Ochu
Platinum Member
- May 13, 2008
- 976
- 50
Vibaka wamkata mapanga ofisa usalama wa taifa
Na Daniel Mjema,Moshi
VIBAKA wanazidi kuutikisa mji wa Moshi na safari hii wamevamia nyumbani kwa mkuu wa idara nyeti ya Usalama wa Taifa mkoani Kilimanjaro na kupora mali zake kabla ya kumjeruhi kwa panga mkono wake wa kulia.
Tukio hilo, ambalo limefanywa siri kubwa, limekuja miezi michache baada ya kamanda wa polisi wa wilaya ya Moshi, Mrakibu Mwandamizi Majjid Kibwana kuvamiwa na vibaka na kujeruhiwa kwa mapanga.
Mbali na uvamizi huo kwenye nyumba za wafanyakazi wa vyombo hivyo vya dola, mwaka jana kundi la vibaka lilivamia nyumbani kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi, Lawrence Mchome eneo la Shanty Town na kupora vitu mbalimbali.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Lucas Nghoboko alisema hajapata taarifa za tukio hilo na kuahidi kulifuatilia na kutoa taarifa rasmi baadaye.
Hata hivyo, habari za uhakika zilizopatikana jana na kuthibitishwa na polisi na baadhi ya viongozi wa serikali zilidai tukio hilo, ambalo limekuwa gumzo, lilitokea usiku wa kuamkia juzi kwenye eneo hilo la Shanty Town.
Eneo hilo ndilo ambalo wanaishi vigogo wa serikali na taasisi zake, akiwemo mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Mohamed Babu na ndilo ambalo sasa linaongoza kwa kuwa na vibaka wengi wanaotembea kwa makundi.
Habari hizo zimedai kuwa ofisa huyo alikurupushwa usingizini baada ya kuhisi mtu anafungua mlango na alipokwenda kuangalia akiamini ni mtumishi wake wa ndani ndipo alipokumbana na kizaazaa hicho.
Alipotoka aliamini ni mfanyakazi wake na alipouliza anataka nini usiku huo, ndipo akajibiwa na kundi la vibaka hao kuwa wao ni majambazi, alisema mtu aliye ndani ya Jeshi la Polisi.
Baada ya kutoa kauli hiyo, vibaka hao waliendelea na kasi ya kuvunja mlango huo na ofisa huyo alijitahidi kuwazuia, lakini bila mafanikio na ndipo walipofanikiwa kuingia na kupora runinga na mashine ya santuri aina ya DVD na baadaye kumjeruhi mkono.
Polisi walifika muda mfupi baadaye na kukagua eneo la tukio. Taarifa zinasema kuwa baadaye walianza msako mkali wa kusaka wahalifu hao, lakini hadi jana hakuna mtu aliyekamatwa.
Tukio hilo limekuwa gumzo mjini hapa huku likizua hisia tofauti na wananchi wakisema kuwa, kama vibaka wanaweza kuvamia maeneo nyeti na kuwajeruhi viongozi wenye ulinzi, basi hali si shwari mkoani Kilimanjaro.
Katika kipindi cha mwezi mmoja sasa kumekuwa na matukio mfululizo ya uhalifu, likiwemo tukio la wiki iliyopita wakati vibaka walipomvamia mlinzi wa duka la kubadilisha fedha la Chase Forex na kumjeruhi vibaya kwa mapanga.
Lakini mbali na vibaka kufanya wanavyotaka katika kipindi cha mwezi mmoja, wimbi la wizi wa magari ambayo baadaye hufumiliwa na kuuzwa kama vipuri vilivyotumika limepamba moto na tayari magari manne yameibwa.
Tofauti na matukio mengi ya vibaka kuvamia nyumba za vigogo bila hofu, SSP Kibwana alivamiwa eneo la Barabara Kuu ya Moshi-Dar eneo la Majengo karibu na mzunguko wa magari wa YMCA wakati akiwa doria.
tuko salama kweli...polisi wawajibike