real G
JF-Expert Member
- Feb 7, 2013
- 5,227
- 5,292
Serikali ya Kenya imefichua kwamba imewakamata raia wanane wa Tanzania waliokuwa katika harakati za kujiunga na kundi la wapiganaji la al-Shabab nchini Somalia.
Katika taarifa iliotumwa katika vyombo vya habari, polisi wanasema raia hao waliokamatwa katika kipindi cha miezi miwili iliopita walikiri kuwa mbioni kujiunga na kundi hilo la ugaidi.
Hatua hiyo inajiri siku chache baada ya kundi la watu wanaojidai kuwa wapiganaji wa Kiislamu kuweka video mtandaoni likidai uwepo wa wapiganaji wa Kiislamu nchini Tanzania
Video hiyo iliwaonyesha wanaume hao wakiwa wamejifunika nyuso zao kwa vitambaa na barakoa.
Wanadai wamo katika mji wa Tanga na kuwahimiza Waislamu katika taifa hilo la Afrika Mashariki kujiunga na kampeni yao.
Polisi wa Kenya pia wanasema wamefanikiwa kutibua njama ya wanachama wa kundi linalojiita Islamic State ya kutekeleza mashambulio nchini humo na kuwakamata washukiwa wawili.
Wawili hao Kiguzo Mwangolo Mgutu na Abubakar Jillo Mohammed walipewa mafunzo ya kuwa na itikadi kali kabla ya kuingizwa katika kundi la IS na Mohammed Ali aliyekamatwa awali na ambaye anasaidia polisi na uchunguzi, polisi wamesema.
Kulingana na taarifa hiyo, kufuatia kukamatwa kwa Mohammed Ali, wafuasi wake wamekuwa wakipanga kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi sana wakilenga sekta ya uchukuzi wa abiria.
Kukamatwa kwa wawili hao, kumezuia kutokea kwa mashambulio katika miji ya Nairobi na Mombasa.
Chanzo: BBC