GE2025 Wagombea ubunge Dar es Salaam wanavyomwaga ahadi zao kwa wapiga kura

GE2025 Wagombea ubunge Dar es Salaam wanavyomwaga ahadi zao kwa wapiga kura

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

Parabolic

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2013
Posts
2,743
Reaction score
2,601
Katika kapneni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, baadhi ya wagombea ubunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, wametoa ahadi wakigusa kero za wananchi.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mwaka 2022 Dar es Salaam ilikuwa na wakazi milioni 5.4 na ni mkoa unaokua kwa kasi zaidi nchini kwa asilimia 5.6 kwa mwaka. Jiji hilo linakadiriwa kuwa na zaidi ya asilimia 12 ya wapiga kura wote nchini.

Majimbo yanayowania ni pamoja na Ilala, Ukonga, Segerea, Kivule, Temeke, Mbagala, Chamazi, Kigamboni, Kibamba, Ubungo, Kawe na Kinondoni.

Katika mikutano ya hadhara, baadhi ya wabunge wamekuwa wakitumia ilani na ahadi zao binafsi kujinaji.

Zungu: Rais Samia ameimarisha amani, utulivu na haki nchini

Mgombea Ubunge wa jimbo la Ilala Mussa Azzan Zungu amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi imara ambaye amefanya kazi kubwa ya kuimarisha amani, utulivu na haki nchini.

Akizungumza leo Agosti 31, 2025 kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM kwa Mkoa wa Dar Es Salaam uliofanyika katika viwanja vya Sokoine,Temeke, Zungu amewaomba wananchi hao kumchagua mgombea Urais wa CCM ambaye ni Dkt. Samia ili aendelee kufanya makubwa nchini.

“Mama Samia kaifanya Tanzania leo katika takwimu zilizotoka kwa bara la Afrika kuwa ndiyo ya kwanza kwa amani uhuru na haki za wananchi wake” amesema Zungu

Aidha Zungu amewataka wanachama wa CCM kujitokeza kupiga kura huku wakiwahamasisha na wenzao ili kuiwezesha CCM kupata kura nyingi kwa nafasi zote za kugombea.

Soma pia: Wagombea ubunge, udiwani Segerea wakijinadi mbele ya wajumbe

Madeleka aja na vipaumbele vitano Kivule
Screenshot 2025-09-10 144035.png

Katika andiko lake, mgombea ubunge wa Chama cha ACT Wazalendo katika jimbo la Kivule, Peter Madeleka amesema iwapo atachaguliwa atatumia taaluma ya sharia na nguvu zake za ushawishi kushinikiza na kutatua kero za muda mrefu za jimbo hilo.

Amezitaja kero hizo kuwa ni pamoja na tatizo la miundombinu na uwajibikaji hafufi wa mbunge aliyepita ndio vimemsukuma kugombea jimbo hilo.

“Nimeamua kugombea ili niwe mtumishi wao. Kuna matatizo mengi, kwa mfano, hakuna ajira, barabara mbovu, kwa hiyo ninashiriki ili kuondoa hizi changamoto.

Vipaumbele vyake ni pamoja na elimu, afya, miundombinu, ajira kwa vijana na wanawake na uwajibikaji.

Katika elimu amesema ataboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari na kuweka mazingira rafiki kwa walimu na wanafunzi (madrasa madawati, vyoo bora).

Pia atasimamia upatikanaji wa vitabu na vivfaa vya kufundishia.

Katika sekta ya afya, amesema atahakikisha kila mwananchi wa Kivule anapata matibabu stahiki, kuboresha vituo vya afya na kujenga vingine kwenye maeneo yenye mahitaji makubwa, kupsimamia upatikanaji wa vifaa toba muda wote na kuhakikisha mama wajawazito na watoto wachanga wanapata huduma bora.

Katika ajira na uwezeshaji, Madeleka amesema ataanzisha programu za ujasiriamali kwa vijana na wanawake kupitia vikundi vya kijamii, akiwawezesha vijana kupata mikopo midogo kuanzisha biashara.

Pia ataweka msukumu kwenye mafunzo ya ufundi stadi (VETA).

Katika eneo la miundombinu na huduma za jamii, Madeleka amesema ataboresha barabara ziweze kupitika muda wote wa mwaka, kusimamia upatikanaji wa huduma za maji, umeme kwenyue mitaa yote ya jimbo na kufuatilia miradi ya maendeleo iliyokwama.

Katika kuonyesha uwajibikaji kwa wananchi waliomchagua, amesema ataripoti mara kwa mara kazi za ubunge na maendeleo ya jimbo, kusimamia matumizi ya fedha za jimbo kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa. “Nitasimama bungeni kama jicho la wananchi kusimamia haki, uwazi na maendeleo ya wote.”

Katika usafi wa mazingira, amesema atasimamia kampuni za usadi na uhifadhi wa mazingira, kusimamia ukusanyaji wa taka na ujenzi wa dampo na kuanzisha bustani kwa ajili ya mapunziko.

Kupitia kauli mbiu yake ya “Maendeleo kwa wote, uwajibikaji kwanza,” Madeleka amesema ameshaanza kusaidia wananchi hasa kero za migogoro ya ardhi 17, ambayo kesi 32 zipo kwenye mahakama mbalimbali, huku pia akisaidia familia 17 kulipa gharama za kuhifadhi maiti hospitalini.

Katika michezo, amesema atashirikiana na Serikali kutenga maeneo makubwa kwa ajili ya michezo na kuhakikisha wananchi wenye vipaji wanafika mbali.

Profesa Kitila Mkumbo aahidi kilometa 43 za barabara Ubungo
maxresdefault-1.jpg

Akifungua kampeni zake Septemba 6, 2025, mgombea ubunge wa Ubungo kupitia CCM, Profesa Kitila Mkumbo amejikita katika ahadi ya kuboresha miundombinu ya barabara.

Amesema jimbo la Ubungo lina kilometa 169 za barabara, akisema wakati anaingi madarakani mwaka 2020 barabara za lami na zege zilikuwa asilimia asilimia 12 peke yake.

“Angalau sasa tuna kilometa 49 za lami ikitupeleka kwenye asilimia 27. Barabara zilizokuwa zinapitika, zilikuwa asilimia 41 peke yake na sasa tumeshafikia asilimia 75. Barabara za Shekilango, NIT kuja mpaka Makurumla zote hazikuwa na lami na tumeshaweka.

“Katika kipindi hii tunakwenda kuongeza kilometa 25 za DMDP, kilometa nane za Tanroads na kilometa 10 za Tarura jumla tunapata kilometa 43.

“Kwa hiyo tutaongeza barabara za lami kutoka kilometa 27 mpaka kilometa 60 ndani ya jimbo la Ubungo.”

Jamali Rwambo – ACT Wazalendo

Mgombea Ubunge kupitia ACT Wazalendo Jimbo la Mbagala, Jamal Rwambow, amesema viongozi wengi waliopewa nafasi ya kutoa huduma ya kiuongozi katika eneo hilo hawajazitendea haki, hivyo amejitokeza kama mtumishi wa wananchi.

Rwambow ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi mstaafu ametaja kero za wananchi wa Mbagala kuwa ni pamoja na kuwa mbali na huduma za jamii zikiwemo za elimu, afya na miundombinu.

“Kwa mfano nitakutajia tu eneo moja la Kichemchem, ninavyoijua hivi sasa ipo Dar es Salaam, jimbo la Mbagala. Huwezi kuamini mpaka sasa halina shule ya msingi, kwa hiyo inabidi watoto watoke kwenda maeneo mengine kutafuta elimu ya msingi.

“Hata hiyo shule ya sekondari ambayo ina elimu ya juu ya sekondari, haina uzio, hivyo inafanya eneo hilo lipitiwe na watu, wavuta bangi hali inayowavuruga watoto wanaposoma.

“Barabara tunapoambiwa zimejengwa vizuri, nenda Kichemchem, ile sio barabara ya kumpeleka mgonjwa zahanati.

“Eneo hilo lina milima ya mchanga, sasa mvua inaponyesha inasomba mchanga wote unakwenda barabarani na kwenye maeneo ya watu, hivyo kulazimisha wananchi kuwa na lundo la viroba vya mchanga kuzuia mchanga. Hata greda linapokuja kuchonga barabara linaondoa mchanga na kutengeneza njia ya maji yanayokwenda kwenye makazi ya watu,” amesema.

Ametaja pia maeneo ya Kibulugwa, Kibonde maji na mengineyo yakiwa na kero kama hizo.

Yachitwi wa ACT kuwatetea Wamachinga

Mgombea ubunge wa Ilala kupitia ACT Wazalendo, Friday Yachitwi, ameweka kipaumbele chake kwa wafanyabiashara wadogo maarufu Wamachinga, akisema atalitumia soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam kuwanufaisha.

“Ilala ni kituo cha biashara cha Afrika Mashariki na kati. Nitakapokuwa Mbunge wa Ilala nitatumia fursa hiyo kutetea masuala ya biashara.

“Mikakati yangu mitatu: kwanza nitawatetea wamachinga, pili nitawatetea askari mgambo kwa sababu wanachonganishwa na wafanyabiashara kutokana na kukosekana kwa maeneo ya kufanyia biashara, lakini limeundwa jeshi la kuwadhibiti vijana wameacha kuwa wezi, majambazi wakakopa hela wafanye biashara, halafu jiji linawanyang’anya biashara zao.

“Nikichaguliwa kuwa mbunge wa Ilala hakuna mgambo atakayewanyang’anya wamachinga biashara zao na nitawatetea mgambo wapewe mishahara mizuri,” amesema.

Kuhusu sekta ya afya, amesema atahakikisha Hospitali ya rufaa ya Amana inakuwa na huduma bora.

“Nitahakikisha watu wanaokwenda kutibiwa wasizuiwe wanaposhindwa kulipa gharama. Ninasikitika sana, mimi ni daktari natibu watu kwa kutumia dawa za asili, watu wengi wanakuja wakisema wamezuiliwa wagonjwa wao, halafu hawatibiwi.”



Kinabo wa CHAUMMA awalilia bodaboda
Screenshot 2025-09-10 142806.png

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni zake, mgombea ubunge wa Jimbo la Kibamba, kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Edward Kinabo, Septemba 2, 2025, ameahidi kushughulikia kero za waendesha pikipiki maarufu bodaboda.

Akiwa katika Kata ya Saranga, Kinabo alisema kuwa waendesha bodaboda wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo unyanyasaji unaotokana na mifumo ya usafirishaji kwa njia ya mtandao.

Ameeleza kuwa bodaboda ni kundi kubwa linalochangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa vijana na familia zao, lakini mara nyingi wamekuwa wakikosa utetezi wa kweli, hivyo ameahidi kuwa akipewa ridhaa ya kuwa Mbunge, atahakikisha maslahi yao yanaboreshwa kwa kuweka mifumo rafiki zaidi ya kisheria na kiutendaji.

Septemba 8, 2025, Kinabo, aliendelea na kampeni zake za mtaa kwa mtaa katika Kata ya Goba, mtaa wa Matosa, ambapo pamoja na mengine alimwita mgombea Ubunge wa CCM Anjellah Kairuki katika jimbo hilo kushiriki naye katika mdahalo wa wazi mbele ya waandishi wa habari ili kila mgombea aeleze sera zake na wananchi wapime hoja kujua nani anafaa.

Alisema wananchi wa Kibamba hawapaswi kuuziwa mbuzi kwenye gunia bali wapewe nafasi ya kutathmini wagombea kwa uwazi.

Alisema CCM walidhani watapita bila upinzani baada ya CHADEMA kutojiridhisha kushiriki uchaguzi jambo ambalo limeshindikana.

Moza Ally-CHAUMMA

Mgombea Ubunge jimbo la Kinondoni kupitia CHAUMMA, Moza Ally amesema amejipanga kushinda Jimbo hilo, licha ya ugumu wa Mbunge wa sasa anayewakilisha Chama tawala.

Moza amesema anafahamu matatizo mengi ya watu wa Kinondoni hivo itakuwa kazi nyepesi kwake kufikisha matatizo yao bungeni na kuwaletea maendeleo.

Mwago wa CHAUMMA aahidi mikopo wanawake
Screenshot 2025-09-10 142630.png

Mgombea ubunge wa Jimbo la Mbagala kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Khadija Mwago, ametoa wito kwa wananchi wa jimbo hilo kuikataa CCM akidai haijaleta maendeleo huku akiahidi kuwaletea maendeleo, kuwezesha mikopo kwa wanawake na vijana ili wajikwamue kiuchumi.

Khadija ameyasema hayo Septemba 7, 2025 katika ufunguzi wa kampeni za jimbo hilo, akisema uamuzi wake wa kuomba tena ridhaa ya wana Mbagala unatokana na dhamira ya kuwatumikia na kuwasemea bungeni.

Amesisitiza kuwa kipaumbele chake ni kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.

Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo ameahidi kuanzisha kituo cha ujasiriamali kwa vijana na kushirikiana na kampuni za mikopo ili waweze kupata mikopo nafuu ya kuwawezesha kujiajiri.

Katika sekta ya afya, Khadija ameweka mkakati wa kuanzisha na kuboresha huduma kwa kujenga kituo cha afya cha mama na mtoto, kitakachowezesha wazazi kupata huduma za uzazi kwa gharama nafuu.

Amesema utekelezaji wa mipango hiyo unategemea uamuzi wa wananchi kumpa ridhaa ya kuwa mbunge wao katika uchaguzi ujao.

Agnesta wa CHAUMMA ampongeza Rais Samia
Screenshot 2025-09-10 142403.png

Mgombea Ubunge Jimbo la Segerea kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Agnesta Lambert Kaiza amemsifia Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha anatenga fedha za kutosha kwenye mikopo kwa ajili ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Agnesta amezungumza haya alipokuwa katika mkutano wake wa kwanza wa kampeni katika uwanja wa Msikate Tamaa, Vingunguti jijini Dar Es Salaam.

"Mama Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani akasema Marais Wenzangu walikuwa wanatoa mikopo inayoitwa mikopo ya riba nafuu, alipowaangalia wanawake wa Kitanzania alipowaangalia vijana na walemavu akawaona akina mama.

“Mama yetu Samia Suluhu Hassan akasema nakwenda kushusha fedha katika kila Halmashauri hiyo fedha akina mama vijana na wenye ulemavu wakopeshwe fedha bila riba" amesema Agnesta.

Mbali na hoja hiyo, Agnesta amesema endapo akichaguliwa kuliwakilisha jimbo hilo atayaweka mbele maslahi ya wananchi kabla ya maslahi yake binafsi.

"Niwahakikishie Wana-Segerea ikiwa mtanichagua kwa kura za kutosha changamoto zenu zitakuwa ni za kwangu nitatanguluiza maslahi yenu wana-Segerea lakini ya kwangu yatakuwa baadae"

Ameongeza kuwa miongoni mwa changamoto atazohakikisha anazitatua ni uwepo wa kituo cha afya katika Kata ya Buguruni ili kurahisisha upatikanaji huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo.

Omari Mkwaya Said –SAU ajikita kwenye barabara mbovu
Screenshot 2025-09-10 143124.png

Mgombea ubunge wa Segerea kwa tiketi ya chama cha Sauti ya Umma (SAU), Omari Mkwaya Said amegusa kero za upatikanaji wa maji na barabara akisema atazipa kipaumbele katika kampeni zake.

“Matarajio yangu kwa wana Segerea ni kutatua kero zao zote na hasa tatizo la maji, barabara ni mbovu.

“Kuna suala la utozaji wa tozo za taka, nitahakikisha naiondoa tozo hii ili wananchi wenzangu wafaidi keki ya Taifa,” amesema Said alipozungumza na waandishi wa habari hivi karibuni.

NCCR Mageuzi walia na barabara Ukonga
Screenshot 2025-09-10 143321.png

Mgombea Ubunge wa Ukonga – NCCR Mageuzi Kenny Raphael Gehaz pia ni katibu mwenezi wa chama hicho, pia amegusia ubovu wa barabara katika jimbo hilo.

“Jimbo la Ukonga lina mapungufu mengi, kwa mfano barabara ni mbovu, wananchi wana matatizo mengi makubwa,” amesema alipozungumza na waandishi wa habari.

Mgombea NRA agusa barabara, elimu, ardhi Ukonga

Mgombea ubunge jimbo la Ukonga kupitia NRA, Murshid Kabirika pia amegusia kero ya barabara, elimu na migogoro ya ardhi.

“Jimbo la Ukonga lina matatizo mengi na tumehangaika kwa muda mrefu, kwa mfano kero ya barabara. Ni kata moja tu imepewa barabara (hajaitaja) sasa inakuwa ni aibu.

“Kwenye elimu kuna kero nyingi tangu shule za msingi hadi sekondari watoto wetu wanakaa chini, wanalala chini, kwa nini wakati uwezo upo?

“Kuna watu walibomolewa nyumba zao huko Ulongoni B lakini hawakutatuiliwa kero zao, mimi nitazitatua. Kuna watu walifukuzwa kwenye msitu huko pia nakwenda kuwasikiliza maana hawakusikilizwa, kama walinyang’anywa shamba lao nitahakikisha shamba lao linarudi,” amesema.

Mgombea Chama cha Makini alilia wenye ulemavu
Screenshot 2025-09-10 143635.png

Mwanaidi Mustafa mgombea ubunge jimbo la Chamazi kupitia Chama cha Makini amesema kipaumbele chake ni kwa watu wenye ulemavu wanaokosa fursa za maendeleo.

“Nikipata ridhaa ya kuingia bungeni, hakika watu wenye mahitaji maalum na hasa wenye ulemavu tutawapa kipaumbele sana, tutaweka mbinu mbalimbali kuhakikisha hawazagai barabarani kuombaomba.

“Huwa inaniuma sana, ninapoona wenzangu wapo barabarani wanaomba kwa sababu ya ulemavu,” amesema.
 
Back
Top Bottom