Wachezaji wafundishwe zaidi ya Soka

Mphamvu

JF-Expert Member
Jan 28, 2011
10,711
2,000
Kutoka Mwananchi la 26 Mei 2014
Na Mphamvu Daniel
Dirisha la usajili katika ligi Kuu Bara bado liko wazi. Kama tulivyozoea, hiki ndio kipindi cha vituko pengine kuliko vyote katika kalenda ya Soka la hapa nyumbani.

Vioja kadhaa vilionekana wakati dirisha lilipofunguliwa, klabu ya Azam ilituhumiwa kusajili wachezaji kinyume na utaratibu kwa kuingilia kambi ya timu ya Taifa iliyokuwa jijini Mbeya na meneja wake kushikiliwa na Jeshi la Polisi.

Kwa mdau mzoefu wa Soka letu atasema kuwa huo ni mwanzo tu, bado tulishuhudia na tutaendelea kushuhudia vituko vingi hadi kipindi cha usajili kitakapoisha.

Watu watateka wachezaji makambini na viwanja vya ndege, zipo timu zitakazotangaza kuwa zimemsainisha mchezaji na kisha tukamwona akichezea timu nyingine msimu unaofuata, wapo viongozi watakaoapa kwa mbingu na ardhi kuwa wachezaji fulani hawatachezea huko walikosajili na kelele zingine nyingi.

Washabiki, sehemu muhimu kabisa na wateja wakubwa wa soka wamekuwa na maoni tofauti juu ya vioja hivi. Kundi fulani hulaumu viongozi kwa kushindwa kufanya vitu kwa kisasa na kwa kufuata utaratibu uliowekwa.

Kundi jingine hulaumu wachezaji wetu kuwa watu wasiojielewa na wasiothamini kazi zao. Hoja za kundi la pili ndizo nitakazojadili katika andiko langu la leo.

Wadau wanaosema kuwa wachezaji wetu wanakosa sifa za kuwa wa kisasa na hawajielewi wana hoja za msingi. Hawa wachezaji wetu wengi hawana taaluma nyingine zaidi ya soka, inakuwaje mtu unapuuza ofisi yako?

Naungana nao katika madai ya kuwa wachezaji wetu wana safari ndefu ya kujitambua na kufanya mchezo huu uwalipe kadiri ya umaarufu wao mitaani.

Upande wa pili, wadau hawa wakosoaji hawatoi suluhisho makini kwa tatizo hili zaidi ya kuishia kutoa lawama. Wanasahau ukweli kuwa mpira wa miguu unaweza kutazamwa kwa macho mawili; kwanza kama kipaji na pili kama kazi.

Ukweli ni kuwa kipaji ni zawadi toka kwa Mungu, na kama mtu anajua soka anajua tu. Kuwa na kipaji pekee hakutoshi, bado kuna wajibu wa kufanya kipaji kiwe kazi na kikulipe na hapa ndipo hapa wachezaji wetu walipokwama (sio kushindwa).

Huko ambako Soka limepiga hatua kubwa, wachezaji huandaliwa tangu wakiwa wadogo, fursa ambayo kizazi chetu cha sasa kiliikosa kwa sababu moja ama nyingine. Wao huandaliwa sio tu kama wachezaji, bali pia wafanyakazi na watu maarufu wa baadae.

Kwa kuwa elimu haina mwisho, bado kuna nafasi ya kuwaendeleza wachezaji wetu kwa kuwafundisha taaluma mbalimbali ambazo zitasaidia kufanya maisha yao ya soka kuwa ya ufanisi kuliko ilivyo sasa.
Wadau wangu niliowanukuu mwanzo wanaweza kudai kuwa huu ni wajibu wa wachezaji wenyewe, lakini mimi naweza kusema kuwa huu ni wajibu wa viongozi wa Soka, wa vilabu, shirikisho na hata vyama vya mikoa.

Mchezaji wa kawaida wa Ligi Kuu anakuwa na elimu ya kidato cha nne au pengine darasa la saba, tena wakati wa kusoma alilazimika kukatisha au kutomakinikia masomo kwa ajili ya soka. Ni vigumu kwa mtu wa kiwango cha elimu tajwa, tena ambaye ameshakuwa maarufu kufikiri kwa mapana kiasi hiki.

Vilabu vinaweza kutenga muda wa kuwafundisha wachezaji wake Soka katika mtazamo wa kazi (professionalism). Sio lazima yawe masomo ya mkazo mkali kama ya darasani, masaa machache tu kwa wiki yanatosha kumfumbua mchezaji kwa kumpa misingi ya mwanzo kazi.

Hii itasaidia wachezaji hawa kujua nafasi ya soka katika maisha yao ya kila siku, na hatutasikia tena kesi za wachezaji kutoroka kambini na kwenda kucheza ndondo mitaani, kama ilivyokuwa msimu uliopita kwa wachezaji wa Yanga.

Wachezaji hawa wanaweza pia kupewa misingi ya sheria za kazi na sheria za mikataba. Zipo kesi kadhaa za wachezaji kusaini na timu mbili, laiti kama wangefahamu walau kidogo sheria za mikataba yote haya yasingetokea.

Kipengele kingine ambacho vilabu vina wajibu wa kuwafundisha wachezaji wake ni misingi ya afya ya mwanamichezo, lishe na kujitunza. Vilabu vina waganga ambao hutibu wachezaji, lakini sina hakika kama huzungumza nao kuhusu namna gani wanatakiwa wajitunze wanapokuwa nje ya kambi, vyakula gani waepuke na tabia zipi ni hatari kwa kiwango cha mchezaji.
Wachezaji hawa wanatakiwa pia kufundishwa mbinu za ujasiriamali kwani miaka inaenda na maisha ya Soka yatafikia ukomo wake. Tunayo mifano ya wazi ya wachezaji wa zamani ambao hali zao za kiuchumi ni mbaya kutokana na kushindwa kuwekeza pesa walizozipata wakati wanacheza soka.

Jambo la mwisho ni nidhamu na uhusiano wa kijamii. Wachezaji wa Ligi Kuu kama ilivyo watu wengi maarufu wana tatizo la ulimbukeni. Wanashindwa kufahamu nafasi kama watu maarufu na vioo vya jamii, vitendo vya kutukana washabiki, kurushiana maneno hadharani na katika mitandao ya kijamii vimetokea mara kadhaa miongoni mwa wachezaji wetu maarufu (rejea tukio la John Bocco katika Facebook).

Si lazima timu au shirikisho liajiri wataalamu wote hawa kwani ni gharama kubwa, upo uwezekano wa kuandaa utaratibu kwa kutumia walimu na wataalamu waliopo kutoka vyuo vya elimu ya juu kuja kuwapa semina 'mastaa' wetu kwa manufaa yao na kizazi chetu cha Soka.

Pamoja na kuwa makala hii imewalenga wachezaji wa Soka pekee, hata wachezaji wa michezo mingine waneza pia kujifunza kutoka hapa. Mashirikisho, vilabu na mameneja wanaweza pia kuwa na utaratibu wa kuwafunza wachezaji hawa stadi mbalimbali za kuwafaa katika taaluma zao.

+255 713 049 852
mphamvudaniel@gmail.com
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Top Bottom