Watoto 300 wanakufa kwa kukosa lishe

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
Watoto 300 walio chini ya miaka mitano nchini hufa kila siku kutokana na magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa lishe na asilimia 42 chini ya umri huo hudumaa kutokana na tatizo hilo, ripoti ya shirika lisilo la kiserikali la Save the Chidren imebainisha.

Kutokana na hali hiyo Profesa Joyce Kinabo toka Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua) aliye kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa ripoti hiyo jijini Dar es Salaam jana, aliiasa jamii kujielimisha na kuanza kutumia vyakula vya asili vyenye lishe vinavyopatikana nchini ili kupunguza tatizo hilo.

Profesa Kinabo alisema katika uzinduzi uliowashirikisha watoto kutoka katika wilaya za Kinondoni na Temeke, jamii ya kitanzania inaweza ikaliondoa tatizo hilo kwa kutumia vyakula vyenye lishe kwa kila mlo visivyokuwa vya gharama na vinavyokidhi viwango vya Dola moja kwa mlo, vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa.

Mmoja wa watoto walioshiriki katika uzinduzi huo, ambaye pia ni Mwenyekiti Msaidizi wa Baraza la Watoto manispaa ya Temeke, Wastara Athumani, aliitaka serikali itenge fedha za kutosha mijini na vijijini kwa ajili ya kuhudumia bajeti ya vyakula mashuleni ili

kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri katika masomo.



CHANZO: NIPASHE
 
Tuenzi vyakula vya asili kulinda watoto wetu


Habari kwamba watoto 300 walio chini ya umri wa miaka mitano nchini hufa kila siku kutokana na magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa lishe na asilimia 42 chini ya umri huo wakidumaa kutokana na tatizo hilo, ni za kusikitisha na ambazo zinahitaji jamii kuchukua hatua za haraka kurekebisha hali hiyo.

Katika habari hizo ambazo ziliripoti shirika lisilo la kiserikali la Save the Chidren na kuchapishwa na gazeti hili toleo la jana, hali hii inaelezwa kujitokeza wakati taifa hili limejaliwa vyakula vingi vya asili ambavyo kama vingelitumika vizuri basi janga hilo lingekuwa ni historia.

Rais Yoweri Museveni mwaka 2002 akihutubia Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu jijini Kampala, alipata kusema kuwa tatizo kubwa la Waafrika ni ulimbukeni katika mambo mengi, mojawapo katika vyakula.

Alisema wakati bara hilo limejaliwa vyakula vingi vya asili, wenyeji wake wamekuwa na juhudi kubwa ya kuviacha na kujikita kula vyakula vya kigeni ambavyo aghalab ni ghali na havitabiriki upatikanaji wake.

Museveni alitolea mfano wa nchi yake ambayo hupata mvua ya kutosha wakati wote kiasi cha kustawisha kwa wingi vyakula hivyo, lakini ni ajabu kusikia watu wakilalamika kuwa hawana chakula. Kwa kifupi dhana ya kukosekana kwa chakula inaweza kuwa ni tatizo la kimtazamo zaidi hasa katika kuiga mambo mapya kutoka nje.

Ukweli huu unaongezewa nguvu na mfumo wa maisha wa watu wa bara la Afrika, hususan Watanzania ambao wengi wanaamini katika kuiga staili ya maisha ya ugaibuni kuwa ni kupiga hatua za maendeleo hata kama ni kujitumbukiza katika mambo ya kuangamiza maisha yao, hususan vyakula vya kuharibu miili.

Ni ukweli usiokuwa na chembe ya shaka kwamba watu wengi wanapoona kipato chao kinaongezeka si tu wanaachana na ulaji wa vyakula vyao vya asili, bali pia wanaingiwa na ulimbukeni kiasi cha kutumia hata hivyo vya kuja kwa kiwango cha kupitiliza kiasi cha kuleta madhara kwenye miili yao.

Kwa mfano, ni vigumu sana kuingia katika maduka makubwa (super market) na kukuta vyakula vya asili vya Kitanzania vikiuzwa; yaani vitu kama magimbi, viazi vikuu, mihogo, mboga za majani za asili kama mchicha pori, ambavyo vinajulikana wazi kuwa vina virutubisho vingi.

Wakazi wengi wa mjini hata wale waliozaliwa vijijini na kuhamia mijini wakiwa watu wazima baada ya kusoma wakiwa vijijini, waingiapo mjini kama walikuwa wanakula viazi vya kuchoma vijijini wakiwa mjini watakula chipsi na kuamini kwamba wanakula kwa afya zao, wapo

waliokuwa wanakula ugali wa dona kijijini, lakini wakishaingia mjini na kipato kuongezeka wanaamini kwamba ugali mzuri ni ule wa sembe, yaani mahindi yanakobolewa kwanza kisha yanasagwa!

Tunataja mifano hii kuthibitisha kwamba tuna tatizo la kutambua uzuri wa vyakula vya asili, ambavyo kwanza ni rahisi kustawi katika mazingira yetu, pili vina virutubisho vingi na tatu ni rahisi kulisha watu wetu kwa sababu upatikanaji wake ni wa uhakika zaidi.

Kama kila mmoja wetu akiamua kuenzi na kukuza vyakula vya asili, hakika tunaweza kama taifa kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa chakula kwa watoto wetu, hivyo kupunguza idadi ya vifo kama vinavyotokea kwa sasa.

Zipo baadhi ya nchi za Kiafrika watu wake wanaenzi sana tamaduni zao, miongoni mwazo ni za Afrika Magharibi, pamoja na ukweli kwamba walitawaliwa kama sisi, lakini bado wameendelea kung’ang’ania tamaduni zao kwa kiwango kikubwa, eneo mojawapo wanaloonyesha mfano wa kuigwa ni kwenye vyakula. Hawa wanakula vyakula vya kwao, wakiwa ndani ya nchi zao na hata wakiwa ughaibuni. Wanaenzi vyao.

Tabia ya namna hiyo si tu inakuza utamaduni wao, bali pia inasaidia kujitegemea kwa chakula, kwa kustawisha na kula vyakula vyao vya asili. Ni dhahiri kama tukiongeza nguvu kulima na kutumia vyakula vya asili kama taifa tunaweza sana kupunguza madhara kama haya ya

watoto wetu kwa mamia kupoteza maisha kwa sababu tu ya lishe duni.
Mahatma Gandhi alipata kusema, yuko tayari kufungua milango na madirisha yake upepo wa tamaduni zote uingie kwake, lakini hayuko tayari kupeperushwa na tamaduni hizo. Ni vema tukubali sasa kusimika miguu yetu chini na kuenzi vya kwetu.

CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom