Utawala bora huu hapa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Utawala bora huu hapa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Candid Scope, Jan 13, 2011.

 1. Candid Scope

  Candid Scope JF-Expert Member

  #1
  Jan 13, 2011
  Joined: Nov 8, 2010
  Messages: 11,896
  Likes Received: 119
  Trophy Points: 160
  Yaliyotokea Arusha ni kulipiza kisasi kwa Kikwete na CCM?

  KUNA mfanano wa hali ya juu kati ya mauaji ya Zanzibar mwaka 2001 na ya Arusha yaliyotokea wiki iliyopita.
  Kila kitu kinaelekea kufanana isipokuwa tarehe na chama kilichoathiriwa na mauaji yale. Zanzibar ilikuwa ni mwaka 2001, Arusha ni mwaka 2011, yaani miaka kumi baadaye. Zanzibar ilikuwa ni tarehe 21 Januari, Arusha ilikuwa ni tarehe 5 Januari. Zanzibar ilikuwa ni dhuluma ya uchaguzi wa Rais, Arusha ni dhuluma ya uchaguzi wa Meya. Zanzibar ni mji wa kitalii, Arusha kadhalika ni mji wa kitalii.
  Zanzibar CUF ilidhulumiwa, Arusha ni CHADEMA iliyodhulumiwa. Zanzibar kulikuwa na wakimbizi kwenda Kenya, Arusha walikimbilia nyumba za ibada wakafuatwa na kupigwa humo humo.
  Zanzibar makamanda wa Polisi waliohusika, wiki iliyofuata walipandishwa vyeo na Rais Benjamin Mkapa, Arusha tunasubiri wapandishwe vyeo, si kupandishwa kizimbani!
  Mfanano huu japo si wa kupangwa kwa maana ya watu kukaa ili kuupanga ili ufanane, lakini ni mwendelezo wa mazoea mabaya katika Taifa. Mazoea ambayo yanaendekezwa na tabaka fulani la watawala walioamua kujiweka juu ya sheria. Taifa letu limeingizwa katika utamaduni usiothamini uhai wa mwanadamu.
  Wakati katika nchi nyingine tunaona mtawala kuteleza ulimi tu kunamgharimu kujiuzulu nafasi yake, sisi hapa kwetu kuangamiza makumi ya watu, si kwamba tu hakuna hata uchunguzi wa kiini macho, bali hata wahusika wanaweza kupandishwa vyeo na kupewa medali.

  Wiki iliyopita huko Arizona Marekani, mtu mmoja alimimina risasi na kuua watu sita akiwamo na jaji na kujeruhi wengine akiwamo mbunge. Licha ya kuwa muuaji huyo alikamatwa hapo hapo, lakini uchunguzi umeanza tayari na kwa kasi ya ajabu. Muuaji atachunguzwa, marehemu watachunguzwa, vyombo vya dola vitachunguzwa, ofisi ya mbunge na wasaidizi wake watachunguzwa, chama cha mbunge kitachunguzwa, aliyetoa kibali cha kumiliki silaha atachunguzwa, na si ajabu mtengenezaji wa silaha atachunguzwa na matokeo yatakuwa hadharani muda si mrefu.

  (Nyongeza yangu) Rais Obama wa marekani jana 01/12/11 ameongoza maelefu ya waombolezaji.

  Sababu kubwa iliyo nyuma ya uchunguzi wote huo ni kwa sababu kwanza uhai wa mtu umetoweka, na pili, kuzuia jambo hili lisitokee tena. Bila uchunguzi wa kina kila mauaji yanapotokea mikononi mwa vyombo vya dola, yafuatayo yanaweza kutokea.
  Kwanza, itajengeka imani kuwa mauaji hayo yaliidhinishwa na serikali. Minong'ono imetanda Arusha kuwa kulikuwa na aina fulani ya amri kwa askari ya kufyatua risasi za moto endapo kwa mtazamo wao wataona hali inaruhusu kufanya hivyo. Kama ni kweli, kumpa askari mamlaka ya kuua "bila kusubiri amri nyingine kutoka nyuma", ni kosa linalohitaji uchunguzi wa kina.
  Pili, kwa kuwa askari aliyeua au kujeruhi kwa risasi za moto ni zaidi ya mmoja, ni wazi kuwa mamlaka ya kuamua kuua ilikuwa mikononi mwa zaidi ya kamanda wa polisi; yaani askari wote waliohusika katika operesheni hiyo walikuwa na ruhusa ya kuua. Nani atapinga hili endapo hakuna maandishi yanayozuia au kuonya hali hii kwa askari waliohusika katika operesheni hiyo?............., wenye dhamana ya kulinda uhai wetu na mali zetu, waachie ngazi.

  Hii si kuwaonea kwa sababu hatutarajii kuhalalisha mauaji ya binadamu yoyote. Maadam kuna uhai umepotea, kuna sababu ya kuwajibishana. Tatu, askari na makamanda ni wanadamu wenye mahusiano na watu, na kwa hiyo hata wao wanaweza kuwa na visasi.
  Visasi hivi vinaweza kuwa dhidi ya wakuu wao wa polisi au dhidi ya raia na wana siasa. Kwamba; lilipojitokeza suala la kwenda kuzuia maandamano, kwao ilikuwa fursa inayotakiwa kutumiwa vizuri ili kulipa visasi vyao vya siku nyingi.
  Unaweza kuzuiaje tafsiri hii wakati wakuu wa polisi kwa sababu wanazozijua, waliamua kuita vikosi kutoka mikoa ya jirani bila maandalizi yoyote na kuwaingiza polisi jijini Arusha? Hili lisipochunguzwa na kuwekwa wazi, litakuza chuki na uhasama kati ya polisi na raia.
  Dhana ya kulipa visasi inajitokeza hata kwa kuangalia mtandao wa siasa za taifa letu kwa sasa. Hivi sasa tuna Rais aliyejeruhiwa na mambo mengi. Rais Kikwete licha ya kuingia madarakani kwa kishindo kikubwa, utawala wake umefunikwa na kashfa nyingi ambazo pamoja na kuudhalilisha utawala wake, zimeuimarisha upinzani nchini.
  Chama cha CHADEMA kimekuwa msitari wa mbele kuibua kashfa nyingi zinazomgusa Kikwete na serikali yake. Kibinadamu lazima Kikwete achukie na hata mwanae, Ridhiwani, amepata kuzungumza na vyombo vya habari na kubainisha hilo.
  Ni CHADEMA ambacho kimekuwa kikidai kuwa Rais Kikwete hawezi kukwepa kutajwa kwenye kashfa nyingi: Ufisadi Richmond, Dowans na EPA. Matokeo ya madai haya ya CHADEMA yamemuathiri Kikwete kama mgombea wa CCM pale umaarufu wake uliposhuka kutoka asilimia 80 hadi 60.
  Umaarufu wa CHADEMA ambao kwa sehemu kubwa umejengwa katika msingi wa udhaifu wa Kikwete umekwenda mbali na kusababisha mitafaruku na mipasuko ndani ya CCM. Wako wanaohubiri kuwa kifo cha CCM kitatokea mikononi mwa Kikwete. Madai haya yanatamkwa na wana CCM wenyewe..........

  Mfululizo wa matukio haya kwa rais anayependa umaarufu ni wazi utachochea visasi. Marafiki wa Kikwete wa sasa na wa zamani wanakubaliana kwa jambo moja kuu kuwa Kikwete ni mtu wa visasi. Ni vigumu kutokuamini kuwa hakukuwa na maagizo kuwa dola itumike kuhujumu maandamano ya CHADEMA kule Arusha.
  Kitendo cha kuwapiga, kuwadhalilisha, kuwakamata na kuwalaza ndani wabunge wa CHADEMA, ni ushahidi wa kisasi dhidi ya CHADEMA. Kuliepusha hili ni kuruhusu uchunguzi huru utakaowahakikishia Watanzania kuwa ama wanaongozwa na Rais mwenye visasi au anasingiziwa.
  Matumizi ya nguvu dhidi ya wawakilishi wa wananchi ni utamaduni mpya unaoweza tu kuhalalishwa na ulipizaji visasi lakini unafichwa ndani ya matumizi ya utawala wa sheria za nchi. Tumewaona wabunge wa CCM wakivunja sheria na kupewa shikamoo na saluti badala ya kukamatwa.
  Huko nyuma tulizoea kuambiwa kuwa wananchi wakichagua vyama vya upinzani, Serikali haitawapa maendeleo kama adhabu ya ukaidi wao ...........

  Watu wazima na akili zao, badala ya kuangalia udhalimu waliofanyiwa wakazi wa Arusha na mauaji ya kinyama, wanaibua fikra za udini katika matukio yale ya kutia aibu!
  Kamanda Thobias Andengenye aliyeongoza kikosi cha Arusha ni Mkristo na haiwezekani kuwa alitekeleza amri kwa kutii mamlaka ya kidini. Ni dini gani hiyo inayoruhusu kuua, kupotosha ukweli, kulinda udhalimu kwa mtutu wa bunduki na upotoshaji haki katika uchaguzi wa Meya wa Arusha?
  Kama alivyosema Baba wa Taifa, fikra za udini ni dalili ya kufilisika kisiasa na hivi sasa tunashuhudia kufilisika kwa hali ya juu kama wapambe wa serikali na chama tawala wanaweza kusimama mbele ya vyombo vya habari na kudai kuna udini katika maandamano ya CHADEMA.
  Fikra hizi zikiachwa kuendelea zitawafanya hata wengine kuhoji ni kwa nini CUF waliandamana hawakurushiwa risasi za moto lakini CHADEMA waliandamana wakarushiwa risasi za moto?
  Kwangu mimi, tofauti ya hatua za Serikali dhidi ya CHADEMA na CUF haitokani na udini, bali kisasi cha CCM, Kikwete na serikali yao dhidi ya chama kilichosababisha upungufu wa umaarufu.

  Source: Raia mwema 01-12-11
  [​IMG]
   
Loading...