Wagombea wanaoendekeza rushwa wakataeni ? Dk. Shein

Serayamajimbo

Senior Member
Apr 15, 2009
191
38
na Sauli Giliard na Hellen Ngoromera


amka2.gif

WAKATI joto la uchaguzi mkuu likizidi kupanda katika maeneo mengi nchini, wananchi wametahadharishwa na kutakiwa kuwa na dhamira ya dhati kuwakataa wagombea watakaojaribu kuiendekeza rushwa kwa njia mbalimbali.
Wa kwanza kutoa tahadhari hiyo juzi usiku ni Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein katika mkesha wa mwaka mpya uliofanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Alisema wakati nchi inajiandaa na uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, wananchi wanapaswa kuwa na dhamira ya dhati kuwakataa wagombea wa aina hiyo.
Dk. Shein alikiri kwamba upungufu wa uadilifu miongoni mwa watu wengi nchini unatokana na tatizo la rushwa ambalo pia ni miongoni mwa changamoto kubwa dhidi ya amani, utulivu na mshikamano.
“Kama tunavyofahamu, rushwa ni adui wa haki kwa kuwa ni tatizo linaloleta dhuluma, uonevu, uhasama, utengano, umaskini na matatizo mbalimbali yanayoifanya jamii kukosa amani, utulivu na mshikamano, tudhamirie kuwakataa wagombea watakaoendekeza rushwa,” alisema Dk. Shein.
Aidha, aliwakumbusha viongozi wa dini kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kuelimisha na kuhimiza wananchi kuyazingatia na kuyafuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu ili kujenga waumini na raia wema na kuongeza kuwa serikali inaendeleza mikakati madhubuti yenye lengo la kuitokomeza rushwa.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka viongozi wa dini nchini na wananchi kwa ujumla kuumboea uchaguzi huo ili uwe wa amani na utulivu.
Alisema viongozi na wananchi wana mchango mkubwa wa kutoa, ili kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu huo utakapofanyika utakuwa wa amani, utulivu na mafanikio.
Dk. Shein alisema uchaguzi ni utaratibu wa kidemokrasia wa kuiwezesha nchi kupata viongozi bora watakaoliongoza taifa katika kujiletea maendeleo yake na kwamba si jambo la mapambano na wala si fursa kwa watu kujenga na kupandikiza chuki, uhasama na utengano miongoni mwa wananchi dhidi ya serikali yao na dhidi yao wenyewe.
“Kwa hakika, kuchochea chuki na uhasama ni kudhoofisha na kubomoa misingi yetu imara ya amani, usalama, utulivu, upendo, mshikamano na umoja tuliojijengea katika taifa letu,” alisema.
Alisema mfumo wa vyama vingi vya siasa unasisitiza kutofautiana kifikra bila ya kuzozana na kwamba wakati umefika sasa kwa watu kujenga utamaduni wa kushindana kwa sera na kifikra badala ya kuendeleza chuki na fitina hali inayohatarisha amani na umoja wa taifa.
Akizungumza katika mkesha huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mkesha Kitaifa, Askofu Godfrey Malassy alisema ibada hiyo ya mkesha wa mwaka mpya inatoa fursa kwa Watanzania kukusanyika pamoja na kumshukuru Mungu kwa kuumaliza mwaka na kuukaribisha mwaka mpya na kuliombea taifa amani na utulivu.
Wakati huohuo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa amewataka wananchi kutowachagua mafisadi katika uchaguzi mkuu ujao.
Pia aliwataka kuwa makini na viongozi wanaotoa rushwa, ili waweze kuchaguliwa upya kwa kuwa huko ni kuwapofusha macho matokeo yake ni taifa kupata viongozi wasiofaa.
Akizungumza na Tanzania Daima katika mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake iliyopo katika Kanisa la Azania Front, jijini Dar es Salaam jana, askofu huyo alisema kwa sasa uadilifu miongoni mwa watu umepungua na kuwa wajanja wajanja.
“Rushwa ni dhambi inayopofusha. Mwaka huu tunaingia kwenye uchaguzi, inatupasa kuwa makini tusiwachague mafisadi wa kweli. Japokuwa hatupaswi kuhukumu,” Malasusa alisisitiza.
Alikwenda mbali zaidi na kuwataka wale walionyooshewa vidole wawajibike kwa kujihoji sababu za wao kuhusishwa na kashfa za rushwa japokuwa alisisitiza kwamba kuna watu hawapaswi kuhukumiwa kabla ya kuonekana wana hatia.
Katika hoja yake hiyo, Dk. Malasusa alizitaka mamlaka husika, ikiwemo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU) kutekeleza wajibu wake ipasavyo kwa kuwahoji wanaohusishwa na ufisadi, kwani kutofanya hivyo kunawaweka wananchi katika wakati mgumu wa kujua kweli wanaotuhumiwa ni mafisadi ama la.
“Mamlaka husika kama TAKUKURU zifanye kazi yake ipasavyo, kuna masuala mengi bado hayajafikiwa hitimisho,” aliongeza.
Akizungumzia mwaka uliopita, mkuu huyo wa KKKT alisema wananchi wengi kwa sasa wamekuwa na mwamko ulioonyeshwa na wananchi kwa kipindi cha hivi karibuni ni ishara ya kwamba wamefunguka macho.
Alieleza ugumu wa maisha unaowakabili wananchi, kushuka kwa thamani ya shilingi huku utandawazi ukiendelea kukuwa kunazidi kuwafungua wananchi macho na kuwafanya wahoji.
Kutokana na hali huyo, Dk. Malasusa aliwageuzia kibao viongozi kwa kuwataka wajihoji kutokea kwa hali hiyo kwa sasa inayosababisha kuendelea kuwa katika hali ya kubishana huku watu wakiongezeka kuwa ‘wajanjawajanja’.
Akitoa ujumbe wa mwaka mpya kwa Watanzania wote, kiongozi huyo wa dini aliwataka kuishi katika hali ya uadilifu ikiwa ni pamoja na kumtegemea Mungu.
Aliwataka mwaka huu kubadilika kwa kuachana na tamaa za mali kama ilivyokuwa mwaka jana na kusisitiza kwamba, jambo jema kwa mwaka huu ni kumrudia Mwenyezi Mungu.
“Ujumbe wa mwaka huu hasa unasisitiza watu kumtegemea Mungu...kuhusu uadilifu, wanatakiwa kuacha tamaa za mali na kumrudia Mungu. Kwa sasa kuna kubishanabishana na ujanjaujanja mwingi,” alisema. Kauli huyo ya Askofu Malasusa ya kuwataka wanachi kuwa makini na viongozi wabovu hasa wanaotuhumiwa kwa ufisadi ni mwendelezo wa ujumbe unaotolewa na viongozi wa dini wa kukemea rushwa. Katika siku za hivi karibuni, viongozi wengi wa dini wanaopata fursa ya kupanda jukwaani, wamekuwa wakiwaasa wananchi kutowachagua viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
 
Back
Top Bottom