VIJANA CHADEMA TARIME NA UTUMWA NDANI YA CHADEMA
Nimesikitika kusikia taarifa ya kukamatwa kwa Diwani wa Kata ya Turwa (Tarime Mjini), huko Maswa, mkoa wa Simiyu. Kwa mujibu wa vijana wa chadema wanasema alikamatwa akiwa wakala katika kituo cha kupigia kura (sina hakika maana sijasikia statement ya jeshi la Polisi, maana sidhani kama unaweza kukamatwa tu kwa kuwa umekuwa wakala na ukapelekwa mahakamani, huenda kuna jambo wanaficha).
Jambo la kwanza la kujiuliza wananchi wa Kata yako walikuchagua kama diwani ili uwe muwakilishi wao na ushirikiane nao kutatua kero zao au uende kuwa wakala katika mikoa ya mbali? Ina maana wanachadema wa huko Maswa hawana uwezo wa kuwa mawakala? Au 2020 wakati wa uchaguzi mkuu pia vijana wa Chadema Tarime watasambazwa nchi nzima kuwa mawakala? Unaposhindwa kuwajengea uwezo wanachama wako na kuwaletea majeshi ya kukodi unategemea lini watakuwa na uwezo wa kujisimamia?
Bahati mbaya Diwani wetu huyo nimepata taarifa kakosa dhamana na karudishwa rumande hadi Disemba 7, 2017. Hali hii inasikitisha maana wapiga kura wake wanahitaji awepo Tarime kuwatumikia, zaidi ya yote hata akipata dhamana atalazimika kuwa akienda Maswa kwenye kesi, na Chadema wakishakutumikisha hata nauli ya kesi haupewi, mwisho unabaki mzigo wako na familia yako, pole sana Mh. Diwani.
KIFO CHA MARWA DOGO, BIHARAMULO 2009 KATIKA KAZI ZA CHADEMA
Mwaka 2009, katika uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Biharamulo, kama ilivyo ada vijana wa Tarime waliopelekwa kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo la Busanda walihamishiwa jimbo la Biharamulo kufanya operesheni kabla na wakati wa uchaguzi.
Vijana hawa wakipelekwa huko kazi wanazofanya ni zaidi ya siasa, wakifikishwa kule wananunuliwa ‘fimbo’ (hiyo ni code name wanayoitumia wakimaanisha “PANGA”), huelekezwa kazi za kufanya na moja wapo ni kuwashambulia wapinzani wao wakuu ili wasifanye harakati zao kwa uhuru. Hali hii imepelekea vijana hawa wengi kukamatwa na jeshi la Polisi, kupelekwa mahakamani, Chadema inawatelekeza kuwapa msaada wa kisheria na kipesa baadae wanageuka kuwa omba omba walau wapate nauli kwenda kuhudhuria kesi.
Mwaka huo, 2009 ilitokea ajali iliyohusisha gari la Mbunge wa Kawe kwa sasa, wakati huo akiwa mbunge wa viti Maalum, Mh. Halima Mdee. Ajali hiyo ilitokea wakati gari la mbunge huyo likiwa linafukuza gari lililokuwa na wafuasi wa CCM, nia yao ya kuwafukuza huenda ilikuwa ni kuwashambulia.
Gari hilo la Mh. Mdee lilipata ajali iliyopelekea kifo cha Kijana wa Tarime (Makamo ya Kati, kama miaka 40 hivi), ambaye alikuwa ni baba wa familia. Kwanza viongozi wakuu wa Chadema hawakwenda Tarime kushiriki mazishi, pili walituma salaam za rambirambi kuwa wataijengea familia ya marehemu nyumba na kumuajiri mjane wa Marwa Dogo kuwa Katibu Muhitasi katika ofisi ya Chadema – Tarime ili aweze kujikimu yeye na wanae, zaidi ya yote waliahidi kusomesha watoto wake.
Lakini baada ya msiba ule, uongozi wa chadema – Taifa haukutekeleza ahadi yake, zaidi ya yote hata pesa za BIMA ambazo alilipwa Mh. Halima Mdee hakuna pesa ambazo zilipelekwa kwenye familia ya marehemu, japo inasemekana BIMA ililipa gari pamoja na fidia kwa marehemu kwenda kwa familia yake, historia ya Marwa Dogo ikaishia hapo na hadi leo ni vijana wa Tarime na sio wa Moshi hupelekwa kama majeshi ya kukodi nyakati za chaguzi mbalimbali kwa faida ya watu wachache.
CHACHA HECHE NI KINARA WA KUWAUZA VIJANA WA TARIME AKISHIRIKIANA NA KAKA YAKE
Mwaka 2010 baada ya Mwita Waitara kumshinda John Heche kwenye kura za maoni za Chadema na hatimaye kuteuliwa kuwa mgombea Ubinge jimbo la Tarime, ili kumhujumu Waitara, Chacha Heche kwa kushirikiana na John Heche waliona bora wapige ndege wawili kwa jiwe moja.
Kwanza waondoe wale vijana wapiganaji katika uchaguzi Tarime na kuwapeleka kwingine ili Waitara akose rasilimali watu muhimu na hatimaye alishindwa uchaguzi huo. Pili waliwapeleka kwa wagombea kwa makubaliano ya ujira baada ya kazi.
Waliwasambaza vijana hao majimbo na mikoa mbalimbali, na tuhuma zipo kuwa baada ya uchaguzi katika majimbo waliyoshinda walimpa Chacha Heche mkono wa shukrani kwa vijana wale ila pesa hizo alizitumia kununua HIACE na kuanza biashara ya daladala, Tarime to Mugumu.
Mgogoro ulitokea baada ya vijana waliokwenda Hai kupata taarifa kuwa Mh. Freeman Mbowe alimpa Chacha milioni 20 na hazikufika kwao, ilitokea mtifuano hadi baadhi ya vijana hao wakaamua kuhamia CCM kwa kuchukizwa na kitendo cha kufanyishwa watumwa kwa faida ya kina Heche.
KWA NINI VIJANA WA TARIME (MARA) NA SIO WA MOSHI (KILIMANJARO)
Kauli iliyotolewa na Patrobas Katambi kuwa vijana wa Chadema ni makarai ni tafsiri sahihi kwa muktadha wa kinachoendelea ndani ya vijana wa chadema Tarime.
Jambo la kusikitisha, kushangaza na kufedhehesha ni kuwa nikiwa ndani ya chadema, hata baada ya kutoka sijawahi kuona, wala kusikia vijana kutoka mkoa wa Kilimanajro wakipelekwa katika operesheni za Chadema kufanya matendo ambayo vijana wa Tarime hupelekwa kufanya.
AJIRA ZA VIJANA WA CHADEMA, JE VIJANA WA TARIME HUFIKIRIWA?
Jibu, ni hapana. Baada ya uchaguzi wa 2010, chadema ilijivunia kura nyingi na hivyo kupata ruzuku kubwa, na ukumbuke kura hizi zilipatikana kwa juhudi kubwa na kujitoa kwa vijana wa Tarime kama sehemu ya wadau waliosambazwa majimbo mbalimbali kuipigania chadema.
Baada ya uchaguzi huo, kutokana na ongezeko kubwa la ruzuku, Chadema ilinunua magari mengi, na ajira za madereva zikatolewa. Pamoja na vijana wengi wa Chadema Tarime kuwa ni madereva na wenye leseni, hakuna hata mmoja aliyeajiriwa bali asilimia 80 hadi 90 ya vijana walioajiriwa makao makuu ya chadema kama madereva walikuwa wanatoka mkoa wa Kilimanjaro, ndio hapo unaambiwa karai kazi yake ni kutumika na baada ya kumaliza kazi hutupwa hadi wakati mwingine wa ujenzi ufike.
VIJANA WA CHADEMA NA TUHUMA ZA KULAWITIWA KALENGA-IRINGA
Mwaka 2014, baada ya kifo cha Mh. William Mgimwa, kulikuwa na uchaguzi katika jimbo la Kalenga. Kama ilivyo kawaida vijana wa Chadema Tarime walichukuliwa na kupelekwa huko kwenye uchaguzi.
Baada ya uchaguzi huo mmoja wa vijana hao alinipigia simu kuwa baada ya uchaguzi walitelekezwa na hivyo hana nauli ya kurudi Tarime, nikamueleza aje Dar es Salaam, akafika ofisini nikazungumza nae na kuhakikisha kwanza anapata nauli kurudi Tarime. Nimekuwa nikiwasaidia ndugu zangu maana najua wanatumikishwa kwa kutojitambua, kuna kijana maarufu wa chadema Tarime, baada ya kumfanyia vurugu DC Igunga katika uchaguzi, Chadema walimtoroshea Dar es Salaam na kumtelekeza ikabidi nimtafutie tiketi arudi Tarime kuungana na mkewe na wanae. Hii tabia zimekuwa zikiendelea na hawajifunzi, na hawa wote hata uchaguzi huu uliopita walipelekwa mikoa mbalimbali na taarifa ninazo.
Kijana huyo aliyetoka katika uchaguzi mdogo wa Kalenga – Iringa alinitaarifu kuwa vijana wenzake wote aliotoka nao Tarime, kwa vile hawakuwa na uenyeji wowote Iringa walijikuta wametumbukia katika mikono ya watu wasiowatambua, watu hao wakawateka, wakawapiga na kuwalawiti. Aliendelea kunihakikishia kuwa katika vijana wote aliokwenda nao Iringa kutoka Tarime, walilawitiwa kasoro yeye tu. Hizo taarifa zilinisikitisha sana na nikamuasa kwa nini wasiache kufanya kazi zisizo na faida kwao? Na kwa nini wakubali kutumikishwa bila kuangaliwa kesho yao ilihali ruzuku inatoka kubwa na wanaofaidi ni wachache?
WITO KWA VIJANA WA CHADEMA TARIME.
Kwanza wajitambue, pili wajue umri unakwenda, na asilimia kubwa ya hao wana familia, huenda mikono mitupu na kurudi mikono mitupu. Wafanye harakati huku wakitumikia akili na sio hisia za kukunjishwa ngumi pekee na kudekishwa rami, ujuha huo wapunguze. Watu wasitumie ujasiri wao vibaya na kwa maslahi yao pekee.
NB: Ukiwauliza vijana kama Waiboga ambaye aliamua kuachana na chadema atakueleza matendo ambayo wamekuwa wakitumwa kuyafanya na viongozi wa Chadema bila kuangalia usalama wao.