Waimbaji Injili wakipitie mbali kikombe cha utapeli

Waimbaji Injili wakipitie mbali kikombe cha utapeli

Mzalendo_Mkweli

JF-Expert Member
Joined
Jan 30, 2012
Posts
2,058
Reaction score
1,305
IMEKUWA nikiandika uchambuzi wa maoni juu ya waimbaji wa muziki wa Injili, ambapo pamoja na kazi nzuri wanayoifanya ya kufikisha ujumbe wa Neno la Mungu kwa njia ya kuburudisha, baadhi yao wamekuwa wakienda kinyume cha maadili, kwa kujihusisha na vitendo vya utapeli. Utapeli ninaozungumzia hapa ni kitendo cha mwimbaji kuchukua fedha, iwe yote au sehemu ya malipo kwa ajili ya kutoa huduma katika tukio fulani, lakini asifike, jambo ambalo limekuwa likitokea mara kadhaa na kuleta manung’uniko na hisia mbaya.
Ndiyo maana katika hali ya kuwekana sawa ili kutetea hadhi na heshima ya uimbaji, nimeamua kulisema hili, kwani vitendo kama hivi havimpi Mungu utukufu, licha ya umuhimu wao katika mahubiri, iwe kanisani au sehemu yoyote ile ya mkusanyiko.
Niliwahi kuwaonya waimbaji wa nyimbo za Injili wanaojichubua kupita kiasi, wanaovaa mavazi ya ajabu, wanaosuka mitindo ya ajabu pamoja na tungo za mipasho na vijembe, nashukuru nilieleweka katika hayo kwa wahusika kubadilika taratibu kwani wakati mwingine ilibidi nitumie maneno makali yenye kuumiza ili kuweka msisitizo.
”Sijui itakuwaje hukumu yangu, nitakaposimamishwa kwenye kizimba nikikosa mtetezi itakuwaje? Wewe mimi? Matendo yangu ya siri…’’ Hiki ni kipande cha mashairi ya wimbo ulioimbwa na kwaya ya Mtakatifu Andrea, Kanisa la Anglikana Magomeni, jijini Dar es Salaam, ambao ndio kiini cha mtazamo wangu leo.
Leo nitazungumzia wasanii wa muziki wa Injili ambao hawatimizi wajibu wao wanapoitwa kwenda kufanya huduma au matamasha mahali, lakini hawafiki au wanafika muda ambao wanajua kabisa shughuli itakuwa imekwisha.
Binafsi ninakerwa na wasanii hawa kwa kuwa ni sawa na matapeli wa duniani, ambao hawana huruma na binadamu wenzao.
Ninasema haya kwa sababu ilishatokea kwa msanii mmoja wa kike nchini ambaye aliwahi kualikwa huko mikoani, lakini licha ya kuchukua sehemu ya malipo alishindwa kutokea kabisa na hata alipoulizwa ni vipi, hakuwa na majibu ya maana zaidi ya kusema tu angehudhuria wakati mwingine, Je, huu si utapeli?
Mwimbaji mwingine naye aliwahi kupata mwaliko ambapo pamoja na kwenda, aliishia kufanya vituko vya ajabu kwa kubaki hotelini akijiandaa kupita kiasi hadi akachelewa muda wa kutumbuiza, hivyo alipofika eneo la tukio alikuwa tayari amechelewa.
Je, ni kweli mmeitwa kwa ajili ya kumtukanisha Kristo kwa utapeli uliokithiri, ambao pia mnashindwa kutofautisha huduma na matamasha?
Sote tunafahamu mnatumia gharama kubwa katika kurekodi, lakini je, ni sababu ya msingi ya kuwafanya ninyi muwe na tamaa zaidi ya fisi? Ni lazima mtambue kila jambo lina kiasi na hata Mungu pia hupendezwa na wanaofanya mambo kwa kiasi, na ndiyo maana hubarikiwa.
Lakini pia tunafahamu kwamba kila linalowezekana leo, lisingoje kesho na wakati unaokubalika mbele za Mungu ni sasa, je, unavyopanga waakti mwingine wa kuhudumia ilhali wakati uliopangwa ni ule ulioukosa kwa makusudi na njaa zako, unategemea nini? Utafidia vipi wakati?
Kama haitoshi, unapopoteza muda hotelini ‘kujipura’ kwa kuficha mabonde na kuungua uso kulikotokana na matumizi ya mkorogo uliokuchubua ilhali watu wa Mungu wakiwemo watumishi wanasubiri huduma yako, hivi unataka nini zaidi?
Huu ni wakati wa kuonyana kwa tenzi na zaburi, hivyo ondoeni aibu hii kwa kurudisha hadhi na dhana ya muziki wa Injili kwa kuvua viatu vya utapeli, kuimba kwa mazoea, mavazi ya ajabu na mengineyo mengi ambayo yako nje ya maadili yanayosababisha kumtukanisha Kristo. Tambueni ninyi ni barua, mnaosomwa na watu wote.
source : Tanzania Daima – Waimbaji Injili wakipitie mbali kikombe cha utapeli
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom