Vifaa bandia: Changamoto mpya ya umeme wa jua | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Vifaa bandia: Changamoto mpya ya umeme wa jua

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Aug 26, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Aug 26, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,617
  Trophy Points: 280

  ASILIMIA 12 tu ya Watanzania ndiyo waliounganishwa na nishati ya umeme kutoka katika mfumo wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

  Karibu asilimia 90 ya wananchi hawatumii umeme kwa sababu mfumo wa umeme wa Tanesco ama haujafika kwenye maeneo yao au hawana uwezo wa kumudu gharama za kuunganisha nishati hiyo pamoja na gharama za uendeshaji.

  Moja ya vipimo vya maendeleo katika nchi yoyote duniani hutokana na namna idadi kuwa ya wananchi wake wanavyotumia nishati ya umeme. Bei kubwa ya kuunganisha umeme, pamoja na gharama kubwa za matumizi ni kikwazo cha kuipata huduma hiyo.

  Matokeo yake, watu wasiokuwa na umeme wanatumia koroboi, mishumaa na kandili. Matumizi ya mishumaa na koroboi yanaongeza uwezekano wa ajali za moto ambazo zinasababisha vifo vya watu wengi, upotevu wa mali kama ilivyowahi kutokea katika Shule ya Sekondari Idodi, Iringa.

  Upatikanaji wa nishati ya umeme katika maeneo hasa ya vijijini ni moja ya changamoto zilizopo nchini hasa katika sekta za afya na elimu. Vituo vya huduma za afya vinahitaji umeme kwa ajili ya kutunza dawa na mwanga kwa huduma bora.

  Upatikanaji wa mwanga bora unainua kiwango cha huduma za kina mama kujifungua salama. Kupatikana kwa umeme vijijini kutainua kiwango cha huduma za afya huku gharama zikibaki chini.

  Vituo vya elimu, hasa shule za sekondari, vinahitaji umeme kwa ajili ya mwanga kuwezesha usomaji wa usiku, matumizi ya kompyuta kwa ajili ya ofisi na mtandao wa intenet.

  Wanafunzi katika maeneo yasiyo na umeme hujisomea kwa kutumia vibatali, mishumaa na taa za mafuta ambazo hutoa mwanga hafifu huku vikitoa moshi ambao ni hatari kwa afya pamoja na kusababisha ajali za moto.

  Katibu Mtendaji wa Chama cha Nishati Jadidifu Tanzania (Tarea), Mhandisi Mathew Matimbwi anatoa wito kwa wamiliki wa shule za bweni zisizo na nishati kutoka katika mfumo Tanesco kutumia umeme wa jua ili kukabiliana na matatizo ambayo hujitokeza.

  Kuendelea kutumia mishumaa na koroboi nyakati za usiku kwa ajili ya kujisomea kunakaribisha maafa ambayo yanaweza kuzuilika. Anasema taifa limeshuhudia wanafunzi wakiteketea kwa moto kutokana na matumizi ya vibatari na mishumaa.

  "Maelfu ya wanafunzi wanaojisomea hawana jinsi ya kupata mwanga zaidi ya kutumia koroboi na mishumaa, matokeo yake kosa dogo tu linaweza kusababisha ajali ya moto," anasema.

  Katibu anasema matumizi ya umeme wa jua ni muafaka kwenye maeneo hayo kwa vile hauna madhara kwa wanafunzi wanaojisomea na gharama za uendeshaji ni nafuu.

  Mabwana mipango katika sekta za afya na elimu hawana budi kuingiza mipango ya kufunga mitambo ya umeme wa jua ili kuendeleza vituo vya afya na elimu. Anasema Tarea iko tayari kutoa ushauri wa bure kwa ajili ya uendelezaji wa mitambo ya umeme wa jua.

  Wakati wananchi wakielekezwa kuitumia nishati hiyo, huko pia wanakutana na changamoto nyingi hasa kuwepo kwa vifaa bandia vya umeme wa jua.

  Wakati wananchi wakipewa hamasa ya matumizi ya umeme wa jua, 'kuna wingu zito limetanda' vifaa feki vya umeme wa jua vilivyofurika kwenye soko. Ukifika kwenye maduka, hasa yale yaliyopo Kariakoo Dar es Salaam kuna utitiri wa bidhaa hizo sizizokidhi viwango na nyingine bandia.

  Mwenyekiti wa Tarea, Dk Cuthbert Kimambo anasema kuwepo kwa vifaa feki vya matumizi ya umeme wa jua katika soko ni moja ya changamoto zinazokikabili chama hicho.

  Anasema baadhi ya wananchi wanaokwenda kununua vifaa hivyo hujikuta wakiuziwa vifaa bandia jambo linalowakatisha tamaa ya kuendelea kuipenda nishati hiyo.

  Anasema ili kukabiliana na tatizo hilo, wanashirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kubaini vifaa ambavyo havina ubora.

  Source: Vifaa bandia: Changamoto mpya ya umeme wa jua
   
Loading...