Wanasiasa Maji Moto huu ndio mwaka wenu

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,886
WANASIASA MAJI MOTO NDIO TUNAWATAKA, MAJI BARIDI WAPUMZIKE TU

Na, Robert Heriel

Watanzania tumeshachoka na wanasiasa maji baridi, tunahitaji mabadiliko makubwa kwa wale wanaotuwakilisha. Mwanasiasa akiwa zii hata anaowaongoza huwa zii! Mwanasiasa akiwa kapooza hata wananchi wake huwa mapooza. Mwanasiasa akiwa yupo yupo hata anaowaongoza huwa wapo wapo tu. Yaani wamezubaa zubaa. Lakini Mwanasiasa akiwa mchangamfu hata watu anaowaongoza huwa wachangamfu, mwanasiasa akiwa mtu anayejielewa hata watu wake huwa hivyo.

Mwanasiasa maji moto huunguza pasipo kupuliza, huchoma bila kukoma. Hupika kikaiva, huchemsha kikachemka, maendeleo ya uhakika. Tena huchochea hoja na kuzikoza akiwa kazichunguza.

Mwanasiasa maji moto huwezi kumkuta kalala bungeni kama Mama Mjamzito, huchangia hoja za wananchi wake, huwasilisha matatizo ya watu wake. Hupiga kelele na kukemea pale aonapo jamii yake inaonewa, inagomolewa na wagomoaji walaji wenye matumbo makubwa kwa kula miradi ya wizi.

Hatutaki wanasiasa maji baridi kazi kulala bungeni kisha huota ndoto za posho, na marupurupu. Wabunge wagonga meza na kusahau kugonga fikra zao kwa kutetea maslahi ya taifa hili. Wanasiasa wa hivi hatuwataki.

Mwanasiasa maji Moto ni Icon, kivutio, mtu mashuhuri anayefanya kila aina ya njia kuwakilisha wananchi wake, ni kivutio kwa kizazi kichanga, tena ni maarufu anayetambulisha jimbo fulani kwa taifa. Hatuwezi kukuchagua kiongozi ambaye hulitambulishi jimbo letu kitaifa na kimataifa. Mbunge hujawahi kuitwa hata kwenye vyombo vya habari kuelezea mambo kadhaa kuhusiana na siasa za nchi, na kulitangaza jimbo lako. Wewe ni maji baridi na kamwe raundi hii hatutakuchagua.

Wapo wanasiasa ambao taifa zima linawafahamu na wanawakilisha vyema majimbo yao hata kwa wale wasiowahi kufika huko wanafahamu jimbo fulani kutokana na siasa za mwanasiasa maji moto. Mathalani, Mbunge Msukuma, Sugu, Lema, Halima Mdee, Msigwa, Ester Bulaya, John Heche, Bashe, Zito Kabwe, Lisu, Jumanne Kishimba, miongoni mwa wengine. Ni mfano wa wabunge maji moto.

Sio libunge halina linachofanya bungeni, hata kutangaza jimbo lake kitaifa limeshindwa, maendeleo halileti wala jimbo analoongoza halifahamiki kwani amezubaa zubaa tuu. Jimbo nalo limezubaa zubaa tu, watu wake wamezubaa zubaa tuu. Lakini majimbo yanayoongozwa na wanasias maji moto huwa wamoto kama kiongozi wao, wajanja kama kiongozi wao, wachakarikaji. Sio majimbo yanayoongozwa na mapooza.

Kwa ngazi ya Urais, Kiukweli tuna kiongozi maji moto. Mhe. Rais ni mwanasiasa maji moto japokuwa anakataaga kuwa yeye sio mwanasiasa. Mhe. Rais hajazubaa zubaa kama boya. Na hatutaki mtu aliyezubaa zubaa. Mtu aliyepoa. Rais akizubaa nchi nayo huzubaa, akipooza nchi nayo hupooza. Akiwa maji baridi watu hujikunyata, hatutaki Rais wa hivyo.

Rais Magufuli anatutangaza vyema kimataifa kwa siasa zake maji moto, Siasa zinazounguza, zinazochoma na kuchemka kuivisha maendeleo ya nchi hii. Siasa maji ya moto ni za kibabe, ukora, upende usipende utaiva tuu, utafuata kile kilichopangwa, kwa hiyari au kwa lazima. Sio unachagua jitu linalia lia kama lipumbavu. Jitu likiambiwa fanya hivi linafanya pasipokufikiri hilo halitufai. Likapumzike na familia yake huko.

Napendekeza kwa upande wa upinzani, wamuweke Mhe. Tundu Lissu nafikiri ndio atawezana na Mhe. John pombe Magufuli kwani wote ni siasa maji moto. Sio mtuwekee vitu vya ajabu, vitu vilivyopoa. Hatutaki wanasiasa viporo yaani waliolala wakapigwa na baridi. Mwanasiasa maji baridi ni kama kiporo hata apashwe bado atakuwa kiporo tuu. Hatuwataki.

Ingefaa Mhe. Magufuli angekuwa na umri mdogo walau miaka 50 ili aongoze walau mihula minne ili aichemshe hii nchi mpaka maendeleo yaive.

Wanasiasa wengi wa upinzani ni maji moto, ndio maana Magufuli huwapenda na kuwachukua kwani wanafanana mienendo, sio majitu yaliyopoa. Yanayoshindwa kuitetea nchi. Hao hatuwataki.

Watanzania hatutaki kuzubaishwa na wanasiasa waliozubaa. Huu ni muda wa kuifanya nchi hii iwe taifa kubwa.

Kumekucha!

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
 
Watu wa Kwimba natamani wasome hapa kuna bwana kajimilikisha jimbo huku barabara ya lami kufika tu makao makuu ya wilaya kutoka barabara kuu ya Mwanza Shinyanga kashindwa kuomba iwekwe lami kwa zaidi ya miaka10 na bado anarudi kuomba kura badilikeni nyie watu kama mnasoma hapa Aibu gani hii mmekosa wazawa wa kuwawakilisha?
 
Back
Top Bottom