Wanaosubiri kunyongwa magerezani wafikia 465

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
IDADI ya Watanzania wanaosubiri kunyongwa imekuwa ikiongezeka na hadi sasa imefikia 465 kutokana na hukumu ya kifo kutotekelezwa tangu mwaka 1994. Ripoti iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika mafunzo kwa waandishi wa habari mjini Morogoro juzi, imebainisha kuwa hakuna hukumu yoyote ya kifo iliyosainiwa na Rais ili kutekelezwa hadi Oktoba 2015 kulipofanyika Uchaguzi Mkuu ambao Rais Magufuli aliibuka mshindi.

Ripoti hiyo ya Mpango wa Kujitathmini Kuhusu Hali ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu (UPR), unaotekelezwa kwa mara ya pili nchini, imeonesha kuwa kuna mahabusu 465 wanaosubiri adhabu ya kifo, kati yao wanaume ni 445 na wanawake ni 20.

Wanaharakati Akiwasilisha ripoti hiyo, Ofisa Uchunguzi Mkuu wa Tume hiyo, Philemon Mponezya, alisema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, inaitaka Serikali kufuta adhabu hiyo kwa kuwa haitekelezeki lakini baadhi ya asasi hasa zinazohusika na haki za walemavu wa ngozi, zinapinga kufutwa kwa adhabu hiyo.

Baadhi ya asasi zinazopinga kufutwa kwa hukumu ya kifo ni taasisi ya Under The Same Sun (UTSS), ambayo inasema katika utafiti waliofanya, wahusika wanataka hukumu hiyo hasa inayohusu watu walioua albino, itekelezwe mpaka hapo mauaji hayo yatakapokoma.

Hata hivyo, Mponezya alisema watetezi wengi wa haki za binadamu wanataka adhabu hiyo ifutwe kwa kuwa ni kinyume cha haki za binadamu na kwa Tanzania, imekuwa mbaya zaidi kwa kuwa baadhi ya wahukumiwa wamesubiri zaidi miaka 20 bila hukumu dhidi yao kutekelezwa, jambo linalowaathiri kisaikolojia.

“Tume inasisitiza Serikali iangalie upya hukumu hii na kuiondoa kwa sababu ya utekelezaji wake. Tangu mwaka 1994 hadi leo watu 465 wanasubiri adhabu hiyo, hakuna aliyenyongwa. Kila mlango unapogongwa unahisi ni wewe kumbe la, tunadhani iondolewe maana haitekelezwi,” alisema Mponezya.

Wananchi wagawanyika Tume hiyo ilikiri kwamba, Tanzania imeshindwa kutekeleza adhabu hiyo kwa miaka mingi kutokana na Serikali kueleza kuwa jamii imegawanyika kuhusu hukumu hiyo. Wapo wanaotaka ifutwe lakini wengi wanataka iendelee kutekelezwa kutokana na ongezeko la mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina na albino.

Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mark Mulumbo, alipotakiwa kufafanua kuhusu mtazamo wa kisheria na kiserikali kuhusu utekelezaji wa adhabu hiyo katika mafunzo hayo, alikiri kwamba tafiti zilizofanywa nchini zimeonesha kuwa, kuna mgawanyiko kwa wananchi kuhusu adhabu hiyo.

“Tume kadhaa zilizoundwa kupata maoni ya wananchi, zilitoa matokeo kuwa wananchi wengi bado hawataki adhabu iondolewe, wanataka iendelee kuwapo, sasa Serikali inafanya kazi kwa matakwa ya wananchi, si vinginevyo,” alisema Mulumbo.

Akifafanua zaidi, alisema hata katika mchakato wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hali hiyo ilijitokeza kwamba Watanzania wengi hawaoni kama muda ni mwafaka kufuta adhabu hiyo. Marais Kuhusu marais kushindwa kusaini hukumu hiyo, Mulumbo alisema upo mtazamo wa aina mbili kuhusu jambo hilo; wa kiimani na kisheria.

Alisema pamoja na kwamba nchi haina dini, marais wote waliowahi kuchaguliwa mpaka wa Awamu ya Tano, wana imani za kidini. “Siwasemei kwamba imani zao ni sababu, lakini huenda ni sababu.

Ila kisheria rais hahukumiwi akisaini hukumu hiyo, sasa hilo mimi siwezi kulisemea ila sheria zinaweza kuangaliwa zaidi, ili zimpe rais nafasi ya kumpa mhusika kifungo cha maisha. “Lakini hapo napo kuna mtazamo mwingine, maana kuna hoja kwamba kwa nini aliyeua na kupatikana na hatia afungwe maisha. Je, iko wapi haki ya aliyeuawa?” Alifafanua Mulumbo kwa mtazamo wake.

Wanaoipenda Mwanasheria wa UTSS aliyewasilisha mada katika mafunzo hayo, Perpetua Senkoro, ambaye pia ana ulemavu wa ngozi, aliliambia gazeti hili kwamba, utafiti uliofanywa na taasisi hiyo kwa walemavu wa ngozi (albino) kuhusu hukumu hiyo, umeonesha jamii inataka iendelee kuwapo, na itekelezwe.

Senkoro alisema wana imani sawa na wanaharakati wenzao wa haki za binadamu kuwa dhana ya hukumu ni kumfanya mkosaji abadilike na hukumu ya kifo haitoi nafasi ya kubadilika, lakini kwao kutokana na namna wanavyouliwa kwa imani za kishirikina, hilo si suala la tabia bali ni imani na hivyo muuaji hawezi kubadilika, wanaona heri iendelee kuwapo na itekelezwe.

“Wengi wa jamii yetu wanataka hukumu iendelee kuwapo mpaka hapo mauaji kwa albino yatakapokoma na itekelezwe. Wauaji wa albino wanaua kwa imani si tabia, wanatumwa na watu wenye fedha, kiungo kinauzwa Dola za Marekani 2,000, tena tunaona wanaokamatwa ni vidagaa, bado mapapa hatuyaoni, tunaomba Serikali (ya Magufuli) iwatafute vigogo na tuone hukumu hii ikitekelezwa ili kumaliza imani hizi zinazowanyima haki baadhi yetu ya kuishi,” alisema Senkoro.

Pamoja na Tanzania kuridhia mapendekezo kadha wa kadha ya haki za binadamu, bado Mei 9 hadi 12 mwaka huu, katika mkutano wa Geneva, Uswisi itaulizwa utekelezaji wa mapendekezo mengine na msimamo wa nchi kuhusu kufuta adhabu ya kifo.

Mkutano huo utahudhuriwa na asasi mbalimbali za utetezi wa haki za binadamu nchini, viongozi wa serikali pamoja na tume za haki za binadamu, ambapo nchi zaidi ya 190 zinatarajiwa kushiriki.

Ripoti mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, imeonesha kuwa idadi ya watu waliouawa mwaka 2015 katika utekelezaji wa hukumu ya kifo ni kubwa zaidi tangu mwaka 1990.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 1,634 waliuawa mwaka jana sawa na asimilia 50 ya waliouawa mwaka 2014. Aidha takwimu hizo hazihusu utekelezaji wa hukumu hiyo nchini China, ambako takwimu za adhabu hiyo huwa siri ingawa zinatajwa kuwa kubwa. Nchi zinazotajwa kutekeleza zaidi hukumu hiyo mwaka jana ni Iran, Pakistan na Saudi Arabia ambako asilimia 90 adhabu hiyo ilitekelezwa.
 
Kuua si mchezo mkuu mambo hayo wanaweza waarabu na wazungu huko ila hata km raisi si sign hiyo kitu na watumikie kifungo tu mpaka wafie jela
 
Ningekuwa na mamlaka ningesaini wauwawe kwa sababu watu hawana huruma hata kidogo mtu anaua makusudi kabisa halafu eti haache tu haiwezekani. chukua mfano kuna hawa wanaoua ndugu zetu albino kwa tamaa ya fedha, eti waache tu kisa haki za binadamu. Kama wao wameshindwa kulinda haki ya kuishi za binadamu wenzao, hakuna sababu za kulinda haki zao za kuishi. Upanga kwa upanga
 
Marais wote wanaogopa sana kusaini hati za kunyongwa! Inawezekana sababu ya imani zao za dini! Wakati wa Mwinyi nadhani ukata wa serikali kuhudumia wafungwa ilipungua ndio maana akawapungua kwa kuwanyonga! Kama suala la imani Mzee Mwinyi nae mshika dini hasa!......sehemu wanayokaa .inaitwa "condemn wing"
 
Ningekuwa na mamlaka ningesaini wauwawe kwa sababu watu hawana huruma hata kidogo mtu anaua makusudi kabisa halafu eti haache tu haiwezekani. chukua mfano kuna hawa wanaoua ndugu zetu albino kwa tamaa ya fedha, eti waache tu kisa haki za binadamu. Kama wao wameshindwa kulinda haki ya kuishi za binadamu wenzao, hakuna sababu za kulinda haki zao za kuishi. Upanga kwa upanga
Nchi yetu kwa bahati mbaya imejaa rushwa kupita kiasi. Dhana ya kwamba wany'ongwe inaweza kusababisha hata wale waliofungwa kimakosa kuuawa. Ni vyema adhabu ifutwe maana watakufa watu wasio na hatia
 
Nchi yetu kwa bahati mbaya imejaa rushwa kupita kiasi. Dhana ya kwamba wany'ongwe inaweza kusababisha hata wale waliofungwa kimakosa kuuawa. Ni vyema adhabu ifutwe maana watakufa watu wasio na hatia
hao wa kuonewa ni wadogo kuliko wale wanaostahili kunyongwa, kumbuka hizo takwimu ni kuanzia mwaka 1994, lakini wewe mwenyewe kila siku unasikia majambazi yaua, albino auwawa nk, hivyo bola kuwanyonga tu watu waishi kwa amani.
 
alie uwa kwa upanga afe kwa upanga! nakumbuka mwaka jana kuna raia wa Australia/Marekani/india/south africa! walikamatwa INDONESIA na madawa ya kulevya!na sheria za nchi ya Indonesia zinasema Adhabu ya kukamatwa na madawa ya kulevya ni kifo kwa RISASI! nchi watokazo wakajaribu kuomba! wamarekani wakatuma madiplomasia! waustralia nao! Media za Dunia zikawa na kampain!kumbuka INDONESIA ni nchi ndogo enye Uchumi wa kati!
lakini msamamo ukawa pale pale lazma wafe kwa RISASI! na ilipofika siku wote RISASI na wazungu ilibidi wakubaliane na Sheria na maamuzi ya INDONESIA!
dah ifike mahali Sheria na maamuzi yanatolea ili kuweka heshima katika utawala wa Sheria wa Nchi yeyote na pili kunakuwa na Woga na Heshima katika Sheria ya nchi!
 
hao wa kuonewa ni wadogo kuliko wale wanaostahili kunyongwa, kumbuka hizo takwimu ni kuanzia mwaka 1994, lakini wewe mwenyewe kila siku unasikia majambazi yaua, albino auwawa nk, hivyo bola kuwanyonga tu watu waishi kwa amani.
Kwanza utafiti unaonyesha kuwa kunyonga hakupunguzi uhalifu. Lakini pia hao wachache ambao wako magerezani kwa kuonewa hawastahili kunyongwa. Utawachambua vipi?
 
Mimi napendekeza adhabu ya kifo ibaki kwa mafisadi tu maana ndio wauaji wakubwa. Mabilioni ambayo yangenunua dawa kuokoa maisha ya mama na vichanga vyao wanateketeza na kufanya mama hao na vichanga kufariki.
 
Back
Top Bottom