Utamu wa ushindi

Utamu wa ushindi

Rubawa

JF-Expert Member
Joined
Dec 25, 2015
Posts
2,055
Reaction score
3,266
Utamu wa ushindi

Na Ahmed Rajab

KUNA vitu vitamu. Na kuna mambo matamu. Kila utamu una ladha yake na kila ladha ina utamu wake. Ladha ndio huo utamu na huo utamu ndio ladha yenyewe. Na huwa ladha ya kipekee.

Kuna siasa unazoweza kuzielezea kuwa ni tamu. Lakini sio za Marekani ya leo. Kila uchao siasa nchini humo zinazidi kuwa chapwa licha ya vichekesho vya Rais wake Donald Trump. Zinakuwa chapwa kwa sababu ya udhaifu wa siasa za kibwanyenye. Hizo ndizo siasa zenye “kuchezwa” nchini humo. Kwa kusudi, na kwa msisitizo, natumia neno “kuchezwa” kwa sababu zina aina ya usanii.

Hiyo nadhani ndiyo sababu kubwa inayozifanya siasa za huko, juu ya usanii wake, zikose utamu wa kunogesha. Hata zipikwe vipi hazinogi.

Kati ya vyama viwili vikuu vya Marekani, chama cha Republican cha Rais Trump na kile cha Democratic ni kipi kilichoshinda katika uchaguzi wa Novemba 6?

Ingawa ni wazi kwamba chama cha Democratic kilishinda kwa kupata viti vingi katika Baraza la Wawakilishi na kulirejesha Baraza hilo mikononi mwake, hata hivyo Trump anasema kwamba, kwa jumla, ni chama chake cha Republican kilichopata ushindi.

Kauelezea ushindi huo kuwa ni “mkubwa”. Na alijisifu kwa kumnukuu mchambuzi mmoja aliyesema kwamba ushindi huo ulipatikana kwa sababu ya “uchawi wa Trump”. Akikusudia uchawi wa kisiasa.

Matokeo ya uchaguzi huo yameidhihirisha Marekani jinsi ilivyo. Ukilichukua taifa hilo na ukaliweka mbele ya kioo utaona lilivyogawika. Angalia bunge lake jipya lilivyogawika. Chama cha Democratic kimeweza kulitia mkononi Baraza la Wawakilishi lakini kile cha Republican kimeongeza idadi ya nguvu zake katika Baraza la Juu la Senate.

Kwa sababu hiyo, matokeo ya uchaguzi huo wa Novemba 6 hayakuwafurahisha sana wademocrat wa Marekani na wapinzani wa Trump duniani kote. Ushindi wao haukuwa mtamu kama walivyotarajia.

Wao wakiamini kwamba matokeo ya uchaguzi huo yatakuwa ni wimbi kubwa lenye rangi ya buluu litaloikumba Marekani nzima na kuyafanya mabaraza yote mawili ya bunge yawe chini ya chama cha Democratic. Buluu ndio rangi ya chama cha Democratic. Wimbi hilo halijaibuka.

Lingelitokea basi siasa za Marekani zingekuwa na utamu wa aina yake. Trump asingeliweza kufurukuta. Mabaraza yote mawili ya Bunge yangembana akabanika. Tungeweza hata kumshuhudia akishitakiwa na kuhukumiwa.

Kwa mgawanyiko wa Bunge jipya ulivyo , wajumbe wa upande wa Democratic katika Baraza la Wawakilishi wataweza kujaribu kumshitaki. Lakini hata wakifanikiwa Trump anaweza akanusurika asihukumiwe kwa sababu anaposhitakiwa Rais wa Marekani basi Baraza la Senate ndilo linalokuwa Mahakama ya Jamhuri ya Marekani ya kumshitakia.

Kwa hali ilivyo, tutaukosa utamu huo.

Juu ya hayo, ijapokuwa ushindi wa chama cha Democratic haukuwa mtamu hivyo lakini uliweza kulika. Ilifurahisha kwa mfano kuwaona wanawake wawili wa Kiislamu wakichaguliwa kuingia bungeni kwa tiketi ya chama cha Democratic. Mmoja ana asili ya Palestina na mwengine ni mkimbizi kutoka Somalia. Kuna na kijana mwenye asili ya Eritrea ambaye pia alichaguliwa mbunge.

Ushindi wao una utamu wake. Jengine lililopatikana ambalo si dogo na ambalo labda pia lina utamu wake ni uwezo wa Baraza la Wawakilishi wa kuifunga mikono ya Trump na kumzuia asiweze kuchukua hatua zitazokuwa na madhara kwa Marekani na ulimwengu kwa jumla.

Kwa ufupi, matokeo hayo yameupa kila upande fimbo ya kikatiba ya kuuchapa upande mwingine. Chama cha Democratic kitalitumia Baraza la Wawakilishi na chama cha Republican kitalitumia Baraza la Senate.

Hayo ni matokeo ya siasa za kibwanyenye. Hata viongozi wakibadilishwa kwa kura, kila ninapoziangalia siasa za huko ninazidi kubaini kwamba kuna nyufa nyingi katika demokrasia ya Marekani.

Hamna shaka kwamba imeipita demokrasia changa kama ya Tanzania na za nchi nyingi nyingine. Lakini hicho si kigezo cha kuihesabu demokrasia ya Marekani, ambayo ni ya kibwanyenye, kuwa miongoni mwa za demokrasia za haki na zilizopevuka zaidi ya nyingine. Hasha. Demokrasia ya Marekani ni demokrasia yenye kuyatetea matabaka ya wenye kujiweza.

Demokrasia hiyo si ya kuliwa na walalahoi. Itawasakama kooni tu. Hawatoweza kuila seuze kuuonja utamu wake. Haiwapi wananchi wote haki sawa, licha ya utawala wake wa kisheria na taasisi zake zenye kuilinda katiba, mambo yenye kukosekana katika nchi kama Tanzania.

Ni wazi kwamba kuna demokrasia iliyo pana zaidi na yenye kina kikubwa zaidi kushinda demokrasia hiyo ya kibwanyenye iliyopo Marekani. Kama haipo basi inaweza ikasimamishwa, hususan katika nchi za Kiafrika zenye demokrasia isiyo na mizizi imara.

Licha ya ushindani wa kugombea viti, hakuna mchuano halisi wa kiitikadi baina ya vyama vikuu vya siasa huko Marekani. Hata wafuasi wa chama cha Democratic ukiwasikiliza utawasikia wakiwakosoa wasoshalisti wa nchi za Ulaya sawa na wanavyowakosoa mahasimu wao wa chama cha Republican kwao Marekani.

Kwa upande wao nao, wasoshalisti wa Ulaya, mfano wale wa chama cha Leba cha Uingereza, wanasikitishwa na wafuasi wa chama cha Democratic cha Marekani. Wanawaona kuwa wameelemea zaidi kwenye siasa za mrengo wa kulia.

Halafu amezuka Trump, kiongozi asiyetabirika.

Kuna dhana mbili kumhusu Trump zilizozagaa Marekani na nje ya Marekani. Moja ni kwamba yeye ni kitisho kwa demokrasia ya Marekani na amani ya ulimwengu.

Ya pili ni kwamba Trump ni mwokozi wa uchumi wa Marekani na shujaa wa kuifufua Marekani na kuiweka mbele.

Kwa namna Wamarekani walivyopiga kura Novemba 6 inaonesha kwamba wengi wao wanamuona Trump kuwa ni kiongozi mwenye kuudhi lakini asiye kitisho kwa maisha yao.

Kiongozi huyo, juu ya machachari yake na ubabe wake, bado angali akipendwa na wengi wenye kuvutiwa na uzalendo wake wa kiuchumi na sera zake dhidi ya wahamiaji. Wanaupuuza uongo anaousema mara kwa mara, wanaonesha kama hawajali kuwa hufanya mambo yasiyostahili kufanywa na kiongozi wa hadhi yake.

Trump na Rais John Magufuli wa Tanzania wana mengi yenye kufanana. Na zile dhana mbili zinazomhusu Trump na zilizozagaa ndani na nje ya nchi yake nazo pia zinamhusu Magufuli. Kuna wenye kumuona kuwa ni myongaji wa demokrasia na kuna wenye kumuona kuwa ni mwokozi mwenye kuijenga Tanzania.

Ndio maana wapo wengi wenye kuvutiwa na mbwembwe za Magufuli na propaganda za wapambe wake kuhusika na masuala kadha wa kadha. Hata hivyo, zipo tofauti baina ya viongozi hao.

Tofauti kubwa iliyopo, kwa mfano, ni kwamba Magufuli kwa madaraka makubwa aliyo nayo na kwa namna anavyotawala anaweza akajifanyia atakavyo bila ya hofu ya kuwajibishwa. Wapinzani wake hata wanapojaribu kumtaka ajiwajibishe hushindwa.

Trump, kwa upande wake, hawezi kujifanyia atakavyo. Hawezi kujifanyia hivyo hata akitaka na bila ya shaka atataka. Hawezi kwa sababu taasisi zilizopo Marekani zenye kuilinda katiba zitamzuia. Hazitomuachia kwa sababu mfumo wa demokrasia uliopo nchini mwake hauumpi kiongozi mwenye madaraka makubwa kama yake fursa ya kumwezesha azikalie kichwani taasisi hizo na wananchi wenzake.

Miongoni mwa taasisi hizo ni mabaraza mawili ya Bunge, mahakama na mfumo wao wa kisheria pamoja na vyombo vya habari na waandishi wa vyombo hivyo.

Inavyoelekea ni kwamba kwa mgawanyiko wa bunge uliopo Trump lazima anajiandaa kusumbuliwa na wajumbe wa Democratic katika Baraza la Wawakilishi.

Wajumbe hao watamsaili Trump kwa mengi. Wabunge wa upinzani wa Tanzania huwekewa pingamizi wasiweze kumsaili Rais wao hata kama wakitaka (na bila ya shaka wanataka).

Siasa za Marekani zinazidi kuwa za maudhi na chuki. Ni chapwa na hazina utamu.

Trump hapendezi abele ya macho ya watu fulani, kwao na kwingi duniani, kwa sababu ya siasa zake za chuki, kwa namna anavyoupinda ukweli na kwa namna anavyokoroga mambo katika medani ya siasa za kimataifa.

Tunaona kwa mfano namna alivyoikamia Iran na anavyotamani pawepo na mabadiliko ya uongozi nchini humo. Anafanya hivyo ili kuziridhisha Israel na Saudi Arabia. Israel inaiogopa Iran kwa kuwa nchi pekee katika eneo la Mashariki ya Kati inayosimama kidete kuwapigania Wapalestina na kuzitetea haki zao walizopokonywa na Israel.

Saudi Arabia haiipendi Iran kwa sababu ya tofauti za kimadhehebu. Saudi Arabia inachochea, kwa kusudi, uhasama baina ya wafuasi wa madhehebu ya Sunni na wale wa madhehebu ya Shi‘a.

Iran ina msimamo madhubuti dhidi ya ubeberu na siasa za kuyaonea mataifa ya wanyonge. Saudi Arabia hadi sasa imekuwa upande wa wale wenye kufanya uonevu.

Sera za Trump kuhusu siasa za nje ya nchi yake huenda zikazidi kuzichafua siasa za kimataifa. Kwanza, msimamo wake wa kutousaidia kwa hali na mali Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa utazifanya taasisi hizo ziwe dhaifu. Kadhalika, sera zake zitazifanya nchi zisizoaminiana zizidi kutoaminiana na kuufanya ulimwengu uingie mashaka na ujae bughdha na wasiwasi.
 
Back
Top Bottom