Richmond: Serikali yasema Mwanyika, Hosea wanaweza kushtakiwa
Na Leon Bahati, Dodoma
SERIKALI imesema kuna uwezekano wa kuwafikisha mahakamani Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea ikibainika kuwa walikosea wakati wa kupitisha zabuni tata ya umeme wa dharura iliyoipa ushindi kamapuni ya Richmond.
Akitoa kauli ya serikali juu ya utekelezaji wa maazimio ya bunge kuhusiana na kashfa ya Richmond Development LLC, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema kuwa uchunguzi bado unaendelea dhidi ya vigogo hao.
Kwa sasa kazi hiyo inayoendelea ni vyombo vya dola kufanya uchunguzi zaidi, ili kuona kama kuna makosa yoyote ya jinai yaliyotendwa, alisema Pinda.
Alisema kuwa ripoti ya uchunguzi huo ndiyo itakayoipa serikali dira ya hatua za kuchukua, kama vile kupelekwa mahakamani au hatua za kinidhamu.
Mbali na vigogo hao wawili, Pinda aliwataja wengine ambao wapo kwenye uchunguzi kuwa ni Wakili wa Serikali, Donlad Chidowu na wajumbe wa kamati za wataalamu na majadiliano, ambazo inawahusisha maofisa waandamizi wapatao 12 kutoka wizara na taasisi za umma.
Alifafanua kwamba, taarifa ambazo vyombo hivyo vya dola inazifanyia kazi ni uchunguzi uliofanywa na mamlaka za nidhamu baada ya kuchambua maelezo ya mtumishi mmoja mmoja.
Hatua hiyo ya serikali inatokana na maazimio ya kikao cha bunge mwaka jana, kilichoitaka serikali kuwachukulia hatua watumishi wote waliohusika katika mchakato wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura iliyoipa ushindi kampuni tata ya Richmond.
Katika hatua nyingine, Pinda alisema serikali ipo njia panda kutokana na mikataba mingi ambayo imeivunja na ambayo iko katika taratibu za kuvunjwa.
Pamoja na mkataba kati ya Shirika la Umma Tanzania (Tanesco) na Aggreko na Richmond ambao ulirithiwa na Dowans kuvunjwa, Pinda alisema kuwa wamefungua kesi mahakama za kimataifa pamoja na Mahakama Kuu ya Tanzania.
Pinda alifahamisha kuwa, mkataba wake na Kampuni ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) pia ulikuwa kwenye mchakato wa kuvunjwa, lakini imeshindikana kutokana na wanahisa wake kufungua kesi mahakamani.
Hata hivyo, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliikosoa kauli hiyo ya serikali kwa maelezo kwamba, haikuainisha kiasi cha tozo, ambacho kampuni ya Richmond na Dowans ilitakiwa kulipa kutokana na kuchelewesha kuzalisha umeme katika siku zilizokubaliwa.
Akisoma taarifa ya kamati, Mbunge wa Kibiti, Abdul Marombwa (CCM) alikosoa mtindo wa serikali wa kuwaacha watumishi wa umma wanaotuhumiwa kuendelea na nyadhifa zao wakati wakichunguzwa, akidai kuwa ni rahisi kuingilia uchunguzi.
Kamati inatoa maoni kwamba, uwajibishwaji wa watumishi hao upewe kipaumbele, alisema Marombwa na kupendekeza kuwa zitumike taratibu za kuwasimamisha, kupewa likizo maalumu ama kuhamishwa ili kuepuka kuingilia uchunguzi.
Mwaka jana bunge liliagiza serikali kuwachukulia hatua zinazostahili Mwanyika na Hosea kutokana na kuifanya serikali iingie mkataba na kampuni tata ya Richmond pamoja na Takukuru kuusafisha mchakato uliowezesha kupatikana kwa kampuni hiyo, lakini baadaye kamati ya bunge ilibaini kuwa, ulikuwa na kasoro nyingi na kumfanya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu.