Wala 'kitimoto' hatarini kufa kwa sumu Dar

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
WATU wasiojulikana wanadaiwa kuua nguruwe 25 kwa sumu kali na hatimaye kuibeba mizoga ya nguruwe 18 kwa nia ya kuisambaza kwa walaji katika Jiji la Dar es Salaam.

Mabaki ya nguruweiliyobaki imegundulika kuwa na sumu kali ambayo imeua kunguru, mbwa, paka na kuku walioonja utumbo uliotoka kwenye nguruwe hao.

Kufuatia hali hiyo Ofisa Afya wa Kata ya Kimanga , Elika Sinkonde aliwatahadharisha wakazi wa eneo na Dar es Salaam wanaonunua nyama ya nguruwe kuhakikisha kwamba zimetoka kwa watu wanaojali masuala ya afya.


" Walaji wa nyama ya nguruwe maarufu kama ‘kitimoto' jijini wapo katika hatari ya kufa kwa sumu kama wanunua na kula ovyo nyama kutokana na kugundulika kuwepo watu wanaosambaza nyama yenye sumu", ilielezwa.

Tishio hilo la kuwepo kwa nyama ya nguruwe yenye sumu lilianza kusambaa jana mchana maeneo ya Tabata Shule baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumba ya mkazi wa eneo hilo, Deusdedit Kajuna ambaye ndiye mfugaji wa Nguruwe hao na kuwapa sumu kabla ya kuwaiba wakiwa wamekufa.

Mwananchi lilifika eneo la tukio na kukuta nguruwe wanane kati ya 25 wanaodaiwa kulishwa sumu wakiwa wamekufa huku wakitoka damu puani ambapo mbwa, kunguru, paka na kuku ambao walikula mabaki ya nguruwe hao nao walikufa.


Akisimulia mkasa huo Kajuna alisema, "Waliofanya tukio hili ni wazi kuwa walivamia hapa usiku wa kuamkia jana (juzi), walikuja na vyakula vyao vyenye sumu na kuwapa nguruwe," alisema huku akionyesha vyakula hivyo.


Alifafanua kwamba wezi hao walifanya hivyo kuogopa kugundulika wakiiba nguruwe na kuongeza kuwa baada ya kuwapa sumu waliwabeba na kuwapeleka katika majani na kuwapasua sehemu ya tumboni na kuwatoa utumbo.


"Asubuhi tulipogundua tukio hili tulifuatilia na kukuta utumbo ukiwa katika majani huku pembeni kukiwa na paka, kuku na kunguru wakiwa wamekufa, hawa walikufa baada ya kula ule utumbo ni wazi kuwa ulikuwa na sumu," alisema Kajuna.


Alisema kwamba baada ya watu hao kutoa utumbo wa nguruwe hao 18 waliwabeba na kuondoka nao na kuongeza kuwa mpaka jana licha ya kutoa taarifa polisi bado hajafahamu nyama ya nguruwe hao imeuziwa sehemu gani.


"Inauma sana, tena wamewapa sumu wale nguruwe waliokuwa wamenona, hawa saba waliowaacha walikuwa wadogo, wametumia ujanja wa hali ya juu, sikusikia kabisa tukio hilo licha ya kuwa nililala saa sita usiku," alisema Kajuna.


Baadhi ya majirani waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa tukio hilo hawakulisikia ila ilipofika asubuhi walikuta paka, kunguru, mbwa na kuku wakiwa wamekufa pembeni ya utumbo wa Nguruwe.


Polisi kutoka kituo cha Buguruni aliyejitambulisha kwa jina la Enock alisema kwamba hawezi kuzungumza lolote, lakini akakiri kwamba baadhi ya polisi pamoja na mabwana afya wapo mitaani kukagua nyama za nguruwe zinazouzwa.


"Siwezi kuzungumza lolote kwa sasa kwa kuwa mimi sio msemaji, ila mpaka sasa maofisa afya pamoja na polisi wapo mitaani kukagua uuzaji wa nyama ya nguruwe," alisema Enock.


Naye afisa afya wa kata ya Tabata, Sinkonde alitoa tahadhali kwa wauzaji wa nyama ya nguruwe kutokubali kukunua nyama hiyo kiholela na kuongeza kuwa ni lazima ziwe zimepimwa na kupigwa muhuri.


"Hivi sasa tunasubiri gari ili kuambatana pamoja na askari polisi kwa ajili ya kuzungukia maeneo mbalimbali ya Tabata kukagua uuzaji wa nyama hii, hii ni hatari kwa kuwa nguruwe hawa wamekufa kwa muda mfupi sana," alisema Sinkonde.
 
baada ya watu hao kutoa utumbo wa nguruwe hao 18 waliwabeba na kuondoka nao na kuongeza kuwa mpaka jana licha ya kutoa taarifa polisi bado hajafahamu nyama ya nguruwe hao imeuziwa sehemu gani.

"Inauma sana, tena wamewapa sumu wale nguruwe waliokuwa wamenona, hawa saba waliowaacha walikuwa wadogo, wametumia ujanja wa hali ya juu, sikusikia kabisa tukio hilo licha ya kuwa nililala saa sita usiku," alisema Kajuna.
 
Back
Top Bottom