UZALENDO NA AMANI
Naunga mkono hoja kwa kadri ulivyoijadili ingawa nitaongeza mtizamo wangu kwa kadri ya uelewa.
Kwanza ni kutambua kwamba hili ni suala muhimu sana na la msingi sana kwenye jamii iliyostaarabika na kuendelea.
Tunapozaliwa mara nyingi vichwa vyetu huwa wazi(vacuum) bila maarifa yoyote, hii ni kwa mujibu wa wanasaikolojia ya makuzi). Baada ya hapo mtoto huanza kujazwa maarifa kulingana na wale au yale yaliyomzunguka naye huwa mwanafunzi mwaminifu na baadaye kuja kuwa mwalimu.
Hivyo, msingi wa kwanza wa yote ni maarifa tunayopata wakati tukiwa wadogo na yale tunayoyaona. Maarifa haya ndo huja kuza msingi wa utambuzi wetu wote. Kujua thamani jema na baya na kiasi chake.
Samaki mkunje angali mbichi.
Kwa sababu hiyo, chachu muhimu ya uzalendo inaanza kwenye familia au jamaa waishio pamoja ikijumuisha makuzi yao kwa kila mmoja(mwanajumuiya).
Kujitambua:
Kutambua ubinadamu wako na mahitaji yako(wewe ni nani na unahitaji nini na vitatoka wapi)ni suala muhimu pia. Kama tunavyofahamu ukamilifu wa ubinadamu hautokani maarifa au mali, bali mahusiano na wengine wanaomzunguka. Hivyo, kujifunza thamani ya mahusiano mema ni kitu cha msingi ndani ya jamii yako ya awali. Tambua thamani ya unachopata toka kwenye mazingira na watu wanaokuzunguka. Huwezi kutoa chochote kwa mwenzako au kuwa tayari kutoa chochote bila kujua umuhimu wake kwa kuanzia kwako mwenyewe.
Kumtambua wenzako:
Kuwatambua binadamu mwezako na mahitaji yao. Baada ya safari ya kujitambua, safari inayofuata ni namna gani utamtambua binadamu mwenzako bila mipaka yoyote mfano: mrefu, mfupi, mweupe, aliye au asiye na mali nk. Pia kutambua mahitaji yake ya msingi na kujua kuwa mahitaji mengine yanatoka kwenye himaya yako. Utakapotambua kuwa hitaji la binadamu mwenzako ndilo lako basi kinachofuata ni kujengewa imani/ moyo wa kuthamini binadamu mwenzio. Hapo, utampa thamani linganifu na wewe kulingana na nafasi uliyopata kwenye makuzi yako.
Binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja.
Kujiweka tayari unapohitajika.
Baada ya safari mbili hapo juu, safari inayofuata ni kuuweka tayari moyo wako na akili kujitoa kwa hali na mali wakati wa hitaji na pasipokuwa na hutaji. Kwani mzalendo hasubiri kuhimizwa. Hata pale adui atakapofanikiwa kujipenyeza sehemu yoyote basi atakutana na nguvu ya uzalendo na kujitoa ambayo itampa wakati mgumu kutimiza azma yake.
Tukumbuke hata wakoloni walipokuja na siraha zao za kisasa, sehemu walizokuta umoja na uzalendo basi walipata shida kubwa kutawala. Hivyo, kuwa na idadi kubwa ya watu wenye mioyo ya uzalendo ni nafasi kubwa ya maendeleo na amani kwa taifa. Kama wakiws wachache kulingana na jamii au kizazi mara myingi watashindwa au kuangamizwa.
Umoja ni nguvu
Safari hizo hapo juu zaweza kwenda kwa pamoja ndani ya makuzi mtu. Zimewekwa kwa mafungu ili kuweza kuzieleza vyema.
Kwa msingi huo kaya zetu, jamii zetu, taasisi zetu zitakuwa zimejengwa na misingi ya uzalendo madhubuti. Uzalendo utasukuma kutokuwa tayari kuona haki ya binadamu mmoja inapotea au haki ya jamii au taifa.
Kwa msingi huo pia mnyororo huu uliofungwa ndani ya jamii zetu(uzalendo) utakuwa ndio ngome imara itakayomshinda adui kuibomoa na kupenyeza yasiyofaa.
Amani ni tunda la haki na penye haki pana uzalendo.
Ukitaka kumfumza mtu mkubwa uzalendo, kuna mambo mengi ya kuzinhatia:
1: Umuondoe mhusika kwenye yale aliyokwisha yabeba kichwani mwake(pre-empty), ndo uendelee na mafunzo yako.
2: Wewe unaemfunza basi uwe unauishi uzalendo wa kweli na kimatendo kwani unaemfunza pia ana akili ya kupima hali halisi.
3: Kama hauta ondoa maarifa aliyonayo basi uhakikishe mafunzo ya uzalendo yanabeba uzito wa juu saya kuyazidi aliyokuwa nayo.
4: Utahitaji mazingira mazuri, muda mzuri na wa kutosha ili kufanikisha haya na si crash programme.
Tunachokiona kwa sasa kwenye jamii na taasisi zetu ni mbwa mwitu waliovaa ngozi ya kondoo. Kwa maana ya kwamba mioyo ya watu haiendani na matendo yao. Watu hawajaiva kwenye uzalendo ila wanajua ukionyesha picha ya mzalendo watanufaika sana kwenye maisha yao binafsi. Kwa msingi huo watu wanaigiza uzalendo na wale wanaouishi uzalendo wa kweli wanapata shida hata kutoka kwa wasiojua uzalendo na wanaoigiza uzalendo.
Kiongizi mzalendo, awe ni wa mtaa, kikoba au kikundi cha ngoma hayuko tayari kuishi kwa kuwabebesha mzigo wanakikundi wake. Hatakuwa tayari kuzurula na usafiri wa ghali au misafara ya ghali wakati michango ya walionunua hayo magari au usafiri wako ni hohehahe. Huwezi kila siku unatembea umekalia gari ambalo ni sawa na utatuzi wa shida ya elimu au afya sehemu unayoihudumia. Huwezi kutembea na msafara ambao kwa siku unaweza kumaliza utatuti wa elimu au afya kwenye wilaya na una furaha. Moyo wako utakusuta. Hata kama ni sera utaiondoa ili kuwapa nafuu wanakikundi au umoja.
Hivyo, kabla ya kuulilia uzalendo ni vyema kujiuliza na kutafakari kwa muktadha huu:
1: Je ndani ya familia zetu kuna uzalendo?
2: Je tunajifunza uzalendo ndani ya familia?
3: Je tunaweza kutoa mafunzo ya uzalendo kwa watu wasiojua wala kuelewa umuhimu wa uzalendo tangu walipozaliwa?
4: Je tunaweza kuwafundisha watu uzalendo na wakauvaa bila kuona matunda ya uzalendo au uzalendo ndani yetu?
5: Je ndani ya nchi yetu kuna uzalendo wa kweli?
6: Je viongozi wetu wanaongoza kwa uzalendo wa kweli?