UVCCM ninyi ni watu huru, acheni uchawa. Mnatuharibia Nchi yetu

Almalik mokiwa

Senior Member
Jun 5, 2020
147
157
UVCCM ni umoja uliowekwa na kulelewa katika misingi ya kuimba mapambio ya kusifu na kutukuza watawala hata pale pasipo stahili sifa. ACHENI.

Anaandika Almaliki Mokiwa.

Tuweke mkazo katika kuifahamisha jamii juu ya ujio wa hiki kirusi kipya kinacho itafuna nchi yetu taratibu kinachoishi chini ya kivuli cha jina la UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI.

Tuifahamishe jamii kuwa, vijana wao wanatumika kimkakati kubeba matamanio binafsi ya watawala, kupinga kweli yenye itikadi za kimaendeleo na kulinda matumbo ya watasha.

Twendeni tukaijuze jamii kuwa, watoto wao wanapigana kutetea watawala huku wakisahau kuwa umma unawahitaji zaidi ili kulinda maslahi ya watu na kuhakikisha upatikanaji wa haki ya umma kutoka kwa watawala.

Katika karne hii ya 21 tumeshuhudia kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya vijana walio andaliwa kukingia kifua maslahi ya watawala, vijana waliokunywa damu ya kijani, vijana wasiojua kuhoji mambo yenye kugusa maslahi ya taifa taifa lao bali kupambana na wenye nguvu na utashi wa kuhoji kupindishwa kwa mikakati ya kimaendeleo kwaajili ya jamii na taifa kiujumla.

Wakati Mwalimu Nyerere anaondoka duniani, alikuwa na tamaa ya kutaka kuona wimbi kubwa la vijana jeuri, wenye msimamo na wasio endeshwa, wenye uwezo wa kuhoji.

Zilikuwa ndoto za mwalimu Nyerere (muasisi wa taifa hili) kuacha vijana watakaolinda rasilimali zetu na kutetea wale wasio jiweza. Ni mwalimu Nyerere ambae ni muasisi wa taifa hili aliwahi kunukuliwa akisema "Tunataka kuona katika Taifa hili vijana jeuri na wenye kujiamini; si vijana waoga, akina “ndiyo bwana mkubwa". Vijana wenye ujasiri wa kuhoji na kupiga vita mifumo ya jamii isiyoshabihiana na matakwa na matarajio ya jamii ya Kitanzania. Ni kazi bure kwetu, na kwa kweli ni ubatili mtupu, kuwa na Taifa lenye “silaha” za kisasa lakini vijana wake ni waoga.".

Mzee aliongea kwa uchungu mkubwa, akaondoka duniani akitegemea alio wakabidhi kijiti, watayafikia maono aliyotamani kuyaona akiwa hai. Mambo yamekuwa tofauti, nna imani kungekuwa na uwezekano wa mwalimu kurudi hai angalau aone uelekeo wa vijana alio tamani kuwaona, angeomba arudi kulala usingizi wa kifo. Ni mashudu.

Walio mfatia wamefanya madudu na kuunda jamii ya vijana waoga, na mbwa wa watawala, vijana wasio na pumzi ukiwahoji kuhusu muelekeo wa siasa na maendeleo ya nchi yetu wanapandisha joto na kutusi. Ukijaribu kuwadodosa juu ya muendendo mbaya wa upigwaji wa fedha za umma, mdororo wa maendeleo, kupanda kwa gharama za maisha na kuongezeka kwa tozo huku maendeleo yakionekana hafifu wanajibu kwa hoja nyepesi, ukiwabana koo wanakimbilia kusema "mama anaupiga mwingi". Hata kujenga hoja hawajui. Hohe hahe.

Baba wa taifa, serikali uliyo ipigania kwa jasho na damu, ukatamani ituongoze vijana katika misingi ya kuelewa sera na itikadi za kimaendeleo ya nchi yetu ili kujihusisha asilimia 100 katika kukuza uchumi na kutetea haki za wanyonge katika taifa hili, ndio inawafunza vijana kuwa jeshi la kulinda watawala (chinja chinja).

Mwishoni mwa mwaka 2022 alisikika spika wa bunge ambae ni kiongozi mkubwa wa mhimili na mkono wa serikali akiwaambia vijana wake kuwa “Isitokee Kijana yeyote anaungana na mtu yeyote anayemsema vibaya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais Samia ni Rais wa Nchi lakini pia ni mwenyekiti wa Chama chetu. Asitokee mtu yeyote wa Nje ya Chama, wa Ndani ya Chama akawa anamsema vibaya Rais halafu wewe ukamtazama, shughulika naye, CCM hoyeeeee”

Hakutosheka akaendelea kusema “hata mimi Mbunge wako akiwa ananisema vibaya nyooka naye, unajua sababu ni nini? Hata Diwani, Madiwani wote wa Mbeya Mjini sasa hivi ni CCM, hata akimsema vibaya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, na yeye ni CCM, nyooka naye'’. Baba wa taifa, leo watu ulio waamini wanatoa kauli za kutugawa kwa kutengeneza kundi la watu wanaopambana kuzuia vijana wanao hoji ili kupata utambuzi wa mambo yasio enda sawa kama katiba na misingi ya sheria zetu zilivyo ainisha. Si wewe ulizunguuka nchi nzima kuhubiri ujamaa na muungano? Leo wale wanao isemea na kuipigania haki ni maadui namba moja wa serikali uliyo iamini.

Haikutosha, serikali imeamua kuutambua umoja wa vijana wanao jiita "CHAWA" ambao ni vijana wanao tokana na umoja wa vijana wa CCM.

Vijana hawa wamekuja kuwa sumu inayo itafuna nchi yetu taratibu kwa kufifisha dhana ya utendaji na uwajibikaji wa viongozi wetu wa juu. Dhana hii bora katika kuhuisha maendeleo ya jamii inaminywa na kelele zao za nyimbo za kutukuza na kusifu. Kiongozi asiyewajibika katika dhana ya utashi anasifiwa kwa kazi nzuri wakati hata hizo kazi zenyewe HANA. Sifa zinawajaa na kuamini wanatenda wakati mambo ni tofauti nyuma ya kuta za mapambio.

Hawa vijana wanatetea upigaji na kugegedwa kwa mali ya umma na watawala kwa ahadi za vyeo na vijisenti. Wananunuliwa na utu wao kutwezwa. Wamekosa uzalendo.

Leo hii idadi kubwa ya vijana wanaojiunga na Chama cha mapinduzi wanaingia kwa maslahi yao binafsi, wakiwa na mategemeo makubwa ya kupewa ujira. Vijana mpaka wa vyuo vikuu wameingia katika mkumbo wa kutumia vichwa kama vifuniko vya shingo, wana hadaiwa kuwa, kuwa na kadi ya chama cha Mapinduzi kutawahakikishia ajira, elimu ya chuo kikuu imeshindwa kun'gamua kuwa, wanahadaiwa kisiasa na kununuliwa ili kuongeza idadi ya wapiga kura na wahamasishaji wa siasa za chama cha kijani.

Hili linaweza kuwa pepo. Kwa akili ya kawaida, serikali inawezaje kumuajiri kila kijana mwenye kadi ya sisiemu?? Je ni watu wangapi walikuwa makada wa sisiemu mpaka leo wanalalia ugali na chumvi?? Je serikali imeteua/ inateua vijana wangapi katika nyadhfa za juu kwa mwaka?? Leo hii hadi wakina Mzee wasira wapo wanakula nchi lakini vijana wapo na hawaonekani. Je kuna idadi ya vijana wangapi ambao wameteuliwa katika ngazi za ukuu wa wilaya, mikoa, mawaziri, na je idadi yao inazidi idadi ya wazee na watu wa makamo?

Vijana amkeni acheni uzwazwa. Acheni kutumika kimkakati. Jitambueni, ninyi ni watu huru kifikra, mna nafasi ya kubadili uelekeo wa sa siasa za nchi hii, ni nyie mnaotegemewa kuleta mageuzi ya uchumi katika ardhi hii ya amani. Msikubali kutumika kama mbwa wa watawala.

Vunjeni hiyo monyororo, ionyesheni serikali inapokosea ili ijirekebishe na kuziba matobo ili kudumisha dhana ya utawala bora. Msiishie kusifia kila kitu, msiwe bendera fata upepo. Ninyi ni tegemezi kwa taifa hili. Jamii inawategemea. CCM haitawapa mnachokitaka bali utashi na ukombozi wa fikra zenu pekee. Amkeni.
 
Back
Top Bottom