Waraka wa Katoliki, KKKT na utendaji wa Jeshi la Polisi

Yericko Nyerere

JF-Expert Member
Dec 22, 2010
16,987
20,271
Naomba niangazie mambo mawili muhimu leo, kwanza ni waraka wa viongozi wa Kiroho, TEC na KKKT walioutoa wiki jana kuelekea katika sikukuu yao ya pasaka na pili ni Polisi.

Nimesoma waraka zote mbili neno kwa neno, mstari kwa mstara, na aya kwa aya. Nakili wazi maandiko yao yamejitosheleza na yamejaa hekima na busara ya hali ya juu sana, hali inayoleta tumaini jipya katika nchi yetu niliyoamini baada ya sie wanasiasa kuzima na kufungwa minyororo, basi mnyonge alishakosa sauti yake kusemewe, naaam namuona mnyonge ameinuka.

Ninukuu sehemu ya Waraka mmoja mmoja hapa chini kwaajili ya kuweka kumbukumbu sahihi karne kadhaaa zijazo vitabu vitakapoandika juu ya nchi yetu na mazalia yake.

TEC:

"Ili kuweza kuleta mabadiliko katika nafsi zetu na katika jamii yetu, Kanisa siku zote linatufundisha, kwa busara na hekima ya Roho wa Mungu, ulazima wa kusoma ishara za nyakati ili kujua ni nini kinachoendelea katika jamii. Kuhusu nchi yetu ishara za nyakati tutaziangalia katika maeneo matatu, yaani kisiasa, kijamii na kiuchumi, kwa lengo la kujitathimini.

Kisiasa Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeainisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania. Hata hivyo, shughuli za siasa bado zinaendelea kuzuiwa kwa kutumia vyombo vya dola. Maana yake ni kwamba shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa, kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani, ambayo ni haki ya kila raia, zimekoma mpaka uchaguzi mwingine. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi.

Vile vile baadhi ya vyombo vya habari vimefungiwa au kusimamishwa kwa muda, na hivyo kupunguza uwigo wa uhuru wa wananchi wa kupata habari, maoni na wa kujieleza. Kufungiwa huku kwa vyombo vya habari kumeenda sambamba na kuminya uhuru wa Mahakama na Bunge kwa njia ya kuminya haki ya wabunge na kutowapa nafasi ya mikutano ya hadhara kama haki yao ya msingi ya Kikatiba. Katika mazingira haya ni rahisi kwa jamii kufarakana na hata kujenga chuki kiasi cha kuhatarisha amani, usalama na hadhi ya uhai wa binadamu.

Kumekuwapo pia hali ya vurugu katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi hizi zinaacha nyuma uchungu, hasira, tamaa ya kulipa kisasi na hata kususia chaguzi nyingine. Hali hii ni hatari kwa mustakabali wa Taifa letu. Tukiiachia hali hii izoeleke tushishangae huko mbeleni kujikuta katika mifarakano mikubwa zaidi itakayobomoa misingi ya amani na umoja wa kitaifa.

Kiuchumi Hapa ni vema tukajiuliza maswali ya msingi kabisa kuhusu kujali katika maisha ya walio wanyonge ili umisionari wetu ulete nafuu katika mahitaji ya lazima kwa wale wanyonge, maskini na walio pembezoni mwa jamii. Hebu tujiulize:

Tunazitumiaje mali na rasilimali nyingine tulizokabidhiwa na Mungu kama mawakili wake?
Tunalipa kodi stahiki kwa ajili ya kugharamia huduma za jamii ambazo serikali inapaswa kutoa kwa ajili ya wananchi?

Wale ambao tu waajiri, tunawajali wafanyakazi na wahudumu wetu kwa kuwalipa mishahara ya halali?

Wale ambao tu wafanya biashara, tunalipa kodi zote kihalali?

Wale ambao tumepewa jukumu la kukusanya kodi, ushuru na ada nyingine tunafanya hivyo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu husika?

Tunaepukanaje na kishawishi cha rushwa, hongo, mulungula, magendo au aina yoyote ya ufisadi?

Sasa hivi bado kuna kishawishi cha kupingana na azma ya kuboresha maisha ya kijamii. Hii inajidhihirisha kwa njia ya uhasama, ugomvi, ukatili kwa watoto na wanawake, ujambazi, na maovu mengine kiama hayo miongoni mwa jamii yetu. Kama wamisionari tunaopaswa kuleta habari njema kwa ndugu zetu, kwa nini turuhusu roho ya namna hii ambayo kwa kweli ni roho ya Kaini inayouliza kwa jeuri kabisa: ‘Mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?"

Hizo hapo juu ni hoja za Baraza la Maaskofu Katoliki ambazo mpaka sasa tangu zitolewe zaidi ya siku 14bado hakuna mamlaka ya nchi iliyozijibu zaidi tunashuhudia mwendelezo mchafu wa sissa za ccm na Humphrey Polepole ambao ndio wamejipa haki ya kuzunguka nchi nzima kufanya sisa huku vyama vingine hata kushiriki misiba ni marufuku (rejea Mwanza), achilia mbali vikao tu vya ndai navyo ni marufu.

Nukuu ya pili hapa chini ni kutoka KKKT, hawa wameweka hoja ngumu na nzito sana ambazo ni mwangaza mpya kwa Watanzania.

"2. Maisha ya Siasa

Kwa umoja wetu katika utume, tunatambua siasa safi na uongozi bora kuwa ni misingi iliyoongoza maisha ya siasa katika taifa letu. Ujio wa vyama vingi mnamo 1992, haukuondoa umuhimu wa misingi hii bali ulipanua matumizi ya demokrasia iliyojengwa katika uhuru wa mawazo. Taifa ni mkusanyiko wa taasisi na watu mbalimbali, wenye lengo moja lakini kwa njia mbalimbali. Kutokana na wingi huu, taifa letu daima ni juu ya vyama, taasisi na makundi.

Taifa huongozwa na katiba iliyo kiini cha sheria zote. Taifa haliongozwi na ilani za vyama. Serikali haiongozwi na ilani za vyama. Serikali huongozwa na katiba, sheria, kanuni na mapokeo mema (misingi na tunu za taifa). Serikali husimamiwa na bunge huru lililo sauti ya wananchi. Wananchi ndilo chimbuko la madaraka ya bunge. Bunge halisimamiwi na ilani, chama chochote wala mtu awaye yote. Kwa umoja wetu na kwa nyakati zetu, hivi sasa tunashuhudia matukio yaliyo kinyume na tunu na misingi iliyolilea taifa letu. Baadhi ya matukio hayo ni:

I. Hofu iliyojengwa katika matukio halisi yakiwamo utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.

II. Kupungua na hatimaye kutoweka kwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na kupata habari. Kwa mwenendo huu, kuna hofu kuwa hata uhuru wa kuabudu uko mashakani.

III. Kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi. Hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.

IV. Kukosekana kwa mazingira ya haki na uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi zote zimeghubikwa na ubabe, vurugu, hila, na vitisho.

V. Utekelezaji wa mipango ya maendeleo wenye mwelekeo wa kiitikadi. Hatua hii imeimarisha ubaguzi wa kiitikadi katika taifa letu na kukuza migawanyiko.

VI. Kushamiri kwa chuki mioyoni mwa watu ambalo ni chimbuko la visasi, kukata tamaa, na ushiriki mdogo wa wananchi katika chaguzi na maisha ya siasa.

VII. Udhalilishaji wa kauli njema isemayo "Maendeleo hayana chama". Udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya kutumia fedha nyingi katika chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama ili kuleta maendeleo. Tunajiuliza, kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu anajiuzuru chama fulani, eti kwenda kuleta maendeleo katika chama kingine? Mchezo huu unagharimu fedha nyingi na maisha ya watu wanaokufa, kujeruhiwa na uharibifu wa mali.

Mambo haya ni tishio linalohatarisha umoja na amani ya nchi yetu."

Mwisho wa Kunukuu:

Serikali inaweza kuwa na machaguo mawili tu, ama kukomaza shingo, ama kujisahihisha na kurejea kwenye misingi ya katiba na sheria zetu na sio sheria zao.

POLISI/POLICE

Kumekuwa na malalamiko saba juu ya jeshi letu la polisi, malalamiko haya yanatokana na kwamba polisi ndicho chombo kinacho hamiliana kwa kiwango kikubwa na wananchi mitaani, mauaji yanayohusishwa na pilisi ni moja ya malalamiko jayo ya umma.

Kwanza tujifunze mambo machache, Polisi nini? Hili watu wamekuwa wakilichanganya, Kuwasaidia maana ya neno POLICE ni People's Oorder, Law, lnvestigation and Criminal Enforcements kwamjibu wa Wagiriki, lakini Wazungu wanasema ni Law enforcement and criminal investigation..not vice Verser. Kisha tujifunze utendaji kazi wa huyu mtu aitwaye polisi upoje hapa Tanzania na duniani kote, kwakuwa sheria ni moja japo zinaweza kutofautia kidogo tu kimaumbile na kiutekelezaji lakini msingi wake ni mmoja.

Criminal investigation procedure kupitia criminal investigation Act inamruhusu askari kutumia nguvu pale tu mtuhumiwa anapoonesha ubishi wa kutotii.

Pia sheria hiyohiyo inamtaka, hii ni lazima sio ombi, askari kujitambulisha ikiwa ni Pamoja na kuonesha kitambulisho kabla "hajaanza" utekelezaji wa majukumu yake. Rejea sheria ya haki za mtu anapokamatwa na polisi.

Suala la kutoa/kutumia silaha lina mambo mengi ya kitaalamu, na Kisheria askari popote alipo katika misheni yoyote anatakiwa kuwa "armed" muda wote, lakini kuwa armed si kumpoint gun mtu ambaye ni "unarmed" wala hajaonesha dalili ya madhara kwako. Hili ni kosa kubwa kwa askari yeyote aliyehusika na mauaji yoyote ya rai asiye na silaha.

Polisi anaweza kuwa na utetezi wenye hoja na usipokuwa makini unakubaliana naye kwamba aliona mtu yupo peke yake ndio lakini alikuwa amezungukwa na watu anaoamini ni wafuasi wake. Katika mazingira kama hayo ambayo watu wengi wamejaa ambao kwa tafsiri ya kawaida ni watu wanaomuunga mkono mtuhumiwa, unategemea silaha itoke baada ya vurugu kuanza? Hii ni hoja nzito na inamruhusu askari kutoa silaha, lakini hoja hiyo inakufa kwenye kitendo cha kumuelekeza silaha mtu au watu hao aliyesimama au wanaoandamana na hawna silaha yoyote,

Askari huyu anaweza kujitetea tena kwamba alipomuona mtuhumiwa/watuhumiwa hawa kasimama/wanatembea walikuwa wameweka mikono mfukoni mwa suruali zao hali iliyomfanya yeye askari afikiri hawa watu wana silaha,hivyo akawawahi kwakunyooshea silaha.

Lakini utetezi huu unafutwa na kitendo cha yeye kutofuata taratibu za kijeshi kwenye kwenye oparesheni za kiraia ambapo sheria inamtaka atangaze kwamba kwamjibu wa kifungu flani (akitaje) cha sheria ya Jamhuri, Jeshi linatangaza kutawanyika mara moja kabla halijatumia nguvu kuwatawanya, Tangazo hili linatakiwa kurudiwa zaidi ya mara kumi na atumie kipaza sauti ili raia wasikie.

Baada ya hapo sheria inamtaka askari huyu kutumia mabomu ya machozi au risasi za mpira kuwatawanya na sio risasi za moto, Sheria inakazia risasi hizi za mpira zipigwe hewani. Hakuna mahali katika sheria ya jeshi la Polisi panaposema polisi atumie risasi za moto kwa mtu au kundi la watu wasio na siraha.

Mauaji yoyote yenye kukiuka haya ni moja ya makosa ya uhalifu wa kibinadamu na sheria ni lazima ichukue mkondo kwa askari husika na aliyempa amro ya kutenda kosa hilo. Ni wajibu wa umma kukusanya kila aina ushahidi, siki za usoni utatumika kulipia gharama hii ya haki kwa kila uovu.

Na Yericko Nyerere
 
Nanukuu

Udhalilishaji wa kauli njema isemayo "Maendeleo hayana chama". Udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya kutumia fedha nyingi katika chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama ili kuleta maendeleo.

Tunajiuliza, kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu anajiuzuru chama fulani, eti kwenda kuleta maendeleo katika chama kingine?

Mchezo huu unagharimu fedha nyingi na maisha ya watu wanaokufa, kujeruhiwa na uharibifu wa mali.

Mwisho wa kunukuu
 
Back
Top Bottom