Viongozi kusimamishwa kwa mabango inaashiria nini??

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,720
21,778
Jumamosi iliyopita, msafara wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ulilazimika kusimama njiani baada ya wakazi wa kijiji cha Mkunya wilayani Newala, mkoani Mtwara, kuziba njia wakiwa na mabango huku bango kubwa likimwomba asimame japo kwa dakika 10 tu ili kusikiliza kero zao.

Waziri Mkuu aliyekuwa akielekea kwenye bonde la mto Ruvuma kukagua kituo cha maji cha Mkunya, alilazimika kuteremka kutoka kwenye gari na kuwasikiliza.

Hii si mara ya kwanza kwa misafara ya viongozi kusimamishwa na wananchi wanaolalamikia kero zao za muda mrefu au hata mfupi kutoshughulikuwa.

Hivi karibuni, wakazi wanaohamishwa Kipawa kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege, nao walijaribu kuzuia msafara wa Rais Jakaya Kikwete wakitaka asikilize kilio chao kama mkuu wa nchi.

Wakazi hao, licha ya kuchelewa sana kulipwa mafao yao baada ya kuhamishwa, wanalalamikia kulipwa kwa kutumia sheria ya ardhi ya zamani badala ya ile ya sasa.

Wakati fulani, Rais Kikwete akiwa ziarani mkoani Kigoma, wananchi pia 'waliingilia' msafara wake wakiwa wamebeba madumu na wengine vibatari, wakilalamikia kero ya maji na kero ya umeme wa uhakika katika mji huo.

Sisi 'hatufagilii' tabia hii ya wananchi kuzuia misafara ya viongozi wetu ili kuwafikishia malalamiko yao.

Hatushawishi hili kwani tunaona si jambo la kistaarabu sana na ni jambo linaloingilia ratiba ya viongozi wa kitaifa wenye majukumu mengi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Na huu si utamaduni wa kawaida wa Watanzania na tusingepende ushike mizizi.

Lakini, tumekuwa tunajiuliza maswali kadhaa. Kwamba hii inatoa picha gani na kwa nini inatokea katika wakati huu ambapo kumekuwepo na madai kwamba viongozi wengi tulio nao siku hizi 'wamenunua' uongozi wao.

Tunashawishika kuamini kwamba moja ya sababu ya wananchi kulazimika kutumia nguvu kutaka kumuona kiongozi wa kitaifa, ni kushindwa kwa viongozi wa eneo husika kutatua kero zao.

Hawa ni kuanzia wale wa serikali za mitaa, madiwani, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya, mikoa, wabunge hadi mawaziri.

Kwa mfano, baadhi ya mabango ya wananchi kijiji cha Mkunya yalisomeka: “Maji (hapa kijijini) ni mradi wa wakubwa”; “Walinda chanzo cha maji hawana maji”; “Mfumo wa Stakabadhi Ghalani haufai”; “Korosho kwa mkopo ni ufisadi pia”; na “Malipo ya pili 2005 wakulima wa korosho bado hatujalipwa.”

Na hilo lilidhihirika katika risala yao, waliposema wana kero ya kutopata maji safi na salama, kutolipwa malipo ya korosho na kutopatiwa pembejeo za ruzuku.

Na waliweka wazi kwa Pinda kwamba wakati hali ndio hiyo, uongozi wa wilaya umekuwa ukiwapuuza na kuficha taarifa badala ya kuwasaidia.

Walisema kwamba tatizo la uhaba wa maji katika eneo lao limedumu kwa zaidi ya miaka 15, jambo ambalo linawafanya watumie muda mwingi kusaka maji badala ya kuutumia muda huo kwenye kilimo.

Kuhusu mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani, wakazi hao walisema hawautaki kwa sababu hawalipwi fedha zote Sh. 700 kwa kila kilo kama walivyoahidiwa.

Hebu tujiulize mimi na wewe; je, baadhi ya matatizo ya wananchi hawa kama vile kutolipwa malipo ya korosho kwa wakati, kutopatiwa pembejeo za ruzuku na maji kuonekana kuwa mradi wa wakubwa ni suala ambalo lazima limsubiri Pinda kulitatua?

Lakini akijibu hoja zao, Waziri Mkuu alisema amegundua kuna ukosefu wa maji katika vijiji 12 wakati bomba la maji kuelekea Newala mjini linaanzia kwenye vijiji vyao ambavyo ni chanzo cha maji.

Aliwaahidi wakazi hao kwamba kabla hajaondoka, atakuwa amepata ufumbuzi wa tatizo hilo.

Kuhusu mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani, Waziri Mkuu alisema hauna tatizo ila una kasoro ambazo itabidi ziangaliwe upya na kumtaka Mkuu wa Mkoa huo, Kanali (mstaafu) Anatory Tarimo, kujipanga upya na kusambaza elimu ya mfumo huo kwa wakulima.

Sisi tunaamini yote ambayo viongozi wa kitaifa wamekuwa wakilamikiwa mara kwa mara kwenye ziara zao mikoani, yanaweza kutatuliwa na viongozi wa ngazi za chini isipokuwa wengi wamekalia kujinufaisha binafsi badala ya kuwatumikia wananchi. Sambamba na semina elekezi kadhaa ambazo zimefanyika, tunawashauri viongozi wa kitaifa kuwachukulia hatua kali viongozi wa chini wanapoonekana kushindwa hata kutatua kero za wananchi ambazo ziko ndani ya uwezo wao.
 
hii maana yake ni kuwa wananchi wanapoteza subira na kuna siku watalipuka maana viongozi wanachosema sio wanachokifanya..msipande ma V8 yeye ndo wa kwanza kupanda,usivae suti nchi masikini yeye ndo wa kwanza kutwanga suti..sasa hapo maana yake nini?wanatufanya sisi watoto
 
kweli watu wanazidi kuchoka kila kukicha
ila viongozi wetu jamani loh viziwi, vipofu au??

Hawataki tu wanafikiria wananchi ni manyani kwa hiyo ni udanganyifu mtindo mmoja lakini kuna siku lazima wananchi watasema hapana.
 
Ni dalili za Wananchi kuonyeshwa kutoridhishwa kwao na utendaji wa Serikali iliyopo madarakani. Je, tutaona hali hiyo ikivipatia vyama vya upinzani "ushindi wa kishindo" 2010 au baada ya hongo ya tonge mbili za pilau, fulana za njano na kijani, kilo mbili za unga, mchele na sukari. Watanzania walio wengi wataendelea kuimba kwamba CCM ni nambari one na hivyo kuwapa ushindi kwenye majimbo mengi? Tusubiri jibu la hili hapo October 2010.
 
Watanzania wengi husahau haraka, wanaridhika pasipo sababu na hawafikirii kesho hutengenezwa na leo.
Ni aibu kubwa kwamba kila kukicha viongozi wetu wanasimamishwa katika misafara yao kuelezwa kero za maji, usafiri, jamani, what is this?
Tena si hayo tu, siku hizi wanazomewa kabisa, au watendaji kuzomewa mbele ya Rais. PM, nk. Hii ni dalili ya kuchoka na uvumilivu kupungua.
 
Back
Top Bottom