Uwekezaji kwenye maarifa

Shayu

Platinum Member
May 24, 2011
608
1,653
Ulaya na marekani wamehangaika sana katika uvumbuzi , swali la kujiuliza upande wetu huku Afrika wajibu wetu nini kwa sasa? Muelekeo wetu ni upi?

Ni kweli kwamba kwa vumbuzi zao wameturahisishia kazi . Wajibu wetu ni kutafuta maarifa ya kutengeneza na kuongezea uwezo wa walivyovumbua. Nadhani jitihada zetu ni muhimu ziwepo hapo.


Tutakapowekeza kwenye maarifa ya watu wetu ndio tutakuwa na maendeleo ya kweli. Hatuwezi kuendelea bila kuzalisha (production knowledge ) kuwa nayo. Na kuwa na watu wengi wenye skills za kuzalisha.


Kujitegemea ni kuzalisha vitu vyetu wenyewe kwa maendeleo yetu na kwa biashara. Na kuwa na uwezo wa kufikiri kwa kujitegemea kama taifa.
Bila nguvu hii ( power of creation ) taifa letu haliwezi kukua.
Maendeleo ya binadamu tuliyonayo yamekuja baada ya watu kuanza kugundua.

Tusipofanya hivi tutaendelea kununua bidhaa kutoka nje na kila siku tutaupeleka utajiri wetu huko.

Lakini la pili nguvu yetu ya kiulinzi itakuwa ndogo mno. Kwasababu wao ndio watakao kuwa wakizalisha silaha na kutuuzia na hawatoweza kutuuzia silaha zenye uwezo mkubwa kuliko zao.

Ni muhimu kuwekeza kwenye maarifa na uvumbuzi na kwenye nguvu ya kutengeneza vitu. Uwezo huo tunao. Tatizo ni jinsi tunavyoelekeza mawazo yetu na kuwa tayari kwetu kujiingiza kwenye uzalishaji huo. Kwenye nia kuna njia. Iwepo nia hiyo tu.

Kiongozi mzuri lazima awe na maono hayo. Ni maono ya kimsingi sana. Hatuwezi kuwa taifa la kununua tu. Haiwezekani.
Tunajua wenzetu wako mbali sana lakini bado tunauwezo wa kufika sehemu fulani kama tukijipanga.

Kama jitihada hii itakuwepo kwa vizazi kadhaa na kama tutakuwa na uongozi mzuri wa kutufikisha huko tutafika.
Hauwezi kuwa taifa linalojitegemea kama hatuko huru kifikra na kama hatuna uwezo wa kuzalisha .

Naomba masuala haya ya msingi tuyapatie muda kuyatafakari kwasababu ni mambo ambayo yako ndani ya uwezo wetu.
Nidhamu, jitihada na nia ya dhati italinyanyua taifa hili. Na kama tutajenga msingi bora kwa vizazi vijavyo; wataendeleza yale tuliyoyaanza kwenye msingi imara.

Muhimu ni kujenga elimu ambayo haina malengo ya kibinafsi ila yenye malengo ya kuleta mapinduzi kwenye jamii yetu na taifa letu. Elimu ambayo itasaidia kuinua jamii zetu sio kuziangamiza. Elimu ambayo ina muelekeo wa kitaifa na sio wa kibinafsi. Elimu ambayo itajenga maadili ya watu wetu kwa kujua kati ya sahihi na potofu na kufuata sahihi kwa faida ya taifa letu.

Muelekeo wa taifa letu na baadae yake inategemea sana fikra za watu wetu zikoje. Umoja wao , mahusiano yao na malengo yao ya pamoja yakoje. Tena na tena tuache ubinafsi kwakuwa ubinafsi hauwezi kujenga jamii iliyo imara. Tujenge jamii yenye maadili na yenye kushirikiana na kusaidiana ili kufikia malengo yetu kama taifa.

Watu wanaelimika lakini wanajiangalia wenyewe lakini sio jamii kwahiyo elimu yao inakuwa na manufaa madogo sana katika kuleta mapinduzi kwenye jamii. Elimu lazima ilete mabadiliko kwenye jamii inayotuzunguka hiyo ndio thamani ya elimu.

Kama elimu yetu itatutengenezea wezi na mafisadi ni nini faida yake? Italetaje mabadiliko chanya ambayo tumekusudia kama taifa ? Tunatafuta maarifa ili tuishi maisha mazuri na yenye nidhamu.

Kama elimu yetu ikikosa nidhamu na watu wetu tunaowaelimisha wasipojua njia sahihi kwa kuwa mafisadi na wezi itakuwa na faida gani? Tutaendeleaje ? Haitakuwa na faida hata kidogo na hatutakuwa na maendeleo kama tutakuwa na wasomi ''corrupt'' ambao hawajui kipi sahihi na kipi potofu kwa taifa lao na kwa jamii zao zinazowazunguka.

Tunahitaji elimu itakayoleta positive impact kwa taifa letu na kwa jamii yetu na kuwafanya watu wetu kuwa na maadili, nidhamu na maarifa ya kutosha kuendesha taifa lao na kulifanya lidumu na liendelee.

Ni muhimu kujenga misingi imara sasa ya kimaadili ( values ) ambazo zitatusaidia sana kuendelea. Bila kuwa na misingi hatuwezi kuendelea. Jitihada zetu za kutafuta maarifa lazima zijengwe kwenye values. Na kwa hakika taifa letu haliwezi kuendelea bila watu wetu kuwa na maarifa.

Hatuendelei kwasababu hatuna maarifa ya kutufanya kuendelea, ni wajibu wetu kuyatafuta sasa hivi. Hakuna taifa ambalo watu wake wameendelea bila kuwa na maarifa. Kwahiyo ni muhimu sana kujiingiza katika kujifunza na kusoma bila kuchoka na kutumia maarifa yetu kwa faida ya taifa na jamii kwa ujumla. Maarifa kwenye kuzalisha na kugundua mambo na mbinu mpya ndio hasa zilifanya mataifa makubwa ya ulaya kuendelea. Hakuna maendeleo yeyote makubwa ambayo tunaweza kuyafikia pasipo wananchi kujiingiza moja kwa moja kwenye ujenzi wa taifa lao.

Kuna hii nguvu ya akili kuleta mabadiliko ipo kwa kila binadamu na tuna uwezo huo wa kubadili taifa letu. Kama tutajiingiza kwenye kutafuta maarifa kama taifa. Ni muhimu sana kwa udi na uvumba kupambana na ujinga na matendo yeyote ya kijinga na kujenga mienendo yetu katika njia sahihi. Na kuacha ubinafsi ambao unaturudisha nyuma sana kama taifa. Na tujenge taifa la watu wanaoshirikiana na kuheshimiana.


 
Back
Top Bottom