Elias Msuya
Senior Member
- Dec 23, 2011
- 173
- 671
Wakati Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akipambana na kesi zake mahakamani ikiwamo ya uhaini, wapo pia wanasiasa wa upinzani Afrika walioonja joto ya jiwe kwa serikali wanazozipinga na hata wengine kutupwa jela.
Kesi ya Lissu imekuja wakati akiongoza kampeni ya No Reforms No Election (Hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi), ambapo viongozi wa chama hicho walikuwa wakifanya mikutano ya hadhara mikoani.
Tuhuma za Lissu
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025 wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma muda mfupi baada ya kukamilisha mkutano wake wa jioni na kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam.
Aprili 10, 2025 Lissu alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam na kusomewa mashitaka na upande wa Jamhuri kuwa ni ya uhaini. Kwamba mshitakiwa alitengeneza nia kwa umma kwa kutoa maneno yenye kuashiria uasi.
Mbali na tuhuma hiyo, Lissu pia anatuhumiwa kwa makosa mengine yakiwamo ya kuchapisha taarifa za uongo kwamba, “Uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 uliharibiwa kwa maelekezo ya Rais (YouTube),” “Polisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi. (YouTube)” na “Majaji ni wa CCM hawawezi kutenda haki, ni wateule wa Rais wanataka uteuzi wa majaji wa rufani. (YouTube).”
Kesi ya Lissu iliyozua hisia kali miongoni mwa wanachama wa Chadema na Watanzania kwa ujumla, ilianza kusikilizwa Aprili 24 katika Mahakama ya Kisutu kwa njia ya mtandao.
Hata hivyo, Lissu aliyepo katika Gereza la Ukonga, aligoma kusikiliza kesi yake kwa mtandao, badala yake mawakili wake wapatao 31 walipambana wakiulalamikia upande wa Serikali kwamba haki za mteja wao zimeminywa kwani walikataliwa hata kukutana naye gerezani.
Endapo Lissu atakutwa na hatia katika kesi ya uhaini, hukumu yake ni kunyongwa hadi kufa.
Soma pia: Kesi ya Lissu yaahirishwa
Kesi ya Mbowe
Mwaka 2021, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu walishitakiwa kwa kesi ya ugaidi na walikutwa na hatia.
Mbowe alikamatwa pamoja na wafuasi wengine wa Chadema jijini Mwanza usiku wa kuamkia Julai 21, 2021 siku ambayo kulikua kufanyike kongamano kubwa la kudai katiba mpya lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha).
Siku chache kabla ya kukamatwa kwake, Polisi jijini Mwanza ilitangaza kuzuia kufanyika kwa kongamano hilo kwa sababu za kiusalama, lakini Mbowe alijitokeza mbele ya waandishi wa habari na kutangaza kwamba kongamano hilo lipo pale pale na litafanyika kama ilivyopangwa licha ya zuio hilo la Polisi.
Wafuasi wengine zaidi ya 10 waliokamatwa pamoja na Mbowe jijini Mwanza waliachiliwa huru na jeshi la polisi, ambapo Mbowe aliendelea kushikiliwa kabla ya kuunganishwa na wanaodaiwa kuwa walinzi wake kwenye kesi inayoendelea sasa ya ugaidi.
Katika kesi hiyo Mbowe alikuwa anadaiwa kula njama ya kutenda kosa la ugaidi kati ya Mei na Agosti mwaka 2020 akiwa katika Hoteli ya Aishi Mkoani Kilimanjaro, kosa la pili la Mbowe ni kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi kinyume cha sheria ya ugaidi kati ya tarehe hizo tajwa.
Katika kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imesema, Mbowe na wenzake watatu ambao walikuwa wanajeshi wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), Mohamed Ling'wenya, Halfan Bwire na Adam Kasekwa walikutwa na hatia ya tuhuma mbalimbali zikiwemo za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi.
Hata hivyo, Machi 5, 2022, Serikali iliifuta kesi hiyo ikisema haina nia ya kuendelea nayo na siku hiyo hiyo Mbowe alifika Ikulu ya Dar es Salaam kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan.
Baada ya mazungumzo hayo, CCM ilianza mazungumzo ya maridhiano na Chadema.
Kiiza Besigye
Nchini Uganda nako mambo ni magumu kwa wapinzani, kwani kiongozi wa Chama cha FDC, Kizza Besigye yuko rumande kwa zaidi ya miezi mitatu sasa.
Amewekwa kwenye chumba kidogo, katika jela ya Luzira, moja ya jela zenye ulinzi mkali zaidi Uganda.
Kwa mujibu wa mkewe, Winnie Byanyima chumba hicho chenye giza, ni kama uchochoro, na ni maalumu kwa ajili ya watuhumiwa wa ugaidi. Na kumfikia inakubidi kupitia karibu milango saba iliyofungwa na makufuli.
"Nilimtembelea Kizza Besigye kwenye selo yake, alikuwa amelala kwenye kitanda chumba kidogo ambacho kimechukua chumba kizima. Kulikuwa na milango sita au saba niliyopita mpaka kumfikia,” alisema Winnie akinukuliwa na vyombo vya habari vya Uganda siku chache zilizopita.
Kwa mujibu wa mkewe, Besigye anashikiliwa kwenye mazingira duni akisema kuwa. Lawama nyingi kuhusu yanayomsibu Besigye, yanaelekezwa kwa Rais Yoweri Museveni na serikali yake, ambapo mara kadhaa imekuwa ikikanusha kumpitisha kwenye masaibu.
Hata hivyo, Rais Museveni amekanusha madai hayo akisema ni ulaghai.
''Katika hili, Dk Besigye, alikuwa kwenye mgomo wa kutokula. Hiyo ni sehemu ya sababu ya yeye kuwa dhaifu kunakoonekana kwenye picha zilizoko magazeti. Je, huo sio ulaghai usio na msingi? Amenukuliwa Rais Museveni na Shirika la Habari la Uingereza (BBC).
Besigye alikamatwa jijini Nairobi nchini Kenya, Novemba 16, 2024, alipokwenda kwa shughuli zake binafsi, kisha akasafirishwa usiku wa manane kupelekwa Uganda, kabla ya kufunguliwa mashitaka ya kumiliki silaha kwenye Mahakama ya kijeshi.
Hata hivyo kesi yake ilihamishiwa katika Mahakama ya kiraia na Februari 21, alionekana kwa mara ya kwanza kwenye Mahakama hiyo akiwa kwenye kiti cha magurumu matatu akiendelea kuonekana dhaifu kiafya.
Kuhamishwa kwa kesi hiyo kulikuja baada ya makelele mengi kupigwa bungeni, nje ya bunge na hata jumuia za kimataifa kuhoji ni kwa nini ashitakiwe kwenye Mahakama ya kijeshi wakati yeye si mwanajeshi? alishastaafu miaka mingi
Katika mahakama ya kiraia Dk Besigye alifunguliwa mashataka mapya ya uhaini, na hivyo kuashiria kesi za awali alizokuwa akikabiliwa nazo katika mahakama ya kijeshi zimekufa.
Uamuzi wa Mahakama ya juu nchini humo uliotolewa Januari 31, kisheria uliikata makali mahakama ya kijeshi.
Mbali na kesi ya sasa, Besigye aliyewahi kuwa daktari binafsi wa Rais Museveni na mwanajeshi mstaafu, ameshapitia masaibu mengi
Alianza kionja machungu hayo kuanzia mwaka 1999, baada ya kuchapisha andiko 'kali' lilikosoa Serikali na chama cha Museven cha NRM lililoitwa: "An Insider's View of How the NRM Lost the Broad Base" lililochambua jinsi chama hicho kilivyopoteza ushawishi wake na kuachwa na wafuasi wake wa awali.
Juhudi zake za kuwania urais mara nne na mara zote kushindwa dhidi ya rais Museveni aliyetawala taifa hiyo kwa miongo karibu minne, zimekuwa pia chanzo cha mitafaruku anayopata.
Kwa mujibu wa sheria za Uganda, Besigye akikutwa na hatia ya vitendo vya uhaini adhabu yake ni kifo. Hivyo kwa Besigye, wafuasi wake na wengine wanaomuunga mkono, kesi hii ina maana kubwa kwa upande wao. Kwa sababu kama atakutwa na hatia kwenye kesi ya sasa maana yake adhabu itakayomkabili Besigye ni hukumu ya adhabu ya kifo.
Haya ni masaibu aliokutana nayo si mara moja, kutokana na aina za kesi zinazomkabili. Serikali na hata Rais Museveni mara kadhaa, amekana kuhusika na yanayompata Kizza. Hoja hapa, je atavuka kiunzi cha masaibu haya, akianza na kesi inayomkabili sasa yenye adhabu ya kifo?
Wapinzani Tunisia watupwa jela
Mahakama nchini Tunisia imewahukumu kundi la wanasiasa wa upinzani, wafanyabiashara na mawakili kifungo cha muda mrefu jela kwa makosa ya kula njama na ugaidi.
Washtakiwa walipewa kifungo cha hadi miaka 66.
Ni pamoja na viongozi wa National Salvation Front, muungano mkuu wa upinzani, ambao walikamatwa mnamo 2023.
Mashirika ya haki za binadamu yalielezea kesi hiyo kama jaribio la kuzima upinzani.
Rais Kais Saied alivunja Bunge baada ya kuchaguliwa mwaka 2019.
Mwaka jana alishinda muhula wa pili kwa kishindo, baada ya kuwafunga jela wapinzani na washindani wake.
Hata hivyo, mamia ya wananchi waliandamana katika mji mkuu wa Tunisia, Tunis, siku ya Jumapili Aprili 9, 2025 wakitaka kuachiliwa huru kwa wapinzani 20 wa Rais Kais Saied waliokamatwa tangu mwezi Februari.
Takribani waandamanaji 300 kutoka vyama vya upinzani walipeperusha bendera za Tunisia na kubeba mabango yenye picha za wafungwa kwenye maandamano yalixoandaliwa na muungano mkuu wa upinzani, National Salvation Front.
Tangu mwezi Februari mamlaka katika taifa hilo la Afrika Kaskazini zimewakamata zaidi ya wapinzani 20 wa kisiasa na watu binafsi.
Miongoni mwa waliokamatwa ni wanasiasa wa upinzani, mawaziri wa zamani, wafanyabiasha, wanaharakati wa vyama vya wafanyakazi pamoja na mmiliki wa kituo mashuhuri cha redio nchini humo, Mosaique FM, hatua ambayo imekosolewa vikali na watetezi wa haki za binaadamu kimataifa.
Rais Saied ambaye amechukua karibu mamlaka yote tangu alipolisimamisha bunge na kuifuta serikali, anadai waliokamatwa walikuwa magaidi waliohusika katika njama dhidi ya usalama wa taifa.
Wapinzani wanamshutumu kwa kuirejesha nchi hiyo iliyokuwa ya kidemokrasia katika utawala wa kiimla.
Reckya Madougou
Mwaka 2021 ulikuwa mbaya kwa kiongozi wa chama cha Les Démocrates nchini Benin, Reckya Madougou, baada ya kufungwa jela miaka 20 kufuatia kesi ya ugaidi iliyokuwa ikimkabili.
Madougou alihukumiwa kwa ufadhili wa ugaidi na mahakama maalum Desemba 13, 2021.
Alikuwa mtu wa pili kutoka upinzani kufungwa ndani ya kipindi cha wiki moja.
Benin, ambayo hapo awali ilisifiwa kama demokrasia ya vyama vingi, sasa imechukua mwelekeo wa kiimla chini ya Rais Patrice Talon, kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu.
Talon alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2016, akimshinda mgombea aliyependekezwa na rais aliyemaliza muda wake.
