Wanawake waathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,008
1,030
VCG11468503808.jpg

Kila ifikapo tarehe 8 Machi dunia inaadhimisha siku ya wanawake, yakiangaliwa mafanikio na juhudi za wanawake katika upande wa kihistoria, kiutamaduni na kisiasa. Siku hii pia inaangazia na kuunga mkono hatua zinazochukuliwa dhidi ya ukosefu wa usawa wa kijinsia duniani kote. Sote tunajua kuwa dunia isingeweza kuendelea mbele bila ya uwepo wa wanawake, ikimaanisha kuwa wanawake ni mhimili mkubwa katika sayari hii.

Kauli mbiu ya mwaka huu iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ni "Usawa wa kijinsia leo, kwa ajili ya kesho endelevu", ambayo inatambua mchango wa wanawake na wasichana duniani kote, wanaoongoza katika kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ili kujenga mustakabali endelevu zaidi kwa wote.

Kuendeleza usawa wa kijinsia katika msukosuko wa hali ya hewa na kupunguza hatari ya maafa ni moja ya changamoto kubwa zaidi ulimwenguni katika karne hii ya 21.

Suala ya mabadiliko ya tabianchi limekuwa na litaendelea kuwa na madhara makubwa na ya kudumu kwa mazingira yetu, maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Wanawake wanazidi kuonekana kama watu walio katika hatari zaidi ya kuathirika na mabadiliko ya tabianchi kuliko wanaume, kwani wengi wao ndio masikini duniani na wanategemea zaidi maliasili ambazo kwa sasa zimekuwa kwenye hatari kubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwenye mkutano wa mabadiliko ya tabianchi COP26 uliofanyika mwaka jana huko Glasgow, tulishuhudia wanawake wakitawala jukwaa hilo na kuonesha kwamba mabadiliko ya tabianchi hayana usawa wa kijinsia na kwamba hatua zinazochukuliwa katika nyanja hii zinahitaji ushiriki wa wanawake.

Tunapaswa kufahamu kwamba kuwekeza kwa wanawake na wasichana kunaleta matokeo makubwa ambayo yanaigusa jamii nzima, na maarifa waliyonayo wanawake yanahitajika sasa kuliko wakati mwingine wowote ule.

Katika nchi zinazoendelea, wanawake huwa wa kwanza kusimamia mazingira yanayowazunguka. Wanawake duniani hutumia maliasili na mifumo ya ikolojia kila siku, hasa pale wanapokwenda kuchota maji kwa ajili ya kupikia au kusafisha, kutumia ardhi kwa ajili ya kilimo na mifugo, kupata chakula kwenye mito na kukusanya kuni.

Kwa mujibu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, wanawake pia ni watu wa kwanza kuhisi madhara ya mabadiliko ya tabianchi, mathalan nchini Kenya baadhi ya wanawake wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 10 kutafuta kile wanachohitaji ili kulisha familia zao pamoja na kutafuta maji, muda ambao ungeweza kutumiwa kufanya mambo mengine muhimu. Lakini pia asilimia 80 ya watu wanaolazimika kuhama makazi yao kutokana na mabadiliko ya tabianchi ni wanawake.

Kwa China hatua kubwa imepigwa katika kulipa kipaumbele suala la mazingira na kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika kulinda mazingira na kukabiliana na madiliko ya tabianchi. Serikali ya China kila siku imekuwa ikijaribu kuboresha mazingira ya kuishi na maendeleo ya wanawake, na kuwafanya wanawake hawa kutekeleza wajibu wao kikamilifu katika kulinda na kuboresha mazingira, pamoja na kuwawezesha kuishi na kujiendeleza katika mazingira mazuri.

Kwa mujibu wa Ajenda ya 21 ya China na mahitaji ya kufikia lengo la Maendeleo ya Wanawake wa China, serikali katika ngazi zote zimehimiza kikamilifu ushiriki wa wanawake katika masuala ya utafiti wa kisayansi, tathmini, mipango, ubunifu na usimamizi wa mazingira.

Kwa sasa, idadi kubwa ya wanawake wanafanyakazi katika idara zinazohusiana na ulinzi wa mazingira katika ngazi mbalimbali, na wengine hata kuchukua nafasi za uongozi, huku takriban asilimia 30 ya maafisa wa ufuatiliaji wa mazingira na watekelezaji sheria nchini China wakiwa ni wanawake, jambo ambalo linahimiza wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli zisizo za kiserikali za ulinzi wa mazingira.

Likiungwa mkono na serikali, Shirikisho la Wanawake la China limeendesha kampeni za kuhamasisha jamii kama vile Mradi wa Kijani wa Machi 8, ambao unahusisha wanawake wanaojitolea zaidi ya milioni 100 kwa mwaka katika upandaji miti, ujenzi wa uzio wa miti au vichaka vinavyopandwa ili kulinda eneo, hasa eneo la shamba lisidhuriwe na upepo mkali na mmomonyoko unaosababishwa na upepo, na kudhibiti maeneo madogo ya mifereji ya maji.

Wahenga wanasema mcheza kwao hutuzwa, Mwaka 1999, Shirikisho la Wanawake la China lilishinda Tuzo ya Kimataifa ya “Global 500” iliyotolewa na Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa UNEP, kutokana na mchango wake mkubwa wa kuhamasisha wanawake kulinda mazingira, pamoja na jitihada zake za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
 
Back
Top Bottom