Wafanyakazi watoro Manispaa Iringa kukiona

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
BAADHI ya wafanyakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wanadaiwa kutumia muda wa kuwahudumia wananchi kufanya kazi zao binafsi nje ya ofisi.

Wamekuwa wakifanya hivyo, wakiamini kwamba Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) kina uwezo wa kuwatetea endapo watafukuzwa kazi.

Ili kuongeza tija katika kuwaletea wananchi maendeleo, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Theresia Mahongo amewataka wafanyakazi wa idara zote manispaa kuzingatia muda wa saa za kazi na kuepuka kutumia muda wa saa za kazi katika shughuli zao za nje.

Akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Idara ya Afya ya manispaa hiyo, Mahongo alisema tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo miezi michache iliyopita, ametumia muda wake mwingi kusoma mazingira ya utendaji wa kazi kwa wafanyakazi wa idara zote za manispaa hiyo na kubaini kuwepo na tatizo hilo.

“Nawaombeni mzingatie sheria, kanuni na taratibu za kazi, ni makosa kwa mfanyakazi kuacha ofisi yake bila maagizo yoyote ya kiserikali na kuutumia muda wa kuwepo kazini kwa shughuli zake binafsi,” alisema.

Mahongo alisema baadhi ya wafanyakazi katika manispaa yake hiyo, wanayo desturi ya kufika kazini na kujiandikisha katika kitabu cha mahudhurio, na kisha kutokomea kusikojulikana na wanapoyakuta majukumu mezani kwao hudai muda wa ziada wa saa za kazi.

“Katika kuhakikisha watumishi wanatimiza wajibu wao, TALGWU nao wana nafasi yao, kwa hiyo nawaomba tushirikiane ili kujenga heshima ya halmashauri yetu kwa wananchi tunawatumikia na taifa kwa ujumla,” alisema.

Alisema kuwatetea au kuwabeba kwa namna yoyote ile watumishi wazembe, na wavivu ni kurudisha nyuma maendeleo ya wakazi wa halmashauri hiyo na taifa na kuonya kuwa, kuanzia sasa watumishi wote watakaokiuka sheria, kanuni na taratibu za kazi watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake Ofisa Tabibu wa TALGWU, Rebecca Maganga alisema kamwe chama hicho hakitawaunga mkono watumishi wa aina hiyo na badala yake kitashirikiana na ofisi ya Mkurugenzi kuhakikisha nidhamu kazini inakuwepo.

Alisema kati ya mwaka 2006 na 2010, tawi la TALGWU katika halmashauri hiyo lilishughulikia kesi 15 za watumishi ambao walishinda na mahakama kuamuru mwajiri awarudishe kazini.
 
Back
Top Bottom