Vigogo wa siasa, dini njia panda | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Vigogo wa siasa, dini njia panda

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Jun 7, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Jun 7, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Waandishi Wetu

  Toleo la 242
  6 Jun 2012


  • Zanzibar yawatatiza, bajeti kuu ya Serikali mtego mwingine
  • Mawaziri kukiona cha moto bungeni wakiwasilisha bajeti
  • Mpambano kati ya CHADEMA, NCCR na CCM wafunika kombe


  HALI ya kisiasa na kiutawala imeendelea kuwa tete nchini kutokana na matukio mbalimbali na uamuzi wa viongozi wakuu kuhusu namna ya kupata suluhu ya matukio hayo ambayo baadhi ni hatari kwa amani ya nchi.

  Kwa baadhi ya matukio na hasa vurugu za hivi karibuni visiwani Zanzibar zilizohusisha uchomaji wa makanisa na baadhi ya vitega uchumi vya watu binafsi, unasubiriwa mwongozo wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

  Mwongozo huo unasubiriwa ili kupimwa na wananchi pamoja na viongozi wa dini ili kujiridhisha kama utaibua suluhu ya matukio hayo kujitokeza tena.


  Lakini wakati mwongozo huo ukisubiriwa, kwa upande mwingine, hatua ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumkamata na kumfungulia mashitaka Mbunge wa Bahi, mkoani Dodoma, Omar Badwel wiki hii, l imewasilisha ujumbe tofauti miongoni mwa wabunge na viongozi wengine wa kitaifa.


  Kuna hali ya wasiwasi miongoni mwa viongozi hao, hasa wale ambao wamekwishakuwahi kuhojiwa na maofisa wa TAKUKURU kuhusu baadhi ya taarifa zinazowahusisha katika vitendo vya rushwa.


  Kama vile ni mwendelezo wa hali ya sintofahamu, mawaziri takriban wapya nao wanakabiliwa na mtihani mzito wa kutetea bajeti zao ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikielezwa kuwa, kutokana na udhaifu sugu katika wizara hizo, mawaziri hao bila kujali kuwa ni wapya, watakumbana na mazingira magumu pindi bajeti za wizara wanazoongoza zitakapokuwa zikijadiliwa bungeni.


  Hali ya Zanzibar

  Hadi sasa, mijadala mizito inaripotiwa kuendelea miongoni mwa viongozi wa dini licha viongozi hao kwa upande wa kikristo, kupitia kwa Askofu Valentino Mokiwa, kuweka msimamo unaoweka bayana kuwa waumini wao visiwani Zanzibar wamekuwa ‘wakitazamwa' kama raia wa daraja la pili.

  Kwa upande mwingine, baadhi ya viongozi wa kiislamu wakionyesha msimamo wa kutounga mkono hali ya kukosekana kwa uvumilivu wa kidini miongoni mwa raia wa nchi moja.


  Taarifa zilizotufikia zinaeleza kuwa viongozi hao wa dini kwa njia zao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu hatua za uchunguzi unaoendelea kuhusu matukio hayo ya vurugu Zanzibar.


  "Tunafuatilia kwa karibu hali ya Zanzibar na ufumbuzi unaotarajiwa kutolewa kwa upande wa Serikali. Nasi tunazo namna zetu za kujiridhisha pia, kwa hiyo tutafanya ulinganisho kati ya kile tutakachokibaini na kile kitakachowekwa bayana na Serikali. Lakini kwa kweli hatukuridhishwa na usimamizi wa Katiba ya nchi," alieleza mmoja wa viongozi wa dini aliyezungumza na mwandishi wetu kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini.


  Mawaziri mapya na mtihani wa kwanza

  Taarifa kutoka duru za Bunge zinaeleza kuwa mawaziri wapya takriban 10 wapo katika mtihani mzito kuhusu utetezi wa bajeti za wizara zao. Kama vile imepangwa au la, karibu mawaziri wote hao ni wasomi wa kiwango cha shahada ya uzamivu (PhD).

  Mawaziri hao ni Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, ambaye anacho kibarua cha kutetea bajeti ya Taifa bungeni, Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harisson Mwakyembe na Waziri wa Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa.


  Wengine ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Afya, Dk. Hussein Mwinyi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Profesa Mbarawa Mnyaa.


  Kwa upande mwingine, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia na Waziri wa Utumishi, Celina Kombani nao hawako salama dhidi ya mashambulizi ya hoja kutoka kwa wabunge.


  Kutokana na bajeti ya mwaka ujao wa fedha kujikita zaidi katika vipaumbele vya miundombinu ambavyo vimechanganuliwa kuwa ni reli, viwanja vya ndege na umeme, hoja za wabunge watakaosuguana na mawaziri hao zinatarajiwa kujikita zaidi kuhusu udhaifu wa kiutendaji katika wizara zao sambamba na udhaifu katika wakala zilizoko chini ya wizara hizo.


  Waziri wa Uchukuzi, Dk. Mwekyembe anatarajiwa kuwa na kibarua kigumu kitakachomsukuma kuamua kukiri udhaifu wa baadhi ya watendaji au kuutetea. Lakini hata hivyo, tayari Mwakyembe amekwishanukuliwa na gazeti hili akitoa maelezo yanayoonyesha kutokuwa tayari kuvumilia watendaji wanaonekana kuwa chanzo cha wizara hiyo kuzorota.


  Naye Profesa Muhongo wa Nishati na Madini, akisaidiwa na naibu mawaziri wake, George Simbachawene na Steven Masele, anakabiliwa na kibarua kizito na hasa kwa kuzingatia ahadi lukuki za miradi ya umeme ambazo nyingi bado hazijatekelezwa.


  Waziri wa Utalii, Balozi Kagasheki bado kivuli cha ulinzi dhaifu wa rasimali za taifa kitamwandama ndani ya Bunge kama ilivyo kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Kigoda ambaye baadhi ya wakala zilizoko chini ya wizara hiyo viongozi wake wako kwenye utata kiutendaji akiwamo Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).


  Profesa Tibaijuka wa Wizara ya Ardhi bado anazongwa na makosa yanayoendelea kufanywa na baadhi ya maofisa walioko chini ya Wizara hiyo kama ilivyo kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi ambaye amerudi kwenye wizara hiyo akikutana na mgogoro ulioahirishwa kwa muda unaohusisha madaktari na baadhi ya watendaji wa wizara yake.


  Yanayotarajiwa katika bajeti ijayo

  Miongoni mwa masuala yanayotarajiwa kufanyiwa kazi katika bajeti ijayo ni pamoja na Serikali kuainisha mikakati ya kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa na huduma muhimu nchini.

  Kuendelea kuweka mikakati ya kudhibiti biashara ya uuzaji na usambazaji wa nishati ya mafuta, kurekebisha mgawanyo katika bajeti za sekta muhimu kama elimu, afya, kilimo na miundombinu.


  Kinga ya vigogo wala rushwa

  Tukio la kukamatwa na kufunguliwa mashitaka kwa Mbunge wa Bahi, Omar Baduwel limepeleka ujumbe mwingine mpya kwa wabunge kuwa hawako salama, na hususan wale ambao wamekuwa wakijihusisha na uombaji rushwa.

  Kwa muda mrefu sasa kumekuwapo na malalamiko yanayowahusu wabunge kuomba rushwa katika matukio mbalimbali. Miongoni mwa matukio ambayo yamehusishwa na wabunge kuomba rushwa ni pamoja na uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki, uliofanyika katika mkutano uliopita wa Bunge, mjini Dodoma.


  Mbali na tukio hilo, matukio mengine yanayotajwa kuhusisha baadhi ya wabunge kuomba rushwa ni pamoja na wakati wa kutungwa kwa sheria inayohusu uwindaji wa wanyapori na sheria nyingine mbalimbali zinazoelekea kuathiri maslahi fulani ya kibiashara kwa wafanyabiashara zinazohusu baadhi ya sekta muhimu nchini.


  Hali ndani ya vyama vya siasa

  Wakati hali ikiwa hiyo katika baadhi ya maeneo ya kiutawala, ndani ya vyama vya siasa na hususan vyama mashuhuri nchini si ya kuridhisha, hofu ya kuzidiana ujanja wa kisiasa miongoni mwa makundi ikijitokeza.

  Tofauti na mazoea ya muda mrefu kwamba hali ya kuviziana kisiasa imekuwa ni utamaduni ndani ya CCM, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nako kuna hali ya kuviziana kisiasa, na miongoni mwa wanaoviziwa ili kudhibitiwa au kufukuzwa ni pamoja na Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda na baadhi ya madiwani wa chama hicho jijini Mwanza.


  Hata hivyo, wakati hali ya kisiasa ndani ya CCM na CHADEMA ikiwa hivyo kama ilivyo katika vyama vya CUF (uongozi dhidi ya Mbunge wa Wawi, Rashid Mohamed) na NCCR-Mageuzi (uongozi dhidi ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila), vyama hivyo kwa ujumla wake vimekuwa vikijitokeza ‘kupambana' katika jukwaa la kisiasa nje ya siasa za vyama.


  Katika siasa nje ya vyama hivyo, kumekuwa na hali ya mkwaruzano kati ya vyama vya upinzani. Katika mvutano huo, baadhi ya viongozi wa CHADEMA wamekuwa wakivichafua kisiasa vyama vya NCCR na CUF kuwa ni mawakala wa CCM kutokana na sababu mbalimbali ambazo kati yake, nyingine zinahusisha uamuzi wa wananchi kama Katiba ya Zanzibar kuridhia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kumpa nafasi Rais wa Tanzania kuteua wabunge 10 kuingia katika Bunge la Jamhuri.   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Jun 7, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Lakini hii itasaidia kuteua watu wenye Akili, hekima wa kuweza kumudu masuala yote ya Nchi; kuliko kuteuliana kiurafiki na kuwa waziri na kupumzika.
   
Loading...