Wananchi wanahitaji kuelimishwa zaidi

drclark

Member
Feb 10, 2016
57
95
wananchi+waelmishwe_1.jpg

Bomoabomoa ya vibanda vya biashara na nyumba zilizojengwa kinyume na sheria katika maeneo ya wazi, kwenye vyanzo vya maji au kwenye hifadhi za barabara imekuwa ikiendelea katika maeneo mbalimbali nchini. Mara zote waathirika wamekuwa wakiilaumu Serikali kwa kutozingatia masilahi yao na kwa kweli wengi wao wameachwa katika hali ya umaskini uliotopea.

Mamia kwa maelfu ya wananchi wameathirika na bomoabomoa hii katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuitaja michache Dar es Salaam, Arusha, Kilimajaro, Mwanza, Shinyanga na Mbeya. Ni mchakato wenye dhamira nzuri ya kuweka miji na majiji safi na kutunza vyanzo vya maji na hifadhi za barabara. Hata hivyo, mpaka tatizo hilo linakua, inaonyesha kuwa mamlaka husika zilikuwa hazifanyi kazi zake ipasavyo.

Wananchi wanaonekana wanachimba misingi katika maeneo wasiyopaswa kujenga, wanapandisha kuta, wanapaua na kuweka bati, milango na madirisha kisha wanaunga miundombinu yote muhimu kama vile maji na umeme. Wanajenga shule, hospitali na maduka, mji unakua na unatanuka, wadai kodi wanawapitia na wanalipwa, mara siku moja Serikali inashtuka kutoka usingizini na kuwaambia wahame.

Wapo wanaopewa fidia na wapo wasiopewa kwa sababu tokea awali eneo lilikuwa limeshaelezwa matumizi yake na wananchi wamelivamia. Tunachojiuliza ni je, wakati watu wakijenga katika hifadhi za barabara, serikali za mitaa na halmashauri za miji zilikuwa wapi?

Kama wananchi hao hawakupaswa kuwapo kwenye maeneo hayo waliyovamia kwa nini walipelekewa huduma muhimu kama maji na umeme? Wananchi hawa wanalipa bili, kodi za majengo na leseni za biashara, wakati wakifanya hivyo hawaulizwi makazi au majengo yao ya biashara yako wapi, hawaulizwi kama yako kihalali au la? Mamlaka zinachojali ni makusanyo tu, kwa kufanya hivyo kimsingi Serikali haiwatendei haki wananchi hawa waliojenga matumaini ya maisha katika maeneo wanayoishi au wanayofanyia kazi.

Tunadhani mamlaka husika zina wajibu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujenga au kufanya biashara katika maeneo ya wazi na hifadhi za barabara. Wenye mamlaka wanapaswa wadhibiti mapema ujenzi holela, wasingojee mpaka wananchi wawe wameshastakimu ndipo wawabomolee walivyovijenga, kwani kwa kufanya hivyo huhisi kuwa wameonewa hivyo, kujenga chuki kwa Serikali. Familia nyingi zimepoteza wapendwa wao kutokana na mishtuko iliyotokana na hatua hizi, zimepoteza nyumba na mali zao na kuharibiwa mustakabali wa maisha yao.

Binadamu yeyote anayo haki ya kupata makazi. Haki hii inapaswa itimizwe na Serikali kwa upande mmoja na mtu mwenyewe kwa upande wa pili. Serikali yetu haina uwezo wa kutekeleza haki hii kwa raia wake wote, lakini wapo raia waliojaribu kujitafutia makazi na hatimaye wakajikuta wametimuliwa kwa kuwa walipojenga hapakustahili, ni eneo la wazi au ni hifadhi ya barabara.

Hawa wanahitaji waeleweshwe taratibu mapema kabla hawajapoteza fedha na nguvu zao, mwishowe wataelewa na watafuata sheria, tofauti na sasa ambapo wanapotenda kinyume cha sheria wanaangaliwa tu kwani iko siku Serikali itawakomesha. Serikali haiko kwa ajili ya kukomesha wananchi, bali kuwasaidia.

Utii bila shuruti katika jambo lolote lile unawezekana, lakini kwanza wananchi wanahitaji wapewe elimu ya kutosha kuhusu nini wanapaswa kufanya ambacho ni sawa na nini hawapaswi kukitenda kwa sababu ni kinyume na sheria.


Chanzo: Mwananchi
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom