Vigogo Deci wasota polisi, Mtikila awatetea | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Vigogo Deci wasota polisi, Mtikila awatetea

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Pdidy, Apr 18, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Apr 18, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,572
  Likes Received: 5,761
  Trophy Points: 280
  Vigogo Deci wasota polisi, Mtikila awatetea

  Na Waandishi Wetu

  SAKATA la Taasisi ya Development Entrepreneurship Community Initiative (Deci), sasa liko rasmi mikononi mwa vyombo vya dola baada ya watendaji wakuu, akiwemo mkurugenzi mtendaji, Timothy Loitinye, kuhojiwa na polisi kwa siku mbili mfululizo.


  Taasisi hiyo imesimamisha shughuli zake baada ya kutokea utata kutokana na kauli za Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Benki Kuu (BoT), kutahadharisha wananchi kuwekeza fedha zao kwenye mchezo wa kupanda na kuvuna mbegu, kwa maelezo kuwa utaumiza washiriki baadaye.


  Pia Deci wametakiwa kurudisha fedha za washiriki wapya baada ya kikao baina ya viongozi wake kukutana na timu ya maofisa waandamizi kutoka taasisi mbalimbali za serikali.


  Timu hiyo, ambayo iko chini ya Gavana wa BoT, Prof. Beno Ndulu, inaundwa na maofisa kutoka Kurugenzi ya Upelelezi ya Makosa ya Jinai (CID), Usalama wa Taifa, Kitengo cha Intelejensia ya Fedha Chafu (Financial Intelligency Unit-FIU) na BoT.


  Habari za kuaminika kutoka makao makuu ya polisi zinasema kuwa vigogo hao, wakiongozwa na Loitinye, walianza kuhojiwa juzi na mahojiano yaliendelea jana yakilenga kujua kazi na za taasisi hiyo.


  Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba aliiambia Mwananchi kuwa, kazi hiyo imefanywa na jopo maalumu lilioundwa kuichunguza Deci, akisema linaongozwa na Prof. Ndulu.


  "Watu ambao waliwahoji ni timu maalumu... nafikiri wao wana nafasi nzuri kuzungumzia hilo. Timu iko chini ya gavana," alisema DCI Manumba.


  Hata hivyo, juhudi za kumpata Gavana Ndulu hazikuweza kufanikiwa baada ya kuelezwa kuwa katika mkutano nyeti.


  Wakati DCI akiweka bayana hilo, habari zinasema kuwa miongoni mwa mambo ambayo vigogo hao wameulizwa ni uhalali wa kazi yao na kutaka ufafanuzi wa chanzo cha mtaji wao, wadau wakuu na mchezo huo wa kupanda na kuvuna, ambao umeelezwa kuwa ni Upatu.


  Katika mchezo huo, washiriki hutakiwa kuwekeza kati ya Sh10,000 na baada ya wiki sita hadi 20 huvuna mara mbili ya kiasi walichopanda. Haijulikani taasisi hiyo huwekeza fedha wapi ili zizalishe faida ambayo hulipwa wanachama kwa maelezo kuwa wanavuna walichopanda.


  Wasiwasi huo wa Deci kutowekeza fedha sehemu ambayo inaweza kuzalisha faida, ndio imefanya ulinganishwe na Upatu, ambao kawaida watu wengi huchangia wachache wanaowahi kabla ya mchezo kufa ghafla.  Katika hatua nyingine, mwenyekiti wa DP, Mch. Christopher Mtikila ameonya kwamba endapo Deci itafungwa, itakuwa ni dhuluma kwa walala hoi ambao ndio wamepanda mbegu kwenye taasisi hiyo.


  Mtikila, ambaye ni mwanasiasa machachari nchini, alisema tangu taasisi hiyo ianze kufanya shughuli zake hapa nchini imewakomboa wananchi wengi kiuchumi na kusisitiza kuwa hakuna aliyewahi kulalamika kuibiwa.


  “Watu wakidhulumiwa ni pigo kubwa sana kwani wengi wao wamepata pesa zao kwa shida na kila mbegu iliyoenda kupandwa Deci imefanyiwa kazi,” alisema Mtikila.


  Mchungaji huyo alisema yeye hajapanda mbegu Deci, lakini ataendelea kuitetea kwa madai kuwa haijavunja sheria na imekuwa ikilipa kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


  Alisema Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipaswa kuwapongeza Deci kwani wamewawezesha watu kujikomboa kiuchumi na kwamba waendeshaji walipata maono ya Mungu.


  Tangu kutokea kwa mkanganyiko juu ya mchezo wa kupanda na kuvuna, Deci imetangaza kupata hasara ya Sh11 bilioni ambazo imesema ni mbegu za wanachama.


  Wakati Deci ikisuasua, washiriki wa mchezo wa kupanda mbegu wanaonekana kusaka taasisi nyingine kuwekeza fedha zao ili wapate faida mara mbili.


  Mwananchi jana lilifika katika taasisi ya Tumaini Revolving Fund (TRFI) iliyo Tabata jijini Dar es Saam na kushuhudia wakazi mbalimbali wakiomba kupewa maelezo ya jinsi ya kujiunga na taasisi hiyo huku wengine wakivuna fedha zao.


  Kwa mujibu wa masharti ya taasisi hiyo mshiriki anayetaka kujiunga anatakiwa kuweka fedha kwenye akaunti iliyo benki ya Dar es Salaam Community (DCB).


  “Mimi ndio nimekuja kujiunga nataka kupata maelekezo tu maana huko Deci hata hakufai. Serikali imewavalia njuga viongozi wetu mpaka wamesitisha huduma,” alisema mmoja wa watu aliyekuwa kwenye ofisi hizo.


  “Lakini walichokifanya wala sio suluhisho kwani tutazidi kupanda na kuvuna. Hapa nimesikia mpaka mikopo wanatoa tena kwenye vikundi... unaona sasa Mungu anatupenda; inakufa Deci, tunaibukia sehemu nyingine,” alisema mtu mwingine aliyefika katika taasisi ya TRFI.


  Mmoja wa wafanyakazi waliokuwa wakielekeza watu jinsi ya kujiunga na taasisi hiyo, akiwatahadharisha kutoihusisha taasisi hiyo ya

  TRFI na Deci kwa madai kuwa ni vitu viwili tofauti.


  “Hii ni tofauti sana na Deci naomba msiifananishe kabisa. Masharti yetu ni kwamba kila mwanachama anayetaka mkopo anatakiwa kuwa katika kikundi cha watu watano hadi 50. Tunawahimiza wanachama wapya kufika ofisini na kupewa maelekezo kabla ya kuweka fedha kwenye akaunti ya DCB,” alisema akielekeza wanachama hao watarajiwa.


  "Kwa awamu ya kwanza hadi ya tatu, mwanachama atachukua wezesho tu, lakini awamu ya nne mwanachama atachukua mbegu yake na ongezeko la asilimia 15 tu, baada ya kumaliza awamu ya nne ya mzunguko wa kwanza mwanachama anaweza kuanza mzunguko mwingine kwa kiingilio pungufu cha asilimia 20.


  "Mwanachama anayejiunga atalipa kiingilio kutegemeana na kianzio anachotaka kuweka."


  Kwa mujibu wa masharti ya taasisi hiyo ya mikopo midogo iliyosajiliwa kwa ajili ya kusaidia wale wenye kipato kidogo kama ilivyo Deci kianzio chake ni Sh10,000 na kiingilio kinaanzia Sh5,000. Wezesho linaanzia Sh4,400 kwa miezi miwili na Sh6,600 kwa miezi mitatu.


  Mmoja wa wanachama waliofika katika kituo hicho ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa yeye alianza kuweka fedha katika taasisi hiyo siku nyingi na kufafanua kuwa, mpaka hivi sasa ameshafaidika vya kutosha, hivyo hata ikifungwa hatakuwa na hasara kama wale wanaojiunga hivi sasa.


  Mwananchi mwingine alisema amewekeza fedha zake Deci, TRFI na taasisi nyingine aliyoitaja kwa jina la Malingumu Investment aliyodai ipo maeneo ya Kitunda Jijini Dar es Salaam.


  “Mimi hapa nimeanza kuja baada ya kuanza kuona Deci mambo hayaendi vizuri, kule Malingumu nimeanza kama miezi miwili iliyopita, na kule tunavuna bwana sio kama hapa,” alisema mwananchi huyo akionyesha baadhi ya fomu za Malingumu.


  Fomu hizo zinaonyesha kuwa mwanachama anaanza kupanda Sh 20,000 hadi 1,000,000 na kuvuna fedha mara moja na nusu ya fedha aliyoipanda katika kipindi cha wiki nne mpaka 12.


  Katika ofisi za makao makuu ya Deci zilizo Mabibo kulikuwa na makundi ya wanachama walioonekana kutoamini kuwa ofisi hizo zimefungwa, lakini wakaondolewa na ofisa mmoja mwandamizi wa polisi aliyewataka watawanyike.


  Kutoka Tanga, Burhan Yakub anaripoti kuwa washiriki wa Deci wanatarajia kukutana leo kutangaza msimamo wao kuhusu kusimamishwa kwa shughuli za taasisi hiyo mkoani hapa.


  Wanachama hao walifika jana kwenye ofisi za Deci zilizo Mabanda ya Papa na kukuta tangazo hilo la kusitishwa wa huduma ya kupanda na kuvuna na baada ya majadiliano walibandika bango lao la kuwataka wanachama wenzao kufika mapema leo asubuhi ili kutangaza msimamo wao.


  Taarifa hii imeandaliwa na Ramadhan Semtawa, Nora Damian, Fidelis Butahe na Aziza Athuman.
   
 2. Msanii

  Msanii JF-Expert Member

  #2
  Apr 20, 2009
  Joined: Jul 4, 2007
  Messages: 6,427
  Likes Received: 370
  Trophy Points: 180
  Hapo nilipobold hakika sijamuelewa huyu mchunga kondoo wa Bwana.
  Hakuwastua wanakondoo wake kwamba wanachezea sharubu za SIMBA? huu ni umbumbumbu mwingine ambao unapaswa kurekebishwa ktk JAMII
   
 3. Kang

  Kang JF-Expert Member

  #3
  Apr 20, 2009
  Joined: Jun 24, 2008
  Messages: 5,122
  Likes Received: 617
  Trophy Points: 280
  Nadhani anatafuta umaarufu tu, hakujua lolote!
   
Loading...