Wananchi wamechoka, watawala wamekwisha | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Wananchi wamechoka, watawala wamekwisha

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Sokomoko, Oct 19, 2008.

 1. Sokomoko

  Sokomoko JF-Expert Member

  #1
  Oct 19, 2008
  Joined: Mar 29, 2008
  Messages: 1,918
  Likes Received: 22
  Trophy Points: 135
  NILIWAHI kuandika habari za kiongozi mmoja wa juu wa CCM ambaye alikifananisha chama chake na puto lililojaa pumzi; kwamba sasa linakaribia kupasuka.

  Alikifananisha pia na himaya ya Kirumi iliyodumu na kutamba kwa karne kadhaa, lakini hatimaye ikaangushwa na wapambe wa Kaizari.

  Wiki hii, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad, amesema nchi imevimba, inakaribia kupasuka. Ana ujumbe ule ule, mzito kwa watawala.

  Nina hakika kwamba watawala wanayaona na kuyasikia yanayotokea sasa nchini; na wanajua chanzo chake – kiburi na jeuri yao! Naamini hakuna kiongozi yeyote wa serikali atakayesimama na kutamka hadharani, walau kwa sasa, kwamba Tanzania ni nchi ya amani. Amani haipo tena!

  Sina shaka pia kwamba viongozi hawa watakiri, walau kwa mara ya kwanza, kwamba ‘upendo’ wa wananchi kwa serikali ya awamu ya nne umekwisha.

  Kama hawataki kukiri ukweli huu (kwamba amani imetoweka na kwamba wananchi wameichoka serikali), basi wakubali kuendelea kupigwa mawe na wananchi kwa visingizio mbalimbali.

  Naamini pia kwamba wakati mapambano ya walimu yanaendelea, zamu ya polisi na wauguzi inakaribia, maana wote hawa wamo katika kundi la watumishi wa umma wanaonyonywa, wanaodharauliwa na kupuuzwa na serikali ile ile kwa muda mrefu.

  Kwa bahati mbaya, makundi haya, hasa walimu na polisi wamekuwa wakitumiwa na serikali (na CCM) kuendekeza na kupalilia unyonyaji huu – hasa wakati wa uchaguzi.

  Matokeo ya ushabiki wa polisi na walimu kwa CCM – kwa visingizio vya nidhamu ya utumishi na posho za kuwadhalilisha – ni sehemu ya tatizo lililowafikisha hapo walipo; wao na jamii nzima.

  Kwa sababu serikali imezoea kuwatumia wakatumika, imewafanya wao kuwa sehemu ya vyombo vyao vya kunyanyasia wananchi. Serikali inasahu kwamba polisi na walimu ni dada, kaka, baba, mama, wajomba na shangazi zetu. Wana mahitaji yale yale kama wananchi wengine; na wanastahili heshima na haki zile zile wanazopewa watumishi wengine wanaolipwa manono.

  Imewachukua muda mrefu sana walimu kutambua nafasi yao katika jamii na kutetea haki zao. Kwa taaluma yao, walimu ndio walipaswa kuisaidia jamii kujitambua, kujitetea na kujikwamua.

  Walimu wanapaswa kuwa werevu, na wana jukumu la kuendelea kutufundisha kuhusu misingi na mbinu za kujinasua katika manyanyaso ya serikali. Wao ni wanyanyasika kama sisi. Wanachofanya sasa, ni sehemu ndogo ya elimu ya uraia kwa vitendo.

  Naamini kwamba baada ya mapambano haya ya walimu na serikali, kama walimu hawatanywea na kujikomba tena kwa mwajiri asiyejali maslahi yao, heshima ya walimu itapanda, na maslahi yao yataongezeka; na hawatakubai tena kuwa vibaraka wa mafisadi.

  Kwa jinsi tunavyojua uvumilivu na uungwana nwa walimu wetu, kama wamefikia mahali pa kumshambuliwa rais wao kwa mawe, viti na chupa za maji (kwa kauli yake ya kuahirisha mgomo wao) ni ishara kwamba serikali imewamefikisha pabaya.

  Watanzania hawatawalaumu walimu, bali serikali iliyowafikisha hapo. Na sasa ujasiri wa walimu hao umeigwa na wazee wastaafu Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika 1977, ambao kama ilivyo kwa walimu, nao wamechoshwa na unyanyasaji wa serikali.

  Wiki hii wamekusanyika mbele ya Wizara ya Fedha kudai haki zao, wakazuia magari kuingia na kutoka wizarani; serikali ikawaitia polisi ambao waliamua kutumia nguvu kuingiza magari hayo. Lakini wazee wakaamua kuyadhibiti kwa kupasua kioo cha gari mojawapo.

  Polisi walikosea. Harakati za wazee hawa si fujo kwa mtu yeyote. Wanatafuta haki yao, na wanawatetea hata polisi wenyewe; maana yawezekana baadhi yao wana watoto ambao ni askari.

  Na adha ya askari wa Tanzania inafahamika. Leo ni wazee hawa, kesho ni wao. Na hao wanaowatuma polisi kupiga wazee, ndio watakaokuwa wanawatumia polisi wengine kesho kuwapiga polisi wastaafu.

  Na kama polisi nao wangejitambua mapema, wangeibana serikali vilivyo iboreshe maslahi yao sasa kabla vuguvugu la walimu, wanafunzi, wastaafu na watumishi wengine wa umma halijapoa.

  Polisi wetu wasiishie kutii amri za kutembeza vipigo kwa wazazi wao; wanapaswa wawe sehemu ya harakati za kuikomboa jamii. Serikali imezoea kutumia polisi kupambana na nguvu za vijana; na mara kadhaa wamefanikiwa kuwaumiza kaka na dada zao kwa ajili ya kulinda utii wao kwa mafisadi.

  Lakini funzo walilolipata Tarime linapaswa kuwaamsha na kuwajenga upya polisi wetu. Wajue kuwa wananchi sasa wameamka. Wako tayari kupambana na nguvu zozote za giza zinazotumiwa na serikali.

  Kwamba mamia ya askari waliopelekwa Tarime kudhibiti wapinzani kwa kisingizo cha kulinda amani wameshindwa kufurukuta, ni ishara kwamba umma ukiamua, jiwe la haki linaweza kuwa na nguvu kuliko risasi ya dhuluma.

  Katika wiki hii hii, tumesikia pia habari za msafara za Rais Jakaya Kikwete kushambuliwa kwa mawe mkoani Mbeya. Ni habari za kusikitisha. Binafsi, sina kumbukumbu ya msafara wa rais kushambuliwa na wananchi. Lakini naamini serikali itatumia akili katika kulichunguza tukio hili, na kudhibiti mengine kama hayo siku zijazo.

  Wananchi hawa si vichaa. Hata sababu zilizotolewa na serikali kwamba wananchi walishambulia msafara wa rais kwa kuwa walikuwa na kiu ya kumuona lakini hakusimama kijijini kwao kwa sababu ya giza, hazieleweki kwa watu wenye kupenda kufikiri na kutafakati kidogo.

  Wananchi wanaompenda kiongozi wao hawamrushii mawe kumdhuru yeye au watu walioambatana naye. Najua serikali yenyewe haiamini kauli yake, ndiyo maana imemwaga mashushushu mahali hapo kuchunguza sababu za kitendo hicho.

  Hata hivyo, tunapaswa kujiuliza. Kwanini sasa wananchi wanaonekana kushabikia urushaji mawe? Huu ndio ukomo wa uvumilivu wao wa siku nyingi? Ndiyo njia mpya ya kujieleza kwamba wamechoka kupuuzwa?

  Ndiyo njia ya kuwafanya wakubwa wawasikilize? Je, baada ya mawe watatumia silaha gani? Je, wakubwa wapo tayari kujifunza kutokana na mawe wanayorushiwa na wananchi? Au wataendelea kuwatuma polisi warushe risasi kudhibiti mawe hayo? Je, watafanikiwa?

  Baada ya matukio ya Tarime, mgomo wa walimu, wastaafu wa Afrika mashariki na fujo za wananchi Mbeya dhidi ya msafara wa rais, serikali imepata ujumbe?

  Maana inawezekana wakubwa wanaendelea kujidanganya kwa kauli kama zilizotolewa wiki iliyopita na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alipokuwa akilishutumu gazeti la MwanaHALISI kwa habari za kundi la wana-CCM wanaotaka kumwondoa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2010.

  Alisema: “Unamng’oa vipi rais ambaye utendaji wake wa kazi umeleta mafanikio makubwa kwa wananchi na umekuwa mfano wa kuigwa mbele ya mataifa mengine? ‘Hakuna tishio lolote, hakuna njama zozote za kumng’oa rais madarakani, iwe ni leo au mwaka 2010, kama gazeti hilo lilivyodai... kama kungekuwa na njama hizo mtu wa kwanza kujua angekuwa ni rais mwenyewe, kwani rais ana vyombo vya ulinzi na usalama.”

  Ndiyo! Vyombo hivyo vya ulinzi na usalama (wa rais) vinaweza kugeuka leo na kuwa vyombo vya ulinzi na usalama wa wananchi. Havitalinda uozo wa watawala, bali vitawasaidia wananchi kuondokana na tatizo. Na hata kama vyombo hivyo vinahakikisha kwamba rais yuko salama - kama Rweyemamu alivyosema - haina maana kwamba usalama wake ni kukaa madarakani.

  Ukweli ni kwamba wanaotaka kumwondolea rais mzigo wa uongozi wanampenda, na wanaijali nchi yao. Lakini ukweli ni kwamba kauli ya serikali kupitia kwa Rweyemamu inaonyesha upofu wa watawala; au ni mkakati wa makusudi wa kupotosha ukweli katika mazingira magumu.

  Tuulizane. Ni kweli kwamba uongozi wa Rais Kikwete umeleta mafanikio makubwa kwa wananchi?

  Mwaka jana mwishoni, ripoti ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilisema kwamba imani ya Watanzania kwa serikali ya awamu ya nne imeshuka mno.

  Umaarufu wa Rais Kikwete ulikuwa ameshuka kwa asilimia 23. Hiyo ni baada ya miaka miwili tu ya utawala wake. Kati ya Desemba mwaka jana na sasa, hakuna la maana ambalo serikali yake imelifanya kurejesha imani ya wananchi.

  Kwa mtazamo wa jumla, serikali imekwama; uchumi umedorora; maisha ya wananchi yamezidi kuwa magumu kutokana na kupanda kwa gharama za maisha; na ufisadi umekuwa sifa mpya ya serikali ya Kikwete, na umekuwa kichocheo cha harakati mpya za wananchi dhidi ya serikali.

  Nguvu kubwa iliyokuwa imewekezwa kwenye magazeti na vyombo vingine vya habari ili kuijenga serikali (hasa Kikwete binafsi) mbele ya umma, imepwaya kwa sababu maisha halisi ni magumu kuliko makala tamu tamu za wapenzi wa serikali na chama tawala.

  Nguvu ya mashushu wanaojipendekeza kwa serikali imepwaya kwa sababu nao ni binadamu; wanafika mahali wanaona ukweli. Maisha magumu yanawaathiri wao na ndugu zao vile vile.

  Pesa za wizi na halali zilizo mikononi mwa vyombo vya dola na chama tawala zina kikomo. Haziwezi kununua kila kitu. Walau hadi sasa, zimeshindwa kununua mapenzi ya wananchi kwa serikali.

  Haziondoi chuki yao dhidi ya watawala walioahidi maisha bora ambayo hayajapatikana, na dalili hazionyeshi kama yatapatikana wakiwa madarakani.

  Vitisho dhidi ya wakosoaji wa serikali havifajua dafu kwa sababu serikali haina nidhamu; mambo ya kukosoa yanaongezeka. Woga wa wananchi kwa watawala umepungua kwa kiasi kikubwa, na uelewa wao wa masuala ya kisiasa umeongezeka.

  Propaganda za CCM na wapambe wake zimeshindwa kufanya kazi kwa sababu wananchi wa kizazi hiki ni waelewa kuliko wale waliokabidhiwa jukumu la kueneza propaganda za CCM. Matokeo yake, serikali haikubaliki kwa wananchi, na kizazi hiki kimeanza kujitambulisha zaidi na siasa zinazoitaka CCM ipumzike.

  Ni kizazi kinachotaka, na kimedhamiria, kuona CCM ikiachia madaraka katika ngazi za halmshauri, bunge na serikali kuu. Na wanaoyaona haya si wapinzani tu. Hata ndani ya CCM wamo watu wenye akili nzuri, waliochoka siasa za maigizo, wanaotaka kuendana na siasa zinazoakisi hisia na matarajio ya wananchi.

  Ushindani na kuchimbana miongoni mwao, vikichanganyika na kushindwa kwa serikali kuwapa wananchi matumaini, ndivyo vimechochea harakati za baadhi ya wana-CCM kuamua kuipindua serikali yao wenyewe.

  Baadhi yao wanaona aibu kwamba chama kikubwa chenye mizizi mirefu, wanachama wengi na rasilimali nyingi; kinaongozwa na kikundi kidogo cha watu wachache walafi, na wenye uwezo mdogo sana wa kuelewa, kupembua, kuandaa na kusimamia mikakati makini ya kukikwamua chama na taifa.

  Wanakerwa na mbwembwe na usanii unaotangulizwa katika uongozi wa chama na serikali. Wamefikia mahali hawaogopi tena kushindana na viongozi walio madarakani sasa.

  Lakini si wao tu. Wapo pia wale waliokuwa na Rais Kikwete tangu awali, waliomwandalia kila kitu na kumsindikiza hadi Ikulu; waliotarajia kuvuna kwa ari, nguvu na kasi mpya na kuwekeza katika kipindi cha utawala wake.

  Nao wanaona kwamba mwenzao amekwama, na ndiyo sababu hata wao wamekwama. Na wako tayari kujikwamua kwa gharama zote, hata ikibidi wamtose yeye.

  Haya yote yanaonekana, yanasikika. Yanatokana na ukweli kwamba serikali imekwama, wadau wanatapatapa.

  Yanaakisi kauli ya wananchi katika ripoti ya utafiti wa REDET kwamba sababu za wasioridhishwa na utendaji wa Rais Kikwete na asilimia zao zikiwa kwenye mabano, ni pamoja na kushindwa kwake kuboresha maisha kama alivyoahidi (asilimia 30.4), huku wengine wakidai kuwa ameshindwa kutimiza ahadi (asilimia 21.6), kutokufuatilia utekelezaji (asilimia 11.6), kuchagua viongozi wabovu (asilimia 9.1) na kushindwa kupambana na rushwa (asilimia 5.6).

  Wananchi wanaona, wanasema; na hata watumishi serikalini wanaona; wanasema hivyo, na wanalaumiana. Kama wana-CCM wangekuwa na ujasiri kama tulioshuhudia mwezi uliopita nchini Afrika Kusini, wangekuwa wamepiga kura ya kutokuwa na imani na uongozi wao.

  Lakini ukweli wa mambo ni kwamba, katika makundi yao mbalimbali, wana CCM wameshakubaliana kimya kimya kwamba wanahitaji uongozi mpya. Naamini na Watanzania wengine wanahitaji uongozi mpya kitaifa hata kabla ya 2010.

  Labda hii ndiyo tafsiri ya harakati kurusha mawe zinazojionyesha sasa katika makundi mbalimbali ya jamii. Wananchi wamechoka; watawala wanaendelea kudhani wanapendwa. Hawana habari; wamekwisha.

  ansbertn@yahoo.com +447885850425 Utakapojua Hujui Ndipo Utakapojua
   
Loading...