Utafiti wa Synovate wazidi kukosolewa

Josh Michael

JF-Expert Member
Jun 12, 2009
2,523
77
SIKU chache baada ya kampuni ya Synovate kutoa matokeo ya utafiti wao, wasomi nchini wameufananisha utafiti huo na chati za muziki wa kizazi kipya (Bongo Flava) huku wakiwaonya Watanzania kuwa makini na matokeo ya tafiti.

Jumatatu wiki hii, kampuni ya Synovate ilitoa ripoti ya utafiti iliyoufanya kwa kipindi cha miezi mitatu; Oktoba hadi Desemba baada ya kuwahoji uso kwa uso watu 2,000 waliogawanywa sawa na uwiano wa idadi ya Watanzania ambapo CCM iliongozwa kwa kupendwa na wananchi kwa asilimia 70 ikifuatiwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) asilimia 17 na Chama Cha Wananchi (CUF)asilimia tisa. Huku vyama vya UDP, TLP na NCCR-Mageuzi vinapendwa na Watanzania kwa asilimia moja.

Pia utafiti huo ulionyesha kuwa Rais Jakaya Kikwete atashinda kiti cha urais katika uchaguzi kwa asilimia asilimia 75 akifuatiwa na Freeman Mbowe wa Chadema aliyepata asilimia 10 na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF mwenye asilimia tisa.

Lakini, wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti Profesa Abdallah Safari, Mhadhiri wa Chuo Kikuu(UDSM) Bashiru Ally na Profesa Mwesiga Baregu wamesema utafiti huo haujakidhi haja na tija ya Watanzania hususan katika masuala muhimu ya kitaifa na kwamba utafiti huo unapingana na ukweli halisi wa hali ya mambo nchini.

Ally ambaye ni mhadhiri msaidizi (UDSM) aliwataka wananchi kuyachukulia matokeo hayo kwa umakini kwa kuwa hayakuzingatia matukio halisi ya masuala nyeti na tete ambayo yanahitaji tafsiri pana.

"Utafiti sio chati za muziki wa bongo fleva wa kutaka kujua nani zaidi bali ni maoni ya kutaka kujua uhalisia na utete wa masuala mbalimbali ambayo yanahitaji tafsiri pana nchini.

"Sasa leo ukiniambia huyu ana mvuto kuliko huyu maana yake nini. Nawaomba wananchi wawe makini na matokeo ya namna hii kwani hayajengi nchi,"alisema Ally.

Mhadhiri huyo ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa ndani na nje ya nchi alifafanua kwamba ripoti hiyo isichukuliwe kwa uzito mkubwa kwa kuwa Watanzania wapo katika kipindi cha mpito cha masuala nyeti ikiwemo sakata la Richmond, serikali ya mseto Zanzibar, ongezeko la uhalifu pamoja na ongezeko la pengo baina ya waliyonacho na wasiyonacho.

"Kwa sasa nchi haihitaji suala la umaarufu, inahitaji tafsiri pana ya masuala tete kama ongezeko la uhalifu, ongezeko la pengo baina ya waliyonacho na wasionacho, sakata la Richmond, serikali ya mseto Visiwani Zanzibar,"alisema Ally.

Ally alikosoa mfumo wa maswali ulioulizwa ka Synovate kwa kuwa hakuzingatia mahitaji halisi ya Tanzania.
Profesa Safari alisema ripoti hiyo inamtafaruku na kwamba matokeo yanapingana na ukweli ulivyo nchini.

"Hawa Synovate wanatuona Watanzania wote tumelala, kwanza hawajatueleza mbinu walizotumia, aina gani ya watu waliowahoji, maeneo walipofanyia utafiti huo. Ukweli ni kwamba matokeo haya yanapingana na ukweli wa mambo ulivyo nchini," alisema Profesa Safari.

Hata hivyo, Profesa Safari alihoji kuwa kama kweli matokeo hayo ni ya kweli na yanaeleza uhalisia ulivyo kwa nini serikali inaogopa uwepo wa wagombea binafsi katika uchaguzi.

Naye Profesa Baregu alisema mfumo wa maswali uliotumiwa katika kufanya utafiti uliokuwa na tatizo.

"Mfumo wa maswali ulioundwa na Synovate haukidhi haja na tija kutokana na ukweli Tanzania ipo katika kipindi kigumu katika nyanja mbalimbali. Na hili ni tatizo,"alisema Profesa Baregu

Profesa huyo alisema katika utaratibu wa kawaida, utafiti wowote ni lazima uzingatie umetoka wapi, mpo wapi na mnakwenda wapi.

Katika ripoti ya Synovete mbunge wa Kigoma Kasikazini Zitto Kabwe alitajwa kuwa mbunge maarufu kisiasa kuliko wabunge wote, huku akiwaacha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Spika wa Bunge Samuel Sitta wakiporoka. Kwa mujibu wa utafiti huo, Zitto aliongoza kwa kupata asilimia 31 ya kura zote akifuatiwa na Anne Kilango asilimia 13, Dk Wilbroad Slaa asilimia 7, Dk Harrison Mwakyembe asilimia sita, John Magufuli tatu na Lawrence Masha asilimia mbili.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom