Wafanyabiashara waliofanikiwa walianza na hili wazo

Wafanyabiashara waliofanikiwa walianza na hili wazo

youngkato

JF-Expert Member
Joined
Sep 3, 2014
Posts
3,638
Reaction score
3,641
Watu wengi hukosea kwa kuamini kuwa mtaji wa fedha ndio msingi wa kila biashara. Ukweli ni kwamba, biashara huanza na wazo bora, si pesa. Wazo sahihi lina uwezo wa kukuvutia wadau, kukuletea mitaji, na hata kuanza bila senti mkononi.
wazo bora la biashara.png

Wanawake wengi wa nyumbani, vijana waliomaliza shule, na hata wafanyakazi hujikwamisha kwa kushindwa kuwa na wazo linalotekelezeka. Ndiyo maana unawaona wakijaribu kila biashara na kuishia kushindwa. Tatizo si juhudi, ni ukosefu wa wazo lenye mizizi kwenye uhalisia wao.
Wengi wamekopa ili waanze biashara, lakini kwa kukosa mwelekeo na wazo bora, hela hizo huishia kutumika vibaya. Baada ya hapo, mshahara unakatwa kila mwezi huku biashara ikiwa haikuanzishwa kabisa. Mafanikio kwenye biashara hayaamuliwi na kiwango cha pesa kilichowekezwa, bali ubora wa wazo lililobeba ndoto hiyo. Hivyo, kabla ya kuuliza “mtaji nitapata wapi?”, jiulize “nina wazo gani bora?”

1. Wazo Kutokana na Taaluma Yako​

Je, unasoma au umeajiriwa katika taaluma fulani? Hapo ndipo ulipo hazina ya kwanza ya wazo lako la biashara. Mwalimu anaweza kuanzisha kituo cha masomo ya ziada. Katibu muhutasi anaweza kufungua stationary au kutoa huduma za uchapishaji.

Taaluma yako ni silaha yako ya kwanza unayoifahamu, unayoitegemea, na tayari unayo uzoefu nayo. Kwa hivyo, badala ya kubahatisha, anzia hapo ulipo tayari mtaalamu. Hautaanza kutoka sifuri, na uongozi wa biashara hiyo utakuwa rahisi na wa kujiamini.

2. Wazo Kutoka Kwenye Kipaji Chako​

Kila mtu ana kipaji. Unaweza kuwa unapika vizuri kuliko wengine, una uwezo wa kuchora, kushona, kusuka au hata kuzungumza hadharani. Kipaji ni silaha ya asili ambayo hauhitaji kusomea.

Na cha ajabu zaidi mara nyingi watu wanaona kipaji chako kabla hata hujakitambua. Sikiliza maoni ya watu wa karibu, wanaweza kukuonyesha mlango wa mafanikio uliokuwa mbele yako siku zote. Kipaji si tu zawadi, ni nafasi ya pekee ya kuwa huru kifedha.

3. Hobi Yako Inaweza Kukuingizia Kipato​

Hobi ni kitu unachopenda kukifanya hata kama hulipwi. Kama unapenda kupika, vaa vizuri, au kurekodi video basi uko na fursa kubwa mkononi. Ukiigeuza hobi kuwa biashara, utakuwa unafanya kazi unayoipenda huku unapata pesa.

Hii huondoa msongo wa mawazo, na hujenga uaminifu wa hali ya juu kwa wateja kwa sababu wanaona unapenda unachofanya. Hobi yako inaweza kuwa duka la mavazi, mgahawa wa chakula cha haraka, au hata biashara ya mitandaoni bora ifanywe kwa moyo.

4. Angalia Mahitaji ya Mazingira Yako​

Unataka biashara yenye uhakika? Zingatia tatizo lililopo katika mazingira yako. Je, kuna shule nyingi lakini hakuna stationary? Kuna wafanyakazi wengi lakini hakuna mgahawa wa chakula cha mchana? Au kuna duka linalotoa huduma duni lakini watu bado wanalazimika kwenda? Hapo ndipo panapoitwa fursa.

Kitu kinachokosekana kwenye eneo lako ni nafasi yako ya kuibuka mshindi. Na hata kama wengine wataiga baadaye wewe utakuwa wa kwanza, na jina lako litaongoza.

5. Wazo Kutokana na Uzoefu Wako wa Kazi​

Kabla au baada ya kuajiriwa, umewahi kufanya kazi mahali? Labda kwenye duka la vipodozi, hoteli, au hata kazi ya ujenzi? Huo ni uzoefu ambao wengi hawana. Badala ya kuanza biashara usiyoielewa, rudi kwenye eneo ambalo tayari unalielewa. Uzoefu ni mwalimu mkubwa kuliko mtaji.

Kama uliwahi kuuza bidhaa au kutoa huduma fulani, una faida ya kuelewa soko, changamoto, na mahitaji. Tumia hilo kama silaha ya ushindi wako wa biashara ya kweli.

Zingatia Haya Matatu Kabla ya Kuchagua Biashara​

1. Angalia Mazingira Yako​

Biashara nzuri inaweza kuwa mbaya kabisa ikiwa haiendani na mazingira yako. Usifungue biashara ya nyama ya nguruwe kwenye eneo lenye Waislamu wengi. Usianzishe duka la nguo za bei ghali mahali ambapo watu wengi ni wa kipato cha chini. Fanya biashara yako iendane na mahali ulipo, na iwe ndani ya uwezo wako wa kufuatilia hata kama ni mara moja kwa wiki.

2. Pima Muda Wako​

Una muda wa kusimamia biashara? Kama bado umeajiriwa, usianzishe biashara itakayokuhitaji kila siku. Chagua ile unayoweza kuisimamia kwa mbali au kwa saa chache. Hakikisha haitaathiri ajira yako ya sasa kumbuka, mshahara wako wa sasa ndio unaojenga biashara yako ya kesho.

3. Tambua Ushindani wa Soko​

Biashara yoyote ina ushindani, lakini hilo halimaanishi usiingie. Badala yake, tafuta ni wapi wengine wanakosea, halafu ubadilishe makosa hayo kuwa fursa. Weka huduma bora, ongeza thamani, na chagua mbinu za kipekee ambazo wengine hawatumi. Kumbuka: soko ni la ushindani, lakini ushindi ni wa wale walio tayari kuboresha kila siku.

MAMBO MATATU YA KUFANYA ILI BIASHARA YAKO ITOBOE MAPEMA​

1. Fanya Biashara Iwe ya Kipekee​

Hata kama biashara yako si mpya, unaweza kuifanya iwe ya kipekee kwa ubora, vifungashio vya kisasa, au huduma ya kipekee. Mteja akinunua kutoka kwako ajisikie tofauti. Usibaki kwenye kile watu tayari wanafanya toa kitu cha zaidi.

2. Anza kwa Kinachowezekana​

Ndoto yako inaweza kuwa kiwanda au Shopping Mall sawa. Lakini leo, una nini mkononi? Anza kidogo, anza kwa hatua. Ujenzi wa kitu kikubwa huanza na msingi mdogo. Wazo kubwa linafaa, lakini lazima linatekelezeka.

3. Sikiliza Wateja Wako​

Wateja wako ndio dira ya biashara yako. Kama walichopanga kununua hawakitaki badilika. Usibaki kung’ang’ania bidhaa zisizohitajika. Fanya biashara inayotatua tatizo lao moja kwa moja. Kukubali kubadilika ni hatua ya kwanza ya kufanikiwa.
 
Back
Top Bottom