wabunge wawapongeza waandishi wa habari

Ochu

JF-Expert Member
May 13, 2008
976
47
Wabunge wamepongeza kazi zinazofanywa na waandishi wa habari na kukemea tabia ya baadhi ya watu kuwashambulia na kuwatupia lawama waandishi wakati wakitekeleza majukumu yao ya kazi.

Wakichangia hoja baada ya kuwasilishwa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2008/2009 ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo bungeni mjini hapa jana, wabunge hao walisema wanahabari wamezungukwa na changamoto nyingi na kwamba moja ya changamoto hizo ni kutupiwa lawama hata kama kosa limefanywa na mtu mmoja.

Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM) alisema vyombo vya habari vinapaswa kusaidiwa na kwamba imefika mahali serikali sasa inapaswa kuviangalia vyombo vya habari kwa mtazamo chanya. Chegeni alisema vyombo vya habari vinapaswa kuimarishwa ili vifanye kazi zake kwa tija kwani vimesaidia kuleta mapinduzi makubwa ya kimaendeleo nchini.

Alisema mwenendo wa baadhi ya taasisi za serikali kuvinyima vyombo vya habari taarifa ndio chanzo cha baadhi ya waandishi wa habari kuandika habari za kupotosha na hivyo wasilaumiwe. “Habari zinapotoshwa kwa sababu watoa habari hawataki kutoa habari, tumeona hapa habari mfano za EPA ilianza kama habari rojorojo, halafu mwisho wa siku kumbe habari ni ya kweli,” alisema Dk. Chegeni na kuwataka watendaji wa serikali kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete la kutoa taarifa mara kwa mara kwa vyombo vya habari.

Alisema pia tabia ya kuvamia vyombo vya habari na kuvipekua, sio nzuri kwani ni kuwatisha na kuitaka serikali iwe inajibu hoja ya msingi na sio kukurupuka, lakini vile vile aliwataka wanahabari kutokiuka miiko ya taaluma zao na badala yake watoe habari za kujenga nchi. Mbunge wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir (CCM) alisema wanahabari ni watu muhimu katika maendeleo ya nchi, mageuzi ya kisiasa, kujenga uchumi na kufichua maovu.

Mudhihir alisema haifai kuwachukia wanahabari kwani kufanya hivyo ni sawa na kujichukia mwenyewe na kwamba mwanahabari mmoja akienda kinyume cha maadili ya taaluma yake, haina maana wote ni wakosaji. Alivitaka vyombo vya habari kustahimiliana na kuacha tabia ya kupigana majungu na kupelekana mahakamani, lakini vile vile aliiomba serikali kuviwezesha vyombo hivyo kuwa na vifaa na wataalamu.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA) alipongeza juhudi za vyombo vya habari kwa kazi nzuri ya kuhabarisha jamii, lakini akatoa wito kuwa bado kuna haja ya kuboresha maslahi ya waandishi wa habari. Zitto alisema tabia ya baadhi ya wamiliki kuwa na makundi kwa ajili ya kulinda maslahi yao imetoa mwanya kwa wamiliki hao kufukuza au kusimamisha waandishi wa habari bila kuzingatia misingi ya habari.

Alisema Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ni wizara inayogusa vyombo vyote vya habari na hivyo serikali iamue moja, iwapo italifanya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) lijiendeshe kama taasisi huru kibiashara au kuipa ruzuku ya asilimia 100. Mbunge wa Viti Maalumu, Faida Mohamed Bakar (CCM), alisema wizara hiyo imetengewa bajeti finyu na kwamba ndio inasababisha vyombo vya habari kushindwa kuifikia vizuri jamii.
 
Back
Top Bottom