Vita ndani ya Chadema bado mbichi

Vita ndani ya Chadema bado mbichi

Parabolic

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2013
Posts
2,743
Reaction score
2,601
bawacha-px.jpg

Madai ya kupigwa na kujeruhiwa kwa Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Sigrada Mligo, yameibua upya mzozo wa kambi zinazosigana ndani ya chama hicho, ambazo ni kati ya Mwenyekiti Tundu Lissu na mtangulizi wake, Freeman Mbowe.

Sigrada anadaiwa kushambuliwa na mmoja wa walinzi wa Chadema Machi 25, 2025 baada ya kutokea sintofahamu katika kikao cha ndani cha viongozi wa chama hicho kilichofanyika mkoani Njombe chini ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche muda mfupi baada ya moja ya mikutano ya kauli mbiu ya No reforms no election (hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi).

Kwa mujibu wa polisi, baada ya kutokea majibizano hayo kwenye kikao, Sigrada aliamriwa kutoka nje ya kikao na alipotoka, baadaye alitakiwa kurudi, lakini kabla hajarudi, mmoja wa walinzi alishambulia na kutoweka eneo hilo.

Ghafla tukio hilo likadakwa na CCM wakilaumu kwa nini Chadema wamshambulie kada wao. Katika mkutano na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Mary Chatanda alihoji kwa nini Bawacha hawajatoa kauli kwa kiongozi wao kushambuliwa.

Kama hiyo haitoshi, makada wa CCM wakafika hospitali aliyokuwa amelazwa Sigrada mkoani Njombe kumjulia hali. Ghafla tukasikia amepewa rufaa kwenda katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Benjamin Mkapa.

Ni kwa nini CCM wameingilia ugomvi usiowahusu? Je, Sigrada alikuwa mauhututi kiasi cha kupelekwa hospitali ya rufaa? Je, Mkoa wa Njombe hauna hospitali ya rufaa mpaka apelekwe Dodoma? Kwa nini sio mkoa mwingine?

Hiyo yote ni kuonyesha kwamba kwenye vita hakuna silaha ndogo, kitu chochote kinaweza kutumiwa kama silaha na kamwe usije ukamdharau adui yako. Inawezekana Chadema walilichukulia tukio hilo kirahisi, lakini wenzao CCM wamelichukulia kwa uzito wakiamini kuwa wanaweza kuingilia hapo kuwavuruga.

Mgawanyiko Chadema

CCM haifurahishwi na operesheni ya Chadema inayoendelea ya No reforms no election, ndio maana kila viongozi wao wakisimama kwenye mikutano ya hadhara wanaikosoa na wanajibu hoja moja baada ya nyingine zinazotolewa na Chadema. Wanajua kampeni hiyo ni hatari, inaweza kulipua nchi nzima.

Wakati CCM wakilipua hivyo, tunaona sasa ndani ya Chadema napo moto unawaka. Baada ya uongozi wa Chadema kutoa tamko la kuchunguza tukio hilo Machi 31, baadhi ya makada akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Uhusiano, Itifaki na Mambo ya Nje, John Mrema na kada mwingine James Mbowe wamehoji sababu ya chama hicho kuwa kimya wakati kada wao ameshambuliwa.

Itakumbukwa kuwa Sigrada anatajwa kuwa miongoni mwa makada wa Chadema waliokuwa wakimuunga mkono Mbowe na wameendelea kuonyesha mapenzi kwa kiongozi huyo hata baada ya kushindwa uchaguzi.

Wakati sakata la Sigrada linaendelea, hivi karibuni Mwenyekiti wa Chadema wilayani Mwanga, Lembrus Mchome alimwandikia barua Msajili wa Vyama vya Siasa akimtaka aingilie kati madai ya chama hicho kuvunja Katiba yake wakati Mwenyekiti wake, Tundu Lissu alipoteua wajumbe wa kamati kuu Januari 22, 2025, akisema baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu hawakuwa na sifa ya kupiga kura na kwamba akidi haikutimia.

Mchome ambaye pia alikuwa mpiga kampeni wa Mbowe katika uchaguzi wa chama, alianza chokochoko zake mapema Februari 2025 alipomwandikia barua Katibu Mkuu wa chama hicho, akidai kuwa uteuzi wa wajumbe wake na Katibu mkuu mwenyewe haikuwa halali.

Chokochoko zote hizi zinakuja wakati mwenyekiti mstaafu Mbowe akiwa kimya. Japo yeye ni mjumbe wa kamati kuu, hajawahi kushiriki kikao chochote tangu uongozi mpya ulipoingia madarakani.

Akihutubia Januari 22 baada ya uchaguzi huo, Mbowe aliutaka uongozi mpya kuponya majeraha ya uchaguzi. Ilitarajiwa kumwona pia Mbowe akivunja kambi yake ili kuusaidia uongozi mpya kutekeleza majukumu yake kwa amani, lakini kinachoonekana sasa ni baadhi ya wafuasi wake kuanza kuuchokonoa uongozi mpya.

Wakati huu ambao chama kinapambana na kampeni yake No reforms no election, makada waliokuwa wakimuunga mkono Mbowe, wanachokonoa uongozi mpya. Leo watahoji hili, kesho watahoji lile. Hizo ni hujuma kwa uongozi mpya na lawama zinaweza kumwendea Mbowe kwa sababu anao uwezo wa kuwanyamazisha.

Ukimya wa Mbowe unaweza kutafsiriwa kuwa ni kuuunga mkono chokochoko zinazoendelea ndani ya chama hicho.

Kama kweli Mbowe anakitakia mema chama chake alichokipambania kwa miaka mingi, basi ajitokeze hadharani akemee chokochoko zinazojitokeza na awaonye wanaozifanya. Awatake wafuasi wake wauunge mkono uongozi mpya na wajenge chama chao.

Ingependeza kumwona Mbowe akishiriki mikutano ya No reforms no election na hata makada waliokuwa wakimuunga mkono waunge mkono mikakati ya chama hicho na sio kusubiri mambo yaharibike, halafu walaumu.

Kwa uongozi mpya wa Tundu Lissu na Makamu wake, John Heche wasichukulie mambo kirahisi wakati huu unaoonekana kuwa mgumu kwao. Kwa sababu wanapigwa vita nje na CCM na ndani wanapigwa na kambi nyingine.

Sakata la kushambuliwa kwa Sigrada lilipaswa kumalizwa na chama haraka iwezekanavyo, sio kuwaachia CCM wajichukulie ushindi. Wangejitokeza waeleze kilichotokea na waonyeshe kusikitishwa na kisha wamhudumie kada wao, sio kumwacha tu.

Kama nilivyoeleza, hakuna vita ndogo. Vita ni vita. Jambo hili la Sigrada linaweza kuwatoa kwenye reli na kuanza kushambuliana wao kwa wao, wakati bado kuba vita kubwa mbele yao inawasubiri.
 
Narudia, Kuna mshamba flani atatema au kutemeshwa bungo muda si mrefu
 
Back
Top Bottom