SoC01 Wanajali hela zetu hawajali afya zetu

Stories of Change - 2021 Competition

Prof Sankara

Member
Sep 17, 2021
6
10
Bila kujali wazee, vilema, watoto, akina mama wenye mimba, watu hupigana vikumbo kila siku kugombea viti kwenye daladala na mabasi ya mwendokasi.

Adha hii inayowawakabili wakazi wa jijini la Dar es Salaam na miji mingine mikubwa,haionekani kupata ufumbuzi bado.Katika purukushani hizo wakati mwingine huzua matusi machafu na ugomvi miongoni mwa watu wasio wastaarabu kwani hushindwa kujizuia pale wanapobanwa ama kukanyagwa lakini siyo kwa makusudi.

Yaani hii ni vita! nani akae nani,asimamame na nauli tumelipa sawa?.Bahati nzuri umepata siti, unajibwaga bila kuangalia kiti ulichokalia kina hali gani,je kipo safi? La!! Kimejaa vumbi tele nguo safi uliyoivaa inasawiri uchafu.

Kwa sababu umepata nafasi ya kukaa (kiti) kwa shida inakuwia vigumu kujiuliza swali hili.Hivyo unajikuta umekalia kiti ambacho hakijawahi kuoga maji ya Tanzania, kimejaa vumbi na chakavu,unalazimika kukaa tu kwa kuwa inakulazimu ili ufikie kilele cha safari yako.

Siyo hali ya kufurahisha wala kunyamaziwa kamwe, ni hatari kwa afya za watu, kwa kuwa njia mbadala ya usafiri ni ghali basi wengi tunadumbukia katika shimo hili hatari kwa afya zetu.

Wimbo wa wa kufokafoka (2013) wa msanii mzungu anayejiita Bodawi Poa unasadifu vizuri namna hali ya usafiri ilivyo ngumu Dar es Salaam. Wimbo huu unaoitwa Shika Bomba una mistari inasema.

Asubuhi tunaenda posta tumeshika bomba, kwenye daladala tumehika bomba.

Tunarudi kimara tumeshika bomba, wengine wamesimama wameshika bomba

Masista duu wanashika bomba, masharobaro wanashika bomba

Wanakanyagana wagombana, wamebanana wate wanashika bomba

Polisi na maofisa wanashika bomba, wote pamoja tunasonga.



Ukisikiliza na kutazama video ya wimbo huu unaweza kujiuliza kwanini huyu mzungu kaimba hivyo. Bila shaka anasema hali halisi ya usafiri ilivyo hapa Bongo akilinganisha na kwao Ulaya. Kwa maana nyingine anatukumbusha kuwa hali ya usafiri ni kwetu ni mbaya .

Dar es salaam ni jiji lenye joto kali, watu wengi na shughuli nyingi. Usafiri ni wa shida ndiyo maana Daladala zinajaza abiria hadi zinaenda upande. Abiria hubanana kukanyagana, kuvuta hewa nzito iliyochanganyika na harufu mbaya na jasho la abiria.

Swali ambalo haliulizwi sana na abiria ni kwanini tunasafiri katika magari (daladala) machafu namna hii? Afya zetu tunaziweka katika mazingira hatarishi na urahisi wa kuambukizwa magonjwa, vipi hali hii na madhara yake katika afya za abiria.

Kwa sababu ya uwepo ugonjwa wa UVIKO, pamekuwa na miongozo kadhaa juu ya utaratibu kwa vyombo wa usafiri wa umma. Moja ya maelekezo ya serikali ni kunawa mikono na kuvaa barakoa. Maelekezo hayo hayazingatiwi sana kwa wasafiri hata madereva. Hali ambayo inaongeza uwezekano wa maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO na magonjwa mengine yanayoambukizwa kwa njia ya hewa.

Ndani Daladala chafu, naingia bila kunawa mikono, sijavaa barakoa, nashika bomba, nikitoka nje sinawi naendelea na maisha.

Polisi wa usalama barabarani hukagua magari na kuhakiki leseni za madereva,sheria za usalama barabarani, na vifaa muhimu ndani ya gari ili kuwa na hakika usalama wa abiria wakati wote. Suala la usafi ndani ya gari halimo katika ukaguzi huo.Ndiyo maana daladala licha ya uchakavu zimejaa vumbi, na uchafu ambao ni hatari kwa afya za watu.

Mamlaka ya jiji miaka ya karibuni ilitagaza kwa madereva na Makondakta kuhakikisha ndani ya gari kuna kifaa cha kuhifadhia taka.Agizo hilo lilizingatiwa kiasi,ingawa vikapu venyewe vya kuhifadhia taka ni chakavu na vimetoboka toboka ovyo, mamlaka ilivyolegeza kamba hali ikarejea kama awali.

Usafi ndani ya daladala hauzingatiwi kabisa, makondakta,madereva ndio wahusika katika hili, mtu mwingine anaweza kuuliza inawezekanaje Kondakta na Dereva kusafisha gari ili hali yeye amavaa sare chafu ,iliyochanika na viraka juu?. Ni budi maafisa usalama barabarani wakaanzisha utaratibu wa kukagua usafi ndani ya gari na ikiwezekana sheria itungwe.

Miaka ya Sabini serikali ya Mwalimu Nyerere ilipitisha sera ya “Mtu ni Afya” kujaribu kuhimiza si tu usafi wa mwili bali mazingira na vyoo. Uzuri wa sera hiyo ulikuwa si tu kujenga mwamko wa lishe bali kuhimiza, siha na usafi kwa watu wote.

Suala a afya ni hitaji namba moja kwa maisha ya mwanadamu. Bila afya njema haiwezekani kufanya shughuli za kimaendeleo.

Wito kwa mamlaka husika kutoa mwongozo kwa wasafirishaji kuzingatia usafi katika vyombo vya usafiri ili kulinda afya za abiria.
 
Back
Top Bottom