Waraka wa MTOI kwa mama Maria Nyerere | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Waraka wa MTOI kwa mama Maria Nyerere

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Reyes, Sep 4, 2010.

 1. R

  Reyes Senior Member

  #1
  Sep 4, 2010
  Joined: Sep 1, 2010
  Messages: 188
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Kwa mpendwa Mama Maria (Mama wa Taifa ), Natumaini yubuheri wa afya hasa baada ya kukuona amemsindikiza mgombea uraisi kwa tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM) chama alichokiasisi na kukiongoza marehemu baba wa taifa (Mumewe) kwa uadillifu mkubwa na usio kifani, alisimamia na kujali rasilimali za taifa na kutaka zitumike kwa maslahi ya taifa, alichukia rushwa na matumizi mabaya ya madaraka lakini pia chini ya uongozi wake chama kilikuwa na nidhamu na kuwajali wakulima na wanafanyakazi maana walikuwa ndio nguzo kuu ya chama hata wakapewa heshima kwenye bendera ya chama ikawekwa nembo ya jembe na nyundo, jembe likiwakilisha wakulima na nyundo ikiwakilisha wafanyakazi.

  Mama yangu kipenzi, Binafsi naamini kama Baba wa taifa angekuwa hai na kuona jinsi chama alicho kiasisi na kukijenga kwa misingi imara jinsi kilivyopoteza muelekeo na kukumbatia wafanya biashara na mafisadi basi asingetamani hata kidogo kuona uozo uliopo ndani ya chama hicho na bila shaka angekwisha watupia virago na kuwarejeshea kadi yao na hivyo kujiunga na mojawapo ya chama pinzani kwani alishawahi kutamka kwa kinywa chake kwamba CCM si mama yake na naamini hata wewe usingekuwa kwenye msafara wa kumsindikiza Kikwete kuchukuwa fomu ya ugombea kama jinsi ulivyofanya.

  Mama jinsi Baba wa taifa alivyokuwa na kiu ya kuona watanzania wanaelemika ili wazifaidi mali asili za nchi yao iliyojaliwa angesononeshwa sana na wala asingefurahi kabisa kuona ujenzi holela wa shule zisizokuwa na matundu ya choo, walimu, vitabu vya kufundishia na kujifunzia huku watoto wakikaa chini lakini wabunge wao wakitanua na mashangingi ya mamilioni ya fedha. Wanaosoma kwenye shule hizo wengi ni watoto wa maskini na zimekuwa kama magenge ya kukusanya watoto hao ambao mwisho wao ni kuwa watumwa kwa watoto wa vigogo wanaosoma nje ya nchi au kwenye mashule bora ya kimataifa, matokeo tumesha anza kuyaona kuanzia wakuu wa wilaya, wabunge, na hata kweye maofisi, idara na taasisi nyeti za serikali wamejaa huko.

  Mama iko wapi nafasi na thamani ya mtoto wa maskini ndani ya nchi hii baada ya kutoweka kwa baba wa Taifa wakati wanaopewa nafasi kubwa ya kugombea ubunge ni watoto wa vigogo? Mama hata kule kwenye ule mkutano wa NEC pale ukumbi wa kizota kwenye uchaguzi wa wagombea uraisi MC (Mshereheshaji) alikuwa mtoto wa mbunge kigogo wa siku nyingi marufu kama mzee wa mabomu, Mbona mwalimu hakufanya hivyo kwa watoto wake vipenzi? Nina imani hukuwahi kumshawishi na hata ungefanya hivyo kwa uadilifu wake asingekubali.

  Kipenzi mama yangu, mabinti zako wanataabika sana na wengine hata kupoteza maisha kwa kukosa huduma bora za afya wanapojifungua kwenye hospitali na zahanati hazina madawa ya kutosha, wanalala mzungu wa nne lakini pia wahudumu ni wachache na baadhi yao waliopo hawajui vizuri misingi ya kazi zao. Kwa kweli mama sikugemea kukuona umeandamana na mgombea yule aliyeoko kwenye chama kilichoshindwa kuboresha huduma hizi kwa miaka 10 sasa tangu Baba wa taifa afariki wakati wewe kama mzazi unajua vizuri uchungu wa mwana na idadi kubwa ya vifo vya kinamama wajawazito. Takwimu zinaonyesha kila wanawake 100 wanaojifungua 4 hupoteza maisha.

  Naajiuliza maswali mengi mama yangu amekuhadaa na nini hata usiendelee na shughuri zako kule Butiama na kuja DSM kumsindikiza Kikwete achukuwe fomu ya uraisi? Mama mlipoishi Ikulu wewe na baba wa taifa hamkupageuza ikulu kuwa pango la ulanguzi maana baba wa taifa alikuwa muadilifu na msafi. Lakini kilichofuata kwa walioendelea kuingia Ikulu walianzisha biashara na mifuko ya wake zao ambayo wewe hukuwahi kuwa nao. Japo ungewatolea uvivu basi uwaulize fedha za kuendesha mifuko hiyo wanazitoa wapi?

  Mama nchi imekosa dira na haina vipaumbele wala mikakati thabiti ya nini kifanyike kwanza kabla ya kingine, huku shule zikiwa hazina vifaa muhimu na walimu, huduma za afya nazo zikidorora walioachiwa chama imara chenye mikakati imara hawana maono wanafikiria kuongoza idadi ya mikoa, wilaya na majimbo ya ubunge ambapo kimahesabu utaongelea mashangingi, nyumba, samahani za kianasa na ujenzi wa majengo ya utawala. Mama hapa ni kutengenezeana nafasi za ulaji kwa jamaa za watawala kwani kipaaumbele kwa watoto wanao kaa chini au mama wajawazito wanao lala mzungu wa nne sio majimbo, wilaya au kuzalisha mikoa mipya. Hivi kweli mama Baba wa Taifa ameshawahi kuwa na ukame wa maaoni kama jinsi hao walio kuita uwasindiikize kuchukua fomu za ugombea wanavyofanya?

  Eti mama yangu kipenzi serikali adilifu aliyoiongoza baba wa tafia inaweza kufanya hayo madudu? Naamini baba wa Taifa angekuwepo asinge kuruhusu uwasindikize watu walio potea ki maono kama hao! Mama wasikusumbue fanya kazi zako hawana maono hata kidogo maana wamediriki kutoa msamaha wa zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa makampuni makubwa yanayo vuna madini yetu tena kwa mikataba isiyokuwa na tija kwa Taifa hili halafu serikali hiyo hiyo inatoza kodi ya shilingi 500 hadi 1000 kwa waendesha bodaboda, bajaji na wanaoendesha biashara ya kuuza chakula mitaani. Mama haya yanahitaji kuyapazia sauti yako ya ukali maana wewe ndio umeachiwa nyumba hii (nchi) nasi kukubali waitumie haiba yako kwa faida yao isiyokuwa na tija kwa nchi hii.

  Mpendwa mama yangu kipenzi nilitegemea kabla hujaandama na mgombea yule (Kikwete) ungepata ujasiri kama aliokuwa nao baba wa taifa maana kama yeye angekuwepo angehitaji kupata majibu ya kina juu ya Deep Green Finance Company LTD iliyochota zaidi ya 10 bilioni kutoka benki kuu (BOT) kwenda kwenye kampuni isiyojulikana na bado serikali inapata kigugumizi na kushindwa kutoa taarifa juu ya suala zito kama hili na matokeo yake hata kuwachukiza wahisani hivyo kufuta misaada na kupelekea serikali kukopa benki ya kibiashara wakati kuna fedha zetu zilizochotwa BoT zimepelekwa kwenye kampuni iliyogubikwa na utata; kwa kumsindikiza mgombea wa CCM hii ni dharau kubwa si kwako tu mama kwa kushindwa kuhoji kama mama uliyeachiwa nyumba na watoto lakini pia dharau kwa Taifa zima.

  Mama ungehitaji kujua kupata ukweli juu ya kampuni ya Tangold Limited ambayo ilisajiliwa katika kisiwa cha Mauritius tarehe 05 April 2005 ikiwa na hati ya usajili namba 553334 na kupata Global Business License (C2/GBL) tarehe 8 April 2005 wakati huo hapa nchini inaonekana ilitimizaa masharti ya biashara na kupata cheti tarehe 20 Februari 2006 huku taarifa zilizopo ni kuwa Tangold imekuwa na akaunti NBC Corporation Branch akaunti namba 011103024840 iliyo funguliwa tarehe 1 Januari 2003 ambapo ni miaka miwili kabla haijasajiliwa Mauritius na takribani miaka 4 tangu imepata hati ya kutimiza masharti nchini. Mama ulihitaji kupata majibu ya kina nasi kukaa kimya au kumsindikiza kikwete. Baba wa taifa angekuwepo asingekuruhusu uende lakini pia asinge kubali kuona uvundo kama huo ndani ya serikali inayoongozwa na chama alicho kiasisi, angehitaji kupata majibu yenye mashiko na kina kama Tanglod ni kampuni ya serikali kwa 100% kama alivyosema waziri wa CCM au ni mali ya mtu binafsi?

  Mama japo ungeulizaa kimyakimya basi juu ya kampuni ya Meremeta inayo tuhumiwa kwa matumizi ya shilingi 155 bilioni ambayo ni zaidi ya shilingi 133 bilioni zilizokwapuliwa katika akaunti ya madeni ya nje EPA ndani ya benki kuu (BoT), mama ungeuliza kiasi cha shilingi 155 bilioni ambacho kampuni ya meremeta imezikwapua zimetumika kwenye nini wakati wajukuu zako hawana vitabu vya kutosha, matunndu ya vyoo ya kutosha, madarasa ya kutosha hivyo wengine kusomea chini ya miti, lakini isitoshe mabinti zako wengi wamepoteza maisha wakati wa kujifungua kwa kukosa huduma bora, wengine wanalala mzungu wa nne, uhaba wa madawa na vifaa kwenye mahospitali na zahanati, kwenye maeneo yao hawana miundo mbinu ya maji, umeme wala barabara nzuri. Mama nilifurahi kukuona mwenye afya njema lakini furaha yangu iliingia shubiri nilipogundua umemsindikiza Kikwete, kwani mama una unga mkono yanayofanywa na watawala hao kwenye nyumba iliyokuwa na uadilifu na misingi mizuri aliyokuachia marehemu baba wa Taifa?

  Mama ungeonyesha kukasirishwa basi na yaliyofanywa na kampuni ya Kagoda kupitia EPA ambayo mpaka sasa wananchi hatujui bayana mmiliki wa kampuni ni nani, ukaguzi uliofanywa na kampuni ya Ernest&Young umeonyesha wazi kuwepo kwa ufisadi uliotumia hati za kughushi, malipo ya viwango visivyo sahihi au kutumia viwango visivyo sahihi vya kubadilishia fedha, ukaguzi ulionyesha kati ya shilingi 133 bilioni malipo ya zaidi 90.3 bilioni yalifanyika kwa kutumia hati za kughushi nyaraka ikiwa ni pamoja na kampuni ya Kagoda Agriculture LTD iliyokuwa kinara wa wizi kwa kuchota shilingi 40 bilioni. Mama ulihitaji kupata majibu ya kina ili utujulishe wanao tuliofichwa ukweli kwa muda mrefu ili tujue kilichosibu serikali yetu hadi kupata kihoro na kigugumizi cha kueleza ukweli au hatua gani muafaka zilizochukuliwa au inafikiria kuchukua hatua gani dhidi ya watendaji wake au watendaji na viongozi wa serikali waliohusika na udhalimu huo. Ulikosea sana mama yangu kumsindikiza Kikwete.

  Mama yangu kipenzi kama baba wa Taifa angekuwepo na kuona hali ya mambo jinsi yalivyo hobela hobela ndani ya CCM au huko aliko (Mwenyezi Mungu amlaze pema) angekuwa anayaona yanayofanywa na serikali ya CCM na angekuona ukiwaunga mkono kwa kuandamana nao wazidi kufanya waliyoyafanya tena kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi bila hata ya kuwapata mrejesho wananchi wake nina imani angekukemea si tu kuungana nao katika masuala ya chama lakini hata kuandama na kiongozi yeyote wa CCM maana hakika waliyoyafanya na kuyasimamia pasipo kukemeana yamemongÂ’onyoa kabisa misingi na hadhi ya chama adilifu alicho kiasisi.

  Mama natumaini sakata la ununuzi wa RADA unalifahamu na naamini mchakato mzima ulivyoendeshwa kifisadi utakuwa umepata taarifa zake hata kufikia hatua ufisadi huo kujadiliwa kwenye Bunge la Uingereza (House of Commons) mara kadhaa na uchunguzi kufanywa na shirika la kipelelezi (SFO) Hili pia mama hujajiuliza kabla ya kumsindikiza Kikwete kuchukuwa fomu? Kwa nini usimtake akupe majibu ya kina yeye kama kiongozi wa nyumba (Nchi)? Kwa nini mpaka watu wa nje wafikie hatua ya kuvaa matatizo yetu kwa kutuonea huruma huku sisi tukinyamaza kimya na kuendelea kulindana? Mama umeshindwa hata kuwapa sharti la kukueleza ukweli na hatua walizo chukua kwa wahusika waliotuingiza kwenye mkenge huo angalau uridhike ndio uandamanee nao au ulishapewa majibu ukaridhika ndipo ukaamua kuaandamana nao? Mbona basi hujatuambia wanao?

  Mama nakuandikia waraka huu nikiamini kuwa wewe si mgeni na CCM baada ya kifo cha Baba, chama kimegumbatia matajiri na kusahau wanyonge, leo hii kuna watu wamegeuka mchwa wa kuitafuna nchi kupitia kivuli cha CCM. Mwanao Kikwete ameshindwa kujenga hoja za msingi kwa wafanyakazi ambao baadhi yao wanashindwa hata kusomesha watoto na kupata mahitaji muhimu ya kila siku badala yake amekuwa mtu wa vitisho na kejeli hata kutapika kauli kuwa KURA ZA WAFANYAKAZI HAZITAKI kisa shinikizo la kuongeza mishahara hii inamaanisha ile nembo ya nyundo inayowakilisha wafanyakazi kwenye bendera ya CCM itolewe ili iwekwe picha ya Manoti iwakilishe wafanya biashara? Hiki kiburi kimetoka wapi? Baba alishawahi kuwa na majibu ya mayai viza kama haya kwa wafanya kazi mlipo ishi ikulu?

  Kwani mama angepunguza safari za nje, serikali yake kuacha anasa kwa kutotenga fungu nono kwa ajili ya chai, ununuzi wa mashangingi, kupunguza posho nene kwa wabunge (Mbunge mmoja analipwa milioni 7 kwa mwezi, kila kikao kimoja laki moja na sitini, na anaposafiri analipwa elfu 80 zote hizo bila kodi) samani za ndani kila mwaka, kudhibiti mfumuko wa bei, posho nono wanazolipana kwa vikao vilivyo kwenye majukumu ya kazi za kawaida na kusimamia vizuri rasilmali za nchi hii ikiwa ni pamoja na kutoza 700 bilioni walizosamehe, kweli mama kulikuwa na haja ya kutoa kauli za shombo au alikosa ushawishi wa kujenga hoja zenye mashiko kwa wafanyakazi? Mama raslimali za nchi hii zikisimamiwa vizuri na kuwepo nidhamu nzuri na uadilifu kwenye matumizi ya pesa inawezekana hata kulipa kima cha chini cha 315,000/= kwa wafanyakazi maana tayari kuna watu wanalipwa milioni 7 tena bila kodi.

  Mpendwa kipenzi mama yangu nahitimisha kwa uchungu hasa ninaposikia yanayoendelea kwenye chaguzi za CCM, haya tunayo yaona na kuyasikia ndio taswira halisi ya chama cha mapinduzi, taswira inaonyesha kuwa ni CCM ni rushwa na rushwa ni CCM hivi kabla mfumo huu mpya unao fichua maovu yao mambo yalikuwaje? Kama wao na rushwa ni damu damu basi pia sitakosea nikisema CCM na ufisadi ni chanda na pete. Mama ulipaswa kutafakari kwa kina kabla ya kumsindikiza mgombea wa CCM. nitafurahi kama utachukua hatua na kupewa majibu kwa maswali niliyokusaidia kukufunilia. Msalimie sana kaka yangu Madaraka, Makongoro na Dada Maria waambie nikipata nauli nitaonana nao nitakapokuja kuzuru kaburi la baba.

  Wasalamu mwanao MTOI
   
 2. Mahesabu

  Mahesabu JF-Expert Member

  #2
  Sep 4, 2010
  Joined: Jan 27, 2008
  Messages: 5,043
  Likes Received: 666
  Trophy Points: 280
  MAMA USIKATISHWE TAMAA NA WENYE AJENDA ZAO ZA KICHAMA......UNABAKI MAMA UNAYEHESHIMIKA,USIYE NA MAKUU.....UNABAKI MAMA AMBAYE BADO HUJAONA CHAMA MBADALA....AMBACHO KINGETOKEA HATA LEO UNGEJIUNGA NACHO....MAMA YETU MWEMA MWENYE WATOTO WASIOLITIA AIBU TAIFA KWA UFISADI NA UCHAFU MWINGINE NA WANGEPENDA ULIVYO MSAFI KAMA BABA YETU MWALIMU UJIUNGE NAO WAUTUMIE USAFI WAKO KUJITANGAZA LAKINI UMEBAKI MADHUBUTI.......MAMA UJUAYE MALEZI....ANGEKUWA MWINGINE ANGEJIKWEZA, nakupenda mama...nakupenda mamaLAKINI WEWE UMEBAKI KUWA WEWE....MCHA MUNGU,MTII,MPOLE NA EWE NDIYE MAMA WA TAIFA HILI
  MAHESABU
   
Loading...