Wasichana waliokatishwa masomo: Prof. Sigalla Vs DC Mtanda

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Tofauti Ya Mtazamo, Upi Ni Sahihi?

Profesa Norman Sigalla Vs DC Said Mtanda

Ndugu zangu,

Profesa Norman Sigalla akichangia hoja Bungeni jana amekuja na mtazamo huo pichani. Wakati DC Said Mtanda wa Nkasi, Rukwa ameripotiwa gazetini leo akitoa mtazamo huo, pichani.

Nionavyo kama Mwenyekiti wa Jukwaa hili;

Wakati hakuna tafiti zenye kuonyesha tatizo analoliona Profesa, kuna tafiti nyingi zenye kuonyesha, kuwa wasichana waliopewa nafasi ya pili maishani, baada ya kupata uja uzito, wameweza kufanya vema na kuendelea kuwa raia wema na wenye kushiriki ujenzi wa uchumi wa jamii wanazoishi, ikiwamo kustawisha vema familia zao hususan malezi ya watoto.

Wengine wameweza hata kushika nafasi za uongozi. Kimsingi hakuna tafiti za kisayansi zenye kuonyesha kuwa mimba zimeongezeka kwenye jamii ambazo zimewapa raia wake waliopata uja uzito wakiwa shuleni nafasi ya kuendelea na masomo. Angalia mfano wa Zanzibar.

Profesa Sigalla anapaswa pia kuelewa, kuwa kumpa nafasi mtoto wa kike kuendelea na masomo hata baada ya kupata kupata uja uzito kwa sababu mbali mbali ikiwamo umasikini na ukatili wa kijinsia ni suala la HAKI.

Hapa Profesa Sigalla anapaswa kukumbushwa, kuwa Serikali imesaini utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu kidunia. Haya ni maazimio ya Umoja Wa Mataifa na sisi kama nchi wanachama.

Sasa basi, lengo nambari 4 la Maendeleo Endelevu linahusu :

"Kuhakikisha Elimu Bora, na yenye Usawa kwa Wote na Kutoa
Fursa kwa Wote Kujiendeleza."

Hilo si Azimio la Mwenyekiti wa mjadala huu, Mjengwablog - Habari, Picha na Matukio ni la Umoja wa Mataifa ambapo sisi kama nchi sio tu tumeridhia kwa kutia saini, bali tumeanza Utekelezaji wake si kwa kulazamishwa, bali kwa kutambua tuna wajibu huo kwa vile, kama taifa, changamoto hiyo tunayo.

Kamwe hatuwezi kujifanya mbuni kwa kuviingiza vichwa vyetu mchangani huku tumeacha viwiliwili vyetu vinaonekana. Na njia nyepesi ya wenye kuchagua njia hii ni kukimbilia kwenye mila na desturi, na wakati mwingine imani za dini. Tunayafanya hayo kiunafiki na kwa kuangalia faida za kisiasa huku bila huruma, tukiwaangalia wasichana wetu, wengi wao wa familia za kimasikini, wakizama kwenye lindi la umasikini linalochangiwa na kunyimwa fursa ya kuendelea na elimu hata baada ya kufanyiwa matendo maovu ikiwamo ubakaji. Ni masikini hawa, tofauti na wasichana kutoka familia zenye uwezo, hawana namna ya kuzitoa mimba hizo.

Naliongea hili nikiwa pia na mfano hai kutoka familia yangu. Dada yangu wa tumbo moja alikatishwa masomo akiwa darasa la sita kwa uja uzito.

Miaka hiyo ya 90 kulikuwa na kituo cha UMATI kule Temeke kilichowasaidia wasichana waliokatishwa masomo kwa uja uzito. Sikuwa na taarifa juu ya kituo hicho. Siku moja, miaka ile ya 90 mwanzoni nikiwa nje Wizara ya jengo la wizara ya Elimu, nikakutana na aliyekuwa Mwalimu wangu wa Darasa na wa somo la Bilogy, Mama Betty Nalingigwa, huyu ndiye aliponiambia kuwa anaratibu kituo hicho ndipo nilipomwelezea kilichomkuta dada yangu.

Basi, akaniambia nimpeleke akajisajili. Nikafanya hivyo, akamaliza darasa la saba na akaendelea na masomo ya Sekondari. Leo ameajriwa na anajitegemea. Sijui ingekuwaje kwake kama angeishia darasa la sita. Bila shaka, kuna wengine ambao hili la wasichana wanaokatishwa masomo linawahusu pia, kwamba kuna ndugu au jamaa, au hata mtoto wa jirani aliyeathirika na tatizo hilo. Profesa Sigalla naye anaweza kuwa mmoja wapo.

Na ukweli si kwamba watoto wa kike wa wazazi wenye uwezo huwa hawapati uja uzito wakiwa shuleni, lakini, mara nyingi hata wazazi wao wa kiume huwa hawajui. Yote humalizwa na wazazi wa kike. Mimba hizo hutolewa kwa gharama za fedha na watasoma na watafika vyuo vikuu. Tuache kuwa wanafiki na kufanya dhihaka kwenye mateso ya wanyonge wasio na uwezo na wenye kuathirika na mifumo yetu kandamizi ya hata mahusiano ya kijamii.

Nyongeza kwa Profesa wangu Sigalla, ni kumwambia , kuwa asome pia lengo nambari 5 la Maendeleo Endelevu lenye kutamka;"

Kuwepo na Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake
na Wasichana Wote ."

Hivyo, Profesa wangu Sigalla, Haki ya msichana huyu aliyekatishwa masomo kutokana na uja uzito inasisitizwa itolewe hata kwenye malengo mawili ya Maendeleo Endelevu yenye kufuatana kati ya malengo 16.

DC Said Mtanda katika hili, ameliona tatizo pia, kuwa kama zitaendelewa kukaliwa polisi na kutofikishwa mahakamani, kesi za wenye kutenda matendo ya kupelekea mimba kwa wasichana wetu na mara nyingi ni ubakaji na kuwarubuni wasichana na hata other forms za sex abuse, ndipo hapo inapotokea hatari zaidi.

Na hapa ni ukweli wasichana wetu mashuleni wanaendelea kufanyiwa matendo yenye kupelekea mimba huku tukiwanyima haki yao ya kuendelea na masomo. DC Said Mtanda ameona mbali katika hili. Kama Mwenyekiti wa mjadala, nampongeza.

Nakaribisha michango ya wajumbe.

Maggid Mjengwa.
0754 678 252/ 0688 37 36 52
 

Attachments

  • 4.jpg
    4.jpg
    28.2 KB · Views: 29
  • 2.jpg
    2.jpg
    25.9 KB · Views: 29
Yote kwa yote tuangalie uwezekano wa kuondoa hili tatizo ktk jamii yetu, tunapo wapa nafasi ya pili wahanga wa janga hili kurudi shule inaweza kuwa ni kichocheo zaidi cha mimba kuongezeka endapo hatuta kuwa na njia bora na sahihi ktk hili.
 
Back
Top Bottom