Warioba ahofia mpasuko wa umoja Tanzania | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Warioba ahofia mpasuko wa umoja Tanzania

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Josh Michael, Sep 30, 2009.

 1. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #1
  Sep 30, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  WAZIRI mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba ametahadharisha kuwa nchi inaelekea kubaya anapoangalia jinsi mambo mbalimbali yanavyoendeshwa, huku akisema kuwa serikali haitaweza kushinda vita dhidi ya rushwa iwapo haitaelekeza nguvu zake katika kupambana na mfumo unaolea tatizo hilo.

  Warioba, ambaye alishika nafasi hiyo ya mtendaji mkuu wa serikali kwenye miaka ya themanini, alisema kwa sasa taifa linakabiliwa na matatizo mengi kuanzia ya ukosefu wa maadili ya uongozi, rushwa na hata utaratibu mzima wa kuendesha mambo na kubainisha kuwa kuna pengo kubwa katika kuaminika kwa serikali.

  �Naanza kuwa na wasiwasi na tunakokwenda kama umoja wetu utadumu,� alisema Warioba wakati alipozungumza na waandishi ofisini kwake jana.

  Jaji Warioba alisema hivi sasa kuna dalili ya umoja wa Watanzania kusambaratishwa, watu kugawanywa makundi kwa udini na ukabila pamoja kuwepo kwa matabaka ya matajiri na masikini.

  �Uongozi hivi sasa uko karibu sana na matajiri kuliko wananchi; kwa sasa matajiri ndio wenye sauti," alisema.

  Jaji Warioba alisema anaogopa kuona sasa wananchi wanaanza kutumia nguvu ya umma, badala ya kufuata utaratibu wa kawaida wa ngazi za uongozi za serikali.

  �Kuna maandamano ya kila aina, watu wanavuka ngazi za uongozi katika maeneo yao wanakwenda moja kwa moja kwa waziri mkuu; wananchi wanavamia ardhi, wanaona wafanye mambo yao kwa utaratibu wao; tusipoangalia tutakuta kuna utawala wa nchi lakini watu wanafanya mambo yao kwa mtindo wao. Hii inaonyesha kwamba kuna �credibility gap� (kutokuwepo kwa kuaminika kwa serikali),� alisema.

  Warioba, ambaye aliongoza tume iliyoundwa na Rais Benjamin Mkapa kuangalia mianya ya rushwa kisheria na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kuiondoa, pia alizungumzia vita inayoendelea dhidi ya ufisadi, akisema haoni kama serikali inaweza kushinda.

  Warioba alisema vita iliyopo hivi sasa ni ya kupambana na rushwa yenyewe badala ya kupambana na mfumo. Alisema vita hiyo itafanikiwa kama nchi itafanya jitihada za kuondoa mfumo mzima wa rushwa.

  Tayari mawaziri wawili wa zamani, katibu wa wizara, balozi, maofisa waandamizi wa Benki Kuu (BoT) na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma mbalimbali, zikiwemo za kutumia vibaya ofisi, kushiriki kula njama, uzembe na wizi wa fedha za umma.

  Kuhusu ushughulikiaji wa matatizo makubwa yanayoikumba jamii, Jaji Warioba alisema mtindo uliozuka wa kuunda tume katika kufuatilia mambo ya kisheria haufai kwa kuwa utaratibu huo hautoi uhakika wa kupata mafanikio kwa kuwa tume nyingi zinakuwa na msukumo wa kisiasa.

  �Kesi zilizoundiwa tume na baadaye kupelekwa mahakamani, sina uhakika kama zimefuata utaratibu wa kisheria," alisema mwanasheria huyo na baadaye kutoa mfano wa jinsi kesi ya mauaji dhidi ya mkuu wa zamani wa upelelezi mkoani Dar es salaam, Abdallah Zombe ilivyoshughulikiwa.

  �Wapelelezi wanapewa muda... ingawa Tume ya Jaji Kipenka, kwa mfano, iliridhika kuwa kweli kuna watu waliouawa, lakini kwa kuwa kesi ile ilipelekwa mahakamani kwa msukumo wa kisiasa, ni wazi kuwa lazima makosa ya kisheria yajitokeze.�

  Katika kesi hiyo ambayo Zombe na wenzake walishtakiwa kwa tuhuma za kuua wafanyabiashara watatu wa Morogoro na dereva mmoja wa Dar es salaam, washtakiwa waliachiwa huru na mahakama baada ya kuonekana kuwa hawakushiriki kwenye mauaji, licha ya Mahakama Kuu kuridhika kuwa watu hao wanne waliuawa.

  Jaji Warioba pia alizungumzia kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kutangaza kuwa kuna kesi tatu kubwa za rushwa ambazo zitafikishwa mahakamani wakati wowote, akisema inaonyesha kuwa rais anashirikishwa kwenye mambo ambayo yanashughulikiwa na vyombo vyake.

  �Naogopa sana wanapomhusisha rais kwenye masuala ya kesi. Si vyema kumhusisha rais katika hatua za mwanzo, siyo mahala pake,� alisema Warioba.

  �Hata katika kesi za EPA walimshauri rais awaambie waliochukua fedha wazirudishe. Wako waliorudisha na wako waliofikishwa mahakamani. Sasa hapa tunachanganya mambo; sijui itakuwaje mahakama ikiamua kuwa wale waliorudisha fedha hawana kesi ya kujibu. Hawa hawa wanaomshauri rais, watamruka,� alisema Warioba.

  Alisema kwa mtazamo wake hapo pia pana tatizo la kutoaminika kwa serikali sababu wengine waliorudisha fedha wamepelekwa mahakamani na wengine hawajapelekwa.

  Kuhusu viongozi kupishana kauli, Warioba alisema kuwa hapo pia panaonyesha ukosefu wa kuaminika katika uongozi kwa kuwa
  leo linasemwa hili, kesho linasemwa jingine tena mara nyingine na kiongozi yule yule na kujihoji �mimi sasa sijui niamini kipi.�

  Warioba alisema kuwa ndani ya jamii kuna mambo mengi ya kuchunguzwa na kama kiongozi asipoyatolea ufafanuzi wa kuridhisha hali ya kuaminika inashuka.

  Kuhusu makundi ndani ya vyama vya siasa, Jaji Warioba alisema hali hiyo ndiyo inayowagawa wananchi na kwamba inasikitisha kuona sasa kila kundi linalotaka uongozi hutengeneza mtandao wake ambapo alionya kuwa kwa hali hiyo mwisho wa siku lazima kutakuwa na mgawanyiko mkubwa.

  Alitolea mfano wa mgawanyiko ndani ya CCM na kusema kwa kuwa ni chama kilichopo madarakani kwa muda mrefu (incumbent), lakini migogoro ndani yake huliathiri taifa.

  �Mgawanyiko ndani ya CCM maana yake ni mgawanyiko wa nchi kwa sababu CCM ina ushawishi mkubwa,� alisema.

  Jaji Warioba pia aliweka bayana kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), haziwezi kufanya kazi katika mazingira ya haki kwa sababu haziko huru kwa maana katika utendaji vinaagizwa zaidi na serikali.

  Takukuru imeongezewa nguvu na serikali baada ya kufanyiwa marekebisho sheria ya rushwa ambayo awali ilikuwa na makosa manne tu na sasa yamefikia 16, huku chombo hicho kikipewa madaraka ya kushitaki watuhumiwa.

  Akizungumzia udini na ukabila vinavyotishia kuwagawa wananchi, Jaji Warioba alisema kuwa zamani ukabila ulikuwa ni utani tu, lakini hivi sasa watu wanatazamana kikanda na kikabila badala ya kitaifa.

  Kuhusu dini alisema: �Haya mambo ya (Jumuiya ya Nchi za Kiislam) OIC yaliibuka tangu mwaka 1993, lakini msingi wa mjadala wa OIC haukuwa wa udini, ulikuwa wa utaifa. Tulikataa Zanzibar kuingia OIC peke yake na tuliridhia kuangalia kama kuna faida kwa nchi kuingia OIC.�

  Jaji Warioba alisema anashangaa kuona kuwa hivi sasa suala la OIC likizungumzwa bungeni linawagawa wabunge kwa misingi ya dini zao, hali kadhalika suala la Mahakama ya Kadhi.

  Jaji Warioba pia alisema haoni msingi wa tatizo la waraka wa Kanisa Katoliki kwa sababu kanisa hilo limekuwa likitoa nyaraka kila wakati uchaguzi unapokaribia, ikiwa ni elimu ya uraia tu.
  �Sasa hili suala la kusema nchi hii itageuka kama Lebanon liinatoka wapi?� Warioba alihoji.

   
Loading...