Utakapooa usisahau mambo haya

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,031
50,933
UTAKAPOOA/KUOLEWA USISAHAU MAMBO HAYA

Na, Robert Heriel

Kwa Wanangu, damu yangu, watu wa kabila langu, taifa na jamii yangu, Muishi vyema sawa sawa na mipango ile tuliyoijia katika Ulimwengu huu. Mimi Baba yenu, ndiye Taikon, nimewaandikia haya nikiwa katika Mji wa Morogoro, majira ya masika, hali ya hewa ikiwa ni mawingu mazito na manyunyu, katika mwaka wa tano wa kumiliki kwake John Pombe Magufuli, Rais wa Tanzania, mwezi wa nne katika mwaka 2020 kulingana na Calenda ya Gregori.

Nami nimeona nikuandikie mambo haya ili upate kuishi kwa furaha, ukimfurahia mke wako naam kwa mwana wa kike ukimfurahia mume wako.

Nawe ukiona jua likichomoza basi tambua hiyo ni asubuhi, nalo likizima fahamu hiyo ni jioni. Nawe ukiona nyota nyingi angani basi fahamu huo ni usiku mnene. Upendo huzama na kuchomoza kama jua. Upendo ukichomoza ndani ya nyumba nuru ya mafanikio huimulika nyumba yenu, nanyi mtakuwa na furaha siku zote.

Walakini msisahau kuna siku upendo huzama machweo kama vile Jua lizamavyo. Nao ukizama giza huikumba nyumba yenu, mtaishi kwa huzuni na kuchukizana, kila mmoja akimuona mwenzake ndiye mkosaji. Hii ni kwa sababu upendo uzamapo watu hutumia tochi(kurunzi) kumulika makosa ya wengine ilhali upendo uwapo mchana mwanga wa mapenzi hupofusha mboni za wapendanao.

Basi hata upendo ukizama kama jua na giza likitawala ndani ya nyumba yenu, usiache kuona nyota njema za umpendaye. Hata kama ni ndogo ndogo, hizo hizo zishikilie na zifanye kuwa kubwa ukivumilia mpaka asubuhi itapofika utakapoliona jua la mapenzi yenu.

Nawe tafuta mwanamke mzuri umpendaye mwenye sifa uzitakazo. Mwenye uzuri wa umbo na sura itakayoufurahisha moyo wako pindi umtazamapo wakati wa shida, na huzuni, na kero za maisha. Kwa maana ni jambo gani linalofurahisha zaidi ya mwanamke mzuri?

Mwanamke mzuri wa sura ni dawa kwa moyo wenye huzuni, ni kicheko wakati wa kilio. Je ni mwanaume yupi asiyechangamka amuonapo mwanamke mwenye umbo zuri la kuvutia. Basi ikiwa utaamua kuoa, oa mwanamke mzuri wa sura na umbo, tena mwenye sauti nzuri kama mwanamke, hata rangi ile uipendayo usisahau.

Mtapanga siku ya sherehe yenu, wewe na huyo mkeo. Mtaita watu waje wajumuike nanyi katika sherehe yenu. Tena msiache kuwaita wazazi wenu, walio wazaa, waliowalea, walio wasaidia na watu wote waliowema kwenu, hao wote mtawaita bila ya kukosa. Mkiwapasha habari ya ndoa yenu mwezi mmoja kabla kila mmoja kwa umuhimu wake.

Hata kama mzazi mmoja aliyekuzaa hakukulea iwe kwa makusudi au kwa bahati mbaya, lakini ilimradi yupo hai na unajua wapi alipo basi utampa habari ya sherehe yenu, aje asherekee harusi ya mtoto wake, siku hiyo itakuwa siku ya furaha baina yenu wawili, huku mkisamehe yaliyopita na kuanza upya maisha mapya.

Tena msiache kumualika Mungu wa Baba yenu, ndiye baba yenu Taikon. Huyo mtamualika miezi saba kabla ya harusi yenu. Kila siku ya saba katika miezi hiyo saba mtafunga mkimuita na kumuomba ahudhurie kwenye sherehe yenu, iwe kwa uwakilishi au yeye mwenyewe, Lakini sharti aje. Hivyo kila mwezi katika hiyo miezi saba ya kutuma mualiko kwa Mungu wa Taikon, mtafunga siku nne. Basi mpaka siku ya harusi mtakuwa mmefunga siku 28 naam ndiyo miandamo ya mwezi mpya katika ndoa yenu.

Hivyo muundo wa mualiko utakuwa kama ifuatavyo;
!. Awamu ya kwanza ataalikwa Mungu wa Taikon
2. Awamu ya pili Wazazi/ Walezi wa pande mbili
3. Ndugu, jamaa na marafiki
4. Makundi maalumu na uwakilishi wao. Hapa nazungumzia walemavu kwa aina zao kila kundi litawakilishwa na mmoja, wafungwa(mmoja wa kike na wakiume), watoto wa mtaani( mtoto wa kike na wakiume)
5. Watu mashuhuri: viongozi, wasanii, wanamichezo na wanataaluma miongoni mwa wengine.
6. Awamu ya sita ataalikwa Shetani. (anaweza kuja yeye au mwakilishi wake mmoja)
7. Wanyama na ndege.
8. Muwakilishi kutoka kwa Wafu

Basi usisahau kuyaalika makundi hayo kwa maana kila kundi litakuja kuwakilisha jamii zao.

Tena siku hiyo isiwe siku ya wengine kujisikia vibaya kwaajili yenu. Wala msifanye kwa kujitukuza ninyi bali fanyeni kwa kufurahia uwepo wenu duniani na uwepo wa hao mliowaalika. Mkijua Mungu wa Taikon ndiye astahiliye sifa na utukufu.

Siku hiyo msichinje, wala msile nyama, tena msile chakula cha kiumbe yeyote mwenye damu. Naam msile nyama siku hiyo, kwa maana hamtaweza kuiita siku ya furaha kwa kuchinja na kumwaga damu za viumbe wengine.
Mtakula vyakula jamii ya nafaka, mboga, matunda, mizizi na mbegu. Tena mtatengeneza na vinywaji katika siku hiyo. Mkiwagawa watu makundi makundi kulingana na mahitaji yao ya unywaji, tena kama mtaweka vile, basi hakikisheni watu wasilewe katika siku yenu ya sherehe, ila msiwazuie kutumia kileo kwa wale wapendao.

Tena mtavaa mavazi yenye utukufu na heshima kwa maana siku hiyo watakuwepo watu wote na Mungu wa Baba yenu Taikon.

Tena kila uwakilishi utavaa sare yake, na kukaa kwenye siti zao.

Kwa habari za Muziki, siku hiyo itapigwa miziki ya kumpendeza Mungu wa Taikon, kisha itapigwa miziki ya kukupendeza wewe, ikitaja majina yako na sifa zako, tena ikisifia uzuri wa mke wako kwa majina yake. Basi utawaambia wasanii wa kuimba watunge nyimbo hizo zenye kukusifu wewe, mkeo na Mungu wako, katika siku hiyo.

Tena harusi itakuwa na masaa saba tuu tokea ianze, ikipendeza masaa matatu mchana, masaa matatu usiku na lisaa limoja ni mapumziko na muda wa mambo ya dharura.

Tena utakapo kula kiapo, kumbuka atakuwepo Mungu wa Baba yako, huyo aliyemkuu na asiye na mshirika. Basi utaapa kwa jina lake ambalo nilikupa, tena shetani atakuwepo naye atasikia kiapo chenu, na watu wote. Basi ukila kiapo usiogope kusema mbele zao ikiwa utasema kwa haki. Na haki ndio hii;
umche Mungu na kushika maagizo yake.

Na hivi ndivyo utakavyo kula kiapo, utasema;
" Naapa kwa Mungu, Muumba wa mbingu na nchi, yeye aliye na nguvu, muweza wa yote. Mwenye upendo na rehema; Nitakupenda siku zote (majina ya mke wako), na kukulinda. Sitakuacha mpaka pale mambo haya yatakapotokea; Mauti kututenganisha, usaliti wa mapenzi, au kukukuta na ushirikina na uchawi wa namna yoyote ile. Lau kama mambo haya hayatotokea basi naahidi mbele ya Mungu wangu, na nafsi yangu nitakupenda daima na kamwe sitokuacha Mke wangu( Majina ya mke wako)"

Utakuwa umenyosha mkono wako wa kulia huku mkeo akiwa nyuma yako na wote mkiwa mmesimama jukwaani.
Kisha mke wako naye atasimama zamu yake kuapa, Ataapa kwa maneno haya au yanayofanana na haya:
" Naapa kwa Mungu wa Mume wangu, ambaye kwa sasa ndiye Mungu wangu, Muumba wa mbingu na nchi, yeye aliye na nguvu, muweza wa yote. Mwenye upendo na rehema; Nitakupenda siku zote (majina ya mume) na kukutii. Nakubali kuwa hutoniacha wala kutengana nawe mpaka pale kifo kitakapotutenganisha, usaliti wa mapenzi na kama utanikuta na ushirikina na uchawi wa aina yoyote. Naahidi sitofanya mambo mawili kati ya hayo ndio usaliti wa mapenzi na uchawi. Naahidi kukupenda na kukutii mbele ya Mungu wako(majina ya mume) na kamwe sitofanya hila kukuacha"

