 ya Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa lengo la kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanakidhi soko la ajira.

Kuendelea Kuongeza Fursa na Ubora wa Elimu ya Juu

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Juu nchini, Serikali itatekeleza kazi zifuatazo:

itaratibu udahili wa wanafunzi 133,000 wa mwaka wa kwanza wanaotarajiwa kuomba udahili katika Vyuo vya Elimu ya Juu kwa lengo la kujiunga na programu mbalimbali za masomo kwa ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada ya Kwanza na Shahada ya Umahiri. Vilevile, itaanzisha mpango wa fursa za ziada kwa wanawake kwa kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike katika programu za sayansi (Science, Technology, Engineering and Mathematics (STEM);

itaratibu maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu nchini kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu vyuo na programu mbalimbali zitolewazo;

itaratibu maombi, uchambuzi na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi 205,893 katika Taasisi za Elimu ya Juu. Aidha, itafanya ukaguzi kwa waajiri 8,000 kwa lengo la kuwabaini wanufaika wapya takribani 30,000 ili kuwezesha ukusanyaji wa Shilingi 241,419,005,000.00 kutokana na mikopo iliyoiva kutoka Shilingi 201,319,005,000.00 za mwaka wa fedha 2021/22;

itahuisha mwongozo wa utoaji mikopo kwa lengo la kuboresha utoaji wa mikopo kwa wanufaika; na

(v)\ itaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika taasisi 19 za Elimu ya Juu katika ufundishaji, ujifunzaji na usimamizi kwa lengo la kuimarisha mazingira ya utoaji wa elimu katika ngazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya kugharimia Elimu ya Juu nchini kwa lengo la kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Juu ili kuendana na mahitaji yanayotokana na ongezeko kubwa la uhitaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu. Katika kufanikisha hilo, Benki ya NMB imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 200 kwa kuanzia
katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kuanza kutoa mikopo ya elimu.

Mheshimiwa Spika, Fedha hizo zitasimamiwa na NMB Benki kwa utaratibu maalum wa kibenki na kwa mujibu wa makubaliano rasmi kati ya Wizara na NMB ambapo mikopo hiyo itaongozwa na masharti yafuatayo:


(i)\ itatolewa kwa riba nafuu;

(ii)\ itatolewa kuanzia ngazi ya stashahada (Diploma) na masomo ya Umahiri (Postgraduate) ambapo Bodi ya mikopo haijaanza kutoa mikopo katika ngazi hizo; na

(iii)\ itatolewa kwa wazazi au walezi ambao ni waajiriwa wa Serikali na sekta binafsi/ au kwa wafanyakazi wanaotaka kujiendeleza.


115.\ Mheshimiwa Spika hii itasaidia kupunguza idadi ya waajiriwa wanaowaombea watoto wao mikopo Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na hivyo kutoa fursa zaidi kwa waombaji wenye uhitaji

zaidi. Kutokana na fursa hiyo, Kipekee naomba niishukuru Benki ya NMB kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za ugharamiaji wa Elimu ya Juu. Vilevile, nitambue uwepo wa Mtendaji Mkuu NMB Benki Bi. Ruth Zaipuna ambaye tumemkaribisha katika Bunge lako tukufu. Aidha, nitoe wito kwa taasisi nyingine kuunga mkono jitihada za Serikali za kugharimia elimu nchini.

116.\ Mheshimiwa Spika, katika kuwajengea uwezo wa utendaji kazi watumishi katika taasisi za Elimu ya Juu nchini, Serikali itaendelea kutoa ufadhili kwa Wanataaluma na Wataalam 1,401 kuhudhuria masomo ya muda mfupi 500 na muda mrefu

Aidha, Serikali itatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 65 wenye ufaulu uliojipambanua katika masomo ya sayansi hususan wanafunzi wa kike waliohitimu mitihani ya Kitaifa ya Kidato cha 6 na Shahada ya Kwanza.


117.\ Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha uhusiano na mataifa mengine katika uendelezaji wa Elimu ya Juu nchini kwa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa kigeni 10 wa Shahada ya Umahiri katika Lugha ya Kiswahili. Vilevile, itaratibu nafasi 200 za ufadhili wa masomo kutoka nchi rafiki na mashirika mbalimbali nje ya Bara la Afrika.


Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za mikopo kwa wanufaika kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa kutekeleza yafuatayo:

itaunganisha mifumo ya TEHAMA ya Bodi na wadau wa kimkakati kwa lengo la kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa za utoaji na urejeshaji wa mikopo; na

itaendelea kusajili wanafunzi walionufaika na mikopo katika mfumo wa malipo wa kielektroniki (DIDiS) kwa lengo la kuwezesha wanufaika kupata mikopo kwa wakati na kurahisisha ufuatiliaji wa mikopo iliyotolewa.

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Vyuo Vikuu, Serikali itatekeleza kazi zifuatazo:

itajenga maabara 21, mabweni 19, madarasa 77, kumbi za mihadhara 13, maktaba tisa, ofisi 71, mifumo ya maji minne, vituo atamizi vitatu na studio moja;

itaendelea na ukarabati wa mabweni 11, madarasa 50, maabara mbili, nyumba za watumishi 15 na ofisi 25;

itanunua magari mawili na kuongeza vitendea kazi katika ofisi ya Makao Makuu Dodoma na Kituo Mahsusi cha Wateja - Dedicated Customer Relations Centre cha Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha huduma za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu; na

itajenga Ndaki ya Uchumi na Mafunzo ya Biashara awamu ya pili katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
na Ndaki ya uchumi na mafunzo ya biashara katika Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia - Butiama.


Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Elimu ya Juu inayotolewa nchini inaendana na mahitaji ya soko la ajira, Serikali itaandaa mitaala ya programu nane mipya katika ngazi ya Shahada ya Kwanza na Umahiri pamoja na kuanzisha Shahada mpya za awali tano na Shahada za Uzamili tatu. Aidha, Serikali itaanzisha programu nne na kuhuisha mitaala ya programu 24 kwa lengo la kuwezesha wahitimu kujiajiri na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.


Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini, Serikali itaongeza vitengo mbalimbali katika taasisi za Elimu ya Juu ikiwemo shule ya meno na kuanza mpango wa ujenzi wa Kliniki ya Uporoto (Uporoto Polyclinic) kwa lengo la kuimarisha huduma za tafiti na tiba. Vilevile, itaendeleza vituo atamizi, mashamba darasa, semina na kozi fupi ili kuongeza uzalishaji wenye tija.

Kutegemeza Matumizi ya Sayansi na Teknolojia Katika Ufundishaji na Ujifunzaji kwa Maendeleo ya Taifa


Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuwaibua, kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu nchini kwa lengo la kuendeleza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika ajenda ya maendeleo. Katika kufikia azma hiyo, Serikali itatekeleza yafuatayo:

itawaibua, kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu na wagunduzi wachanga kupitia Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) kwa lengo la kuwezesha ubunifu wao katika kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Wabunifu hao watatoka katika Shule za Msingi na Sekondari, Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi, Vyuo vya Ufundi, Vyuo Vikuu, Vituo vya kuendeleza teknolojia, Taasisi za Utafiti na Maendeleo pamoja na Mfumo usio rasmi;


itaratibu maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu Kitaifa kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya bunifu na teknolojia katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii;


itaandaa mkutano wa wadau wa sayansi teknolojia na ubunifu na Watanzania wanaoishi nje ya nchi utakaojulikana kama The First Multistakeholder and Diaspora Forum on Science Technology and Innovation kwa lengo la kujadili ushiriki wao katika kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini;


itaandaa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi kwa ajili ya kuhamasisha ushiriki wao katika kukuza mchango wa sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati kwenye maendeleo ya kiuchumi na kijamii; na itawaendeleza wabunifu 70 walioibuliwa kupitia MAKISATU katika mwaka wa fedha 2021/22.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wabunifu na wagunduzi wapya wanatambuliwa pamoja na kazi zao kufikia hatua za ubiasharishaji, Serikali itaimarisha uratibu wa shughuli za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika ngazi mbalimbali kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa lengo la kuwafikia wabunifu na wagunduzi wachanga hususan katika maeneo ya vijijini.


Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA nchini kwa kuunganisha taasisi za utafiti na Mkongo wa Taifa. Vilevile, itajenga kituo cha kikanda cha umahiri wa TEHAMA chenye hadhi ya kimataifa, itaandaa mfumo wa uhawilishaji wa teknolojia kupitia uwekezaji nje ya nchi na itahakiki teknolojia zinazoibukia - Inventory of emerging technologies.


Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha utoaji wa mafunzo ya sayansi, teknolojia na ubunifu, Serikali itaanza ujenzi wa majengo ya Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia, Ndaki ya Usanifu majengo na Teknolojia ya Ujenzi na Kujenga jengo la kitaaluma la Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya - Kampasi ya Rukwa.


Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) itaendelea kuimarisha usimamizi, udhibiti na matumizi salama ya mionzi ya nyuklia nchini kwa kutekeleza yafuatayo:

itapokea na kutathmini maombi 600 ya vibali vya umiliki, utumiaji na usafirishaji wa vyanzo vya mionzi ili kuhakikisha usalama wa wananchi;

itaendelea kuendesha kituo cha kupima uchafuzi wa hewa katika anga unaotokana na majaribio ya silaha za nyuklia chini ya mkataba wa kimataifa wa Comprehensive Nuclear Test - Ban Treaty (CTBT) for Non-Proliferation Test (NPT) of Nuclear weapons;

itapima na kudhibiti viwango vya mionzi kwa wafanyakazi 2,064 wanaofanya kazi kwenye mazingira ya vyanzo vya mionzi;

itaimarisha na kupima mionzi katika mazingira kwenye vituo 40 ambavyo vimekuwa vikiendeshwa kwa ushirikiano na Taasisi nyingine; na

itafanya ukaguzi katika vituo 120 vinavyotoa mionzi isiyoayonisha (Non-Ionizing Radiation) kwa mfano minara ya simu, redio, runinga na vifaa vingine vya mionzi ili kubaini usalama wa wakazi wa maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, Katika kuimarisha huduma ya teknolojia ya nyuklia zinazotolewa na TAEC, Serikali itatekeleza yafuatayo:

itasajili vituo vipya 60 vinavyotumia vyanzo vya mionzi ambapo ongezeko hilo litawezesha kufikia vituo 1,129 vilivyosajiliwa nchini;

itaanzisha kituo cha mafunzo ya usalama wa mionzi na nyukilia ili kuongeza wataalamu na wigo wa udhibiti wa matukio hatarishi ya kinyuklia;

itaendelea na ujenzi wa maabara na ofisi katika Kanda ya Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza;

itaendelea kupima sampuli 28,000 za vyakula, mbolea na tumbaku na bidhaa nyingine zote katika mnyororo wa chakula zinazotoka na kuingia nchini kwa lengo la kubaini endapo hazina madhara ya mionzi;

itafungua ofisi tatu katika Kanda na mipaka mbalimbali nchini ili kuongeza uwezo wa udhibiti mionzi na kuwahudumia wananchi;

itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuhifadhi mazao ya kilimo ikiwemo vyakula viharibikavyo kirahisi (perishable), vifaa tiba na vya viwandani kwa kutumia teknolojia ya mionzi - Multipurpose Irradiator Facility;


itakagua vituo 600 vyenye vyanzo vya mionzi ili kubaini hali ya usalama wa mionzi kwa wagonjwa, wafanyakazi na umma kwa ujumla. Vilevile, itakagua migodi saba ya madini kwa lengo la kubaini hali ya usalama wa mionzi kwa wafanyakazi katika migodi hiyo; na

itaendelea na ujenzi wa maabara za kanda katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na kuanza ujenzi wa maabara katika Mkoa wa Mbeya na Zanzibar kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki. Aidha, itaendelea na ujenzi wa maabara changamano (Complex Multipurpose Laboratory) awamu ya pili kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika taasisi za sayansi, teknolojia na ubunifu, Serikali itatekeleza yafuatayo:

itaanza ujenzi wa jengo la ghorofa sita lenye vyumba vya madarasa, ofisi na maabara katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam;

itajenga mabweni mawili katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 600 na kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi wa bweni moja katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 180;

itaanza ujenzi wa jengo la utawala katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST);

itajenga viwanda vinne vya kufundishia na kujifunzia kwa vitendo - teaching factory katika taasisi ya DIT, MUST, SUA na ATC;

itajenga hosteli mbili katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 160 na kukamilisha ujenzi wa hosteli mbili katika Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 800 kwa wakati mmoja; na

itanunua vifaa vya kisasa vya maabara na karakana kwa lengo la kuboresha utoaji wa mafunzo katika fani mbalimbali za sayansi na teknolojia ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza ufanisi kwa wataalamu na wanataaluma wa taasisi za sayansi, teknolojia na ubunifu nchini, Serikali itafadhili watumishi 300 kuhudhuria masomo ya muda mfupi ndani na nje ya nchi. Aidha, itaendesha kozi fupi za ubobezi katika TEHAMA, Sayansi ya Maabara na Teknolojia ya Ngozi kwa washiriki 250.

Mheshimiwa Spika,
katika kuimarisha mafunzo kwa vitendo katika taasisi zinazosimamia na kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu nchini, serikali itatekeleza yafuatayo:

itaendeleza dhana ya mafunzo viwandani - industrial attachment itakayowawezesha wahitimu katika kila ngazi kupata ujuzi unaokidhi soko la ajira; na

itawezesha ujenzi wa viwanda vya kufundishia na kujifunzia (teaching factories) katika Chuo cha ufundi Arusha (ATC), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo (SUA).

Kuimarisha na Kuendeleza Tafiti na Matumizi ya

Matokeo yake katika Ajenda ya Maendeleo

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa ndani wa kufanya tafiti na kutumia matokeo ya tafiti katika kuchangia ajenda ya maendeleo ya nchi kwa kutekeleza yafuatayo:

itafanya tafiti 252 katika maeneo ya mazingira, TEHAMA, nishati, kilimo na chakula, uongozi na biashara, maendeleo ya utalii, sheria, uthibiti wa ubora, utawala na maendeleo, watu wenye ulemavu na mahitaji maalum, maliasili, umaskini, utamaduni, haki za binadamu, maendeleo ya watu na mawasiliano, mifugo, biashara, uvuvi, elimu, sayansi, lugha na fasihi;

itaongeza utoaji wa elimu na ushauri kwa washiriki 2,500 wakiwemo wakulima, maafisa ugani na watafiti kwa kutumia mbinu mbalimbali kama vile vituo atamizi, mashamba darasa, semina, kozi fupi, runinga na redio ili kuongeza uzalishaji wenye tija. Aidha, itatoa huduma za ushauri wa kitaalam kuhusu matumizi bora ya ardhi, upimaji na tathmini, usanifu majengo na usimamizi wa ujenzi;

itaimarisha makundi ya kitafiti - Research Clusters na kutoa mafunzo kwa viongozi wa makundi hayo ili kujenga uwezo wa ndani wa kuandaa na kufanya tafiti zenye tija katika kutatua changamoto mbalimbali; na

itatoa tuzo kwa tafiti bora zitakazochapishwa katika majarida yenye hadhi ya juu Kimataifa “High Impact Factor Journals” kwa lengo la kuongeza hamasa ya watafiti.

Mheshimiwa Spika, katika kuzijengea uwezo wa kuandaa na kufanya tafiti zenye tija kwa taasisi zinazoendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu nchini, Serikali itafanya tafiti 34 na kutoa huduma 34 za ushauri elekezi.

TUME YA TAIFA YA UNESCO (FUNGU 18)

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO itaendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Tume kama ifuatavyo:

itaendelea kusimamia utekelezaji wa programu na miradi mbalimbali iliyopitishwa katika mpango wa Tume wa Mwaka 2022 – 2029 katika nyanja za elimu, sayansi, utamaduni, habari na mawasiliano;

itaratibu vikao vya Kamati ya Kitaifa ya kudhibiti matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo;

itakarabati jengo la ofisi la Tume, itaboresha mifumo ya TEHAMA na kununua gari moja na samani za ofisi; na

itafungua ofisi ya Tume mjini Unguja, Zanzibar kwa lengo la kusogeza huduma za Tume katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya Tume unazingatia kanuni, sheria, taratibu na miongozo, Serikali kupitia Tume itatekeleza kazi zifuatazo:

itafuatilia na kutathmini utelekezaji wa mikataba 10 ya Tume iliyoridhiwa pamoja na miradi inayotekelezwa hapa nchini;

itatathmini utekelezaji wa maamuzi ya Kamati ya Urithi

wa Dunia katika maeneo yaliyo katika orodha ya urithi wa dunia ambayo ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, Eneo la Hifadhi la Ngorongoro, Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, Michoro ya Miambani ya Kondoa, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Magofu ya Songo Mnara;

itatathmini ushiriki wa wananchi katika uhifadhi na utalii wa maeneo ya urithi wa dunia na kijiolojia pamoja na kuhamasisha wananchi kuhama kwa hiari kutoka eneo la urithi wa dunia la Hifadhi ya Ngorongoro; na

itapitia sheria na muundo wa Tume kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Tume.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume itaendelea kuratibu maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambayo itakuwa ikifanyika tarehe 7 Julai kila mwaka. Aidha, itaongeza idadi ya Taasisi za Elimu zinazojiunga na Mitandao ya Elimu ya UNESCO (ASPnet, UNESCO Chairs, UNEVOC Networks na UNESCO Global Networks of Learning Cities) kwa lengo la kuongeza maarifa.


SHUKRANI

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Omary Juma Kipanga (Mb), Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa jinsi tunavyofanya kazi vizuri pamoja na mchango wake katika kuandaa wasilisho hili. Katibu Mkuu, Profesa Eliamani Sedoyeka na Naibu Makatibu Wakuu, Profesa James Mdoe na Profesa Carolyne Nombo wameongoza kwa umakini na juhudi kubwa timu ya wakurugenzi, wakuu wa taasisi

na watumishi wote katika kuandaa hotuba hii. Ninawashukuru kwa dhati kwa juhudi hizi na kwa kazi kubwa wanazofanya.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwashukuru Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi, watumishi wa Wizara na Taasisi zake, Walimu, Wanafunzi, na Wadau wote wa Elimu kwa ushirikiano wao. Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Wamiliki na Mameneja wa Shule, Vyuo na Taasisi binafsi ambao wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika kutoa huduma ya elimu nchini.

Mheshimiwa Spika,
nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Rombo kwa kuniamini na kunichagua kuwa mwakilishi wao. Nawaahidi utumishi uliotukuka.

Mheshimiwa Spika,
napenda pia kuwashukuru Washirika wa Maendeleo na Wadau wa Elimu wote ambao wamechangia kufanikisha utekelezaji wa Mipango na Miradi ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Naomba kuwatambua baadhi yao kama ifuatavyo: Serikali za: Algeria, Umoja wa Falme za Kiarabu, Austria, Brazil, Canada, China, Cuba, Finland, Hungary, India, Indonesia, Italia, Israel, Japan, Korea ya Kusini, Marekani, Malaysia, Misri, Morocco, Zimbabwe, Netherland, New Zealand, Norway, Palestina, Romania, Saudi Arabia, Sweden, Thailand, Ufaransa, Urusi, Uswisi, Uingereza, Uholanzi, Ujerumani na Venezuela. Aidha, natambua pia mchango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Spika
, napenda pia kushukuru Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa yaliyochangia kufanikisha miradi na programu za Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo ni pamoja na: Benki ya Dunia, Foreign, Commonwealth and Development


Office (FCDO), Swedish International Development Agency (SIDA), Umoja wa Nchi za Ulaya, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Jumuiya ya Madola, Global Partnership in Education (GPE), United Nations International Children’s Emergency Fund (UNICEF), United Nations Development Programme (UNDP), United Nations Educational, Scientific and Cultural Organization (UNESCO), United States Agency for International Development (USAID), Inter University Council for East Africa (IUCEA), Human Development Innovation Fund (HDIF), Deutscher Akademischer Austauschdienst (DAAD), British Council, Campaign for Female Education (CAMFED), Commonwealth Secretariat, Aga Khan Education Services, Japan International Cooperation Agency (JICA), Karibu Tanzania Organization (KTO), Korea International Cooperation Agency (KOICA), Water Aid, Plan International, Tanzania Education Network/Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Christian Social Services Commission (CSSC), Mo Foundation na Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA).


MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2022/23

Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha utekelezaji wa malengo kwa mwaka wa fedha 2022/23, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Fungu 46) inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,493,004,355,000.00 kwa mchanganuo ufuatao:

Shilingi 533,456,916,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara ambapo Shilingi 500,196,732,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara na Shilingi 33,260,184,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo; na

Shilingi 959,547,439,000.00 zinaombwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 778,083,678,000.00 ni fedha za ndani na Shilingi 181,463,761,000.00 fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya UNESCO (Fungu 18) inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 2,709,163,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida (Mishahara ni Shilingi 1,176,870,000.00 na Matumizi Mengineyo ni Shilingi 1,532,293,000.00).


Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa naomba sasa Bunge lako tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Bajeti ya Fungu 46 na Fungu 18 yenye jumla ya

Shilingi 1,495,713,518,000.00.Mheshimiwa Spika, napenda kuhitimisha kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.


Mheshimiwa Spika, Hotuba hii inapatikana katika tovuti ya Wizara .


Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
 

Attachments

  • HOTUBA YA BAJETI YA WyEST MWAKA 2022-23.pdf
    4.5 MB · Views: 19
Hivi ilikuwaje mwaka huu wanafunzi wa kidato cha sita kusimamiwa mitihani na walimu wa shule za msingi?
 
Professor Mkenda na Ndalichako inatakiwa sasa waweke career advice offices kwenye shule za sekondari na vyuo vikuu kwa sababu zifuatazo:
  • Kuwashauri wanafunzi wa O’level michepuko ya kuchagua A level ili kwa kuangalia future employability chances.
  • Kuwashauri wanafunzi wa A’level kuangalia uhalisia wa job market na kuchagua degree zenye optional ya kujiajiri mara baada ya kuhitimu.
  • Kufundisha module ya entrepreneurship kwa degree za biashara na kilimo; inayo cover mambo ya kuendesha biashara, namna ya kutafuta mitaji, business models, business legal status and so forth with their sector.
Watanzania wengi sana wanaenda shule na kusoma degree au courses ambazo ajira wanategemea serikalini.

Kwenye job market serikali ni mwajiri tu kama ilivyo kwa private, Kwa ivyo serikali ata toa nafasi kutokana na mahitaji yake not otherwise.

Tatizo watanzania wengi sana wamekariri kupata ajira serikalini ni rights yao baada ya kuhitimu, matokeo yake awafikirii degree za kusoma based on research ya job opportunity zilizopo sokoni au chances za kuweza kujiajiri baada ya kuhitimu.

Ni hivi zinahitajika jitihada kubwa sana ya kubadili fikra za watanzania. Wengi wana huu mtazamo life is supposed to be easy there are very few real life hustlers with can do attitude kwenye nchi ambayo bado ina fursa kibao azijatumiwa.

Mtu anaenda shule ajira anategemea serikali, mtu anaanzisha biashara afanye na serikali, mtu anataka utajiri hela za serikali; yaani njia ya kutoka kwenye maisha asilimia kubwa wanafikiria ni kupitia serikali tu.
 
Huyu prof kweli sio chuplichupli km yule mama mtangulizi wake asiyejua inglish
 
Back
Top Bottom