Usiniue Mama Yangu

Usiniue Mama Yangu

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
34,115
Reaction score
79,523
USINIUE MAMA YANGU

Na, Robert Heriel
Taikon wa Fasihi.

Mama mimi ni mwanao (Kwa sauti ya huzuni). Mimi! Mimi ni mtoto wako. Usiniue.

Ilikuwa ni sauti ya kijusi kilichokatika tumbo la Bertha ambayo ilipenyeza katika mfumo wa ufahamu wa Bertha aliyekuwa yupo kitandani akilia kwa uchungu. Bertha alikuwa katika njia panda, hakujua ashike njia ipi itakayompa furaha.

Uso wote ulilowa kwa machozi hali iliyomfanya aone ukungu mbele ya macho yake. Mkononi alikuwa ameshika vidonge vya kutolea Mimba. Alijua anachotaka kukifanya ni dhambi tena dhambi kubwa inayohusu damu yake yeye mwenyewe.

Alisimama mbele ya kabati lenye kioo kisha akaanza kuliangalia tumbo lake huku akilishika shika. Macho yake bado yalikuwa kwenye kioo.

"Nisamehe mwanangu"

Aliongea huku akianza kulia tena kwa sauti mdomo ukitetemeka. Aliona sura yake kwenye kioo jinsi alivyokuwa akilia. Ni wazi uso wake ulizingirwa na mikunjo mingi ya huzuni.

"Usiniletee upumbavu, tafuta aliyekupa hiyo mimba, malaya wewe"

Alikumbuka maneno ya Devis kijana ambaye aliamini ndiye alimpa huo ujauzito. Maneno hayo yalimpandisha kisirani akafungua zile dawa na kuziangalia kana kwamba anahesabu mpaka tatu.

"Mama usiniue Mwanao, wewe ndio mlango wangu wa kufika duniani. Nakutegemea Mama yangu"

Sauti ya kijusi kilichopo tumboni ilinong'ona kwenye fahamu za Bertha ambaye alionyesha dalili zote za kufanya jambo baya na hatari kwa maisha yake na ya kilichokuwa tumboni.

"Nisamehe mwanangu, Baba yako ndiye chanzo"

Bertha aliongea kwa hisia kali kisha akafumba macho na kubwia vidonge akivisindikizia na maji. Alibaki akiwa kafumba macho akisubiri kitakachofuata. Punde tumbo likaanza kumuuma. Awali aliwahi chomwa na miba akiwa kijijini akiokota kuni lakini maumivu yake hayakufikia hata robo ya maumivu aliyokuwa akiyapata. Pia aliwahi kuungua na maji ya moto lakini maumivu yake hayafikii maumivu ya siku ile. Alihisi kifo na lango la kuzimu aliliona kwa mbali.

Ghafla alihisi kizungu zungu kilichomfanya aone dunia inazunguka. Tofauti na wataalamu wa jiografia wanaodai kuwa dunia inazunguka kutoka magharibi kuelekea mashariki lakini Bertha aliona dunia inazunguka hovyo hovyo kama pia tupu.

*Mama hukutaka nije duniani. Hukutaka niuone ulimwengu. Hukutaka nicheze na wenzangu walio katika matumbo ya mama zao. Umeamua kuniua kwa mikono yako mwenyewe. Bora hata ningeuawa na wengine lakini ni wewe mama yangu umetoa uhai wangu.

Nimekosa nini Mama yangu. Najua unasoma, sijui ni elimu ya upili au ya chuo mimi bado ni mdogo sielewi lakini je elimu hiyo ni muhimu kuliko mimi mwanao. Mama embu ni jibu basi. Elimu ndio imekufanya uniue mimi mwanao. Nalia! Nalia mimi.

Mama ni nini nimekosa mpaka uniue na madawa makali kama haya. Yanaunguza sana ngozi yangu laini. Ona yanavyonichoma na kupasua macho yangu ambayo ningeyatumia kuona. Mama hujui naumia. Ona damu inavyonitoka, tazama mama ubongo unavyomwagika huu ungetumika kubuni mambo kadhaa huko duniani. Mama naungua na kemikali za madawa uliyomeza.

Mama ulipenda ujana kuliko kunipenda mimi. Ukaona mimi nitakuharibia kula sijui mnaita Bata. Mimi bado ubongo wangu haujakomaa hivyo sielewi. Lakini kweli mama Bata na ujana ni muhimu kuliko mimi mwanao. Mama embu fikiria kidogo. Samahani lakini sio kama nakufundisha kwa wewe ndiye mama yangu na ndiye mkubwa. Mama niambie basi bata na ujana ndicho kilichoniponza mimi mwanao.

Mama nilitamani kuyanywa maziwa yako. Nilihadithiwa maziwa ya mama ni matamu hivyo nilitamani kuyanywa maziwa ya mama yangu. Lakini umenikatili badala ya kunywa maziwa unaninywesha madawa makali yenye sumu. Badala ya kutunzwa vyema leo natupwa chooni. Mama nimekukosea nini.

Mama hata kama Baba amekukataa lakini adhabu unayonipa mimi ni kubwa sana. Kwa nini usisubiri hiyo miezi iliyobaki unizae. Mbona wengine wanaishi hata kama wana maisha ya kifukara. Mama mimi sikuhitaji utajiri ndio maana nilizaliwa uchi. Nilichohitaji ni upendo wako kama mama lakini wewe umeonyesha ukatili. Baba anamakosa yake lakini wewe ndiye muamuzi wa mwisho hivyo nilikutegemea sana wewe.

Mama hukutaka hata kuniona ninafananaje.Hukutaka kujua hata jinsia yangu, na rangi yangu. Kweli ulinichukia.

Kwa heri mama Yangu, Nilikupenda ila wewe umenichukia**

Lilikuwa lalamiko la kijusi kilichokuwa kinahangaika tumboni kikipambana na makali ya dawa . Bertha alikuwa ameshapoteza fahamu. Alizinduka kesho yake akajikuta hospitali kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Alikumbuka maneno ya mwanae ambayo aliambiwa kwenye fikara zake.

Usiniue mama yangu

Niite Taikon wa Fasihi
Robert Heriel
0693322300/ 0711345431

1580298586349.png
 
Sijasoma ujumbe huu zaidi ya mstari mmoja lakini machozi yameanza...
 
Back
Top Bottom