Wakili Mwambukusi tembea kifua mbele, hukumu ya mahakama imekuinua

Etwege

JF-Expert Member
Jul 4, 2018
5,753
15,227
TATHIMINI YA HUKUMU YA KESI YA BANDARI

Kimantiki WALIOSHINDA ni wa WALALAMIKAJI kwani Mahakama Kuu imekiri Mkataba wa IGA una mapungufu kadhaa;

1. Umevunja Sheria za Natural Wealth and Resources, Sura za 449 na 450 za 2017 ambazo zimekataza Migogoro juu ya uwekezaji kwenye rasilimali isipelekwe Nje ya Nchi na isitumie sheria za nje kutatua Migogoro hiyo.

IGA imesema Migogoro itatatuliwa Afrika Kusini na sheria za Uingereza ndizo zitatumika.

2. Mahakama imeshangaa inakuwaje IGA inatumia sheria za Uingereza na mgogoro utapelekwa Afrika Kusini wakati HGA zitatumia sheria za ndani na mahakama za ndani.

3. Mahakama imekiri Tangazo la Bunge la saa 23 kualika maoni ya Wananchi ulikuwa ni muda mfupi sana na kwamba inaondoa mantiki ya Public Constitution.

4. Mahakama imekiri pia Dubai haina Legal Personality katika Sheria za Kimataifa (Montevideo Convention na Vienna Convention) kwani inakosa Sovereignty.

5. Mahakama imetilia mashaka imekuwaje Dubai amesaini IGA wakati haina kigezo muhimu cha Sovereignty.

6. Mahakama imeshangaa inakuwaje Mkataba wa IGA umekosa ukomo wa muda wake.

7. Pia Mahakama imekiri kwamba kitendo cha IGA kusema haitawezekana kujitoa hata kama kuna Uvunjifu mkubwa wa Masharti yake, kwamba ni dosari kubwa na kwamba inakiuka hata Vienna Convention ambayo Serikali ilijikita sana kuutumia kama rejea kujenga hoja kwamba IGA ni International agreement.

B: Katika Public Interests Litigation and Advocacy, sisi tumeshinda zaidi kwa sababu hizi;

1. Uwepo wa Kesi hii Mbeya, imehamisha Mjadala wa Kitaifa kuelekeza macho yote Mbeya. Wananchi kutoka kona zote za Nchi wamekuwa wamifuatilia yanayojiri Mahakama Kuu - Mbeya.

2. Kesi hii imewafanya Wakazi wa Mbeya waliofika Mahakamani kupata uelewa mkubwa zaidi (Awareness) juu ya Undani wa Mkataba huo na tafsiri ya Vifungu vyake kadiri ya Hoja za Pande mbili katika mnyukano ndani ya Mahakama.

3. Kesi hii imehamisha Mamlaka za Nchi kuelekeza macho na masikio yake Jijini Mbeya. Katika ya uwepo wa kesi hii Mbeya, Makamu wa Rais Dr. Mpango amefika Mbeya, Waziri Mkuu Majaliwa amefika Mbeya na Rais amefika Mbeya pia.

Hii imeenda sambamba na Mawaziri wengi kufika jijini Mbeya pamoja na Viongozi wengine wakubwa katika Taasisi za Umma, bila kusahau Mkutano mkubwa wa Kanda wa CCM kukutanisha Mikoa mitano na Viongozi wake wote wa Chama na Serikali, umefaika Mbeya.

SPIKA wa Bunge Tulia Ackson pia ameendelea kufanya mikutano mingi sana katika Kata mbalimbali za Jiji la Mbeya, akijitetea na kufafanua mambo kadhaa yaliyopelekwa Mahakamani.

4. Kesi hii imethibitisha Wasiwasi wa Watanzania katika mkataba wa IGA na rasmi Mahakama imeungana na Wananchi kuonyesha dosari zote zilizoibua Mjadala miongoni mwa Watanzania.

Kwa Kesi hii na Hukumu ya Mahakama, wale waliosema Mkataba wa IGA uko "perfect" hauna dosari na unafaa kwa kila namna, wamekanushwa rasmi.

5. Kesi hii na Hukumu yake zimesaidia kuonyesha kwamba Waliofungua Kesi, Mawakili wao pamoja na Watanzania waliounga mkono kesi hiyo, walikuwa na Nia njema na wamekuwa na hoja zenye mashiko kuliko waliobeza na kuwatukana.

Aibu imfikie RC JUMA HOMERA wa Mkoa wa Mbeya na wengine waliojaribu kutumia nguvu nyingi kuutasaka Mkataba wa IGA na kuutetea kwamba ni Mkataba bora. Mahakama imewapiga breki rasmi. Wajitathimini!

6. Kesi ya Bandari imesaidia kurejesha Umoja na Ushikiano wa Wananchi katika jambo linalowahusu. Watu wamechangia hela zao kusaidia kesi hiyo kuanzia mwanzo hadi mwisho. Utanganyika umeimarika na kuthibitika kwa mara nyingine baada ya G55.

Dosari za Muungano zimeendelea kuonyeshwa katika uwazi zaidi kipindi hiki.

7. Kesi hii imesaidia kuondoa Matabaka na migawanyiko ya Jamii ya Watanzania kisiasa na kidini. Kesi hii imewavuta Wananchi katika UTANZANIA wao bila kuangalia dini zao wala itikadi za kisiasa. Waliochangia na kutoa maoni yao hawakujizuia kwa sababu za tofauti za namna hiyo.

Watu walisimama kwa mantiki ya Kulinda Rasilimali zao!

KWAHIYO, Serikali imeshinda KISIASA Walalamikaji/Wananchi wameshinda KISHERIA na KIMANTIKI.

C: Kesi hii imedokeza Hoja muhimu ya UHURU WA MAHAKAMA nchini Tanzania;

1. Imekumbusha Kauli ya Hayati Rais JPM aliyesema Mihimili mmoja (Executive) ni mkubwa zaidi umejichimbia mizizi chini zaidi na una nguvu dhidi ya mihimili mingine.

2. Imekumbusha pia Kauli ya JAJI MKUU wa Tanzania, Mhe. Prof. IBRAHIM JUMA alipotamka mbele ya umma kwamba, Mahakama zetu Tanzania zinapotoa Hukumu ziangalie Mihimili mingine inasema nini au inataka nini.

3. Imeonyesha jinsi ambavyo Mahakama ya Tanzania inaiogopa Serikali na Bunge, na haijavaa ipasavyo Mamlaka yake chini ya Ibara ya 107A.

Mahakama yetu inatoa AMRI kwa kesi zinazohusu mashauri/Kesi binafsi, ila haipo tayari kuvaa viatu vyake kutoa Amri dhidi ya Mihimili mingine inapotenda makosa au dosari katika majukumu yake.

4. Imeibua hoja kwamba Mfumo wetu wa Check and Balance ni KILEMA na hauna afya kwa maendeleo ya nchi yetu.

5. Imekumbusha umuhimu wa Kuanzisha Taasisi imara katika mfumo wa Check and Balance katika Mihimili yetu mitatu (Bunge, Serikali na Mahakama).

6. Imesaidia kuwaonyesha Watanzania kwamba kuna wakati ni rahisi Mihimili yote kula njama (collusion) kulindana katika Maovu ya Watawala na Wawakilishi wa Wananchi.

7. Imesaidia kuonyesha tatizo la msingi la Watawala wetu wanapoenda Kuzungumza na Kuingia mikataba, wanajiongoza kama vile Nchi yao haina Sheria na wanajiongoza bila mipaka kiasi kwamba wanaweza kusaini mikataba inayokiuka Sheria za Nchi yetu. Hii ni dosari ya hatari sana.

Kesi hii imewakumbusha Wanasiasa Viongozi wetu kwamba nchi hii ina Katiba na Sheria, wasijisahau sana wakatiririka bila mipaka.

8. Imeibua tahadhari kwa Watanzania kwamba kuna "Mentality" ya Watawala wetu kwamba wanaweza kuvunja Sheria na Katiba yetu kwa Mgongo wa kuwa Wamesaini Mkataba wa Kimataifa ambao hautakiwi kupimwa au kuhojiwa kwa Sheria za ndani ya Nchi yetu.

Mentality hii ilijengewa Utetezi mkubwa sana na Mawakili wa Serikali katika Hoja zao ndani ya Mahakama. Hii ni hatari sana.

Kesi hii inawakumbusha Mawakili wa Serikali kuwakumbusha Viongozi wetu Mipaka yao katika kila tendo na hatua ndani au nje ya nchi, wajue Katiba na Sheria zetu ndio Kipimo chao na Kioo cha Kujitazama.

Mawakili wa Serikali wawakumbushe Viongozi wetu kwamba Sheria za Kimataifa au International Agreement sio Kichaka cha Kukanyaga na kutweza Katiba na Sheria zetu.

D: Zaidi ya yote, Tanzania imeshinda dhidi ya Mikataba yenye sura za ugandamizaji katika Ulimwengu wa Ushindani wa Kibiashara na Ujasusi wa Maendeleo ya Kibepari;

1. Watanzania kupitia Kesi hii ya Mkataba wa Bandari, wamepata nafasi ya kukumbushana juu ya Uwepo wa Matabaka ya Dunia ya Kwanza na ya Pili, na Setting ya Uchumi wa Dunia kati ya Matabaka hayo.

2. Watanzania wamejikumbusha kwamba Wazungu na Waarabu wanapokuja kwetu, sio Wajomba au Shangazi zetu wanaokuja kwa lengo au mantiki ya kutuletea Maendeleo, bali wamekuja kusaka Utajiri kwaajili ya Maendeleo yao.

3. Watanzania wamejikumbusha kwamba katika Matabaka ya Dunia, tunapokutana na jamii ya Matabaka hayo tunahitaji kuwa Makini zaidi, kusimama na maslahi ya Taifa sio kuwapa Imani watu ambao sio ndugu zenu.


4. Tumejikumbusha kwamba, tunaposaini Mikataba tushiriki kuandika katika Ukamilifu ili Mambo muhimu yote yawepo na Mkataba unatakiwa Kujitetea wenyewe bila kusubiri Mikutano ya Chama kuzunguka nchi nzima kuutetea ubora au wema wake.

5. Tumejikumbusha pia kwamba Serikali ni WATU, ni Binadamu. Wanakosea na kupitiwa kama Binadamu wengine. Kwenye Mkataba wa IGA Serikali ilitereza na isimame upya kwa makini ili Tanzania ipate vitu bora kutoka huko Duniani.

6. Watanzania wamepata kujua TABIA ya DP WORLD huko duniani, pale inapokutana na Mataifa ya Matabaka ya juu (Sweden, UK, USA) na inapokutana na Mataifa ya tabaka la chini kama Tanzania, Djibouti, Somalia, nk.

Hii itasaidia kuongeza umakini zaidi tunapodili na watu wa aina hiyo kwa kujifunza kwa wenzetu wanyonge na wenye nguvu.

Hii itasaidia kuwachambua na kuwachunguza kabla ya kuingia kwenye Mikataba.

SISI NI TAIFA MOJA.

KESI HII IMETUMIKA KAMA NJIA YA KUREKEBISHANA KWA NIA MOJA YA KUJENGA TAIFA LA TANZANIA.

Hatuhitaji kutazamana usoni kwa Chuki, Hasira au Nia ovu na kutakiana mabaya.

Penye marekebisho muhimu tukarekebishe IGA ili kuweka nyaraka bora kwa maendeleo yetu sote.

Adv. Livino Ngalimitumba
 
Mwenye maono ya lini na nani wa kuoa ni mwanaume ila ndoa ni ya mwanamke
Mwenye kujenga mjengo wa kuishi ni mwanaume ila nyumba ni ya mwanamke
 
Back
Top Bottom