dudus
JF-Expert Member
- Feb 28, 2011
- 22,125
- 49,384
- Watakaofeli mwaka huu kurudia darasa
- Kiwango cha ufaulu sasa ni alama 30
Serikali imetangaza rasmi kuurudisha mtihani wa kidato cha pili kwa shule zake na binafsi kwa lengo la kukabiliana na matokeo mabaya ya kidato cha nne.
Chini ya utaratibu huo, watahiniwa watakaofeli kwa kushindwa kupata wastani wa alama asilimia 30 kuanzia mwaka huu, hawataruhusiwa kuingia kidato cha tatu, badala yake watarudia darasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema serikali imeamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuona ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne umeshuka kwa asilimia kubwa.
Kuanzia mwaka 2012 mwanafunzi atakayepata wastani wa chini ya asilimia 30 katika mtihani wa kidato cha pili hataruhusiwa kuendelea na kidato cha tatu, alisema Mulugo na kuongeza:
Mwanafunzi huyo atatakiwa kurudia kidato cha pili na fursa hii itatolewa mara moja tu, na endapo atashindwa kwa mara ya pili kufikisha wastani wa asilimia 30 ataondolewa kabisa.
Aliongezea kuwa kutokana na uendeshaji wa mtihani huo kuwa mgumu kufuatia ongezeko la gharama za uendeshaji linaloendana na ongezeko la idadi ya shule na wanafunzi mwaka hadi mwaka, wazazi na walezi watatakiwa kuchangia Sh. 10,000 kwa kila mwanafunzi kwa shule za serikali na za binafsi.
Kila mzazi na mlezi atatakiwa kuchangia gharama za uendeshaji wa mtihani huo, kutokana na ongezeko la gharama za uendeshaji kuwa mkubwa, mtihani lazima utungwe, usaihishwe, matokeo yatolewe, hivyo gharama ya uchangiaji inahitajika, alisema.
Aliongeza kuwa mitihani ya taifa kwa kidato cha sita na nne kuanzia mwaka 2012 gharama yake itakuwa Sh. 35,000 kwa kila mwanafunzi.
Ikumbukwe kuwa gharama hizi ni zile ambazo wazazi na walezi walikuwa wakichangia kati ya mwaka 1999 na 2009 kabla ya serikali haijaamua kusitisha uchangiaji huo, alisema.
Mtihani wa Taifa wa kidato cha pili umekuwa ukigharimiwa na serikali toka ulipoanzishwa mwaka 1984 hadi 1994 ulipositishwa, na mtihani huo ulirejeshwa mwaka 1999 na wazazi walichangia gharama za uendeshaji hadi mwaka 2009 wakati serikali ilipoamua kuugharimia kwa kusitisha ada ya mtihani kwa shule za serikali.
Awali, Serikali iliondoa vikwazo kwa wanafunzi wa kidato cha pili pindi waingiapo kidato cha tatu kwa kuvuka pasipo pingamizi lolote.
SOURCE: NIPASHE - 12th January 2012