Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imewakumbusha wateja juu ya umuhimu wa kuzingatia zoezi la usomaji na uhakiki wa mita mara baada ya kupokea ujumbe wa usomaji mita kwenye simu zao ili kuongeza uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma.
Zoezi la usomaji mita limeanza leo, Machi 10,2026 na linaendelea kwenye maeneo mbalimbali ya Kihuduma ya DAWASA ikiwemo Ilala, ikiwa ni utaratibu wa Mamlaka wa kuongeza wigo wa huduma.
Afisa Ankara DAWASA Ilala, Ndugu Magreth Anyimike amesema ni muhimu Wananchi na hususani Wateja wenye Dira za Maji za DAWASA kushiriki usomaji na uhakiki wa mita pamoja na kutoa taarifa ili kuzuia changamoto za ankara ya maji.
“DAWASA inaendelea kuimarisha huduma zake kwa kuhakikisha wateja wanapata bili kulingana na matumizi yao, wanahimizwa kutoa ushirikiano kwa wafanyakazi ili kuboresha utendaji kazi” alisisitiza Magreth
Zoezi la usomaji wa mita za maji hufanyika tarehe 10 hadi 15 ya kila Mwezi katika maeneo ya Kihuduma DAWASA.
Wananchi wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hili ili kubaini matumizi yao ya maji, pamoja na kutoa taarifa kupitia namba ya Huduma kwa Wateja 181 (Bure) ili kupata ufafanuzi wa matumizi yako ya maji kabla ya bili kamili.