Kisha baada ya viapo, zitachukuliwa glass mbili zilizowekwa maji yaliyoombewa kwa miezi saba na siku 28 za mifungo. Glass moja utashika wewe na mkeo atashika ya pili.
Kisha mtasujudu mkiwa mmeelekeana uso kwa macho. Kila mmoja atamnywesha mwenzake maji hayo, na wote mtasema maneno haya;
" Hili ni agano la mioyo yetu, upendo wetu. Maisha yetu, kizazi chetu. Kama ilivyoleo basi hata milele maneno haya yaishi ndani yetu baada ya kunywa maji haya. Kama tulivyofunga miezi saba, mifungo 28, ndivyo maadui zetu walivyofungwa, tumefunga laana kwetu na kizazi chetu"

Mkishakunywa maji ya zile glass, mtasimama. kisha mtageuka mahali ambapo mlipatenga kwa ajili ya kuketi Mungu wenu. Mtatoa heshima, kisha mume atachukua karatasi mliyoandika maono yenu, mipango yenu, na vile mtakavyo kizazi chenu kiwe. karatasi hiyo iwe ya rangi ya samawati na maandishi meupe. Kisha mume utaenda na mshumaa mbele ya kiti alichowekewa Mungu wenu, utasujudu mbele ya kiti hicho na kuchoma hiyo karatasi huku ukinuiza maneno kimoyo moyo wewe kama Baba.

Tena asiwepo mtu yeyote ajuaye habari ya hiyo karatasi na kilichomo ndani yake. bali watu waone tuu mambo hayo mkiyafanya.

Ikiwa huna mali za kufanikisha mambo yote hayo, basi utafanya sherehe ya kawaida, ukiwaalika watu ambao hawatakuja lakini utaacha siti wazi kwa kila muwakilishi. Na kila siti iliyowazi utaiandika mtu aliyepaswa kuikalia. Kwa mfano; Ikiwa ulitaka kumualika Mtu mashuhuri lakini kutokana na hadhi yako ya kimaisha ukashindwa, basi utaandika jina la mtu huyo kwenye siti iliyowazi, hapo hatakalia mtu. Hivyo ndivyo utakavyofanya

Ikiwa mwanamke wako hukumkuta Bikra, Basi atatubu mbele zako siku hiyo ya sherehe kwa kutokuwa mwaminifu na kutokuwa msafi. Tena ikiwa hukumkuta bikra basi utakula fungate kwa siku tatu tuu. Kama uliikuta Bikra utakula fungate kwa siku saba na zaidi kulingana na uwezo na mazingira ya wakati wenu. Lakini sharti fungate isipungue siku saba.

Tena kama Ulikuta bikra, utatangaza hadharani kuwa mwanamke uliyemuoa ni bikra, tena utamshukuru Mungu kwa habari hiyo. Lakini kama hukukuta bikra basi usisema kitu siku hiyo, lakini mwanamke atawajibika kuomba msamaha kwa lugha ya utuuzima. Kamwe usijeongopa mbele ya madhabahu siku hiyo.

Basi ikiwa katika ndoa yatakuwepo mambo ya uchawi na ushirikina kutoka nje yaani adui zenu. Basi usitishwe na mambo hayo, wala usiyaogope, kwa maana ukiyaogopa utayakimbilia. Nawe utafunga na kuomba kama nilivyokufundisha, naye mchawi na jamii zake hawatokuweza kamwe.

Ikiwa unataka upate mtoto, basi kabla ya kumpa mkeo mimba, utafunga siku saba, kisha baada ya siku saba utakula na kuiweka afya yako vizuri kwa mwezi mmoja huku ukimuomba Mungu na kunuiza maneno ya mtoto umtakaye. Baaada ya mwezi wa kula vizuri kuisha jumla itakuwa ni siku 37. basi siku ya 38 mpaka 45 utamuingilia mke wako kwa ajili ya habari za mimba. Naye akipata mimba, utamsemea maneno kila baada ya siku saba, ukilishika tumbo la mke wako ukisema maneno ya baraka kwa mwanao.

Ikiwa utakuwa kwenye chumba cha kupanga isiyo na faragha yaani kwa juu haina rufu(silling board) basi utaongeza sauti ya sabufa ili watu wasisikie mkisherekea. Hata hivyo haifai kila siku kuliza sabufa kwani bado haitakuwa faragha. Basi kwa mwezi walau mara moja utaenda na mkeo nyumba za wageni kuchukua chumba ili mpate ule ukimya wa faragha huku mihemuko yenu ikipiga kelele mkifurahia miili yenu. Siku hizo mfanye kwa kiwango cha juu ili kuzikausha hamu za kila mmoja wenu.

Ikiwa Mungu amekujalia kuwa na nyumba kubwa yenye uzio, basi kwa mwezi usisahu walau mara moja kupeana mapenzi usiku mkiwa nje huku miili yenu ikipigwa na upepo wa nje na nyota za angani zikiwashuduia.

Itaendelea wakati mwingine.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
0711345431
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom