Katika hali inayoonyesha kuwa na majibizano kati ya Rais Magufuli na Kituo Cha Haki za Binadamu LHRC kinachoongozwa na Dr. Hellen Kijo Bisimba, leo Rais Magufuli hadharani kasema wanaosema amekiuka haki za binadamu kumsimamisha ndugu Kabwe hadharani walitakiwa pia waseme vivyo hivyo kipindi anamuapisha hadharani kwa kuwa ni mteule wake.
Hivyo, ni vyema wakaiacha serikali ikafanya kazi yake, na ikiwezekana itabidi awachunguze credibility yao kama wanatetea mambo maovu.
=================
Magazeti hivi ndivyo yalivyoandika;
====================
Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana aliamua kuwatolea uvivu wadau waliopinga kitendo chake cha kutumia hadhara kumsimamisha kazi mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe.
Rais alimsimamisha kazi Kabwe baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumchongea mtendaji huyo wa jiji kuwa alisaini mikataba miwili ya huduma za usafiri na kusababisha jiji lipoteze mabilioni ya fedha.
Baada ya kusikilia maelezo hayo ya Makonda, Rais Magufuli aliuliza wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa Daraja la Mwalimu Nyerere kuwa achukue uamuzi gani na kujibiwa ‘mtumbue’, na hapo hapo akatangaza kumsimamisha kazi kwa uchunguzi.
Kitendo hicho kimepingwa na wadau mbalimbali wa haki za binadamu na utawala bora, ambao waliiambia Mwananchi juzi kuwa Rais alitakiwa kwanza kupokea taarifa hiyo na kufanya uchunguzi ambao ungempa Kabwe haki yake ya msingi ya kusikilizwa kabla ya kusimamishwa kwa tamko la hadharani.
Jana, akiongea na viongozi wa ngazi tofauti wa CCM katika hafla ya kuwashukuru kwa kazi waliyoonyesha wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, Rais Magufuli alisema kama watu anaowatumbua hadharani pia waliiba hadharani, ni lazima watumbuliwe hadharani.
Magufuli alisema katika mkanda wa video uliosambazwa jana kuwa mateso waliyopata mamilioni ya Watanzania kutokana na kuibiwa, yanafanywa na hao wachache lazima nao waanze kupata mateso hayohayo.
“Kwa hiyo ziko haki za binadamu kwa matajiri tu kwa hawa walioibiwa hakuna haki,” aliuliza Rais Magufuli.
“Kwa hiyo unaweza kuona hawa wanaowatetea nao ni majipu. Tutaanza kuwafuatilia. Hata ukimtoa huyo, nikimsema hadharani wanasema eti nimefanya kosa.”
Rais Magufuli alisema kwa bahati nzuri aliwateua yeye na kuwatangaza hadharani, hivyo akahoji sababu za kutotangazwa hadharani siku ya kutenguliwa kwa kuwa ndiyo saizi yake aliyewateua.
“Kama ni mkurugenzi wa manispaa au wa wapi nimemteua mimi. Eti wanasema apewe muda wa kujieleza. Ajieleze yeye aliwapa muda wananchi kujieleza alipokuwa anawaibia? Napenda niwahakikishie tutaendelea kusimama imara,” alisema Dk Magufuli.
Rais na mawaziri wake wamekuwa na mtindo wa kusimamisha kazi au kutengua uteuzi wa watumishi wa umma hadharani wakati wa shughuli mbalimbali, wakitangulia kutoa mlolongo wa tuhuma dhidi yao na baadaye kuagiza uchunguzi ufanyike.
Awali jana, msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka alitoa taarifa kwamba Rais amewataka viongozi wa chama hicho kuisimamia Serikali ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano yanafikiwa kwa wakati muafaka.
Viongozi hao ni wenyeviti wa mikoa na wilaya na makatibu wa mikoa na wilaya.
Taarifa hiyo ya Ole Sendeka ilisema kuwa Magufuli aliahidi kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kupambana na kila aina ya maovu, kurejesha nidhamu na uwajibikaji serikalini na kuhakikisha kuwa mapato na rasilimali za Taifa zinatumika kwa maslahi ya Watanzania.
Kwa mujibu wa Ole Sendeka, viongozi hao wameeleza kuridhishwa na kasi na umakini wa Serikali yake kurejesha nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Pia kupunguza matumizi, kuongeza kasi ya kutoa huduma na kusimamia shughuli za maendeleo ya wananchi kwa lengo la kutekeleza Ilani ya CCM.
Viongozi hao kwa mujibu wa taarifa ya Ole Sendeka wameahidi kuendelea kumuunga mkono Rais na Serikali yake ili kuhakikisha anatekeleza majukumu yake bila kikwazo.
Chanzo: Mwananchi