Wafanyakazi wasema awadanganyiki 2010

Msharika

JF-Expert Member
May 15, 2009
947
69
VYAMA vinavyounda Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) vimeanza kutoa mwongozo kwa wanachama wao, kuunga mkono mgomo wa wafanyakazi nchini nzima, ikiwa ni pamoja na kuwashawishi kushiriki.

Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ni miongoni mwa vyama 14 vinavyounda Tucta, kilichotoa tamko jana kuunga mkono na kuwataka wanachama waondoe hofu kushiriki mgomo huo wa Mei 5, mwaka huu. Rais wa CWT, Gratian Mukoba, alisema uamuzi huo wa kuwasisitiza walimu unatokana na kilichoridhiwa na shirikisho, kwamba vyama vyote vinavyounda Tucta, kila kimoja kwa wakati wake kitoe mwongozo kuhimiza wanachama washiriki mgomo.

Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi Tanzania (COTWU) pia kimepanga wiki ijayo kutoa tamko la kuunga mkono mgomo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mukoba alisema hiyo ni sehemu ya uhamasishaji kupitia kwa viongozi wa vyama hivyo, ambao wako karibu na wanachama waitikie tamko la Shirikisho la kugoma.

“Leo ni CWT, vyama vingine navyo vitatoa matamko kwa wanachama wao kwa wakati wao. Walimu ni CWT kwa hiyo tumeamua kila mtu awahimize wanachama wake,” alisema Mukoba.

Wakati vyama vishiriki vya Tucta vikiendelea na kazi hiyo ya kuwapa msimamo wanachama juu ya mgomo, Tucta imekataa ombi la Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya la kukutana nao leo kujadili suala hilo.

Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya, aliiambia HabariLeo juzi kwamba Waziri Kapuya aliomba kamati ya kuratibu mgomo ikutane naye, lakini wameona wanaopaswa kukutana nao ni watendaji na si Waziri.

Licha ya Kapuya, Mgaya alisema pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, alivitaka vyama vya wafanyakazi wa umma kufanya majadiliano naye kuhusu mgomo lakini pia akakataliwa.

Profesa Kapuya alisema Serikali itatafuta namna ya kumaliza suala hilo, kwa kuwa Tucta wana haki ya kudai haki zao na hakuna dhambi waliyoifanya.

Akizungumzia mantiki ya kuwakatalia mawaziri hao kufanya nao majadiliano, Mgaya alisema ni kwa sababu mazungumzo ya sasa hayakidhi Sheria ya Majadiliano ya mwaka 2003 inayoelekeza kila mwaka, ifikapo Desemba 15 majadiliano baina ya wafanyakazi na Serikali yawe yamekamilika.

Alisema ni takribani miaka miwili majadiliano hayo hayajawahi kuwapo, zaidi ya Serikali kufanya uamuzi inavyotaka. Kwa kuzingatia mazingira hayo, Mgaya alisema shirikisho limeona kwamba majadiliano ya sasa hayawezi kukidhi mahitaji ya wafanyakazi kwa kuwa bajeti ijayo imeshapangwa.

Licha ya Rais Jakaya Kikwete kuwasihi Tucta wasifanye mgomo wiki iliyopita, shirikisho hilo limeendelea na msimamo wake kwamba mgomo huo utakuwapo na utafanikiwa.

Rais alisema anaamini Tucta itatumia busara na si kugoma katika kipindi hiki ambacho Serikali inatafuta utatuzi wa matatizo yao.

MAONI YANGU: RAIS AMESIKIA LINI KILIO HICHI CHA WAFANYAKAZI? AMECHUKUA HATUA GANI KWA LOLOTE? HAWA MAWAZIRI WAKE JE?
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom