Waraka maalumu kwa wana CHADEMA

Kurunzi

JF-Expert Member
Jul 31, 2009
9,277
9,912
Wanabodi

Wanabodi chama cha mapiduzi wapo katika mkutano mkuu wa chama chao, Wao wanajua kwamba mkutano huu ni muhimu sana kuliko mkutano mwingine wowote kwasababu kuu mbili hali ya kisiasa ni tofauti sana kuliko wakati uliopita, makundi ndani ya chama yannaendelea kiujizatiti pia CDM kimeleta changomoto kubwa sana hivyo kutishia ushindi wa chama hicho katika uchaguzi ujao.

Lakini wakati upande wa CCM hali ikiwa hivyo ni vema upande wa CDM wakatumia muda huu kujipanga vema hasa kujiimarisha ngazi ya chini kabisa, Nimekutana na makala ya Samson Mwigamba ambayo ukiwa kama mwanachadema ni vema ukaisoma na wewe ujue wajibu wako tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao 2015.


NI mara yangu ya kwanza kuandika waraka kama huu kwa wana CHADEMA wa nchi nzima.

Niliwahi kufanya hivi kwa wana CCM na nikawaambia sitawaandikia tena mpaka pale chama chao kitakapokuwa kimeng’olewa madarakani kama hawatayafanyia kazi yale niliyowaeleza.

Leo naomba nichukue fursa hii kuongea na wanachama wa chama changu, CHADEMA.

Huko nyuma niliwahi kutumia makala mbili kujibu hoja za rafiki yangu na msomaji mahiri wa makala zangu msomi mwanafalsafa, Dk. Masomo Lupembe (PhD). Hoja ya Dk. Lupembe ilikuwa ni kwamba: “Shamra-shamra, hemwa-hemwa, mapokezi na shangwe kinazopata chama chako (CHADEMA) ni very 'deceptive' and 'misleading'! ….Watanzania hawako tayari kwa mabadiliko!...jamii yenye kiu ya mabadiliko huyatafuta mabadiliko bila kusukumwa-sukumwa au kuhamasishwa na watu wengine (wanasiasa, wanaharakati, wasomi, nk)…. ishara ya kutaka mabadiliko haiwezi kupimwa kutokana na wingi wa watu wanaohudhuria katika mikutano mbalimbali inayoendeshwa na chama chako!

Zaidi ya nusu ya Watanzania wenye sifa za kupiga kura hawajiandikishi kupiga kura! Kati ya wachache wanaojiandikisha, nusu yao hawaendi kupiga kura!

Achilia mbali wanaouza shahada zao! Haka ka 'percentage' kanakobaki ambako almost ni sawa na robo ya robo ndiko kanako piga kura na kwa mazoea kanaipigia CCM”. Mwisho wa kunukuu.

Kwa wenye kumbukumbu nzuri watakumbuka kwamba mara baada tu ya kunukuu ujumbe huo wa Dk. Lupembe, aya iliyofuatia nukuu hiyo nilisema maneno haya: “Ujumbe wa Dk. Lupembe ni mzito sana, kwa namna fulani unakera kwa kusikia maneno ya kukata tamaa kutoka kwa msomi wa nchi hii …. Naamini baadhi ya wasomaji wa kalamu hii watakaposoma maneno ya Dk. Lupembe wataanza kulalamika na kumshutumu. Lakini naomba tutulie kidogo na kutafakari! Bora tuchukulie hali iko kama Dk. alivyosema ili tuongeze nguvu ya kutafuta mabadiliko kuliko tudharau ujumbe wake halafu tukajikuta tunabweteka na shamra shamra tunazoziona na hatimaye mwaka 2015 tukashindwa kuleta mabadiliko tunayoyatarajia.”

Kisha nilisema: “…Pamoja na kukubaliana naye kama nilivyosema hapo juu kwa makusudi ya kuongeza bidii katika kutafuta mabadiliko tunayoyapigania, naona kama ujumbe wake ni wa kukatisha tamaa sana isivyo lazima.” Nikasema mwitikio wa wananchi kuipokea CHADEMA kwenye mikutano “nakubaliana naye kama angesema si ishara pekee, lakini ni moja ya ishara ya watu kutaka mabadiliko.

Kwamba tukiangalia hiyo hali tukatulia na kudhani tayari tumeshinda tutakuwa tunajidanganya. Lakini ni kweli kwamba hiyo ni ishara mojawapo ya utayari wa wananchi kufanya mabadiliko.”

Lingine ni hili la kwamba “…Watanzania hawajitambui! Walirogwa vibaya mno na mfumo wa chama kimoja (CCM) uliowatawala vibaya mno!

Kuwarudisha Watanzania katika hali ya kawaida ya kujitambua kama wanadamu, inahitajika miaka isiyopungua hamsini (kizazi kizima) ya intensive campaign and inducement.”

Nikamweleza Dk. kwamba “ni kweli walirogwa vibaya mno na mfumo wa chama kimoja uliowatawala vibaya mno na wakadhani miaka yote taifa hili litaongozwa na rais kama Nyerere”. Lakini nikamwambia Dk. Lupembe, “kazi hiyo ya kuleta matumaini kwa Watanzania na hatimaye kuwabadilisha na kuwatayarisha kufanya mabadiliko haiwezi kufika miaka 50… Tusikatishwe tamaa kiasi hicho! Ukombozi u karibu na hilo linajulikana kwa kila mtu.”

Kama msomaji (na hasa wewe mwanachama, mfuasi, mpenzi na shabiki wa CHADEMA) umesoma vizuri maneno hayo ambayo niliyaandika tarehe 16 mwezi Mei mwaka huu (miezi zaidi ya mitano kabla ya uchaguzi mdogo wa kata 29), naamini leo unapoyaangalia vizuri matokeo ya uchaguzi huu mdogo wa udiwani katika kata 29 uliofanyika maeneo mbalimbali ya nchi hii mwishoni mwa mwezi uliopita, utakuwa na sababu nyingine ya kushangaa kwa nini Kalamu ya Mwigamba imekuwa ikiandika mambo ambayo baada ya muda yanatokea.

Kusema ukweli hata mimi mwandishi wa ukurasa huu najishangaa mwenyewe! Najikuta wakati mwingine najiuliza kwamba ni Mungu huwa ananiongoza?

Najijibu mbona mimi si nabii! Najiuliza ni elimu ya utabiri? Najijibu hapana, sijawahi wala sifikirii kujihusisha na mambo ya unajimu!

Hivyo mwishoni huishia kusema tu kwamba ni mambo ya kawaida tu ambayo ungemuuliza mtanzania yeyote mwenye akili timamu anaweza kuchambua hali ya nchi tulikotoka, tuliko na hatimaye ukaja mwono wa kweli wa kule tunakoelekea.

Hebu nitumie sasa nafasi iliyobaki kuongea nanyi ndugu zangu, rafiki zangu, wazee kwa vijana, wanaume kwa wanawake, wanafunzi kwa wafanyakazi, wafanyabiashara kwa wakulima, mlio wanachama wa CHADEMA ama mlio wafuasi, wapenzi na mashabiki wa chama hiki.

Naomba awali ya yote niwaeleze kwamba matokeo ambayo mpaka sasa ninayo kuhusiana na uchaguzi wa nilioutaja hapo juu, ni kwamba CCM walirejesha kata zao 22 na kuachia tano, CHADEMA wakarejesha za kwao mbili na kunyakua za CCM 3, TLP wakanyakua ya CCM 1 na CUF nao wakanyakua ya CCM 1.

Matokeo haya ni mazuri sana kwa CHADEMA kuliko CCM (navizungumzia vyama hivi viwili ambavyo kwa sasa ndivyo vilivyo kwenye ushindani mkubwa). Nianze na CCM.

Ni matokeo mabaya sana kwa CCM kwa sababu kama ninavyowajua CCM wataridhika kwamba bado chama kinapendwa na kuishia kwenye tamko lile lililotolewa na Nape Nnauye kwamba chama bado ni imara na kina uhakika wa kushinda tena mwaka 2015.

Kwa jinsi ninavyoifahamu CCM ndo ‘imetoka’ hivyo! Hawatakaa chini kufanya tathmini ya kina na kuangalia ushindi huo wameupataje na nguvu ya upinzani imeongezekaje.

Mfano CCM haikuchukua kiti hata kimoja ambacho hakikuwa chake. Bali wamepoteza viti vyao 5 kati ya 27 (asilimia 18.5).

Lakini asilimia hiyo ni ndogo sana kama tutaangalia kiwango cha kura walizopata ukilinganisha na za 2010.

Katika kata ya Bangata (Arumeru Magharibi) kwa mfano, 2010 CHADEMA wala hatukuwa na mgombea wala hapakuwa na CHADEMA katika kata hiyo zaidi ya watu wawili watatu waliojitokeza na kujitolea kwa kugawana nafasi chache za uongozi wa kata.

Lakini chini ya miezi mitano, tumepata wanachama pale, wamechagua viongozi kuanzia wa kata mpaka matawi na ngazi za msingi, wameshiriki uchaguzi wa diwani mwezi uliopita na kupata kura 860 na CCM 1100.

Hali katika maeneo karibu yote ilikuwa kama hivi. Nguvu ya CHADEMA imeongezeka sana. Sehemu nyingine CCM imeizidi CHADEMA kura chini ya 100 pamoja na nguvu kubwa ya fedha, dola na kila aina ya vitimbi.

Waacheni wana CCM wajione wako salama. Wasifanye tathmini na kujua kwamba katika maeneo mengi ambako wameshinda na hata walikoshindwa, walitumia nguvu kubwa mno ya pesa.

Kwa CHADEMA ushindi huu ni mzuri sana kwetu kwa sababu baadhi yetu hatukutegemea kupata ushindi kama huu.

Tulidhani tunaweza kuwanyang’anya viti vingi CCM na kuchukua udiwani katika kata zaidi ya nusu kama alivyowahi kunukuliwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na baadhi ya magazeti.

Ni kweli, kwa kuangalia kishindo cha operesheni zetu hasa M4C inayokwenda bega kwa bega na ‘vua gamba, vaa gwanda’, wengi tulitegemea makubwa. Na hili ndilo lile nililolizungumza wakati namjibu Dk. Lupembe.

Kwamba hamasa, shamra shamra, shangwe na hemwa-hemwa ambazo chama kinazipata kwenye mikutano ya hadhara ni kweli kwamba ni dalili ya chama kukubalika lakini si dalili pekee ya chama kupata ushindi wa kishindo.

Lazima ziongezewe na mbinu za medani katika kuhakikisha tunapata ushindi. Ni lazima tujikite sasa kuhakikisha chama kinakuwa na mtandao nchi nzima kuanzia ngazi ya taifa mpaka ngazi ya msingi na mabalozi wa nyumba kumi kumi.

Na hii si kazi ya akina Freeman Mbowe, Issa Saidi, Arfi, Slaa, Zitto, Hamad Mussa, ama wakurugenzi na maofisa wa makao makuu ama wabunge kupitia CHADEMA , ni kazi ya mfumo mzima wa chama kuanzia viongozi wa kitaifa, mikoa, wilaya, kata, matawi na wanachama wa kawaida.

Kumekuwa na ugonjwa ndani ya chama wa kufikiria kwamba kazi yoyote ndani ya chama mpaka iguswe na viongozi wa chama wa kitaifa ama wabunge ndo inakuwa imekamilika.

Utakuta viongozi wa chama ngazi za chini wanahaha kukimbizana na ratiba za viongozi wa kitaifa na wabunge ili waje wawafungulie tawi moja.

Hii haiwezi kuwa sawa. Viongozi wa mikoa, wilaya na hata kata tunajishusha sana ndani ya CHADEMA kwa kudhani majukumu ya kueneza na kujenga mtandao wa chama katika maeneo yetu lazima ifanywe na viongozi wa kitaifa.

Tumefika mahali siku hizi mbunge wa jimbo fulani ama viti maalum ndani ya mkoa fulani kupitia CHADEMA anaonekana kama kichama ni kiongozi mkubwa kuliko mwenyekiti wa wilaya ama hata wa mkoa.

Nawapongeza sana wabunge wa chama hiki ambao bado wanakuwa na unyenyekevu na heshima kwa viongozi wao wa chama mkoa na wilaya wanazotoka. Lakini kwa mfumo uliopo wanaweza hata kujitwalia madaraka ya viongozi wa chama.

Katika mkoa wangu nimepiga marufuku suala la viongozi wa chini yangu kuniambia niwatafutie Mh. Mbowe, ama Slaa, ama mwingine yeyote wa huko juu aje afungue tawi ama ofisi ya kata.

Na msimamo wangu umeanza kuzaa matunda. Kule Mto wa Mbu wilayani Monduli ofisi za kata zimefunguliwa mbili na ya tawi moja na hatimaye mkutano wa hadhara uliowavua magamba watu mamia kwa kuongozwa na viongozi wa mkoa na wilaya.

Jumapili iliyopita chama kimeshinda uchaguzi wa mamlaka ya mji mdogo wa Usariver ambapo tulipata viti 6 kati ya 9 na sasa Halmashauri ya Mji mdogo wa Usariver itaongozwa na CHADEMA lakini kazi yote imefanywa na uongozi wa wilaya.

Uchaguzi wa Daraja mbili na Bangata sehemu kubwa umeendeshwa na viongozi wa wilaya mbili za mjini na Meru kwa kusaidiana na wabunge wa maeneo wa mkoa huu.

Viongozi wa mkoa tulipita mara chache sana kuhutubia na kusaidiana nao mawazo na ushauri. Mwenyekiti wa taifa ilitokea tu akafika Arusha tukamwomba akahutubia mkutano mmoja mmoja kwa kila kata.

Hii ndiyo spirit inayohitajika. Wenyeviti wenzangu wa mikoa niwahamasishe tufanye kazi sasa ya kutandaza chama.

Tushuke chini tuhakikishe kila wilaya na majimbo ndani ya mikoa yetu yana uongozi hata kama ni wa muda tukisubiri uchaguzi wa ndani ya chama.

Na vivyo hivyo kwa kata na matawi yaliyo katika mikoa yetu.

Twende tukahamasishe wanachama wapya tupate wa kutosha na humo humo wanachama wenyewe wajichague kupata viongozi makini wa matawi na kata zetu ili uongozi wa majimbo, wilaya na mikoa pia uwe na ushindani wa kutosha, na hapo ndipo tutapata viongozi makini wa kukivusha chama 2015.

Tusisubiri M4C. Hii M4C si kitu ‘physical’ kinachotembea kama mwenge ambacho tunaweza kusubiri mpaka wakimbizaji wake watakapofika kwenye mikoa, wilaya, majimbo, kata na vijiji vyetu.

Hapana! M4C ni vuguvugu la ndani ya mioyo ya watanzania. Nalo limesambaa nchi nzima hata hapo ulipo kwa sasa wewe unayesoma waraka huu, kuna M4C!

Nasema hata nyinyi wanachama na wafuasi mnaopenda CHADEMA, kama mnaona katika mtaa wenu ama kijiji chenu hakuna uongozi wa tawi la CHADEMA, kutaneni wawili watatu mjipe kazi ya kutafuta wanachama wengine ndani ya mtaa ama kijiji chenu.

Mkishafika kuanzia kumi na zaidi chaguaneni viongozi wachache wa muda. Kisha peaneni kazi ya kuzidi kueneza chama na kutafuta wanachama wapya na baadaye mkaripoti kwa uongozi wa kata ili uje usimamie uchaguzi wa tawi.

Kama hakuna uongozi wa kata pia mnaweza kujioganaizi na kupata viongozi wachache wa muda wa kata kwa ajili ya kuhakikisha angalau mitaa ama vijiji visivyopungua nusu kwenye kata vinakuwa na wanachama na viongozi wa matawi kisha mkautaarifu uongozi wa jimbo/wilaya kuja kusimamia uchaguzi wa kata. Ili mradi mtambue kwamba kwa utaratibu uliopo wote wanaochaguliwa kabla ya program ya kitaifa ni wa muda.

Program ile ikifika ikaridhika kwamba wako vizuri itawaendorse rasmi, ikijiridhisha kwamba kuna mambo hayakwenda vizuri katika mchakato wa kuwapata, wanaweza kuitisha uchaguzi mpya.

Lakini tusilale! Tuendelee kuhamasisha chama na kuingiza wanachama wengi kadri iwezekanavyo. Na viongozi wa kitaifa nawasihi waharakishe mchakato wa kupitia na kusimika viongozi nchi nzima. Naamini hawataenda tena na mkakati wa timu moja kwa nchi nzima bali watagawa timu kadhaa kwenye kanda tofauti tofauti nchi nzima ili kukamilisha zoezi la mfumo wa uongozi kuanzia msingi hadi taifa ifikapo 2013 Desemba.

2014 ni mwaka wa kazi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji. Tunahitaji kuhakikisha hakuna mtaa, kijiji wala kitongoji ambacho hakitakuwa na mgombea wa CHADEMA. Tukifanikiwa katika hilo, hata kama hawatashinda wote, tayari tutakuwa na mtandao wa kutosha wa kusimamia kura zetu mwaka 2015.

Mwisho kazi hii si ya malipo. Kazi hii ina tunu mwisho wa wakati tutakapokuwa tumefanikiwa kuleta mabadiliko yanayoliliwa na watanzania na hata mbinguni tutatunukiwa maana hii ni kazi ya Mungu. Nimebahatika kufanya kazi makao makuu ya chama kama mhasibu mkuu kwa mwaka mmoja.

Pesa ya ruzuku inayopatikana pale kwa mwezi ni sawa na asilimia 10 tu ya fedha ambayo inahitajiwa na chama kwa mwezi kwa ajili ya gharama ya kuendesha makao makuu, kutengeneza vifaa vya uenezi kama kadi, bendera nk, kutoa ruzuku mikoani, kugharamia operesheni mbalimbali za chama, kununua vitendea kazi kama magari na vyombo vingine, kuendesha vikao vya chama kama kamati kuu, baraza kuu na mkutano mkuu na ile ya mabaraza ya chama, gharama nyinginezo za kujieneza mfano vyombo vya habari, na zaidi sana kuweka akiba kwa ajili ya gharama za uchaguzi mkuu ujao.

Tukilitambua hilo na tukajitoa kila mtu kwa nafasi yake kufanya kazi ya kuliandaa tumaini hili la ukombozi wa mtanzania, tutakuwa tumefanya kazi kubwa ambayo historia ya nchi hii itatuenzi!

Tukiupuuzia waraka huo muhimu kuanzia viongozi wa kitaifa, mikoa, wilaya, majimbo, hadi chini. Tukauona kama waraka wa mtu aliyekata tamaa sana. Tukaendelea kujilisha upepo na hamasa alizozisema Dk. Lupembe, tushishangae 2015 tukagaragazwa mpaka tukaanza kutafutana!

Kwangu mimi bora tumepigwa kwenye kata 29 ili zitufundishe kwamba bado kuna kazi ya kufanya na tusilale kuliko tukijilisha upepo kwamba kwenye kata 29 sisi ndo washindi eti kwa sababu tu tumerejesha kata zetu na kuwanyang’anya CCM 3. Ikifika 2015 tutashangaa!!!

Tafakuri njema makamanda!
 
mkuu tutatekeleza,baada ya uchaguzi wa juzi kupita niliandika 'Uongozi CDM Mkoa Tabora wajiangalie' katikati nilisema
 
'haiwezekani hata chaguzi ndogo viongozi wa eneo husika hawawezi eti mpaka uongozi taifa uje' ..viongozi chini wanalala.
 
Your a true great thinker , nakuahidi kwamba binafsi nimekuelewa , naanzisha harakati rasmi kuanzia muda huu kwenye kata ya IKIMBA Wilayani KYELA , habari yake utaiona .
 
Shime vijana tutoke nyuma ya key board tukapige kazi mtaani kwa wananchi wakikubali chama na tuhamasishashane sisi kwa sisis juu ya habari ya kujiandikisha na kutunza kadi zetu kwa ajili ya mashambulizi 2015,(mshambuliaji bora ni mfungaji wa magoli ni bore kuvaa mashati na nguo za kiharakati kama bado huna uwezo wa kuambukuza watu harakati)
Binafsi ninapanga safari kwenda kijijini naenda kuanza na baba mama na bibi wakinielewa najua nina watu zaidi ya nani waaminifu na wapiga kura kila mtu akifanya hivi magamba kwanini uyasiabike 2014 na 2015!
 
Makala hii ya Samson Mwigamba ni ya msingi sana kufanyia kazi. Nadhani anachokieleza ni ukweli kabisa.Bila CDM kujizatiti mashinani hakuna muujiza wowote utakaoleta ushindi. At least Mh.Mbowe katangaza kumwaga pikipiki mashinani probably this might bear fruit.
 
Nategemea mikoa na wilaya na makatibu wao watayachukua haya na kutafanyia kazi bila kusahau wapenzi na mashabiki wa CDM watatimiza wajibu wao.
 
Kurunzi si unajua tulivyo wavivu wa kusoma bana,siku hizi viongozi wa Chadema hawaingii sana JF,lakini hapa ingekuwa vizuri zaidi uongozi wa Chama kuchukua idea tofauti kwa sababu sisi tuko nje ya uwanja tunaangalia game na tunaona makosa ambayo yanapaswa kurekebishwa,Chadema kwa sasa hivi kuna mapandikizi kibao kutoka ccm,kazi tunayo
 
Kurunzi si unajua tulivyo wavivu wa kusoma bana,siku hizi viongozi wa Chadema hawaingii sana JF,lakini hapa ingekuwa vizuri zaidi uongozi wa Chama kuchukua idea tofauti kwa sababu sisi tuko nje ya uwanja tunaangalia game na tunaona makosa ambayo yanapaswa kurekebishwa,Chadema kwa sasa hivi kuna mapandikizi kibao kutoka ccm,kazi tunayo

Hapo ndipo naliona tatizo najua kuna watu wakiangalia uzi ulivyo mrefu anapotezea. Lakini ni ushauri mzuri kwa kipindi hiki cha miaka miwili uilyobaki unaweza ukatufikisha mahali fulani penye matumaini.
 
Nimeguswa sana na hii makala. Kama kuna yeyote atakayeisoma kwa umakini na kuifanyia utekelezaji wake, basi chaguzi zijazo itakuwa ushindi wa Kimbunga.
 
Asante sana mkuu kwa kufunua pazia la hali halisi ilivyo. Binafsi nakubaliana na wewe 100% Kama Chama kikizingatia swala la kujitengenezea mtandao nchi nzima na kuwajenga viongozi wapya wengi kila kitongoji, kijiji, kata, wilaya, mikoa, na taifa hapana shaka tutafanikiwa kuyaivisha mabadiliko yanayopikwa kwa moto mkali nchi nzima.

Lakini kuna lingine mkuu. Napendekeza kuwa chama kihakikishe kuwa kina vyombo vyake vya habari kama TV na Radio kabla ya 2015. Kama umemsikia mwenyekiti wa ccm katika hotuba yake leo wamejipanga kuwa na TV muda sio mrefu na kutumia vilivyo vyombo vya habari. Hii ina maana kuwa tusipokuwa na vyombo vyetu kuna hatari kubwa ya kufunikwa kiuenezi kwenye kampeni kwani ni rahisi sana kuvidhibiti vyombo vingine visitupe nafasi wakati wao wakijieneza kwa vile vya kwao.

Lingine, wabunge wetu wawe karibu na wananchi na kufanya mambo yanayoongea kwa sauti kubwa masikioni mwa umma, ili wajihakikishie kudumu na viti hivyo 2015, wasijisahau. Kampeni isisubiri 2015, ianze sasa kwa njia ya hizi juhudi ulizosema na haya niliyoyataja.
 
Asante sana mkuu kwa kufunua pazia la hali halisi ilivyo. Binafsi nakubaliana na wewe 100% Kama Chama kikizingatia swala la kujitengenezea mtandao nchi nzima na kuwajenga viongozi wapya wengi kila kitongoji, kijiji, kata, wilaya, mikoa, na taifa hapana shaka tutafanikiwa kuyaivisha mabadiliko yanayopikwa kwa moto mkali nchi nzima.

Lakini kuna lingine mkuu. Napendekeza kuwa chama kihakikishe kuwa kina vyombo vyake vya habari kama TV na Radio kabla ya 2015. Kama umemsikia mwenyekiti wa ccm katika hotuba yake leo wamejipanga kuwa na TV muda sio mrefu na kutumia vilivyo vyombo vya habari. Hii ina maana kuwa tusipokuwa na vyombo vyetu kuna hatari kubwa ya kufunikwa kiuenezi kwenye kampeni kwani ni rahisi sana kuvidhibiti vyombo vingine visitupe nafasi wakati wao wakijieneza kwa vile vya kwao.

Lingine, wabunge wetu wawe karibu na wananchi na kufanya mambo yanayoongea kwa sauti kubwa masikioni mwa umma, ili wajihakikishie kudumu na viti hivyo 2015, wasijisahau. Kampeni isisubiri 2015, ianze sasa kwa njia ya hizi juhudi ulizosema na haya niliyoyataja.

Kila mmoja kwa nafasi yake aeneze chama bila kusahau ikifika wakati wa uandikishaji wapiga tujitokeze kujiandikisha
 
Back
Top Bottom