Vyama vya msimu vyaleta mvua kali Igunga (storm)

Nikiwa kama mwana CCM, nasikitishwa sana na mwenendo wa kampeni za ubunge kwa jimbo la Igunga. Tatizo kubwa tumekosa cha kuwaambia wananchi wa Igunga, tumebaki tukicheza ngoma ya CDM kwa nyimbo zao wanazotuimbisha. Binafsi mimi si muumini wa siasa za chuki na matusi. Napenda sana siasa zenye kuendeshwa kwa ustaarabu naunyenyekevu wa hali ya juu kwa wapinzani wako.

Binafsi napingana na kitendo cha kumkaribisha RA kwenye kampeni za Igunga, kwani huyu mtu tulishamwambia yeye si msafi hicyo atupishe kwenye chama, sasa inakuwaje tumrejeshe tene? Hapo ndipo tunapokuja kukosa cha kuwaambia wananchi wetu. Hivi kama tungesimama hapo Igunga kwa kauli yetu moja tukipaza kwa sauti kuu, ya kuwa ufisadi na mafisadi kwenye chama chetu hawana nafasi bali walipita kwa bahati mbaya. Kwa kuwa walikuwa wamevaa ngozi ya kondoo ndio maana wakatuhadaa, sasa tumewaona na tunawatimua na huyu aliyekuwa mbunge wenu ndio tumeanza naye.

Potelea mbali hata kama ingetugharimu kukosa jimbo la Igunga lakini kwa jamii tungeanza kurudisha imani kwao. Hapa tulitakiwa tuite jeshi letu lote la wale vinara wa kupambana na mafisadi ili wapate uwanja wa kunene kwa sauti zao ili wananchi wawasikie. Kwa kweli tumeanguka anguko kuu kama chama katika hili suala la kujivua gamba.

Mtazamo wangu hapa kuanzia mwenyekiti wa taifa wa CCM na kamati kuu yoote, hawafai kuongoza chama katika kipindi hiki kigumu sana . Labda ingekuwa enzi hizo. Kwa sasa chama kinamuhitaji sana mtu mwenye uelewa wa juu sana na mwenye muonekano safi kwa jamii na pia mwenye kunena kweli bila kupindisha maneno.

Masikini CCM yangu, unaangamia nikiwa sina msaada wa kukuokoa. Huwa nalia sana nikiwaona viongozi wa mithili ya Tambwe Hiza, Livingstone Lusinde, Sophia Simba, John Chiligati, Steven Wasira, Wiliamu Lukuvi, George Mkuchika na wengine wengi wasio na ufahamu na uwezo wa kuwaongoza watu wao.

Wakuu nawaacha na huu msemo kwa lugha ya kigeni;
A leadership commits a crime against its own people if it hesitates to sharpen its political weapons which have become less effective.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom