Vita vya ujinga: Dhana iliopotoshwa

Aloysius

Member
Mar 1, 2011
80
9
[h=2]
icon1.png
Vita vya ujinga: Dhana iliopotoshwa[/h]

VITA VYA UJINGA: DHANA ILIYOPOTOSHWA​
Kwa muda mrefu hapa nchini nasehemu zingine za Afrika kumekua na dhana ya vita vya kupamba na ‘Ujinga’. Nimeshawishika sana na kuzungumzia vita hivi vikongwe, vya ujinga, kwasababu nyingi. Kuu kuliko zote ambayo lazima niitaje katika aya hii ya kwanza ya uchambuzi wangu ni pale ambapo kwa muda mrefu nimekuwa nikisikia waungwana fulani wakihusisha ujinga na elimu, tena Elimu ya darasani (Formal Education).


Kwa mfano nchini Tanzania kumeshuhudiwa hivi karibuni shule zikijengwa kama uyoga, kama kiashiria cha kupambana na adui ‘Ujinga’ ni kweli Mwasisi wa taifa letu Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliwahi kubainisha kuwa maadui zetu wakubwa ni UMASKINI, NJAA, na UJINGA. Hii haina shaka, ila sasa, hauwezi ukapambana na adui usiyemfahamu hii ni sawa na kukung’uta risasi hewani pasipo kulenga unacho kusudia kukifyatua, kwanza utakua unapoteza risasi ambazo zinathamani, pili utakuwa unapoteza muda wako na tatu adui yako ataendelea ‘kudunda mitaani’, hii ina maana kuwa hautakuwa ni timamu akilini. Mara nyingi katika maisha yangu mafupi nilioishi hapa duniani nimekuwa nikisikia ujinga ukinyooshewa kidole kama chanzo cha dosari au mataizo fulani katika jamii.

Inatokea neno ‘ujinga’ likatumika katika jamii zetu kusaidiana na neno ‘kutoelimika’ mtu anaposema, ‘fulani hawezi… hajasoma’ ana maana kuwa Fulani hana ufahamu (knowledge) maana yake ni ‘mjinga’. Tumewahi kusikia mtu akisema; sehemu kubwa ya watanzania ni wajinga, hii inatakiwa imaanishe nini? Hapo ndipo nikafikiri kuwa umekuja wakati wakujipa muda ili kufahamishana kinaga ubagha juu ya dhana hii. Nita mimina wino wangu kuzungumzia ‘ujinga’ kama dhana, pia tufahamu ‘Ujinga ni nini? Nani ni mjinga na kisha tutafakari kama kuna upotofu wadhana nzima ya ujinga katika jamii zetu.

Kamusi moja inaeleza ujinga kuwa ni; ‘hali ya kutokujua kitu fulani, ubozi au ujahili’ maelezo ya kamusi hii juu ya ujinga bila shaka ni mtihani mkubwa kwa wengi nikiwemo na mimi; inatujaribu kukubali kuwa; kitendo cha kutokujua kitu fulani tayari ni ujinga. Sasa hebu tujiulize, nani anajua kila kitu? Uelewa wangu juu ya fasiri hii ni kuwa mtunga kamusi anaona kila mtu anaweza akawa mjinga wa jambo fulani.

Ukweli ni kwamba dhana nyingi muhimu zimepotoshwa au zimekosewa katika jamii zetu hasa na wanasiasa, kwa sababu ya kutokujipa muda wa kutosha kutafakari juu ya dhana hizo muhimu. Na hii pengine inatujengea jamii isiyo kamili, jamii bandia badala ya jamii halisi, jamii ambazo giza limegeuzwa kuwa nuru na nuru imegeuzwa kua giza . Wakati Fulani mwanamapinduzi maarufu Martin Luther King Jr. aliwahi kusema maneno yafuatayo: “Kuna matatizo mengi muhimu katika jamii yamepatiwa majibu ambayo hayajaokwa kikamilifu, hii ni kwa sababu hamna kinacho watia maumivu baadhi ya watu kama kufikiri”.

Nafikiri hii ni habari mbaya ijapokua ni ya kweli hasilani, watu tumekuwa wavivu wakufikiri mno, matokeo yake tunapatia vitu vipana maana finyu sana . Basi kwa maana hiyo tualikane tuliangalie hili la ujinga ili kubaini adui tunaye pambana naye.

Ugumu wa dhana ya ujinga unadhihirishwa na makosa yaliyo wahi kufanywa hata na baadhi ya wanafalsafa, mfano Hegel Mwanafalsafa Mjerumani maarufu, katika falsafa zake aliwahi kutuhumu jamii ya watu weusi kuwa, ni watu wasioweza kufikiri sawa sawa, ni watu wanaotawaliwa na hisia na sio mawazo, kwa lugha nyingine Hegel alimuona mtu mweusi kama mjinga wa kupindukia. Je haya yalikuwa ni ya kweli? Bila shaka ni makosa ya kifikra lakini jambo la namna hiyo liliwahi kutokea katika historia na likakubadilika na baadhi ya watu. Katika zama hizi zisizo za Hegel nafkiri makosa yanajirudia, watu wa zama hizi hawamtofautishi fukara na ‘ujinga’ au hili ni eleweke vizuri hawamtofautishi ‘mjinga’ na mnyonywaji anayekaushwa damu na kupe-watu.

Hebu tuangalie mawazo ya wanafalsafa mbalimbali juu ya ‘ujinga’ kama unavo chuana na ‘uerevu’. Katika kitabu kiitwacho ‘African Philosphers’ Ambacho kinakusanya mawazo ya wanafalsafa mbalimbali naye Emmanuel Chukundi Eze, chapa ya Blackwell Publishers 2004, UK . 77 kuna hotuba ya Mwalimu Julius K. Nyerere ya mwaka 1966, yenye kichwa cha habari kisemacho ‘Viongozi hawapaswi kuwa Mabwana ‘mungu-watu’ (Leaders should not be Masters) aliyoitoa katika ziara yake katika visiwa vya Mafia. Nitadokoa kipande kidogo tu cha usemi wake. Katika hatua Fulani alisema;

“…niliwaambia watu huko nilikotoka kuwa waniulize maswali, au wanieleze matatizo yanayowasibu katika maisha yao ya kila siku, ila ilikuwa ni ngumu kupata watu wakuniuliza maswali, walinieleza kuwa hawana matatizo yoyote, nakuwa mambo yao yalikuwa murwa. Walihofu kuongea wakifikiri wataadhibiwa...”

Mwalimu alienda mbele zaidi nakunyooshea kidole chanzo cha tatizo hilo , alieleza kuwa chanzo cha desturi hiyo ya ukimya, ni sumu aliyotupulizia mkoloni; Wajerumani, Makaburu, Waingereza na kadhalika kwa kutueleza kuwa sisi ni wajinga.

Zaidi katika juhudi za kuhamasisha wananchi ili wazinduke na kujisikia kuwa nchi ni ya kwao, na mawazo yao ni muhimu katika ujenzi wa taifa alisema;

“…wakati mwingine mama yangu mzazi ananiita na kunipatia ushauri, Ananionya nifanye nini na nisifanye lipi. Ananishauri hata katika mambo ya serikali. Ananishauri ijapokuwa hana ‘elimu ya darasani’. Kwanini? Je inamaanisha kuwa mtu asiyekuwa na elimu ya darasani ni mjinga? Mtu ambaye ajaenda shule anaakili aliyopewa na Mungu...”

Ala ! Kumbe tunaanza kupata picha toka kwa falsafa ya Mwl. Nyerere kuwa kuna werevu nje ya shule. Hebu tuchambue kipande cha ujumbe huu wa Mwaalimu kabla hatuja kwenda mbali.

Mwalimu anasema nani alimfanya mwafrika ajione kuwa ‘hajui’ au ni ‘mjinga’ anasema ni mkoloni, kumbe wakati mwingine mtu wa pili anaweza akapotosha uhalisia wako, hata kwa kutumia nguvu na hata kama ikishindikana kwako iwezekane kwa kizazi chako kijacho, kukufanya upate sura potofu juu ya uasilia wako. Sasa niulize swali la kichokozi viongozi wa leo hawaja chukua nafasi ya mkoloni? Aste tutayapata majibu yote hayo. Mwalimu pia anasema kuwa mtu ambaye haja kwenda shule anaakili aliyopewa na Mungu ( Kumbuka kuna akili na ubongo, ni kama roho na mwili) sasa tujiulize, aliyekwenda shule kapewa akili na nani?

Nafkiri Mwalimu hajakosea kitu, wazo lake nitalitia nguvu na mawazo ya baadhi ya wanafalsafa pia. Kumbe basi elimu ya darasani ni mawazo ya binadamu mmoja aliopewa nafasi ya unguli kwenda kwa binadamu mwingine, yawe mafupi, mabaya, maouvu au pengine mazuri. Hivi tukifuata mnyororo wa chanzo cha elimu ya darasani nini itakua ni chanzo asili cha elimu hiyo. Bila shaka ni akili ya asili. Au kwa lugha nyingine nini ni asili ya nyingine kati ya ujuzi wa asili na elimu ya darasani?

Profesor Weredu katika kitabu chake cha Philosophy and African Culture Cambridge University Press 1980, P. 47 alijikwa pia katika kuwaza; Yeye alisema kuwa waafrika hawana falsafa, hii ina maana kuwa waafrika hawawezi wakafikiri juu ya mambo yanayotatiza akili, hili linapingwa vikali na mtizamo wangu, Anaeleza kuwa falsafa ni lazima iambukizwe, ielezewe kwa kuandikwa na kadhalika.

Katika kitabu cha ‘Africa Philosopher’ (tajwa hapo juu) ukurasa wa tano, mtoa mada ameangazia udhaifu wa dhana ya Weredu, nakusema kuwa; Weredu anazungumzia falsafa ya magharibi, hana heshima kwa falsafa ya kiafrika, kwani waafrika walikuwa na njia zao za kuambukiza ujumbe au busara zao kwa kizazi kingine mbali na njia ya maandishi. Ni wazi kuwa njia ya maandishi ijapokua ni bora zaidi, kwa muktadha wa kuhifadhika, ila sio njia pekee kwa maana ya kutuma au kuhifadhi ujumbe.

Anasema kuwa falsafa ya Mwafrika inadhihirishwa na ushahidi wa aina nyingi kama misemo ya wahenga, Mithali, vitendawili, ngonjera, ngano na vigano, mafumbo na kadhalika. Mwanafalsafa muhimu kumnukuu katika muktadha huu ni Karl Jaspers yeye hana haya yakusema;

Binadamu hawezi kuzuia kuwa mwanafalsafa, au kuwaza kwa kina sana , Kwa maana ya kwamba, katika wakati mmoja au mwingine katika maisha
Yake anajikuta akianganza mambo fulani muhimu juu ya maisha ya
Binadamu au falsafa juu ya fisikia ya ulimwengu”

Mfano, katika misiba, wakati wa ugonjwa, majanga na kadhalika, hapa Karl Jaspers anamuona kila mtu kua si tu kwamba ni mwerevu ila kuwa ni mwerevu wa kiwango cha juu kwa kutilia maanani kuwa ‘falsafa’ ni kiwango cha juu cha kufikiria, basi kwa maneno yake ‘kila mtu ni mwanafalsafa’.

Kwa pumzi ya mazungumzo haya twaweza sema kwa ujumla hakuna mtu ambaye ni mjinga wa asili, ila kuna ‘ujinga’ kwa maana hiyo mtu anaweza akatenda kwa ujinga, niweke mkazo, mtu yoyote; awe Profesor, Msomi wa shahada ya uzamivu, mwanafalsafa, Padre kwa mchungaji, Rais kwa mawaziri au hata mwanafalsafa anayeheshimika kuliko wote.

Hivo ‘ujinga’ ni mfano wa pombe, ukinywa unalewa, mtu yoyote anaweza akanywa pombe kwa kiwango akitakacho, lakini hakuna mtu aliyezaliwa akiwa mlevi, pia hakuna mtu anaye kuwa katika hali ya ulevi masaa 24 ya siku zote za maisha yake, kunawakati tu atazinduka. Upande mwingine, elimu ni sawa na marashi. Manukato au marashi ni molekiuli ndogo zenye harufu ya kunukia ambazo uchanganyikana na hewa punde zinapo pulizwa na kisha kutoa harufu nzuri ya kuvutia, inapendeza pua kuinusa harufu hio, likini wakati mwingine huweza kuleta dosari katika afya, mfano huweza kusababisha mafua, au uweza kuwa hareji kwa baadhi ya watu. Elimu ya asili ni kama pumzi ya asili, ni uhai kwa uhalisi wake, lakini ni kama nyumba isiyo na paa, milango wala madirisha, haigombi ikichafuliwa, ikipotoshwa au kutokomezwa.

Zaidi ifahamike kuwa elimu ya darasani ni moja kati ya vitu vidogo sana ambavyo akili inauwezo wakuvimudu, lakini si kitu cha lazima kwa akili ili iweze kufanya kazi ipasavyo. Tumekwisha ona yakuwa katika historia wanafalsafa fulani waliingia katika hatari ya kuwaona watu fulani kwasababu zao fulani ya kuwa ni wajinga wakupindukia. Hii ni kweli kuhusu sasa pia, kuna kundi la watu ambao kwasababu ya hali zao kuwa duni wote wamejikuta katika kundi la watu waitwao wajinga, na mbinu zinafanywa kuundoa huo ujinga kwao!!! Lakini nafkiri tutakuwa kwenye upande sahihi kama tukisema kuwa, kila mwenye ubongo ni sharti anawaza ila tu kama ni mlemavu wa akili kama ilivo kuwa kila mwenye macho sharti anaona ila tu kama ni kipofu.

Turudi kwenye mfano wa pombe, tumesema ujinga ni sawa na pombe, hakuna kitu hatari kama kunyweshwa pombe kwa kutokujua, mfano kuchanganyiwa pombe kwenye kinywaji laini pengine, kwakuwa kisaikolojia unakuwa haujajiandaa kulewa, hivyo ndivyo ilivo kwa ujinga pia, hakuna ujinga mbaya kama ule wa mtu kukufanya kuamini kuwa wewe ni mjinga na wewe ukaamini hivo, huu ndio ujinga mbaya kuliko wote. Pia ujinga unaoingizia katika madawati ya chuo kikuu sehemu ambapo ulikuwa umejiandaa kuvuma vipand vikubwa vya ufahamu, ujinga wa namna hiyo unaganda katika akili kama zege iliyokauka, kila mara utanukuu yale uliyoyapata darasani. Chukulia mfano wa mtu aliyofundishwa na mwalimu wake wa dini kuwa kesho ni mwiso wa dunia, uzoefu unaonyesha ujinga wa namna hio ulivo na nguvu! Hii inaweza ikawa hivyo hata darasani pia!

Hebu sasa tuligeukie swala la pili la nani ni mjinga? Au mjinga anasifa zipi, ili hatimaye tubaini kama kweli vita vya ujinga vimeelekezwa kwa adui sahihi, au nivita vilivo potoshwa. Mwanafalsafa wa kidini anayekubadilika na dini zote kuu mbili hapa nchini Sulemani mwana wa Daudi katika kitabu chake cha methali, katika vifungu mbali mbali anamtaja mjinga kuwa na sifa zifuatzo:

Kwanza anaaza kwa kusema kuwa maarifa hutoka kwa Mungu, hapa mawazo yake yanakubaliaana na mawazo ya hayati Mwl. Nyerere katika nukuu yake hapo juu. Anasema kuwa mtu mpumbavu haitaji ushauri, na ukimkosoa mnaweza mkadumu kuwa maadui.

Anasema mjinga huwa na tabia ya kujinadi, mahala fulani anasema, kijana mwenye busara ukubali kukosolewa na baba yake ila mjinga hakiri makosa kamwe. Wasifu mwingine ni kuwa; mtu mwenye busara ana busara kwa kua anajua anacho kifanya, ila mjinga ni mjinga kwakuwa anafkiri anajua. Mtu mwenye maarifa utenda kwa taratibu, baada ya kuchunguza, ila mjinga ukurupuka na kufanya jambo.

Sulemani anaenda mbali zaidi na kutofautisha elimu na busara, au kwa lugha za kisasa kutokwenda shule na ujinga, anasema; haimsaidii mjinga kutumia pesa zake katika elimu kwakua hana maarifa. Ala ! Kumbe kuhudhuria shule siyo kigezo pekee cha kuondoa ujinga, bali elimu inawapasa werevu? Haya ndio mawazo ya Sulemani. Pia anasema, mtoto mjinga huleta hasara na majonzi kwa wazazi wake.

Maneno ya mwisho ya Sulemani ninayo panda kuyachukua ni yanayosema kuwa; Uzito wa mawe na mchanga sio kitu kwa hatari ambayo ujinga unaweza kusababisha.

Mwanafalsafa Sulemani anaorodhesha sifa hizo hapo juu miongoni mwa zingine kama wasifu wa mtu mjinga. Kwa mawazo yangu yuko sahihi kwa nguvu zote. Lakini je hayo aliyoyaorodhesha yanatumika kumpima ‘mjinga’ au ‘mwerevu’ katika jamii zetu za sasa? mbali na kwamba ndio ukweli. Utu wa mtu kwa sasa unapimwa kwa pesa au mali , madaraka, unadhifu wa kuvaa au kuongea lugha fulani na anasa za namna hizo pasipo kujali zimepatikanaje. Lakini hii haibadili ukweli, Mwaka 1995, Mei Mosi Hayati Mwanafalsafa maarufu wa Afrika Mwal. Nyerere akihutubia wafanyakazi mbeya alizungumza maneno yafuatayo:
“…wakati wetu enzi za Tanu, pesa ilikuwa kigezo cha kukunyima sifa kuwa mgombea, ila hivi sasa pesa ni kigezo cha kukufanya ukubalike…’

Hii inaonyesha jinsi gani mambo yanaweza kugeuzwa kichwa chini miguu juu kama watu wachache makini wasipokua mbogo. Kuna dhana yakupunguza ujinga kwa kuongeza shule, hii kweli ni dhana hai? Sulemani anatueleza mjinga ni na nani, hebu tuhusishe hizo sifa hapo juu na hali halisi ya kinachoendelea katika jamii zetu ili tuone kuwa nani ni mjinga anayehitaji elimu;

Je umma ambao haujakwenada shule haumchi Mungu hata maradufu, mpaka ikamfanya NABII ISSA kutoa angalizo kuwa tajiri ni vigumu kuingia mbinguni kama ngamia kupita katika tundu la sindano, hivyo basi hawa ndio waliokalia kisima cha chanzo cha maarifa kwa mujibu wa Sulemani. Tumeshuhudia viongozi wa ngapi tena wasomi wasioshaurika wala kuambilika, waliowashupavu kama nyama yakuanikwa kwa mujibu wa sulemani huo ndio ujinga.

Kujinadi; hii ndio kazi ya wasomi walafi wanaotaka kwenda kutumbua kodi za wanachi huko katika ‘paradiso za katikati ya mji’ (mbungeni), watatumia runinga na vyombo vya kila aina kujitia walimbwendo lengo lao likiwa moja tu, kujikosha, baadae upaa kama tai hata wasionekane tena, haja zao zikishatimizwa. Mara ngapi viongozi hao wanaojiita wasomi hufanya utumbo wa waziwazi lakini bado wakawa wagumu mithiri ya gamba la kobe kukiri makosa yao achilia mbali kuomba msamaha, kwa kuwa kuomba msamaha ni kipaji, mwishowe wanaongea kana kamba wao ndio wameonewa napengine ndio wanaostahili kuombwa msamaha, haya ndio sulemani anayaona kuwa ni ujinga wa kupindukia.

Kujitia kujua; hii ni kawaida iliyozoeleka ya ndugu wanao jiita wasomi, kwa muda mrefu wamejiona wajuaji huku wakiita umma wa wale ambao hawaja enda shule kuwa ni jamii ya wajinga. Wanajitia kujua hili hali wanao jiita wanasheria wakichemka kuandaa mikataba ya kimataifa, kiasi kwamba haifanyi vizuri katu zaidi ya makubaliano ya wakina Mwanamutapa, Lobengula, Jaja wa Opobo, Chaka Zulu na machifu wetu wengine wa enzi hizo, tumeshuhudia magavana wakiingizwa mjini, karibu kila sekta hata mpaka ikulu pamoja na kuwepo na majopo ya wanaojiita wataalam. Hizi siku za karibuni watoto wetu wajinga wametufanya kupata hasara na huzuni kubwa hilihalli wakijitia kujua, hosipitalini huko ‘blanda’ ni zile zile uzembe ulio pindukia, hawa ndio wajinga halisi wanao hitaji elimu kwa mujibu wa Sulemani.

Sulemani anataja kuropoka kama moja ya sifa za mjinga, wasomi wa ngapi wanchi hii waliopewa nafasi za kuongoza wanaoropoka kama chiriku, wasiochunguza kwanza rekodi zao, hivi karibuni kwa mfano tumeshuhudia watu fulani wakivuliwa uraia kimakosa kwa ndimi za hao wajiitao wasomi zisizo kuwa na breki, au wakati mwingine kutoa mijiahadi ambayo haitekelezeki au inayo pingana na mipamgo ya kibajeti, Sulemani anamuoana mtu wa nama hii kama muhitaji mkubwa wa elimu na mjinga wakupindukia.

Uamuzi wa kukurupuka; hii tunashuhudia kwa viongozi wetu, kwa kiasi hata cha kupoteza roho zisizo na hatia, mfano hizi siku za karibuni tulishuhudia utata wa amri ilyotolewa bila ya uchunguzi na utaratibu, nakupelekea vifo vya wafanyabiashara raia wema wasio kuwa na hatia, kwa kosa ambalo hata hivyo halikuwa linapaswa kuadhibiwa kwa kifo, na mengine mengi ya namna hiyo, haya ndio matendo ya mjinga wa wajinga kwa maoni ya Sulemani.

Baada ya kuona hayo sasa hebu tujiulize, je, ni kweli tunapambana na adui ujinga? Jibu ni hapana kwakuwa hata ndio bado hatuja jua adui ‘ujinga’ ni nini? Tutapata werevu wakiafrika pale ambapo tutakuwa na watu wanaosema; hapana tunataka chungu badala ya sufuria kwakuwa ndio teknolojia ya mwafrika inayo wezeshwa na mazingira yake, mkaa bado ni njia nzuri ya nishati, ila tupande miti kwa wingi kwa kuwa hatuwezi tukahama kwenda kwenye mafuta hili hali hayapo katika mazingira yetu hiyo inatufanya tuwe tegemezi. Huu ndio usomi na si ule wa kuwa mabibi harusi wa umagharibi. Hauwezi ukatutajia athari za kimazingira za kuchoma kutumia mkaa kama nishati ukaacha kututajia athari za mafuta, kwanzia uchimbaji mpaka matumizi jumlisha adhaa yakuwa tegemezi. Zote zina athari kwa mazingira, kwanini sisi ndio tusasalimu amri? Au kwakuwa tume elimika?

Hitimisho langu ni kuwa kwa hoja hizo hapo juu ni wazi kuwa hii inayo itwa ‘elimu’ imetuongezewa ujinga kiasi cha kutosha, na uvivu wa kufanya kazi zinazoweza kuzalisha, umefika wakati wa waliolemazwa na hii tunay iiita ‘elimu’ kukaa pembeni ili fukara wenye busara zao waongee, hasa kipindi hichi ambao suala kuhusu hatima ya katiba ni ‘kiti moto’ ndio maana sulemani anasema kuwa; “maskini anapozungumza anakua mnyenyekevu na mpole, lakini tajiri anapojibu, hujibu kwa kiburi. Nikunje janvi kwa kusema ingekuwa vita vya ujinga vinamuua alio ubeba wajiiitao wasomi wengi wangekufa kama majani yaliyo liwa na zinge nakuwaacha walala hoi wakitesa. Bado hatuja pata mfumo wa elimu bora kwaajili ya ukombozi wetu sisi kama nchi za ulimengu wa tatu, na elimu kubwa na muhimu kuliko yote haiitaji ubao, ni, UPENDO (uzalendo), kwa nchi na watu wanchi yako, uadilifu, busara, heshima, huruma, na umakini.

Aloys R Rugazia
SAUT University Mwanza
Mwanafunzi wa Kitivo cha Sheria
Phone: 0757 333 036
Email: alyosrugazia@yahoo.com
 
Back
Top Bottom