Utapeli Wa Simu - Epuka

Yona F. Maro

R I P
Nov 2, 2006
4,202
218
Kuna wakati Fulani niliwahi kuona tangazo katika mtandao , jamaa mmoja akawa anauliza jinsi ya kujiondoa katika mchezo wa gulio katika mtandao wa tigo , sina uhakika alifikia wapi katika swali lake hili naamini tigo waliona swali hilo na walimsaidia vizuri .

Tulisikia kuna baadhi ya vikundi vya watu au watu wanawapigia watu simu haswa za mkono kuwapongeza kwa kushinda bahati nasibu hata kama mhusika hakucheza , ukishafika huko unatakiwa kutoa chochote sijui kodi na kadhalika halafu mwisho wa siku ?? unajua mwenyewe .

Wiki iliyopita tu msichana alinibeep , nikampigia kumuuliza nani anashida gani tukabishana kidogo tu lakini hela iliyotumika ni nyingi na kuanzia siku hiyo , namba husika haipatikani tena – mashaka yakanianza

Hayo ni mambo machache ambayo yamewahi kuandama sekta hii ya mawasiliano na hatujawahi kuona tume ya mawasiliano Tanzania ikitoa tamko lolote kwa wananchi kupitia vyombo vya habari au hata katika tovuti yake

Vile vile kampuni za simu ambazo mitandao yao inatumika katika kufanya uhalifu huo nazo hazisemi kitu chochote na hawatoi hata maelekezo yoyote ya kufanya kama mtu akipatwa na mkasa kama huo .

Kwa hakika hizi ni changamoto ambazo inambidi mwananchi aliyekumbwa na mikasa hii ajue mwenyewe afanye nini , manake tume ya mawasiliano haisaidii chochote , watoa huduma ya simu nao wananyamaza , jeshi la polisi nalo unaweza kuambiwa hawana wataalamu wa mambo hayo .

Wakati tunaendelea kujadili mambo hayo na kufikiria mengine zaidi , juzi hapa tumepokea habari njema kwa kampuni ya celtel kuunganishwa katika nchi 12 za afrika kama hiyo haitoshi ni kubadilishwa jina .

Basi leo nikapokea ujumbe wa barua pepe kutoka kwa rafiki yangu akiniuliza mambo kadhaa , kwanza kwa kuipongeza celtel kwa mafanikio hayo na la pili ni suala lingine ambalo limenitia mashaka .

Kati ya hizi nchi 12 Nigeria imo ndani , tunajua Nigeria imetuzidi kwa mambo mengi hii haina ubishi , tunajua historia ya Nigeria haswa katika masuala ya wizi wa mtandao na aina nyingine za utapeli .

Sasa hivi tuko nao katika mtandao mmoja wa simu , naamini Nigeria wana mbinu nyingi za kupambana na hawa wahalifu wa mtandao kuliko sisi kutokana na historia ya matukio haya kuanzia nyumbani kwao .

Sipendi kuongelea zaidi kuhusu Nigeria na mambo mengine yanayoendelea kuhusu nchi hiyo haswa kwa njia ya mtandao , nitamalizia kwa kutoa maelekezo ya jinsi ya kuweza kujilinda dhidi ya tishio lolote la uhalifu ambalo utakumbana nalo kwa njia ya simu kama bahati hiyo ikawa yako .



1 – Ukipokea simu toka kwa mtu au watu usiowafahamu tafadhali uliza jina kamili la mhusika na sehemu alipo na wana au ana mwakilisha nani .

2 – Usitoe taarifa zako au majina yako au vielelezo vyako vyovyote kwa njia ya simu kwa mtu usiyemjua au kama simu hiyo haujapiga wewe kutaka kutoa taarifa hizo .

3 – Ni vizuri usijibu sms au kujibu missed calls kutoka kwa namba ambazo huzijui au ambazo una wasi wasi nazo mitandao ya simu kama Tigo na Vodacom wana huduma ya tafazali nipigie au hamisha salio kama mtu anashida anaweza kutumia huduma hiyo .

4 – Usifanye makubaliano ya biashara kwa njia ya simu , ni vizuri ukaomba makubaliano hayo kwa njia ya maandishi .

5 – Usikubali kutoa taarifa za biashara yako bila kujua zinaenda kutumika kwa shuguli gani na kwa makubaliano gani .

6 – Kama mtu anataka kufanya biashara na wewe ni vizuri ukaomba vithibitisho vyake kuhusu biashara hiyo au tembelea wizara au idara husika ya serikali .

7 – Usijisajili katika michezo au michezo yoyote kwa njia ya simu bila kuwa na taarifa au elimu ya kutosha kuhusu michezo hiyo haswa bahati nasibu .

MFANO YAKIKUTOKEA MAMBO HAYA UFANYAJE ??

1 – Toa taarifa polisi au vyombo vya usalama na uwe na nakala ya maelezo yako kwa uchunguzi au ushahidi wa baadaye , kama nilivyosema hapo juu polisi wengi watakwambia hatuna wataalamu hao lakini jaribu .

2 – Wasiliana na mtoa huduma wako mfano kama uko Celtel piga 100 , sio rahisi warudishe pesa zako kama zimechukuliwa lakini wanaweza kutoa taarifa kwa wateja wengine zaidi .

3 – Pia wasiliana na washika dau wengine ambao ni huru wa masuala haya mawasiliano ambao unafikiri wataweza kukusaidia kwa namna moja au nyingine



4 – Kama ni katika promosheni au bahati nasibu lazima kuna sehemu ya kujitoa katika mchezo huo kama umejitoa na hawataki kukufuta ongea na vyombo husika – kuna mtu alilalamika kuhusu gulio la tigo

5 – Simu yako ina namba 15 maalumu ambazo hazifanani na zingine inayoitwa IMEI (International Mobile Equipment Identity) ambayo inatumika kuitambua simu yako katika mtandao wa GSM . Namba hizo lazima uwe nazo ili kuzuia au kudhibiti wizi wa simu au kutumika kwa namna ambayo siivyo .
Unaweza kupata namba hizi kwa kuangalia chini ya battery au kwa kuandika *#06# sio kwa simu zote lakini , pia inafanya kazi kwa simu ambazo ni original

Haya ni mawazo yangu , kwa kumaliza mimi sio mtaalamu wa masuala ya mawasiliano ya simu ni mtumiaji kama watumiaji wengine wote wenye simu , simuwahikilish mtu wowote wala kikundi chochote wala kampuni na sitetei masilahi au kutangaza biashara ya wowote au kikundi chochote .

Naamini kuna wahusika katika suala hili na wataalamu zaidi wanaoweza kutoa mchango wao wa kitaalamu na kueleza mambo haya kitaalamu zaidi ili watumiaji tuzidi kuamini huduma zao na promosheni zao zingine .
 
Back
Top Bottom