Waraka wa UDASA kwa watanzania kuhusu huduma nchini

George Kahangwa

JF-Expert Member
Oct 18, 2007
547
148
WARAKA WA UDASA KWA WATANZANIA:

HAJA YA KUBORESHA UTOAJI WA HUDUMA KATIKA NYANJA MBALIMBALI NCHINI

Machi 2017

Miaka ya hivi karibuni imeshuhudia ongezeko kubwa la mchango wa sekta ya huduma (inayojumuisha biashara, usafirishaji, malazi, mawasiliano, fedha, elimu na afya) katika kuimarika kwa uchumi wa nchi mbalimbali duniani. Aidha uchumi wa kisasa unaendelea kuhama kutoka sekta zinazotegemea stadi za misuri (hard skills) kuelekea katika kutegemea zaidi stadi laini (soft skills) kama vile umahili wa kuwasiliana, ubunifu, utatuzi wa matatizo na kadhalika. Stadi laini hizo zinatumika zaidi katika huduma.

Wakati hayo yakijiri, mchango wa sekta ya huduma katika uchumi wa Tanzania, japo ni mkubwa kuliko sekta nyinginezo, unaendelea kuwa usioridhisha, na kwa hakika huduma zitolewazo nchini,katika nyanja mbalimbali ni za kiwango duni sana.

UDASA tumeona haja ya kuwasiliana na watanzania katika ujumbe tunaoutoa leo, ili pamoja na kuwafahamisha watanzania kwamba hali ya utoaji huduma nchini inaathiri vibaya ukuaji na maendeleo ya kiuchumi ya Taifa hili, tuwaoneshe pia haja ya kubadilisha utamaduni na mazoea tuliyonayo (wananchi) katika utoaji wa huduma mbalimbali.

Hapa nchini na kwingineko, sekta takribani zote za kiuchumi zina sehemu inayohusiana moja kwa moja na kuwahudumia watu, wateja au walaji. Zipo huduma katika sekta za Elimu, Afya, Usafirishaji, Mawasiliano, uuzaji bidhaa mbalimbali, burudani, ushauri, utalii, fedha, malazi, upangishaji majumba, ulinzi na usalama.

Hata hivyo, katika taaluma ya uchumi sekta ya huduma imetenganishwa kwa namna fulani na sekta nyinginezo (ingawa utoaji huduma ni jambo mtambuka). Hii ni kwa sababu uchumi wa huduma ni uchumi wa ngazi ya juu (ya tatu), ambapo chini yake kuna uchumi wa viwanda (ngazi ya pili), na kilimo cha asili (ngazi ya chini zaidi – ya kwanza). Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa sekta ya huduma nchini inachangia zaidi ya asilimia 40 katika pato la taifa. Ilichangia 43.6% (2009), 43.9% (2010), 40.9% (2014), 40.0 (2015):

Upo uwezekano mkubwa kwamba huduma zingeweza kuchangia zaidi katika uchumi wa taifa, na katika pato la mtu mmoja mmoja, endapo utoaji wa huduma nchini usingekuwa unakabiliwa na mapungufu na matatizo lukuki. Baadhi ya matatizo hayo tunayabainisha katika ujumbe huu.

Taasisi nyingi nchini, ndogo na kubwa zinakabiliwa na tatizo la mapokezi mabovu kwa watu wanaofika katika taasisi hizo kwa ajili ya kuhudumiwa. Watafuta-huduma katika taasisi hizo, hufika ili wahudumiwe lakini mara nyingi hukosa kupokelewa kwa ukarimu na bashasha na hata kutopatiwa maelezo ya namna gani au mahali gani waelekee ndani ya taasisi husika ili wapate huduma waliyoifuata. Tatizo hili linaonekana sana katika ofisi za umma na biashara.

Vilevile, kumekuwa na tatizo la ucheleweshwaji wakati wa kuhudumiwa. Hili linajitokeza kwa sura nyingi, kuanzia uwepo wa foleni ndefu za wateja ilihali huduma inatolewa polepole sana, upangiwaji wa tarehe nyingine ya mbali, ilihali anachokitaka mteja anaweza kukipata ndani ya muda mfupi, kupoteza muda katika kutayarisha na kukabidhi bidhaa anazohitaji mteja, na kutojibu haraka maulizo ya wateja. Tatizo hili linaonekana katika mighahawa, mabenki, ofisi za umma na kwingine.

Aidha, watoa huduma wengi huwahudumia watu katika namna ambayo hafikii matarajio ya wahudumiwa, yaani huduma mbovu isiyomridhisha mteja.

Katika huduma pia kuna tatizo la ulaghai. Wahudumu wengi huwadanganya wateja kwa namna mbalimbali. Mathalani, kuwaambia wateja kwamba huduma fulani wanaiweza kumbe siyo. Wengine husema huduma fulani ina faida kadha wa kadha, kumbe uongo. Wapo watanzania wanaotoa huduma za uongo katika tiba, katika ufundi wa kutengeneza vitu mbalimbali na kadhalika .

Huduma nchini Tanzania zinatatizwa pia na kukithiri kwa uwepo sokoni bidhaa hafifu, feki na zilizochakachuliwa. Kwa sasa, imekuwa kana kwamba ni jambo la kawaida na halali mhudumu kumwambia mteja achague kati ya bidhaa halisi na bidhaa feki. Tatizo hili linaonekana zaidi katika biashara madukani na barabarani kwa (wamachinga). Miaka ya karibuni kwa mfano, tumeshuhudia pia huduma mbaya kupitia uchakachuliwaji wa mafuta ya Petroli na Diseli katika vituo vya mafuta.

Sanjari na bidhaa hafifu, katika huduma kuna tatizo la wizi. Wizi huu hujitokeza kwa mfano, mhudumu anapotoa chenji pungufu kwa mteja, bidhaa zenye ujazo pungufu, bidhaa isiyokuwa sawa na aliyohitaji mteja, na kuuza bidhaa kwa bei isiyokuwa sahihi. Wizi na udanganyifu umejitokeza pia katika tabia ya watoa huduma kuwaambia wateja wachague bei ya bidhaa pamoja na kodi au bei isiyoambatana na kodi (almaarufu VAT).

Mbali na wizi, watoa huduma wengi hawana weledi wa kazi wanazozifanya au kwa makusudi wamepuuza kanuni za weledi husika (professionalism). Hili linachagizwa zaidi na tabia ya waajiri kuwapatia kazi watu wasio na taaluma husika, hususan ili waweze kuwalipa ujira kidogo. Aidha, kupuuza weledi kunachangiwa na tabia za wahudumu kujali wananufaikaje zaidi na huduma wanayoitoa ilihali wakipuuza maslahi ya wateja wao.

Shida nyingine iliyomo katika huduma zitolewazo na watanzania ni upendeleo. Baadhi ya watoa huduma hupendelea wateja fulani, wakawapuuza akina fulani na hata kuwabagua wengine kwa misingi ya kujuana, vyeo vya mamlaka, undugu, nasaba na kabila. Mtoa huduma mwenye upendeleo hujitia hasara yeye mwenyewe kwa kujipunguzia wahudumiwa na kwa kuwa mkengeufu wa maadili. Upendeleo hujitokeza pia kwa waajiri wakati wa kuajiri watoa-huduma husika. Tatizo hili lipo katika pande zote mbili za kisekta, sekta ya umma na ya binafsi.

Wakati mwingine tatizo linalijitokeza katika utoaji huduma ni vitendo vya wanaohudumia kutowajali wateja wao. Hutokea pia kwamba, hata wasimamizi wa kazi nao hawajali kama mtu kahudumiwa ipasavyo au kinyume chake. Watoa huduma wa namna hii hupuuza thamani ya wateja wao na hudhalilisha dhamana walizopewa. Watoa huduma wengine mara kwa mara hutumia kauli mbaya, majibu ya dharau na matusi katika kuwasiliana na wanaowahudumia. Haya yanatokea katika mawasiliano ya uso kwa uso na hata katika mawasiliano kwa njia ya simu.

Tatizo jingine ni umangimeza, unaoambatana na uwepo wa mlolongo mrefu sana wa taratibu, nyingi zikiwa hazina ulazima wa kuwepo. Umangimeza huu upo kwa wingi katika taasisi za umma. Umekuwa chanzo cha watu kuhairisha kufanya jambo wanalokuwa wamekusudia kulifanya (Mathalani manunuzi au safari), na umechochea sana utoaji wa rushwa na takrima.

Aidha taasisi nyingine zinatoa huduma mbovu kwa sababu ya uduni, uchakavu na ubovu wa vifaa vya kazi wanavyovitumia.

Kimsingi matatizo yote haya husababisha hasara ya kukosekana kwa wateja wanaofika kuhudumiwa katika taasisi husika, au hata wakifika (kwa sababu ya kukosa mbadala) huendelea kuichukia taasisi yenyewe na wafanyakazi wake.

Hata hivyo, matatizo yote yakiyomo katika sekta ya huduma nchini yanatatulika. Tunachohitaji ni nia ya dhati ya kuyaondoa kwa kuchukua hatua stahiki.

UDASA tunatoa wito kwa waajiri wote wa watoa-huduma nchini; kwamba wahakikishe waajiriwa wao wameelimishwa na kufunzwa vilivyo namna bora ya utoaji wa huduma. Mafunzo ya watarajari na mafunzo kazini yahusuyo namna ya kuwajali wateja (customer care) yatolewe mahali popote penye huduma.

Kadhalika, wanaojiajiri wote, yaani wanaoendesha shughuli au biashara zao binafsi zinazohusiana na utoaji huduma licha ya kujifunza ‘customer care’ watambue na kuzingatia kuwa, kuwahudumia vizuri wateja wao ni jambo litakalowahakikishia tija, ufanisi na ukuaji wa biashara husika na hatimaye ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia sekta ya huduma.

Waajiriwa nao hawana budi kuheshimu kazi zao na kuongeza utumiaji wa weledi katika kazi hizo. Wafahamu kwamba kuwa na majivuno katika nafasi wanazozishikiria, au kuwa na kiburi kwasababu ya vyeo walivyonavyo kazini huleta hasara mahali pa kazi. Bali kuwahudumia watu kwa ukarimu, heshima na ufasaha huleta faida kwa ofisi husika na humsaidia hata anayehudumia kukuza mtaji wake wa kijamii.


Umetolewa na,

clip_image005.jpg


Dkt. George Leonard Kahangwa

Mwenyekiti wa UDASA
 
Hawa udasa hawaoni mjadala wa kitaifa ni kudai vyeti vya Bashite!
Tuwekewe vyeti vya Daudi Bashite hapa! Mengine baadaye,
 
Customer care ni tatizo kwa nchi nzima. Ubora wa huduma kwa ujumla ni tatizo pia. Hapo UDSM tu kuna huduma bora? Je wanafunzi wanapata huduma nzuri? Pale cafteria huduma zao zimekuwa nzuri siku hizi?

Hivi hata vitu vidogo kama usafi wa vyoo tu bado imekuwa ni tatizo, hadi imekuwa kama ni moja ya sifa za UDSM. Vyoo vichafuuuuu kila mahali kuanzia CoET mpaka sijui CoHU COSS nk.
 
George Kahangwa asante sana kwa bandiko lako zuri na kutuonyesha mtazamo wa UDASA kwenye ishu ya utoaji huduma kwa watanzania.

mie nina vitu vitatu vikubwa ambavyo nataka niwaulize nyie kama UDASA.

1) je ivi kweli kwa Tanzania kuna standards ambazo yapaswa watoa huduma wafikie ama kila mtu anatakiwa tuu afanye kwa kiwango chake? kama hakuna je nyie kama wataaluma ambao mnaelimisha katika ngazi kubwa zaidi wale watoa huduma wetu mnalifikiriaje hilo kulirasimisha?

2) Hivi George umeiona hali ya chuo kikuu kwasasa? jamani umepita hii njia toka coet adi huko education? umeona hali ya uchafu ilivyo na uchakavu wa majengo? je udasa imeona uvujaji wa majengo? na uchafu je? apa science jee?? jamani hiki ni chuo ama nyumba za magofu ya mashambani? ni huduma gani kweli inayotolewa kwenye hali kama hii? huyo mwenye tenda ya kusafisha je anajua kuwa hata majani yanayoota kwenye pavements anatakaiwa ayaondoe?

3) kabla hata ya kuwasema watoa huduma je mmejitathmini katika ngazi ya serikali kwenye nini malengo yao? Hivi UDASA mko kuelimisha watu jinsi ya kutoa huduma ama pia kusaidia serikali iweze kutenda yaipasayo kutenda kwa kuwapa taarifa pevu, na mbinu nzuri na kushauri kwa kina juu ya uendeshaji wa shughuli zake? leo hii unaongelea utoaji mbovu wa huduma mbon hatujaona mjadala ama tamko mkiongelea kuhusu uwepo wa idadi kubwa ya wahitimu mtaani ambao wangeweza kutumika kulijenga taifa? leo hii wahitimu wa toka 2015 wako mtaani, watu hawa hawakopesheki manake hawajaajiriwa na mbaya zaid wana mikopo imesimama ambayo wanatakiwa wailipe hawana mbinu za kulipia. vijana hawa wamekuwa desperate ndio wanaoongoza kulala na ndoto kwa kumlipa muhindi 500 aamke na milioni. kubet ndio kazi waifanyayo, na kutizama mechi tuuu. Hivi haya mmeyafumbia macho kweli?
 
George Kahangwa asante sana kwa bandiko lako zuri na kutuonyesha mtazamo wa UDASA kwenye ishu ya utoaji huduma kwa watanzania.

mie nina vitu vitatu vikubwa ambavyo nataka niwaulize nyie kama UDASA.

1) je ivi kweli kwa Tanzania kuna standards ambazo yapaswa watoa huduma wafikie ama kila mtu anatakiwa tuu afanye kwa kiwango chake? kama hakuna je nyie kama wataaluma ambao mnaelimisha katika ngazi kubwa zaidi wale watoa huduma wetu mnalifikiriaje hilo kulirasimisha?

2) Hivi George umeiona hali ya chuo kikuu kwasasa? jamani umepita hii njia toka coet adi huko education? umeona hali ya uchafu ilivyo na uchakavu wa majengo? je udasa imeona uvujaji wa majengo? na uchafu je? apa science jee?? jamani hiki ni chuo ama nyumba za magofu ya mashambani? ni huduma gani kweli inayotolewa kwenye hali kama hii? huyo mwenye tenda ya kusafisha je anajua kuwa hata majani yanayoota kwenye pavements anatakaiwa ayaondoe?

3) kabla hata ya kuwasema watoa huduma je mmejitathmini katika ngazi ya serikali kwenye nini malengo yao? Hivi UDASA mko kuelimisha watu jinsi ya kutoa huduma ama pia kusaidia serikali iweze kutenda yaipasayo kutenda kwa kuwapa taarifa pevu, na mbinu nzuri na kushauri kwa kina juu ya uendeshaji wa shughuli zake? leo hii unaongelea utoaji mbovu wa huduma mbon hatujaona mjadala ama tamko mkiongelea kuhusu uwepo wa idadi kubwa ya wahitimu mtaani ambao wangeweza kutumika kulijenga taifa? leo hii wahitimu wa toka 2015 wako mtaani, watu hawa hawakopesheki manake hawajaajiriwa na mbaya zaid wana mikopo imesimama ambayo wanatakiwa wailipe hawana mbinu za kulipia. vijana hawa wamekuwa desperate ndio wanaoongoza kulala na ndoto kwa kumlipa muhindi 500 aamke na milioni. kubet ndio kazi waifanyayo, na kutizama mechi tuuu. Hivi haya mmeyafumbia macho kweli?

Gfsonwin na wote mliochangia kwa kusoma na au kuandika maoni,
Awali ya yote, ahsanteni sana.
Nijibu tu kwa ufupi kwa sasa kuwa, hatupuuzi kwamba huduma zitolewazo UDSM na au chuo kikuu kingine chochote nazo zina mapungufu. Kimsingi ujumbe wetu ni kwa watoa huduma wote; Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kikiwemo.

Aidha, masuala ambayo hatujayagusia kwa sasa, haina maana kwamba hatutayazungumzia. Utaratibu wetu wa kutoa nyaraka ni endelevu, na wala yasiwepo mawazo kwamba tulichoanza nacho ndio kipaumbele namba moja.
Maswali yaliyoulizwa katika maoni yenu tutayajibu katika matamko na nyaraka zetu zitakazofuata.
George
 
Back
Top Bottom