Mwaka huo wa uchaguzi (2021), wapinzani wake wakuu wote, akiwemo Madougou, walizuiwa kushiriki katika uchaguzi wa urais, ambao Talon alishinda kwa asilimia 86 ya kura.
Waziri huyo wa zamani wa Sheria alishtakiwa kwa jaribio la kuikosesha nchi utulivu kwa kufadhili watu waliopanga kuwaua wanasiasa mashuhuri. Wafuasi wake walisema mashtaka hayo yalibuniwa.
Awali Madougou alikuwa ametangaza nia yake ya kugombea urais Aprili 1, 2021; hata hivyo, uteuzi wake ulikataliwa kwa sababu hakuwa na saini 16 kutoka kwa mameya au wabunge wanaomuunga mkono.
Alikamatwa wakati wa mkutano na mwanasiasa mwingine wa upinzani huko Porto-Novo.
Msemaji wa serikali alimtuhumu kwa "kupanga kuwaua viongozi kadhaa wa kisiasa", lakini hakutangaza tarehe ya kesi.
Julai 9, 2021, mawakili wa Reckya Madougou waliwasilisha ombi la kumwachilia kwa muda mteja wao kwa mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kukabiliana na Uhalifu wa Kiuchumi na Ugaidi.
Alipatikana na hatia katika kesi hiyo, ambapo hakuna ushahidi uliowasilishwa, kwa mujibu wa timu yake ya mawakili.
“Ni siku ya giza kwa demokrasia nchini,” wakili wa Madougou, Renaud Agbodjo, aliambia BBC baada ya hukumu ya Jumamosi.
“[Hukumu yake] ni ishara ya kukandamizwa kwa demokrasia nchini Benin.”
Kabla ya hukumu kusomwa, Madougou aliambia mahakama: “Sijawahi kuwa, wala sitawahi kuwa gaidi.”
Aliongeza kuwa iwapo hukumu hiyo ya hatia itawafanya watu kutafakari juu ya yanayotokea nchini, basi “sitasema kuwa nimepitia haya bure.”
Wiki moja kabla ya hukumu ya Madougou, mahakama hiyo hiyo katika mji mkuu, Porto-Novo, ilimhukumu kiongozi mwingine wa upinzani, Joël Aïvo, kifungo cha miaka 10 kwa kula njama dhidi ya serikali.
Wapinzani wengine wa kisiasa wamekimbia nchi, na hata jaji mmoja aliyekuwa sehemu ya mahakama iliyomhukumu Madougou alikimbilia uhamishoni, akieleza kuwa alikabiliwa na shinikizo lisilovumilika kutoka kwa serikali.
Alikotokea
Madougou alianza taaluma yake ya kitaaluma kwa kushiriki katika kuendeleza mradi wa Nasuba telecom LC 2 International. Baadaye aliingia katika idara ya Mauzo na Masoko ya kampuni ya simu ya mkononi GSM BB Com.
Kisha akawa Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko katika Tunde Motors, ambao walikuwa na leseni ya kutengeneza magari ya Volkswagen kwa Benin. Mwaka 2006, alianzisha kampuni yake ya ushauri wa utafiti na mikakati iitwayo International Key Consulting.
Madougou alianzisha na kuongoza kampeni ya kiraia ya "Usiguse Katiba Yangu" (kwa Kifaransa: Touche pas à ma Constitution) nchini Benin kutoka mwaka 2004 hadi 2006, ambayo ilihamasisha kampeni zinazofanana nchini Senegal, Burkina Faso na Cameroon.
Madougou alihudumu katika baraza la mawaziri kuanzia mwaka 2008 hadi 2013. Uteuzi wake wa kwanza ulikuwa kama Waziri wa Fedha Ndogo, Vijana na Ajira kwa Wanawake.
Mipango aliyoanzisha iliwasaidia zaidi ya watu milioni mbili, wengi wao wakiwa wanawake, vijana, wajasiriamali wadogo na wakulima. Baadaye akawa Waziri wa Sheria. Baada ya kuondoka katika baraza la mawaziri, aliteuliwa kuwa Mshauri Maalum wa Serikali ya Togo.